HADITHI ZA DINI YA ASILI YA WACHAGGA KABLA YA KUJA KWA WAMISIONARI WA KIKRISTO – 4

DUNIA KUANGAMIZWA KWA MARA YA PILI.

Baada ya Mkechuwa kufariki watoto wake na kizazi chake kwa ujumla kiliongezeka sana na walitajirika sana pia. Hii ilichangiwa pia na mifugo yao kupata majani mengi kwa sababu dunia bado ilikuwa haijawa na watu wengi sana.

Watu matajiri walianza tena kujivuna sana na mali zao pamoja na vyakula tele vilivyokuwepo kwao. Walipokutana na mtu maskini hawakutaka kumsalimia wala kuitikia salamu yake na ilipotokea kwamba mtu maskini au mtu mwenye uhitaji alipotaka msaada kutoka kwao walimjibu; “Tulipokuwa tunafanya kazi na kubarikiwa mali na vyakula, wewe ulikuwa wapi?” na kisha walimfukuza.

Pia walipokutana na mtu maskini ameanguka barabarani na hajiwezi badala ya kumsaidia walisema; “Ulikuwa unalewa wapi mpaka unakuja kuanguka barabarani hovyo katika nyakati hizi?” Maskini huyo alijibu; “Bwana hatujala chochote mpaka sasa, wala kunywa chochote tangu jana mpaka sasa”. Watu hao matajiri waliondoka zao huku wakicheka sana bila aibu.

Ruwa alipoona haya yakitokea alikasirishwa sana tena kwa mara nyingine na matendo ya watu wake na kusema: “Nitawapa funzo jingine kwa mara nyingine”. Hivyo alimwita waziri wake na kuongea naye. Ruwa alimwagiza waziri wake, “Nenda kwa watu wa duniani na utokee kama mtu mwenye majipu mwili mzima na anayejikuna majipu yake mwili mzima”.

Ruwa akaendelea kumwambia waziri wake, “Kisha utaingia kwenye nyumba za watu na uanze kuomba msaada na kuhitaji huruma zao. Watu watakapokuona katika hali hiyo watakuonea huruma. Na kama utaingia nyumbani kwa mtu ukaomba msaada wa chakula akakukatalia nitamgeuza kuwa tembo. Na kama mtu yeyote atakunyanyasa na kukukandamiza na kukunyima chakula kwa sababu ya uchoyo na tamaa zake, nitamgeuza na yeye pia kuwa tembo. Na kwa mtu yeyote atakayekuonea huruma, ambaye atakupokea na kukupa chakula, huyo nitamwongoza na kumsaidia katika mapito yake yote. Pia nitambariki kuwa na watoto wengi na mali nyingi pia. Sasa nenda na ufanye yote nilikuagiza.”

Basi waziri huyu wa Ruwa akatokezea duniani akiwa ni mwenye majipu mwili mzima, huku akiteseka sana kwa kujikuna majipu yake. Pia alikuwa ni mtu aliyedhoofika sana akiwa amekonda mpaka anashangaza.

Kwanza alifika nyumbani kwa mtu tajiri na walipomuona mara moja walianza kumsumbua na kumnyanyasa. Aliomba chakula pamoja na siagi kwa ajili ya kupaka mwili wake. Familia hii ya matajiri walimjibu kwa kumwambia, “Mbona umekosa aibu kiasi hicho? Hivi unajiona wewe na hayo majipu yako mwili mzima unaweza kukaa na sisi matajiri tukala pamoja? Na mafuta yaliyotokana na mifugo yetu tukupe wewe upake kwenye hivyo vidonda vyako?”. Kisha walimfukuza kwa mawe. Kisha wakamtungia jina “Kingusai” ikimaanisha mtu anayejikuna.

Aliendelea kuzunguka kwa watu wote matajiri akiomba msaada wa chakula na mafuta/siagi. Kila alipokwenda kuomba msaada walimnyanyasa na kumkejeli wakiendelea kumwita Kingusai na kumfukuza. Na hivyo ndivyo Kingusai alivyoendelea kwenda.

Mwishowe alifanikiwa kukutana na mtu mwenye huruma ambapo aliingia nyumbani kwake na kuomba chakula na mafuta/siagi. Mtu huyo alishangazwa sana kwamba mtu huyu anakaribia kufa kwa njaa na majipu. Machozi yalimtiririka machoni kwake, kisha akaingia ndani na kutandika chini na kumkaribisha ndani akisema: “Karibu ndani ili upate kukaa na kula chakula.”Kingusai alijaribu kukataa lakini mtu huyo alimhimiza na kumlazimisha na hivyo Kingusai akaingia ndani. Aliweza kukaa na mwenyeji wake huyo alimletea kiburu kwenye sahani akanywa, akashiba na kuridhika sana. Baada ya kushiba na kuridhika mwenyeji wake alimletea maji na kumwosha mwili mzima. Kisha akampaka dawa ya majipu pamoja na siagi mwili mzima wenye majipu.

Baada ya kumaliza alimpa mafuta/siagi nyingi na kumwambia, “Chukua hii na kila unapohisi unataka kuumiza mwili wako kwa kujikuna, yatumie kujipaka”. Hivyo Kingusai alipoona matendo mema ya mtu huyu mwenye huruma alimwambia, “Mimi ni waziri wa Ruwa. Ruwa amenituma niweze kueleza watu wote wabaya na wazuri. Kwa sababu ya matendo yako mema, kama katika nchi hii kuna watu wa ukoo wako pamoja na familia na marafiki zako, waite wote ili mje kuishi pamoja kwenye nyumba yako hii.

Waite kuja kuishi hapa pamoja na mali zao, waje kuishi hapa kwa amri yako. Jitahidi ufanye upesi kwa sababu kuna matukio makubwa yanakuja.” Mtu huyo mwenye huruma alisimama na kwenda kukusanya watu wake wote, na watu wote walikuja na ng’ombe zao, mbuzi na kondoo na mali zao zote.Kingusai alipoona kwamba wameshakamilisha kila kitu aliwaambia, “Mtakaposikia kelele kama za maji mengi yanatiririka kwa nguvu na kwa kasi endeleeni kujishika vizuri na nyumba yenu hii. Na mtakaposikia kelele hizo mkae kimya. Kwa sababu Ruwa anawaonyesha watu nguvu zake.”Hivyo siku ya nane Ruwa alitiririsha maji mengi sana kutoka kwenye msitu wa mlima Kilimanjaro kutokea kwenye ukanda wa juu. Maji hayo mengi sana au mafuriko yalisomba watu wote waovu na wengine pamoja na nyumba zao na vyakula vyao sambamba na mali zao zote. Na mtu huyu mwenye huruma aliposikia maji hayo mengi yakiiharibu nchi alifanya kila kitu kama jinsi alivyoagizwa na Kingusai. Na hivyo wote aliokuwa nao waliokolewa.

Maji hayo kwa nguvu kubwa sana yaliyokuwa nayo yaliweza kubeba watu wote pamoja na ng’ombe zao, mbuzi na kondoo mpaka kwenye tambarare za mbali kabisa. Kisha watu hao waliosombwa na maji Ruwa aliwageuza kuwa tembo. Na ng’ombe wao Ruwa akawageuza kuwa nyati, pongo na wanyama wengine wa aina hiyo. Na kondoo wao Ruwa akawageuza kuwa nguruwe na nungunungu. Na mbwa wao Ruwa akawageuza kuwa chui, fisi na aina hizo za wanyama.Hivyo mtu huyu mwenye huruma alipoamka asubuhi akakuta nchi nzima iko tupu. Hakuna kitu kilichokuwa kimesalia. Alishangazwa sana na kuiangalia mbingu na kutema mate mara tatu akilitaja jina la Ruwa, Mungu wa kweli ambaye amepasua watu(Ruwa mopara wandu) na kuwaweka huru.

Hivyo mtu yule mwenye huruma sambamba na watu wake waliishi, wakazaliana na kuongeza sana na kurudi tena kuwa taifa kubwa la watu wengi. Kuanzia wakati huo wazee wa kichagga wamekuwa wakiwasisitiza watoto wao kwa kuwahadithia hadithi hii kwamba, wasimnyanyasa wala kumtaabisha mgeni yeyote wala kumnyima chakula kama walivyofanya wale watu wabaya walioangamizwa.

Ahsanteni.

Kesho tutaendelea kumwelezea Ruwa/Iruwa na ukuu wake kama alivyokuwa anaaminika na wachagga.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *