MAPENDEKEZO YA PROF. R. SAMBULI MOSHA JUU YA UHIFADHI NA MATUMIZI YA ELIMU YA ASILI.

Kutokana na mapungufu makubwa yaliyopo katika mfumo wa elimu ya kisasa iliyoletwa na mfumo wa elimu wa magharibi na kuendelezwa na serikali zilizoendelea ambao unazingatia elimu ya akili peke yake(intellectualism) na kupuuza elimu ya kiroho(spirituality) na hivyo kushindwa kukidhi mahitaji ya kijamii kama ilivyokuwa kwa mfumo wa elimu ya asili ambao ulizingatia uwiano sawa wa elimu ya akili na elimu ya kiroho, Prof. R. Sambuli Mosha katika kitabu chake cha “The Heartbeat of Indigenous Africa, the Study of Chagga Education System” alihimiza mambo mbalimbali kufanyika kama ifuatavyo.

1. Kuzalisha na kuandika elimu ya asili ili iweze kupatikana kwa watu mbalimbali duniani. Hili linapaswa kufanyika kwa haraka na kwa makini kwa sababu elimu ya asili imepotea sana na inazidi kupotea kabisa kutokana na mitazamo ya kikoloni inayodharau na kupuuza namna za upatikanaji wa maarifa ya elimu ya asili. Taasisi za asili ambazo maarifa hayo yanapatikana zimezidi kupotea kabisa.

2. Kuhimiza mitaala ya shule ambayo itazingatia maarifa haya yanayotokana na elimu ya asili. Hapa njia mbalimbali za kupatikana na kuandikwa kwa maarifa ya na njia za ufundishaji zinapaswa kuzingatiwa badala ya kwenda na mazoea yaliyopo katika mitaala ya elimu iliyozoeleka.

3. Kuhalalisha na kuthibitisha maarifa yanayotoka kwenye elimu ya asili. Ni bahati mbaya kwamba kutokana na mitazamo ya kikoloni na kutukuzwa sana kwa mambo ya kigeni kutokea magharibi maarifa yanayotoka kwenye elimu ya asili hayajawahi kuhalalishwa wala kuthibitishwa badala yake yameendelea kuonekana kama ni mambo duni na yaliyopitwa na wakati. Hilo limepelekea kila kitu cha asili kuonekana ni cha hovyo iwe ni lugha ya asili, historia, miziki, majina n.k. Hili litasaidia hata mambo mengi ya watu wanaoonekana ni wa chini wa kijijini sana kueleweka kwa namna walivyo na mambo yenyewe yalivyo katika uhalisia wake.

4. Kuzalisha njia mpya za tafiti za kujifunza maarifa yanayotoka kwenye elimu ya asili. Hili litasaidia kugundua mambo mengi muhimu na maarifa mengi yenye manufaa makubwa kutoka kwenye elimu ya asili ikiwemo lugha na namna ilivyoweza kuwasilisha elimu ya asili. Pia uvumbuzi wa maandishi ya asili na uendelezaji wake unaweza kusaidia kuwa na utambulisho mpya wa kimaandishi wa jamii husika ambao utaongeza upekee, ufahari na heshima kwa jamii hiyo.

5. Kulinganisha maarifa kutoka kwenye elimu ya asili na maarifa kutoka maeneo mengine duniani hususan kutokea kwenye mfumo wa elimu wa magharibi na hivyo kuweza kuona ni eneo gani wao wameendelea zaidi ambalo linaweza kuingizwa kwenye elimu ya asili na eneo ambalo elimu ya asili imepiga hatua zaidi ambapo watu wa nje wanaweza kujifunza kutokea asili. Hili tuliweza kuliona vizuri kupitia utafiti wa Dr. Bruno Gutmann. Kupitia midahalo mbalimbali ya ana kwa ana na ya kimaandishi ni rahisi kufahamu hilo kwa kina.

6. Kuhamasisha wanafunzi wengi zaidi kujifunza na kufanya tafiti zaidi juu ya mchango wa elimu ya asili kwa maendeleo ya kijamii kwa miaka ya zamani tangu karne nyingi zilizopita na hata sasa. Elimu hii ilikuwa na mchango mpana katika mambo mengi kuanzia ufundi wa vita mbalimbali, kilimo, ufugaji, utabibu, sheria, ujenzi, lishe, historia, lugha, n.k.,Haya yakiwa ni mapendekezo ya kuihifadhi na kuiboresha zaidi elimu ya asili kwa kuchanganya na elimu ya kisasa kuweza kuwa na maarifa mengi zaidi katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za kila siku za kijamii.

Ahsanteni.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *