“THE JEWISH PHENOMENON” “
SEHEMU YA 6”
Siri 7 Zilizowaisaidia Wayahudi Kuwa na Utajiri Mkubwa na Unaodumu
2. JIJALI NA KUJISAIDIA NA WATU WATAKUJALI NA KUKUSAIDIA.
-Wayahudi ndio jamii ambayo imewekeza zaidi katika taasisi zao za kusaidiana kuliko jamii nyingine yoyote ndani ya Marekani.
Wayahudi wana uwezo mkubwa sana wa kuunda vyama vya kijamii na taasisi za kifedha na kutumia nguvu yao ya kiuchumi kuimarisha jamii zao kwa namna mbalimbali kuanzia kiuchumi, kijamii, kitamaduni n.k,.
Kwa Wayahudi swala la kujitolea kwa ajili ya jamii ni jambo takatifu kabisa lililopo katika vitabu vyao vyao vya kidini.
Katika kitabu cha dini ya kiyahudi cha Talmud kuna andiko linasema, “una utajiri mkubwa kadiri ya kiasi unachoweza kutoa”. Wayahudi wanaamini kwamba jamii ambayo inajisaidia yenyewe ndio jamii inayoweza kudhibiti hatma yake, au kujiamulia mambo yake kwa namna ambayo italinda maslahi ya jamii husika kwa kizazi cha sasa na cha baadaye na kwamba kama jamii inategemea misaada kutoka jamii nyingine basi itakuwa inaishi matakwa ya wale ambao wanaipa misaada.
Kwa wastani wayahudi wanajitolea kwenye taasisi za kijamii mara mbili zaidi ya wamarekani wa kawaida.
Taasisi na vyama vya kijamii vya wayahudi vimewasaidia sana wayahudi, kwa mfano miaka ya mwanzoni ya karne ya 20 waliwekewa vikwazo na masharti mengi katika kujiunga na elimu ya juu na hivyo kupitia taasisi zao za kijamii za kifedha waliweza kujenga vyuo vyao ambavyo walisoma kwa wingi na kufikia miaka ya 1930’s tayari walikuwa wengi sana katika taaluma husika. Wayahudi wanatoa michango mikubwa sana katika taasisi za kitaaluma kama vile vyuo vikuu, maktaba kubwa, mahospitali makubwa, makumbusho pamoja na taasisi nyingine za kitaaluma na kijamii.
Wayahudi wa ndani ya Marekani wana jukumu kubwa ambalo wanalitekeleza kwa usahihi sana la kuisaidia nchi yao ya asili ya Israel kwa namna nyingi tofauti tofuati.
Wayahudi pia wamekuwa wakichangia na kushiriki harakati nyingi za kupigania haki mbalimbali ndani ya Marekani, ikiwa hata wao wenyewe ni wahanga wa manyanyaso mengi katika historia. Wayahudi wanaamini kwamba kujitolea na kuchangia harakati za kutetea haki ni jukumu la lazima la kijamii. Hata neno sadaka limetokana na neno la kiyahudi(tzedakah) linalomaanisha haki au kutenda haki. Hivyo kutoa kwao michango ya kusaidia harakati za kupigania haki mbalimbali wanaamini ni jukumu lao la kijamii.
MIKOPO HURU NDANI YA JAMII ZA KIYAHUDI.
Wayahudi wana taasisi zaidi ya 50 ndani ya Marekani ambazo zinatoa mikopo bila riba wala dhamana kwa wayahudi ambao wako duni kiuchumi na wanahitaji kukua.
Wayahudi wanaamini katika maandiko kwenye agano la kale katika kitabu cha Kutoka 22;25 yanayosema “Ukimkopesha fedha mtu yeyote miongoni mwa watu wangu walio maskini, usiwe kwake kama mdai, wala usimtoze riba”.
Hivyo wayahudi wameanzisha taasisi hizi ambapo wanawasaidia wayahudi maskini ambao hawana dhamana wala historia ya kifedha inayoweza kuwasaidia kupata mikopo benki na wanatoa kiasi chochote ambacho hata benki hawawezi kujihangaisha kutoa. Wayahudi wengi wanaoanza maisha wanatumia sana fursa zinazotolewa na hizi taasisi kupiga hatua kiuchumi.
WANAINUANA KWA KUNUNUA ZAIDI KUTOKA KWENYE BIASHARA ZAO WENYEWE.
Ni njia gani bora zaidi mtu unaweza kuitumia kuisaidia jamii yako ili watu wenu waimarike kiuchumi na kuwa na uwezo wa kujitegemea?. Hili unaweza kulidharau lakini lina nguvu kubwa sana, wayahudi ili kukua wanaungishana sana biashara kuanzia makampuni makubwa ya taaluma mbalimbali mpaka biashara ndogo kabisa.
JUMUIYA YA TAASISI ZA KIYAHUDI NA FOUNDATIONS
Wayahudi wameanzisha mifuko mbalimbali ya kijamii(foundations) ambazo zinalenga kuimarisha na kuboresha mambo mbalimbali ndani ya jamii ya wayahudi.
Mifuko hii ambayo inatoa zaidi U.S $ 3 billions kwa mwaka kuimarisha na kukuza tamaduni za wayahudi kama vile kutunza utambulisho wa wayahudi, kutangaza utalii wa Israel, kuhimiza watoto wa kiyahudi kujifunza utamaduni wa kiyahudi na kugharamia safari za mara kwa mara za kwenda Israel kwa safari za kitamaduni kwa vijana wadogo wenye uhitaji n.k.
Wayahudi wamekuwa wakifanya “lobbying” katika siasa za Marekani ambayo ni namna fulani ya kushawishi wanasiasa kutoa kipaumbele kwa sera ambazo zina mchango chanya kwenye mambo yao kwa kutumia njia mbalimbali.
Wayahudi wamekuwa pia wakifanya lobbying pia kwa serikali kuu ya Marekani “Federal Government” kwa niaba ya nchi ya Israel ambayo ni nchi yao ya asili.
Rais wa 33 wa Marekani Harry S. Truman ndiye Rais aliyeitambua nchi ya Israel wakati inaanzishwa mwaka 1948 lakini ni baada ya Wayahudi kujiweka karibu na wanasiasa wenye nguvu Marekani na kufanya lobbying kiasi cha kuisaidia Israel kutambulika licha ya kwamba kumekuwepo migongano ya kimaslahi na mivutano mingi juu ya swala hilo.
Kutokana na lobbying nyingi za wayahudi wa ndani ya Marekani kumekuwepo na misaada mingi ya kifedha na kijeshi kutoka Marekani kwenda Israel.
Kadiri wayahudi wanavyozidi kujitahidi kusukuma agenda zaidi katika maamuzi ya kisiasa ndani ya Marekani ndivyo misaada zaidi kutoka Marekani inavyozidi kupelekwa Israel.
Takwimu zinaonyesha kwamba kwa sasa Israel inapokea 20% ya misaada inayotoka Marekani licha ya kuwa na idadi ndogo sana ya watu, japo hata hivyo na Marekani yenyewe ina maslahi makubwa ndani ya Israel kwani inategemea kuitumia Israel pia katika kudhibiti eneo la mashariki ya kati, hivyo ni kwa maslahi ya wote wawili.
Wayahudi ndani ya Marekani wamekuwa wakishiriki kwa uhakika sana katika siasa za ndani ya Marekani kwa njia mbalimbali hasa katika kuchangia fedha za kampeni na hata kupiga kura ili kumpigania mgombea atakayeweza kujali maslahi yao akishachukua ofisi ya umma.
Wayahudi wenyewe pia wamekuwa wakigombea katika nafasi nyingi za kisiasa katika maeneo mbalimbali na hilo limewaongezea nguvu sana ndani ya siasa za Marekani.
MAMBO AMBAYO SISI KAMA WACHAGGA TUNAWEZA KUJIFUNZA NINI KUTOKA KWA WAYAHUDI
-Kujenga na kuimarisha misingi imara na mitaji ya jamii yetu kiuchumi, kielimu/kitaaluma na hata kiimani, hili linasaidia sana katika kuongeza kujiamini na kupiga sana hatua kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja.
-Kujenga na kuimarisha misingi kwa kuanzisha mifuko ya kijamii kwa malengo ya muda mrefu ya jamii yetu katika nyanja mbalimbali.
-Tusitegemee sana serikali au taasisi nyingine za kitaifa au kimataifa kutusaidia kwani mara nyingi misaada ya hivyo ni kwa maslahi ya anayesaidia na sio kwa maslahi binafsi ya jamii yetu badala yake sisi wenyewe ndio tuzijenge taasisi zetu kwa fedha zetu wenyewe bila kujali kuna changamoto kiasi gani kwani cha msingi ni kuendelea kusonga mbele hata kama sio kwa kasi kubwa.
-Kushiriki kwenye siasa bila kujiweka sana upande fulani badala yake kuwa tayari kumuunga mkono na kufanya kazi na mwanasiasa yeyote atakayefanikiwa kuchukua ofisi huku tukisukuma mbele maslahi yetu kama jamii.
-Kuungishana zaidi biashara za wenyewe kwa wenyewe, hii ni njia bora sana ya kupeleka utajiri nyumbani na ni kwa maslahi mapana ya maendeleo ya nyumbani kwa ujumla.
-Kuunga mkono harakati za kitaifa ambazo zina maslahi pia kwa jamii yetu kwa kuzitangaza na hata kuzichangia fedha.
Ahsanteni
Tutaendelea na Siri Ya 3 Kwenye Makala Inayofuata.
Urithi Wetu Wachagga
urithiwetuwachagga@gmail.com