HAKI ZA MWANAMKE KISHERIA KATIKA NCHI YA WACHAGGA.

Katika nchi ya wachagga hadhi ya mwanamke kisheria na haki zake zilikuwa bayana na zaidi zinaonekana wakati wa ndoa. Hata hivyo mbele ya sheria za wachagga mwanamke alipewa hadhi kubwa zaidi kisheria ukilinganisha na jamii nyingi za kiafrika.

Kwa mfano katika ardhi ya wachagga miaka ya zamani sana wakati wa vita kisheria mwanamke hakuruhusiwa kushambuliwa, na ni mara chache sana walichukuliwa kama mateka wa vita. Hata ilipotokea kwamba mwanamke amechukuliwa kama mateka wa vita badala ya kufanywa mtumwa alipewa hadhi ya kufanywa mke.

Lakini hata hivyo sheria za wachagga zilikataza kuchukua mateka wanawake katika vita na ilitakiwa kuwalinda dhidi ya unyanyasaji wowote katika vita wakati wanaenda au kurudi kutoka sokoni. Mara nyingi wakati wa vita shughuli za sokoni ziliendelea kama kawaida na wapiganaji waliwahurusu wanawake kupita wakienda au kutokea sokoni. Hata hivyo sio mara zote sheria hizi zilizingatiwa licha ya kwamba ndivyo sheria za kichagga zilivyohitaji.

Katika sheria za wachagga pia ilikuwa ni marufuku kwa mtu yeyote isipokuwa baba yake au mume wake kumpiga mwanamke. Hata ikitokea kwamba mwanamke ndiye ameanza kukupiga au kukushambulia haikutakiwa kumrudishia bali kwenda kumshitaki kwa mume wake na kudai kulipwa fidia. Inasemekana kwamba hata mjumbe aliyetumwa na Mangi pia ilikuwa bado ni kosa kumpiga, kupigana au kumshambulia mwanamke asiye mke wake.

Hii ilitokana na hoja kwamba kumpiga mwanamke ni kama kuchukua jukumu au nafasi ya mume wake. Hata hivyo sheria hii iliwaweka wanawake kwenye nafasi ya kipekee sana na kuwapa uhuru mkubwa na kwamba hawakuwajibika kwa yeyote isipokuwa mume wake. Hata mume wake pia hakuruhusiwa kisheria kumpiga mwanamke hovyo au bila sababu ya msingi, mume aliruhusiwa kumpiga mwanamke pale anapofanya makosa makubwa peke yake kama vile kuonyesha dharau ya hali juu au kuchepuka. Hata hivyo sio mara zote sheria hizi zilizingatiwa.

Wazazi na walezi pia hawakuwa na mamlaka makubwa sana kisheria juu ya wanawake. Mwanamke alikuwa na uhuru wote wa kimaamuzi juu ya chaguo lake katika ndoa. Kisheria mwanamke hakulazimika moja kwa moja kung’ang’ana kwenye mkataba wa ndoa yake kama kuna mambo yameshindikana japo kulikuwa na utaratibu maalum wa kufuata. Pia ikitokea mume amefariki mwanamke huyo alikuwa huru kuolewa tena.

Kisheria kwa wachagga wanawake walikuwa na uhuru na haki za kumiliki mali na uhuru wa kuzitumia wanavyotaka ikiwa ni pamoja na kuuza. Mwanaume hakuwa na haki ya kurithi mali za mke wake. Mali hizo mwanamke alikuwa anaweza kuwa amezipata kwa faida aliyopata kutoka kwenye biashara aliyofanya sokoni, au kwa vitu alivyotengeneza nyumbani kama vile vyungu, vyombo vya nyumbani n.k.,

Lakini kwa kawaida mwanamke alianza kupewa mifugo na familia yake kuanzia alipochumbiwa. Baada ya kuolewa mwanamke aliweza pia kupewa mifugo mingi na wazazi wake kutegemea na utajiri wa familia husika. Mara nyingine pia mwanamke aliweza kwenda na mali nyingi kwa mume wake kuliko hata kiasi cha mali kilicholipwa kama mahari kwa baba yake lakini mara nyingi alizipeleka mali hizo baada ya kupata watoto.

Hata hivyo kwa upande mwingine mwanamke katika hali ya kawaida mwanamke hakurithishwa mali ya aina yoyote ile. Lakini pia kisheria katika madai ya aina yoyote mwanamke hakuruhusiwa kwenda kusimama mahakamani kujitetea badala yake alitakiwa kwa kesi yoyote kuwakilishwa na aidha mume wake au mlezi wake mwingine ambaye ni mwanaume.

Hivyo katika nchi ya wachagga wanawake walikuwa na uhuru mkubwa sana. Hakuna mtu aliyefikiria kumwadhibu mwanamke moja kwa moja, hukumu ya makosa yake ilikuwa ni juu ya mume wake au mlezi wake na huyo mlezi wake jambo kubwa sana alilofanya ni kumwonya au kumgombeza.

Mara nyingi pia Mangi au wazee waliweza kupuuza au kutoweka uzito mkubwa sana kwa kosa alilofanya mwanamke ambalo lingeweza kupewa uzito mkubwa kupelekea adhabu kubwa kama lingefanywa na mwanaume.

Kisheria katika nchi ya wachagga wanawake walifikiriwa sana, hata katika mazingira ambayo hawakustahili wakati mwingine na hata katika ngazi ya familia walilindwa sana katika mazingira ambayo mwanaume hakuonyeshwa kujaliwa sana.

NB; Sheria hizi jaoo hazikuzingatiwa mara zote lakini bado zilisaidia sana kupunguza unyanyasi na kutoa uhuru mkubwa sana kwa wanawake wa kichagga ukilinganisha na jamii nyingine nyingi.

Ahsanteni.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *