HADITHI ZA DINI YA ASILI YA WACHAGGA KABLA YA KUJA KWA WAMISIONARI WA KIKRISTO. – 1

Kama tunavyofahamu kila dini duniani ina hadithi zake za mambo ambayo yanaaminika kwamba yalitokea zamani ambazo ndizo zinajenga misingi ya dini husika.

Kwa upande wa dini ya kikristo kuna hadithi za mambo yaliyotokea zamani ndani ya jamii ya Wayahudi au Waisrael ambazo zinahusianishwa na Mungu wa wakristo moja kwa moja. Hadithi zilizoanzia kwenye jamii ya Wayahudi au Waisrael na kuwa muendelezo katika dini ya kikristo ilipoanza ndizo zimejenga misingi ya imani ya kikrsito ya leo.

Hadithi hizi ni kama vile hadithi ya Adam na Hawa katika bustani ya Edeni, hadithi ya Kaini na Habili, Hadithi ya gharika ya Nuhu, hadithi ya Wana wa Israeli utumwani Misri pamoja na nyingine nyingi zilizokuja baadaye. Hadithi nyingine zikiwa zinaingiliana moja kwa moja na historia ya Wayahudi miaka ya baadaye zaidi.

Hivyo dini ya zamani ya wachagga nayo ilikuwa na hadithi zake nyingi za namna hiyo. Lakini jambo la ajabu ni kwamba hadithi hizi za wachagga zinakaribia sana kufanana na hadithi hizi za jamii ya Wayahudi za kwenye biblia. Msingi wa hadithi za dini ya wachagga zamani kupitia Mungu wa wachagga (Ruwa) ni mmoja na hadithi hizi za dini ya Wayahudi/Waisrael japo kuna utofauti mdogo wa masimalizi. Jambo hili lilimshangaza pia Alexander Le Roy katika namna ya utoaji sadaka wa Wachagga ulivyokuwa unafanana na utoaji sadaka wa wayahudi na wakristo wakati alipofanyiwa tambiko takatifu Kilema akichanjia damu ya undugu na Mangi Fumba wa Kilema mwaka 1890.

Pengine hii ndio sababu ya msingi ya baadhi ya watu kujaribu kuja na nadharia kwamba kuna uhusiano kati ya wachagga na Wayahudi/Waisrael au wachagga wametokana na kizazi cha Wayahudi/Waisrael. Hata hivyo hadithi hizi zinasemekana pia kupatikana kwenye baadhi ya jamii nyingine lakini nyingi zikiwa zimepotea na kusahaulika.

Msingi wa hadithi hizi za wachagga kukaribiana sana na hadithi za kwenye biblia hususan katika kitabu cha Agano la Kale uliweza kuwarahisishia sana kazi wamisionari wa kikristo walipofika Uchaggani katika kusambaza injili ya Yesu Kristo kwa wachagga tangu mwishoni mwa karne ya 19. Hii ni kwa sababu waliweza kuhusianisha mambo mengi ya kikristo na hadithi ambazo zilikuwa zimezoeleka kwa wachagga.

MUNGU WA WACHAGGA.

Wachagga kama ilivyokuwa kwa Wayahudi ni moja kati ya jamii chache ambazo zilikuwa zinaamini katika Mungu mmoja(Monotheism). Hii ilikuwa ni tofauti na jamii nyingine nyingi za kale zilizokuwa zinaamini katika miungu wengi(Polytheism). Kwa mfano jamii kama Wayunani au Warumi walikuwa wanaamini kuna Mungu wa kila kitu kama vile mvua, mapenzi, utajiri, muziki n.k,. Ukiachana na Mungu wao mkuu aliyekuwa anaitwa Jupita walikuwa wanaamini pia kwamba kuna miungu mingine tena ya jinsia tofauti tofuati kama vile Mungu wa kike Juno ambaye ni mke wa Jupita, Mungu wa kike Vesta ambaye ni dada yake na Jupita, Mungu Diana, Mungu Apollo n.k.,

Wachagga wao walikuwa wanaamini katika Mungu mmoja tu(Monotheists) kama ilivyokuwa kwa Wayahudi na hata Wakristo na Waislaimu wa leo. Au tunaweza kusema kama ilivyo kwa dini zilizotokana na imani ya Ibrahimu.

Jina la Mungu wa Wachagga ni “Ruwa/Iruwa”, ambalo pia ni jina la Jua kwa Wachagga. Hata hivyo wachagga hawamaanishi moja kwa moja kwamba Jua ndio Mungu kwa sababu kuna hadithi nyingine za Wachagga za mtu kwenda kwa Mungu moja kwa moja baada ya kuvuka anga na kuingia huko juu kabisa ya mawingu na sio kulielekea jua.

Wachagga kabla ya kuja dini za kikristo na kiislamu waliamini kwamba Mungu wao(Ruwa) japo haingilii sana mambo ya wachagga lakini ndiye Mkuu wa kila kitu na mwenye nguvu kuliko chochote kile. Wachagga waliamini kwamba Ruwa ndio mwanzo na mwisho na ndiye mwamuzi wa mwisho wa kila kitu.

Wachagga kabla ya kuja kwa dini za ukristo na usilamu waliamini kwamba Ruwa/Iruwa ni mwenye huruma sana na matendo yake mengi yameelezea kwenye hadithi za kale za Wachagga kama tutakavyoona mbeleni. Wachagga waliamini kwamba yote yanayoendelea duniani yameruhusiwa na Ruwa/Iruwa mwenyewe kama jinsi yalivyoelezewa kwenye hadithi mbalimbali za wachagga za zamani.

Wachagga waliamini kwamba Ruwa/Iruwa kwa miaka mingi alishaacha kujihusisha na mambo yao wala kujali sana kuhusu wao lakini wakati yalipotokea majanga makubwa sana katika jamii, wachagga walimtolea sadaka maalum Ruwa/Iruwa ambayo ilikuwa inaandaliwa rasmi kwa ajiliya Ruwa ili awaepushie na majanga hayo.

Wachagga hawakuwa wanaamini kwamba Ruwa/Iruwa ndiye aliumba Ulimwengu bali waliaamini kwamba Ulimwengu ulikuwepo siku zote, lakini wakati mwingine waliamini kwamba nyota ni watoto wa Ruwa.Katika dini ya wachagga pia hawakuamini kwamba Ruwa/Iruwa ndiye aliyeumba binadamu bali waliamini kwamba Ruwa ndiye aliwaweka huru binadamu kwa kuwapasua kutoka kwenye eneo walilokuwepo na hivyo wakaweza kuendelea na mambo yao kwa uhuru. Hapa wachagga walimwita Mungu wao kwa jina la “Ruwa/Iruwa mopara wandu”.

HADITHI YA ANGUKO LA KWANZA LA BINADAMU KATIKA DINI YA WACHAGGA.

Hadithi hizi zilikuwa zinasimuliwa na wazee wa kichagga kabla ya ukristo kuingia Uchaggani mwishoni mwa karne ya 19 mpaka mwanzoni mwa karne ya 20 na zilirekodiwa na waandishi mbalimbali. Hapa tunaenda kuona hadithi zilisimuliwa na wazee wa kichagga na kurekodiwa na Sir Charles Dundas.Baada ya “Ruwa/Iruwa” kuwaweka huru binadamu kutoka kwenye eneo walilokuwepo na kuweza kuendelea na mambo mengine kwa kupasua na kuwaweka huru(Ruwa mopara wandu), aliweza kuwasaidia namna wataweza kuanza kuishi.

Ruwa aliwapa wachagga vihamba(mashamba) kwa ajili ya kulima na kujipatia vyakula na katika shamba la kiongozi wao mkuu alipanda aina nyingi mbalimbali za viazi. Kisha katikati ya shamba hili la kiongozi wao mkuu akapanda aina ya kiazi kilichoitwa Ula au Ukaho, ambacho kilipandwa karibu na miti mikubwa na miti ya zabibu inayotambaa.

Ruwa akampa maelezo kiongozi wao mkuu kwamba, “Nimewapa mashamba haya na mtakula mavuno yote yalioko shambani, mtakula kila aina ya ndizi na viazi vilivyopo shambani huko. Lakini viazi hivyo aina ya Ula au Ukaho hamruhusiwi kabisa kula”, Ruwa akamwamba, “Wewe wala watu wako msijaribu kabisa kula kiazi hicho, na ikiwa kuna ambaye atathubutu kula mifupa yake itavunjika vunjika na mwishoni atakufa”.Kisha Ruwa/Iruwa akaondoka zake.

Wachagga walitii amri hiyo ya Ruwa na kila siku Ruwa/Iruwa alikuwa akiwatembelea asubuhi na jioni kuwasalimia na kuwajulia hali.Lakini siku moja alikuja mtu mmoja kutokea mbali asiye mchagga akamsalimia kiongozi mkuu wa wachagga na kuomba apatiwe chakula. Kiongozi mkuu wa wachagga akamruhsu mtu huyo kuingia kwenye shambani na kuchuma kila aina ya ndizi na viazi lakini isipokuwa kiazi aina ya Ula/Ukaho ambacho kiongozi wa wachagga alimwambia kwamba “Ruwa” mwenyewe ndiye alipiga marufuku kisiliwe.

Lakini mgeni huyu alimwambia kiongozi mkuu wa wachagga kwamba leo asubuhi Ruwa ameniambia nije kwako unipe sufuria ili nipike kiazi hiki aina ya Ula/Ukaho tuweze kula pamoja na wewe na watu wako kisha tusherehekee na kufurahi.

Kiongozi mkuu wa wachagga aliposikia kwamba Ruwa mwenyewe ndiye ametoa ruhusu hiyo alimpatia sufuria mgeni huyu. Mgeni huyu alichimba kiazi kile kilichokatazwa na “Ruwa” ma kisha kukipika kwenye sufuria kikaiva na kisha watu wote wakaanza kula.

Wakati wanakula msaidizi wa Ruwa alihisi harufu ya chakula kwamba ni harufu ya kiazi kile cha Ula. Msaidizi huyu wa Ruwa/Iruwa aliwakimbilia mara moja na kuwauliza, “mnafanya nini?”, “mnakula nini?”. Mgeni huyu pamoja na kiongozi mkuu wa wachagga wakapigwa na butwaa na kuogopa sana na wakawa hawana cha kujibu. Kisha msaidizi huyo wa Ruwa akachukua sufuria ile ya chakula na kisha kupeleka kwenda kumwonyesha Ruwa/Iruwa.

Ruwa/Iruwa alipoona kwamba wamekiuka maagizo yake alikasirika sana na kisha kumtuma waziri wake kwa mara ya pili kwa kiongozi mkuu wa wachagga na watu wake. Msaidizi wa Ruwa akawaambia, “Kwa kuwa mmekubali kudanganywa na huyo mgeni na kula kiazi changu cha Ula, basi nitavunja vunja mifupa yenu, kupasua macho yenu na mwishowe mtakufa, kisha msaidizi huyo akarudi kwa Ruwa/Iruwa.

Kuanzia siku ile wachagga hawakumuona tena Ruwa, na Ruwa hakuwatumia tena salamu yoyote wala kuwapelekea neno lolote. Kisha kuanzia wakati huo watu walianza kuwa wanadhoofika miili, mifupa kuvunjika, macho kufunga na mwishowe kufariki.

Ahsanteni.

Hadithi hii itaendelea kesho.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *