HADITHI YA “MORILE” KWA WACHAGGA.

Hapo zamani za kale wachagga walifahamu kwamba kulikuwa na Mungu aliyeumba watu ambaye aliishi kwenye juu huko juu mawinguni. Wachagga walijua pia kwamba Mungu huyo amewatendea watu mambo mema mengi sana. Lakini wachagga waliendelea kuliangalia anga la juu na kutamani kufahamu mambo mengi sana kuhusu anga ambalo jua hupita kila siku.

Lakini hawakuweza kupata mtu yeyote wa kuwaambia habari za angani. Walijaribu kuwauliza watabiri wa mambo na waganga ambao walibashiri kwamba, “Jua lenyewe ndiye Ruwa mwenyewe na Ruwa ana mke ambaye ni mwezi. Na watoto wa Ruwa ni nyota za angani.

Lakini hawakuwa na taarifa hii katika akili zao na hivyo waliendelea kudadisi ili kuweza kujua zaidi. Baadaye waliambiwa kulikuwa na mtu mmoja jina lake aliitwa Morile, ambaye aliwahi kupaa kwenda mpaka huko juu mawinguni na kurudi na taarifa za kuhusiana na huko juu mawinguni. Na mtu huyu aliyeita Morile aliwaeleza watu kuhusiana na mwezi, jua na nyota na juu ya yale yaliyokuwa yanafanywa na watu walioishi huko juu mawinguni.

MAISHA YA MORILE NA SAFARI YAKE YA MAWINGUNI.Baba yake Morile alikuwa ni mfinyanzi anayetengeneza vyungu na vyombo vingine vya kupikia kwa ajili ya wachagga. Mama yake Morile alikuwa ni mkulima, hususan ukulima wa mboga mboga na bustani ambapo alikuwa anafanya kazi yake kwa ufanisi wa hali ya juu na mashamba na bustani zako zilikuwa ni zenye kupendeza sana.

Morile alipokuwa mdogo alimsindikiza mama yake kwenda kwenye mashamba ya bustani za visohia(viazi) na kumsaidia mama yake kuchimba viazi. Siku moja Morile alichimba viazi vizuri sana na kumwambia mama yake: “Mama angalia viazi hivi vizuri kama vitoto vya mtu”. Mama yake akamwambia, “Vizuri, vipeleke nyumbani uvipike, ule na kufurahi”. Morile hakufuata ushauri wa mama yake, bali alipuuza maneno yake na kuvipeleka viazi hivyo kwenye pango la mti bila mama yake kujua.

Siku mbili tatu baadaye Morile alienda na mama yake shambani na kwa siri akaenda kuvichungulia vile viazi alivyovipeleka kwenye lile pango la mti. Morile alivikuta viazi vile vikiwa vimekuwa vizuri zaidi kuliko jinsi alivyoviacha mwanzoni. Kisha walirudi nyumbani na mama yake baada ya shughuli za shambani.

Usiku wake huo Morile alitokewa na mtu asiyemjua akamwambia; “Wewe, Morile Ruwa ameona jinsi unapenda vile viazi vyako na jinsi unatamani kama vingekuwa ni watoto. Hivyo Ruwa ameamua kuvibadilisha kuwa watoto. Kwa hiyo kesho asubuhi uchukue vyakula vya watoto na uende kuviangalia.”

Kesho yake Morile aliamka asubuhi sana na kuchukua chakula alichokuwa amepewa na mama yake na kwenda nacho kwenye pango la mti. Morile alichungulia ndani yake na lo! akakuta mtoto analia njaa. Morile alifurahi sana, akatazama angani na kutema mate mara tatu alipokuwa anamshukuru Ruwa. Morile alirudi nyumbani lakini hakusema chochote juu ya yale yaliyotokea ndani ya lile pango la mti.

Siku iliyofuata pia aliendelea kufanya hivyo, alichukua chakula na kupeleka kwenda kumlisha mtoto yule wa kwenye pango. Baada ya hapo alirudi nyumbani lakini hakusema chochote juu ya viazi vile vizuri kubadilika na kuwa mtoto. Morile alifanya hivyo kila siku na chakula alichopeleka ni sehemu ya chakula chake ambacho alikuwa akigawa kile alichopewa na mama yake. Hivyo chakula chake kilipungua na Morile alianza kudhoofika(kukonda) kwa sababu ya kula kugawa chakula chake.

Morile alikiita kitoto kile kwa jina la “Kana” na alipofika katika mti huo alimwimbia mtoto huyo wimbo huu;”Kimana Kii Mbakonyi,(Mtoto aliyepo ndani ya pango la mti)Mbako ya mra, mbako ya mri,(Pango la mti, mti wa kweli)Kiwuke pfo, Kiche na Kunu,(Kitoke huko, kije kunifuata hapa)”.

Baada ya Morile kuimba hivyo mtoto huyo alitoka nje kisha Morile alimpa chakula na baada ya kushiba akarudi kwenye hilo pango la mti. Mama yake Morile alipoona kwamba Morile amedhoofika sana kiafya alihuzunika sana na kumuuliza; “Mwanangu Morile, mbona umekonda sana?”. Morile akamjibu, “Kila siku usiku huwa napigwa sana na homa”. Lakini mama yake hakuridhika na jibu hilo na hakuamini maneno ya Morile.

Siku iliyofuata mama yake alipompa chakula alijaribu kumfuatilia na kuona kwamba Morile amekula kidogo sana kisha akachukua kile chote kilichobaki na kuondoka. Mama yake alimfuata nyuma kwa siri na kumuona akielekea shambani na kwenda mpaka kwenye mti ule wenye pango. Mama yake aliona yote ambayo Morile amefanya na yule mtoto aliyetokea kwenye pango la mti na jinsi Morile alivyoanza kurudi nyumbani.

Mama yake alijificha ili Morile asimwone kwa sababu alijua angekasirika kwa kuwa amefanya hiyo ni siri kwake. Mama yake Morile alirudi na nyumbani na kumwelezea habari zote mume wake na kumwambia jinsi hilo limepelekea Morile kudhoofika sana kiafya. Hivyo wakakubaliana nini wafanye ili mtoto wao Morile asiendelee kukonda zaidi.

Baba na mama yake Morile walikubalina kwamba waende wakakichukue kile kitoto, hivyo walikwenda kwenye lile pango la mti na kukichukua kitoto hicho. Walipofika kwenye pango mama yake Morile aliimba ule wimbo ambao alimsikia Morile akiimba na kitoto kile kilipotoka nje alikichukua na kukipeleka nyumbani kwao na kukificha ndani ya nyumba yao.

Kesho yake Morile alielekea tena kwenye pango hilo la mti kama kawaida yake lakini baada ya kuimba wimbo wake ule hakuweza kusikia sauti yoyote. Kisha aliingia kwenye pango kutafuta yule mtoto lakini hakuona chochote. Morile alilia sana, alilia kwa nguvu na kwa uchungu sana na kurudi nyumbani huku machozi mengi yakiwa yanamtiririka. Morile hakusema chochote zaidi ya kulia tu.

Morile alipewa chakula na mama yake lakini aligoma kabisa kula. Mama yake alimuuliza; “Mwanangu Morile mbona unalia sana?”, Morile alimjibu akamwambia; “moshi umeniingia machoni na kuniumiza”. Mama yake akamwambia; “Kama hiyo ndio sababu basi kaa mbali na moshi, nenda kakae kule karibu na zizi la ng’ombe ambapo hakuna moshi”.

Morile alifanya hivyo lakini hakuacha kububujikwa na machozi. Morile aliendelea kububujikwa na machozi mengi bila kikomo. Mama yake akamuuliza tena; “Mwanangu Morile, mbona bado unalia sana?” Morile akamjibu; “moshi umeendelea kuniwasha zaidi machoni”. Mama yake akamwambia; “Kama ni hivyo kaa mbali zaidi ya moshi ndani ya chumba cha maziwa” Lakini Morile hakuacha kuendelea kulia zaidi na zaidi.

Mama yake aliendelea kumhamishia kwenye vyumba vyote ndani ya nyumba lakini Morile aliendelea kutokwa na machozi mengi zaidi na zaidi. Mama yake alishangaa na mwishowe akamwambia; “Kama tatizo ni hilo mwanangu basi toka kabisa nje ukakae kwenye kiti kilichopo pale nje kilichotengenezwa na baba yako.

Morile alitoka nje na kwenda kukaa kwenye kiti hicho kilichotengenezwa na baba yake. Mara ghafla baada ya Morile kukalia kiti kile, kilianza kurefuka taratibu na kukua mpaka kumfikisha Morile juu mawinguni. Morile alivyokuwa anaendelea kupaishwa juu zaidi mawinguni aliimba wimbo huu.

“Morile Ngarho, Ngarho na wulu,

(Morile napanda, napanda juu)

Morile Ngarho, Ngarho ringo,

(Morile napanda, napanda mawinguni).”

Mama yake Morile aliposikia maneno hayo ya Morile alitoka nje haraka akiwa amemshika yule mtoto “Kana” aliyekuwa amemficha ndani. Kisha alimwonyesha Morile yule mtoto “Kana” na kuanza kulia; “Morile, Morile, mwanangu chukua mtoto wako.” Morile alimjibu simhitaji tena huyo Kana, Sasa naelekea kwake yule aliyenipa huyo Kana nikamuuliza kama Kana hakuwa mali yangu niliyepewa na yeye.

Morile aliendelea kupandishwa juu zaidi na kile kiti. Mama yake aliendelea kumhimiza arudi ampokee Kana wake. Lakini Morile hakurudi tena kumchukua Kana wake. Mama yake aliendelea kumwangalia mwanaye Morile juu mawinguni lakini hakumwona tena. Kulitokea huzuni na maombolezo makubwa kwa baba na mama yake Morile baada ya Morile kutoweka. Waliamza kumwita Kana kwa jina la “Morile wa pili”.

Morile aliendelea kupandishwa juu mpaka alipofika kwenye geti la huko juu mawinguni. Kisha Morile aliwauliza walinzi aliowakuta getini; “Ni njia gani inayoweza kunifikisha kwa mtawala wenu Mangi Tembo Lya Mori?”. Walinzi hao walimjibu Morile, “Fuata njia hii na mbeleni utakutana na watu wanalima na hao wakuonyesha njia ya kufika kwa Mangi Tembo Lya Mori”.

Morile aliifuata njia ile aliyoonyeshwa na mbeleni alikutana na watu wanaolima mashamba na kuwauliza; “Ni njia gani itanifikisha kwa mtawala wenu, Mangi Tembo Lya Mori?”. Wali wanaolima wakamjibu; “Fuata njia hii na mbeleni utakutana na watu wanaootesha mbegu na hao wakuonyesha njia ya kufika kwa Mangi Tembo Lya Mori”.

Morile alifuata kama alivyoelekezwa na mbeleni alikutana na watu wanaopanda mbegu na kuwauliza, “Nyinyi mnaopanda mbegu, ni njia ipi itaweza kunifikisha kwa mtawala wenu, Mangi Tembo Lya Mori?”. Wale wanaopanda mbegu wakamjibu; “Fuata njia hii na mbeleni utakutana na watu wanaovuna mazao na hao watakuonyesha njia ya kufika kwa Mangi Tembo Lya Mori”.

Morile alifuata njia ile aliyoelekezwa na mbeleni alikutana na watu wanaovuna mazao na kuwauliza; “Ni njia gani itanifikisha kwa mtawala wenu, Mangi Tembo Lya Mori?”. Wale watu wanaovuna mazao walimjibu; “Fuata njia hii na mbeleni utakutana na watu wanaotengeneza mizinga ya asili porini na hao watakuonyesha njia ya kufika kwa Mangi Tembo Lya Mori”.

Morile alichukua njia ile na mbeleni alikutana na watu wanatengeneza mizinga ya asili porini na kuwauliza; “Ni njia ipi itanifikisha nyumbani kwa mtawala wenu, Mangi Tembo Lya Mori?”. Wale warina asali waliokuwa wanatengeneza mizinga ya asali walimhibu; “Fuata njia hii na mbeleni utakutana na watu wanaochunga mbuzi na hao watakuonyesha njia ya kufika kwa Mani Tembo Lya Mori”.

Morile aliifuata njia ile aliyoelekezwa na mbeleni alikutana na watu wanaochunga mbuzi akawasalimia kisha akawauliza; “Nyinyi mnaochunga mbuzi, ni njia gani itanifikisha kwa mtawala wenu Mangi Tembo Lya Mori?” Wale watu wanaochunga mbuzi walimjibu Morile, “Fuata njia hii na mbeleni utakutana na watu wanaochunga ng’ombe na hao watakufikisha kwa Mangi Tembo Lya Mori.”

Morile aliifuata njia ile aliyoelekezwa na wale waliokuwa wanachunga mbuzi na mbeleni alikutana na watu wanaochunga ng’ombe. Wale wanaochunga ng’ombe walimwambia Morile, “Tuchunge wote ng’ombe kwa muda kisha tutakupeleka kwa mtawala wetu, Mangi Tembo Lya Mori”.

Morile alikubaliana nao na wakaanza kuchunga ng’ombe wale pamoja. Hivyo walichunga ng’ombe mpaka jioni kisha wakaondoka pamoja na mifugo ya sambamba na Morile mpaka nyumbani kwa Mangi Tembo Lya Mori mwenyewe.

Mangi Tembo Lya Mori alipomuona Morile alimuuliza maswali mengi sana na Morile alijieleza mwanzo mpaka mwisho, (Maana ya Tembo Lya Mori/Meri ni “Msaidzi wa mwezi”.

Baada ya mazungumzo kati ya Morile na Mangi Tembo Lya Mori kufikia mwisho, Morile alipewa nyumba ya kuishi ambayo alilala usiku huo. Jioni hiyo aliletewa chakula ambacho hakujapikwa ile ale na alishangazwa sana kwa nini ale chakula ambacho hakijapikwa na hivyo alienda kumuuliza Mangi Tembo Lya Mori.

Mangi Tembo Lya Mori alimjibu Morile akamwambia; “Watu wa hapa mwezini ni tofauti na watu wa huko duniani. Watu wa duniani wazaliwa, wanakua, wanazeeka na mwisho wanakufa, lakini hapa mwezini watu wanazaliwa wanakuwa na kuishi milele, bila kufa. Watu hapa mwezini wanakua mpaka wanazeeka kisha wanarudi tena kuwa watoto na kukua tena kuwa watu wazima.”

Mangi Tembo Lya Mori akaendelea kumwambia Morile; “Sisi hapa mwezini hatuna shida wala taabu za namna yoyote ile, kwa sababu Ruwa yuko karibu sana na sisi. Tukihitaji kitu chochote tunamwambia Ruwa na anafanya kila kitu kwa ajili yetu. Hata hivyo yote inayonyesha kwenu duniani inatumwa kwanza kwetu na Ruwa na baada ya hapo ndio ikitoka kwetu inakuja kwenu.”

Morile alishangazwa sana na maneno hayo kisha akasema, “Lo! nilipoondoka duniani kuelekea juu mawinguni nilifikiri nitafika hata kwa Ruwa, na nilipofika hapa nilijuwa kwamba nimefika kwa Ruwa, sasa naambiwa hapa sio kwa Ruwa, hapa ni mwezini, sasa Ruwa yuko wapi?”.

Mangi Tembo Lya Mori alimjibu Morile na kumwambia; “Kama ukitoka hapa utapandisha juu kidogo na utafika kwenye jua. Kisha jua lenyewe ndio litakufisha kwa Ruwa mwenyewe. Morile alishangazwa na yote aliyoambiwa na Mangi Tembo Lya Mori.

Morile alichukua kisu chake na kukata vijiti vikavu kwa ajili ya kutengeneza moto na kisha alitengeneza moto. Baada ya kutengeneza moto Morile alipika chakula na kula. Baada ya kushiba alichukua kidogo na kujaribu kumpa Mangi Tembo Lya Mori. Baada ya Mangi Tembo Lya Mori kula kidogo aliona kwamba ni chakula kitamu sana. Mangi Tembo Lya Mori alishangazwa sana na kumuuliza Morile; “Umefanyaje mpaka kukifanya chakula hiki kuwa kitamu sana?”

Morile alimjibu, “Nimekipika na moto ambao nimeutengeneza mwenyewe. Na sisi ndio tumekuwa hivyo tunakula chakula kinachopikwa na moto”. Mangi Tembo Lya Mori akamwambia; “Nipe na mimi huo moto ili niweze kupika chakula pia”.

Morile akamwambia Mangi Tembo Lya Mori; “Wewe nitakupa moto huo bure kabisa, kwa sababu niko kwenye mikono yako, lakini kwa watu wako wote watakaohitaji watanunua kwangu, nami nitawauzia.” Kwa hiyo Morile alichukua moto na kumpatia Mangi Tembo Lya Mori. Kisha alimfundisha namna ya kupika chakula na nyama.

Kisha Mangi Tembo Lya Mori aliwajulisha watu wake wote kwamba yuko na mtaalamu wa kutengeneza moto, na kila atakayehitaji moto huu anatakiwa kuja mbuzi na ng’ombe na ataonyeshwa moto na atanunua. Hivyo watu wote walikuja kwa Mangi Tembo Lya Mori na kumkuta Morile pale. Morile anapowaona watu hao alifurahia sana na kutengeneza moto mwingi, na kuwaonyesha watu namna ya kuwasha moto na namna ya kupika vyakula mbalimbali. Kisha aliwapa chakula kidogo kwa ajili ya kuonja.

Watu wa mwezini walipoona yote haya walishangazwa sana juu ya mambo haya mapya. Morile aliwauzia moto. Cheche moja ya moto aliiuza kwa mbuzi mmoja au kondoo. Kwa cheche mbili mpaka nne za moto aliuza kwa ng’ombe mmoja mzima. Kwa hiyo ilikuwa ni kazi yake kuuza moto kwa watu wa mwezini mpaka kila mtu alipokuwa na moto na kuutumia.

Morile alikusanya mali nyingi sana ambapo utajiri wake ulikuwa ni mkubwa kuliko utajiri wa mtu mwingine yeyote huko mwezini isipokuwa Mangi Tembo Lya Mori peke yake. Watu wa mwezini hawakuwa watu wa kuchinja sana ng’ombe na kupata nyama, lakini yeye Morile alichinja wanyama wengi sana na aliweza kusambaza nyama kwa watu wengi kama vile yeye ndiye Mangi wao.

Watu wa mwezini walikula sana na walimlimia Morile mashamba mengi sana na hivyo Morile akazidi kutajirika sana na utajiri wake ukaongezeka sana na jina lake na heshima yake ikawa kubwa sana huko mwezini. Morile mwenyewe akawa ndiye kama Mangi wao huko mwezini.

Morile baada ya kutajirika sana huko mwezini akatamani sana kurudi nyumbani kwa baba yake na mama yake. Hivyo alianza kupanga safari ya kurudi nyumbani ambapo aliita ndege wote na kuwapa nyama. Baada ya kuwapa ndege hao nyama alichukua mmoja baada ya mwingine na kuwaambia maneno haya; “Nenda kwa mama yangu kule duniani na umwambie maneno haya, Morile mwanao anakuja pamoja na mifugo yake, hivyo unapaswa kusubiri leo, kesho, kesho kutwa kisha siku ya tatu atakuja.” Kisha kila ndege alijaribu kuongea kama binadamu kama alivyoagiza Morile. Lakini hakuna hata ndege mmoja aliweza kufanikiwa kuongea kama alivyohitaji Morile aliwaondoa.

Mwishowe alipata ndege mmoja aliyeitwa “Mnyonyori”. Ndege huyu alikuwa na uwezo kuongea sauti za ndege wengine wote na aliweza pia kuongea kwa sauti ya mtu. Mara kwa mara alimshangaza Morile kwa kuweza kuongea naye. Hivyo Morile alimpa nyama akala. Kisha akamweleza yote ambayo anataka akamwambia mama yake duniani. Morile aliona huyu ndege “Mnyonyori” ana uwezo wa kufikisha ujumbe wake kwa mama yake duniani. Hivyo akamtuma ndege huyu.

Ndege, “Mnyonyori” akapaa kuelekea duniani, alipaa kwa siku mbili na siku ya tatu alifanikiwa kufika duniani na kufika kwa mama yake Morile. Ndege “Mnyonyori” alifika na kutua kwenye mlango wa nyumba ya mama yake Morile na kufikisha ujumbe aliotumwa na Morile. Mama yake Morile aliposikia maneno haya alikasirika sana kukumbushwa juu ya mtoto wake kipenzi aliyepotea miaka mingi. Hivyo alitoka nje kumfukuza ndege huyu mbaya.

Mama yake Morile alipokuwa anatoka nje, ndege “Mnyonyori” alimnyakua kitambaa cha kichwani mwake alichokuwa amevaa na kupaa juu hewani na kuendelee kwenda juu mpaka alipopotelea kabisa mawinguni. Mama yake Morile ashangaa sana na kuogopa sana kwamba atakufa kwa sababu kitambaa chake cha kichwani kimenyakulia.

Ndege Mnyonyori alipaa kwa siku tatu mpaka alipofika tena mwezini kwa Morile. Morile alimuuliza yaliyotokea na ndege “Mnyonyori” alimjibu; “Nimefika mpaka kwa mama yako na nimemkuta ni mzima wa afya. Nimefanikiwa kumfikishia ujumbe wako na hiki ndio kitambaa chake cha kichwani anachovaa” Morile aliona kitambaa kile cha mama yake na kuamini kwamba maneno yale ya ndege “Mnyonyori” ni ya kweli na alifurahi sana.

Hivyo Morile alikusanya mali zake zote na wasaidizi wake hasa waliokuwa wanaangalia mifugo yake na kuandaa safari yake ya kurudi duniani. Msafara wa safari ya Morile ulikuwa ni mkubwa sana. Wakiwa katikati ya safari walikutana na mto mkubwa sana wenye mafauriko na hivyo Morile na msafara wake wakapata changamoto ya kuendelea na safari yao.

Kulikuwa na dume moja kubwa sana la ng’ombe(pung’a) katika safari yao ambalo ndio lilikuwa limezeeka pia zaidi kuliko wanyama wote. Pung’a hili likamwambia Morile; “Kama nitafanikisha kuvusha msafara mzima katika mafuriko haya basi siku nitakapochinjwa au kufa wewe usile nyama yangu kabisa; ujue kabisa kwamba siku utakayokula nyama yangu utakufa.” Morile alimhakikisha Pung’a huyu kwamba kamwe hatakula nyama yake. Hivyo Pung’a huyu aliweza kuvusha msafara mzima wa Morile kwenye mafuriko haya na hivyo kufanikiwa kuyavuka.

Kisha Morile na msafara wake wakasafiri mpaka kufika sehemu ambayo ndio getini kati ya mawinguni na duniani. Walipofika katika geti hili watu wa mawinguni walirudi nyumbani kwao katika himaya ya Mangi Tembo Lya Mori. Kisha Morile na mali zake zote pamoja na yule Pung’a aliyewavusha kwenye mafuriko wakaendelea na safari kuelekea duniani kwa mama na baba yake Morile.

Safari yao ilikuwa hivi. Morile alipofika eneo hili aliita kile kiti cha baba yake ambacho mwanzoni ndio kilimpandisha juu mpaka mawinguni kikapanda tena kuja kumchukua Morile na mali zake zote na kuwashusha mpaka duniani nyumbani kwao kwa mama yake. Morile akashukia nyumbani kwao kwa wazazi wake moja kwa moja. Baba yake na mama yake Morile wakashangazwa na utajiri mkubwa sana wa Morile.Kisha walimsalimia na kumpokea na watu wote walikuwa wakimsubiria. Morile alizidi kutajirika sana na aliheshimiwa sana na watu, kisha alioa na kupata watoto.

Morile aliishi miaka mingi na yule ng’ombe Pung’a mkubwa alizeeka na kufa. Watu walikula nyama ya yule ng’ombe Pung’a lakini Morile hakula chochote kutoka kwa Pung’a yule. Mama yake alipoona kwamba Morile hajala kabisa nyama siku ile pung’a amechinjwa, hivyo alichukua nyama kidogo sana ya mafuta ya yule pung’a na kuweka kwenye chakula cha Morile na kumpa ale.

Morile alipoanza tu kula kile chakula ghafla alisikia sauti ikisema; “Wamenila nawe lazima utaliwa pia”. Morile alianguka hapo hapo akiwa ameshika chakula kile mkononi.Hii ni hadithi ya Morile kama ilivyokuwa ikielezwa na wachagga.

Hadithi za wachagga za zamani ni nyingi sana lakini hapa tunajaribu kugusia baadhi tu kuonyesha namna zilivyokuwa fikra za wachagga zamani.

Ahsanteni sana.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *