KATIKA MWAMKO HUU WA JAMII MBALIMBALI DUNIANI KURUDI KUWEKA KIPAUMBELE KWENYE TAMADUNI ZAO ZA ASILI WACHAGGA TUMEJIANDAAJE?

– Dunia inaendelea kuamka kwa kasi sana na taarifa nyingi muhimu zilizokuwa zimejificha au kufichwa kwa makusudi zinaendelea kuwa hadharani siku hadi siku. Licha ya kwamba usumbufu wa kiteknolojia hususan unaoletwa na simu janja za mikononi(smartphones) umekuwa ni kikwazo kikubwa kwa watu kuweka umakini wao kwenye mambo yanayohitaji utulivu na tafakari za kina lakini bado kuna watu ambao wana shauku kubwa sana vya kutosha kufuatilia mambo hayo, kuyafahamu kwa kina na kujaribu kuja na mapendekezo mbalimbali.

– Watu wa kada mbalimbali ikiwa ni pamoja na wanafalsafa wa karne ya 21 wanaendelea kutafakari mambo mbalimbali na kuhoji kila kitu ambacho kipo na kujiuliza kwa nini kipo vile kilivyo, kina manufaa gani na ni nini chanzo chake. Katika kuhoji huku ndipo wasomi na wanafalsafa mbalimbali wanagundua kwamba kuna mambo mengi ambayo yanahitaji mapinduzi kwa sababu hayako katika usahihi ambao watu wengi wenye kujielewa wanavyoweza kuridhika kuyaona.

– Mambo haya yapo katika nyanja zote kijamii ambapo msingi wake au chanzo chake ni utamaduni husika. Pale ambapo watu wanagundua kwamba mambo mengi wanayotumia sio ya utamaduni wao bali wa kuazima ni jambo ambalo linawachukiza na kuwaumiza. Hii ni kwa sababu linakuwa ni jambo la aibu na fedheha pale mtu anapogundua kwamba alinyang’anya kilicho chake kwa sababu zozote zile ikiwemo hila mbaya na watu ambao walitaka kumfanya dhaifu na asiyejitambua na kisha kuletewa yale yasiyo ya kwake ambayo kamwe hawezi kusimama kifua mbele kujivunia.

– Hilo limepelekea baadhi ya jamii mbalimbali kuanza kudai kurudi katika misingi yao ile ambayo wanaweza kujivunia na kujiamini nayo. Hii ni kwa sababu imekuwa wazi kwamba hakuna sababu wala manufaa yoyote makubwa ya kung’ang’ania tamaduni, mila na desturi za watu wengine dhidi ya zile za wenyeji ukiondoa mambo machache muhimu yasiyokuwa na mbadala.

– Haya mapambano ya jamii mbalimbali kung’ang’ania tamaduni zao hayajaanza leo wala jana katika dunia ya kisasa ukiondoa ile ya kale. Mapambano haya yalishika kasi sana katika karne ya 20 ambapo nchi nyingi licha ya kudai uhuru wao kutoka kwa wakoloni lakini pia walihakikisha wanalinda tamaduni zao kwa kujua kwamba ni msingi muhimu wa kujenga kujiamini na kufanikisha mambo makubwa na ya muhimu. Na kweli jamii na mataifa mengi yaliyobaki katika misingi yao ya asili yamejitahidi kupiga hatua kubwa sana mpaka sasa ukilinganisha na yale yaliyoendelea na tamaduni walizoletewa.

– Hata watalii wengi duniani katika karne ya 21 wanapenda zaidi kutembelea nchi zenye tamaduni zao za kipekee na kuziheshimu zaidi kuliko zile ambazo zinatumia tamaduni za wengine. Upekee ule unajenga shauku kubwa ya watu kujiuliza mengi kuhusiana na jamii husika na kujifunza mengi kuliko jamii zile zenye utamaduni wa kuazima kwa wengine.

– Tunaweza kuona hata katika lile taifa kubwa lililoitwa umoja wa kisovieti maarufu kama U.S.S.R ambalo lilikusanya nchi nyingi sana ndani yake na kujaribu kulazimisha kuwa na utamaduni wa pamoja liliishia kuvunjika na kila mmoja kurudi kwenye misingi yake ya asili. Kuvunjika kwa U.S.S.R sio tu kulitoa uhuru kwa jamii na mataifa yaliyokuwa yanalazimishwa kukaa pamoja na kuua tamaduni zao za asili bali kumejenga hata chuki kwa umoja huo ambao ulikuwa unalazimisha mataifa hayo mengi madogo kwa kutumia propaganda kukaa kwenye umoja huo. Vita ya Urusi na Ukraine pamoja na mitazamo ya watu wa nchi nyingine za Ulaya mashariki ni moja ya dalili kwamba nchi hizo hazikuupenda kabisa umoja ule.

– Nchi nyingi za Asia pia na mashariki ya mbali kwa ujumla kwenye eneo hili la kulinda tamaduni zao walijitahidi kupambana sana katika karne ya 20 kuhakikisha kwamba hawazipotezi wala kuziacha. Leo hii ukiwatazama wengi wamepiga hatua kubwa kiuchumi na kiteknolojia bila kuachana na tamaduni zao. Unaweza kuitazama nchi kama Korea ya kusini zinakotokea simu za Samsung na magari ya Hyundai ikiwa ni kati ya nchi ambazo zilihakikisha kwamba zinabaki na tamaduni zao za asili na mpaka leo zimefikia utukufu mkubwa bila kutegemea tamaduni za kigeni.

– Hakuna kitu kinachoweza kuwajengea watu hasira hata wawe ni wasomi wakubwa kiasi gani kama kuwatenganisha na tamaduni zao za asili halafu wakaja kugundua kwamba hilo lilifanyika kwa maslahi ya mtu/watu binafsi au ya kisiasa huku ukibomoa utukufu wao na ufahari wao. Jambo hili liko kwa asili katika saikolojia ya binadamu ndio maana unaweza kuona kwamba hata kwa vitu visivyokuwa na umuhimu mkubwa kama vile timu za mipira bado vinaweza kuwa na nguvu kubwa ya uzalendo na kuhusisha hisia kali sana.- Sasa duniani kwa sasa kumekuwa na mwamko wa jamii nyingi zaidi hususan Afrika kwa sasa kupitia mapinduzi zaidi ya kifikra kujaribu kupigania kurudisha tamaduni za wenyeji ili kuondokana na fedheha ya kuendelea kutegemea vya watu ambavyo hatuwezi kusimama mbele za watu wa dunia hii na kujivunia. Mwamko huu ni mkubwa na unaendelea kadiri watu wanavyozidi kuamka kiakili na kujitambua hivyo nguvu yake inazidi kuwa kubwa zaidi miongoni mwa wanajamii siku hadi siku.

– Ni dhahiri kwamba kwa hakika endapo watu wengi wangekuwa na uwezo mkubwa kifikra wa kuona na kuelewa mambo haya kwa viwango alivyokuwa anaelewa mtu kama mwanafasihi wa Nigeria Chinua Achebe aliyeandika kitabu maarufu cha fasihi cha “Things Fall Apart” pamoja na waandishi na wanafalsafa wengine, lakini isipokuwa wanasiasa, ni wazi kwamba tungekuwa na jamii iliyojijenga kwenye tamaduni zetu na maendeleo makubwa yaliyojengwa katika misingi yetu. Sio tu Chinua Achebe na baadhi ya waandishi na wanafalsafa mbalimbali bali hata wanafalsafa wa Uchagga Joseph Merinyo Maro na Petro Njau waliliona hili tangu miaka ya 1930’s na walijaribu kupigania kwa nguvu zote kuwa na taifa la Uchagga lililojengwa katika misingi ya tamaduni za wachagga.

– Hili lilipelekea wanafalsafa hawa wa Uchagga kuanzisha chama cha kihafidhina cha Kilimanjaro Chagga Citizens Union (KCCU) kilichotengeneza sera kabisa za kujenga misingi hiyo ya taifa lililoanzishwa kwa kuzingatia tamaduni za wenyeji na kufanikiwa hata kushinda uchaguzi mkuu wa kumchagua Mangi Mkuu wa wachagga aliyetokana na chama hicho. Hata hivyo bado kulikuwa na mivutano mingi na uchakachuaji wa kujaribu kupunguza nguvu ya falsafa yao hiyo kutoka kwa wageni ambao hilo halikuwahusu. Lakini hili ni jambo lililofanywa na jamii zote duniani zilizokuwa zikijitambua, kujipenda na kujijali.- Sasa kuibuka kwa mapinduzi haya ya kifikra ambayo kwa sasa yamekuja kwa namna ya tofauti kidogo kunaambatana na swali moja muhimu la, je tumejiandaaje?

– Maandilizi yake haya ni kuhifadhi tamaduni ambazo tunategemea ndio mbadala wa tamaduni za kigeni tunazoishi kwa sehemu kubwa kwa sasa. Kwa bahati mbaya ni kwamba tamaduni huwa inakuwa na nguvu inapotumika na sio kuhifadhiwa, kwa mfano lugha kama haitumiki inakufa au namna nyingine yoyote ya maisha kama haitumiki inadorora na pengine hata kufa. Lakini hata hivyo, hata kama zitakufa ikiwa hazitumiki bado ni bora zikawa zimehifadhiwa endapo zitahitajika basi ziweze kuwa zinapatikana na zinaweza kutumika, jambo ambalo bado litasaidia sana.

Skyline of downtown Seoul, South Korea from bongeunsa temple

– Kuhifadhiwa kwa tamaduni na desturi kuna njia nyingi ambapo baada ya ile ya kuziishi inafuata njia ya maandishi, kisha simulizi, sanaa mbalimbali kama vile nyimbo maigizo n.k., Kwa kiasi bado kuna tamaduni ambazo tunaweza kuendelea kuziishi hata sasa kama vile taratibu mbalimbali za kwenye maisha kama vile lugha, mavazi, vyakula, vinywaji, taratibu za ndoa, maadhimisho ya sherehe muhimu n.k. Kisha kuna zile ambazo tunaweza kuzihifadhi kwenye maandishi kama vile historia na maandiko mengine ya kuelezea mambo mbalimbali. Halafu kuna kuhifadhi katika sanaa mbalimbali muhimu kama vile nyimbo, sinema, misemo na uchoraji, uchongaji n.k.,

– Kwa namna hii tunaweza kuendelea kutetea tamaduni ambazo zinaweza kuwa na nafasi ya kukua na kuendelea kurudi katika uhai wake kadiri siku zinavyokwenda mbele zaidi.

Karibu kwa Maoni.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *