Hapo zamani za kale katika nchi ya wachagga kulikuwa na mwanamke ambaye hakujaliwa kabisa kupata mtoto hata mmoja. Mwanamke huyu pia umri wake wa kuweza kupata mtoto ulikuwa umepita sana. Kila siku alikuwa akifanya kazi mpaka kufikia kuchoka sana huku wanawake wengine wakimkejeli na kumsanifu kwa kutokuwa na mtoto ambaye angeweza kuwa msaada kwake.
Jambo hili lilimtesa sana na kila siku alikuwa akimlilia Ruwa kwa changamoto hizi alizokuwa anapitia. Siku moja alichukua mbegu za mabuyu na kuziotesha katikati ya shamba lake la migomba. Mbegu hizo ziliota zikamea na kuzaa matunda. Siku moja mwanamke huyu akiwa ndani ya shamba lake aliona mtu mmoja amesimama pale shambani, na mtu huyu alimwambia; “Hudumia mabuyu haya kwa umakini mkubwa kwa sababu yamebeba bahati nzuri sana kwako. Mimi ni waziri wa Ruwa. Ruwa amenituma kwako kukufariji.”
Hivyo mwanamke yule aliendelea kuhudumia vibuyu hivyo mpaka kufikia kuvuna. Kisha akavichukua na kuviweka darini ili vikauke. Hivyo vibuyu hivyo(jamii ya maboga) viliendelea kubaki hapo darini mpaka vilipokauka. Kisha mwanamke yule alichukua kile kibuyu kizuri kuliko vyote na kukiweka karibu na eneo la kupikia jikoni, vile vingine vikabaki darini.
Sasa siku moja alikuja wa waziri/mjumbe wa Ruwa ambaye alikibadilisha kibuyu hiki kilichokuwa jikoni kuwa mtoto. Lakini alikuwa ni mtoto mjinga sana hasa katika namna ya kutembea na kuongea. Kisha vile vibuyu vilivyobaki darini vilibadilishwa na kuwa watoto wenye akili sana na werevu ambao wanaweza kufanya kazi yoyote na hata kuongea vizuri.
Lakini wakati haya yote yanaendelea mwanamke yule hakuwa na habari kabisa. Yeye aliamka asubuhi na kwenda kwenye shughuli zake za kila siku kama kawaida yake. Asubuhi yake ndipo vibuyu hivyo vilibadilishwa na kuwa watoto. Kile kibuyu kilichokuwa pale chini jikoni baada ya kubadilika na kuwa mtoto aliitwa Kitete. Hivyo ilisikika sauti kutoka darini ikimwambia Kitete, “(Kitete, kitete, nipokee kaka yangu)”. Kisha Kitete alisimama na kuwapokea mmoja baada ya mwingine mpaka wote wakawa wameshuka chini kutokea darini.
Kisha walitoka nje ya nyumba na kwenda kumfanyia kazi mwanamke yule. Baadhi walienda kukata majani ya ng’ombe, wengine walienda kupalilia migomba, wengine walifanya usafi wa kufagia kwenye zizi la ng’ombe na wengine walifanya kazi nyingine mbalimbali. Walipomaliza kazi zao zote walirudi ndani ya nyumba na kupanda darini kila mmoja akirudi katika eneo lake. Kisha walibadilika na kurudi kuwa vibuyu tena na hata Kitete naye alibadilika na kurudi kuwa kibuyu.
Hivyo sasa yule mwanamke aliporudi nyumbani kwake alikuta kazi zote zimeshafanyika na hakujua ni nani aliyefanya. Kwa hiyo alienda kwa majirani kuuliza ni nani amefanya kazi hizo. Mwanamke wa jirani akamjibu na kumwambia; “Asubuhi hii tumeona watoto wengi sana wakifanya kazi nyumbani kwako. Lakini hatuwajui, pia hatukuweza kuwauliza wamekuja lini wala ni watoto wa nani.
Hivyo mwanamke yule alirudi nyumbani na kukumbuka maneno ya mjumbe yule wa Ruwa. Kisha alitazama juu mawinguni na kutema mate mara tatu huku akilitaja jina la Ruwa aliyewapa watu uhuru. Kesho yake mwanamke yule akaenda tena kwenye shughuli zake kama kawaida yake. Ilipofika asubuhi vile vibuyu vikageuka tena kuwa watoto. Majirani walisogea karibu na kujificha karibu na nyumba hiyo.
Ghafla walisikia sauti za watoto wakiita, “(Kitete, Kitete, nipokee kaka yangu, mpendwa!).” Mara moja wakaona kundi kubwa la watoto wakitokea ndani ya nyumba ya mwanamke huyo. Kisha walifanya kazi zao zote kama vile walivyofanya siku iliyopita. Yule mwanamke aliporudi kutoka kazini alikuta kazi zake zote za nyumbani zimefanyika kama ilivyokuwa imefanyika jana yake. Alishangazwa sana na hivyo kunyanyua mikono yake kwa Ruwa kumshukuru. Jirani zake walimwelezea kila kilichotokea na kumshauri kwamba siku inayofuata naye ajifiche karibu na nyumba ili aweze kujionea mwenyewe kila kitu.
Mwanamke yule alifuata ushauri wa majirani zake. Kesho yake aliamka na kufunga mlango wa nyumba yake kama kawaida na kujifanya kama anaondoka. Lakini alijificha karibu na nyumba yake. Ghafla alisikia sauti; “Kitete, Kitete, nipokee kaka yangu mpendwa!” Kisha akaona watoto wanafungua mlango. Walitoka watoto wengi sana ndani ya nyumba yake kisha wakajikusanya nje na hapo kila mmoja alitawanyika kwenda kwenye kazi yake.
Lakini kabla hawajafanya hivyo mwanamke yule alijitokeza na kusema; “Kwa hiyo ni nyinyi mmenifanya mambo mazuri kiasi hiki? Ahsanteni sana watoto wangu!” Sasa watoto hao walipigwa na butwaa na hawakuweza tena kujigeuza kuwa vibuyu kwa sababu Kitete alikuwa nje. Hivyo watoto hao wakawa ni watoto wa mwanamke huyo.
Waliishi naye na kufanya kazi zote, na mwanamke huyo alipata kubarikiwa sana kwa vyakula, mbuzi wengi, ng’ombe wengi kupitia kazi walizofanya watoto hao ambao walibadilika kutoka kwenye vibuyu. Mwanamke huyo akawa tajiri sana. Lakini Kitete hakufanya kazi yoyote kwa sababu alikuwa ni mjinga sana. Kazi yake ilikuwa ni kuwasha moto peke yake na alikaa karibu na mama yake wakati anapika.
Baadaye mama yake alikerwa sana na tabia za Kitete lakini hakusema neno lolote. Kitete aliendelea kuwa msumbufu sana kwa mama yake kwa kiasi kikubwa sana kwa miaka mingi. Sasa siku mchana mama yake alitaka kupika chakula lakini Kitete hakumwachia apike bali alimletea usumbufu mkubwa ulimzuia kabisa kupika. Kisha mwanamke yule alikasirika sana na kusema kwa sauti kubwa; “Napata shida sana kuletewa usumbufu na kukasirishwa na hivi vibuyu kila siku.”Hapo hapo Kitete alibadilika kuwa kibuyu na kisha kupasuka. Hivyo hivyo na watoto wengine wote walibadilika kuwa vibuyu mara moja na kisha moja baada ya kingine vilipasuka na kuharibika mpaka kuisha vyote.
Sababu iliyopelekea haya yote ni mwanamke huyo kuwaita watoto hao tena aliopewa na Ruwa “vibuyu”.
Hivyo mwanamke huyo aliendelea kuishi mwenyewe katika umaskini mpaka kufa kwake.
Ahsanteni.
Tutaendelea kesho.
Urithi Wetu Wachagga.
urithiwetuwachagga@gmail.com