#THE JEWISH PHENOMENON#
“SEHEMU YA 10”
#Siri 7 Zilizowasaidia Wayahudi Kuwa na Mafanikio Makubwa#
#SHEREHEKEA UPEKEE NA HIMIZA UBINIFU#
Mwandishi Steven Silbiger anasema kwamba kwa vile dini ya kiyahudi inahimiza historia yake na maandiko ya kidini ya kiyahudi basi watu wengi wanafikiri kwamba wayahudi ni watu wenye utamaduni wa kihafidhina(conservatives) ambapo hawasisitizi sana upekee wa mtu wala ubunifu, mwandishi anasisitiza badala yake sifa hizi za upekee(individuality) na ubunifu(creativity) ndizo sifa za msingi kabisa kwa myahudi.
-Mwandishi Steven Silbiger anasema mwanzo kabisa wa wayahudi kuwa na sifa ya upekee(individuality) na ubunifu(creativity) ulianza kwa baba wa taifa la wayahudi Ibrahimu.
-Mwandishi anasema Ibrahimu alisimama kinyume na mila na tamaduni za wazazi wake na jamii yake za kuabudu sanamu na badala yake akaazimia rasmi kwamba kuna Mungu mmoja anayestahili kuabudiwa wakati ambao kila mtu katika familia na jamii yake alikuwa anaomba na kuabudu sanamu.
-Baba yake Ibrahimu aliyeitwa Terah alikuwa na duka la kuuuza sanamu ambazo watu walinunua na kuziabudu, lakini Ibrahim hakutaka kuamini kwamba sanamu hizo zina nguvu yoyote ya kimungu hivyo alizivunjavunja na kuziharibu. Kuanzia hapo Ibrahimu alisimama na msimamo wa peke yake wa kumwabudu wa Ibrahim na kuwa myahudi wa kwanza.
Ndio huyu huyu Mungu wa Ibrahimu ambaye Ibrahimu alimtambua rasmi, na Ibrahimu kuwa kiyahudi wa kwanza ambaye baadaye mpaka miaka 4,000 leo hii anaendelea kuabudiwa na wakristo, waislamu na hata wayahudi wenyewe.
-Inasemekana kwamba baba yake Ibrahimu aliyeitwa Terah alimpeleka Ibrahimu mbele ya mahakama za kijamii aeleze kwa nini anadharau miungu ya kwao, Ibrahimu aliposimama mahakamani alisema kwamba kama kweli hiyo miungu ya kwao ina nguvu basi isimamishe jua kesho yake lisiamke naye ataacha kuidharau miungu hiyo na kuanza kuibudu. Na huo ndio ukawa mwanzo wa wayahudi kuhoji mamlaka zilizoko juu yao mpaka leo hii.
-Upekee wa wayahudi hauishii hapo, biblia yenyewe inasema kwamba katika kumbukumbu la torati 7:7, “Bwana hawakuwapenda nyinyi wala kuwachagua nyinyi kwa sababu mlikuwa wengi kuliko mataifa yote, maana mlikuwa wachache kuliko watu wote”. Hapa biblia inawatambua wayahudi kwamba wao wamechaguliwa, kwamba ni wateule, yaani wao ni watu wa kipekee. Biblia inawatambua wayahudi kama watu wa kipekee wateule wa Mungu katikati ya mataifa mengine mengi.
-Wayahudi wameendelea kuwa ni watu wa kipekee na mara nyingi wasiotegemea ushawishi wa mtu mmoja au taasisi kufanya mambo yao bali wamekuwa watu wa kuchagua njia yao ya kipekee ya kuiendea kwa mtu mmoja mmoja na hata wayahudi kama jamii nzima.
-Watoto wa kiyahudi katika makongamano mbalimbali wamekuwa wakitakiwa kuonyesha uwezo kwa kuongea mbele za watu kuuliza maswali kujibiwa na hata kuulizwa maswali na kuyajibu.
-Wamama wa kiyahudi wamekuwa wakiwajengea watoto wao hali ya kujivuna na kujivunia ambayo imewaongezea kujiamini sana kuanzia darasani mpaka kwenye maisha ya kazi na taaluma wanazozifanya. -Upekee na ubunifu umewafanya wayahudi kuwa waanzilishi wa vitu vingi duniani na watu wa mwanzo wenye mafanikio kwa wingi katika taaluma na fani mbalimbali duniani.
#MAMBO AMBAYO WACHAGGA TUNAWEZA KUJIFUNZA KUTOKA KWA WAYAHUDI#
1. Kuwapa watoto uhuru wa kutosha kuwa wabunifu badala ya kuwalea kwa ukali na kutumia udikteta kuwakataza kila kitu, lakini hapo hapo kuwalinda sana na kuwaepusha na kujichanganya na watu wa mitaani ambao wana tabia tofauti zisizoeleweka na mara nyingi huwa mbaya.
2. Badala ya kuwaachia watoto kwenda kuzagaa mitaani na kupata ushawishi wa kila mtu na kujifunza utamaduni wa hovyo ni bora kuwaweka karibu yako waone na kuiga unavyofanya kazi kwa bidii, kuwasisitiza kuweka bidii katika elimu na kujenga matamanio ya kuwa na mafanikio ya kitaaluma na kifedha, pamoja na kuwajengea tabia ya kupenda kusoma vitabu na kujifunza vitu mbalimbali.
3. Kumpa mtoto zawadi na kumsifia pale anapojaribu kuja na ubunifu mpya hata kama utafeli, kwani kufeli ndio njia ya kuelekea mafanikio. Hii hali ya kupenda kuwa mbunifu ikiendelezwa inamjengea kujiamini na kufanya ubunifu katika mambo makubwa zaidi mbeleni.
4. Sisi wachagga wenyewe tunahitaji kujisomea na kujifunza mambo mengi sana, na hata kutafuta vyanzo vya vitu na historia mbalimbali ili tuache kutegemea watu wengine kutuongoza na kutuamulia mambo ambao hata uwezo wao ni mdogo lakini kwa kutumia hila za kisiasa na kidini wanatuteka na tunakuwa watumwa wao kupitia ushawishi mkubwa waliojenga kwetu, hususan manabii wengi wa siku hizi ambao kwa sehemu kubwa ni matapeli tu, wanaotumia udhaifu wetu wa kiimani. Wayahudi hawategemei mtu yeyote kuwaamulia au kuwatabiria jambo bali wanajifunza kila kitu kwa kina na kuamua hatma yao. Hata katika taasisi zao wenyewe mbalimbali za kiyahudi hawategemei sana mtu fulani aongeee ndio wafuate kwa sababu kila mtu ana uwezo mkubwa wa kujiamulia mambo yake yote iwe ni ya kiroho au kimwili, na kila mtu ana upekee wake.
5. Kujenga mazingira ya kibunifu nyumbani kama vile kuwa na maktaba ndogo, kuwa na maabara au karakana ya kutengeneza vitu, kuweka vitabu vya kila aina hasa vya kihistoria na kisayansi na kujenga utamaduni wa wanafamilia kusoma na kujifunza vitu mbalimbali mapema katika maisha badala ya kukaa bure kusubiri kupata ushawishi kutoka kwa watu wa nje ambao wengi wana malengo yao binafsi.
6. Kuepuka maneno ya kukatisha tamaa au sheria na kanuni potofu zinazoaminiwa na wengi lakini hazina ukweli wala uhalisia. Kwa mfano kumwambia mtu au mtoto asijaribu jambo fulani kwa sababu haliwezekani, au maneno kama “hilo tulishajaribu limeshindikana”, “fanya kitu kinachowezekana”, “hilo halikuhusu”. Haya ni maneno yanayokatisha tamaa na kuua ubunifu kwa watu.
7. Kosoa na kujaribu kuhoji sana imani nyingi potofu au hofu na woga wa watu katika vitu ambavyo havistahili kuogopwa. 8. Boresha mawazo ambayo watu walibuni na kuyafanyia kazi lakini yanaonekana kama yamepitwa na wakati au hayauzi sana na kuyafanya kwa namna tofauti na iliyo bora zaidi yawe na manufaa zaidi kwa watu na kujipatia mafanikio.
Ahsanteni.
Tutamalizia Siri Ya 7 na Ya Mwisho Kwenye Makala Inayofuata.
Urithi Wetu Wachagga
urithiwetuwachagga@gmail.com