TUANDIKE KUHUSU KOO ZETU.

Wachagga ni jamii yenye watu wengi sana na ni moja kati ya makabila/jamii kubwa na maarufu sana Afrika mashariki na Afrika kwa ujumla. Kupitia Fasihi/Literature wachagga ni kati ya makabila maarufu sana Afrika. Na kabla ya uhuru wa Tanganyika wachagga walikuwa ni kati ya jamii chache zilizokuwa zinaongoza kwa maendeleo makubwa sana sio tu kwa Afrika bali katika nchi zote zilizokuwa makoloni ya Wazungu Afrika na Asia.

Kwa idadi ya watu(population) wachagga ni wengi sana pia. Japo imekuwa inaaminika kupitia takwimu za zamani sana kwamba wachagga ni kabila la tatu kwa watu wengi Tanzania lakini taarifa hii ni ya kutia mashaka. Kwa sababu kwanza serikali ya Tanzania tangu zamani kwa sababu za kisiasa iliamua kutohesabu idadi ya watu kwa kigezo cha dini au kabila. Jambo hili limesababisha kukosekana kwa takwimu sahihi za ndani za idadi ya watu wa jamii husika na hivyo kukosekana kwa takwimu za uhakika za watu hao.

Naamini kwamba kikwazo hiki cha kukosekana kwa takwimu sahihi za idaidi ya watu kutokana na takwimu husika kina madhara yake kwa namna mbalimbali kuanzia kwenye wizara ya mambo ya tamaduni, utalii na hata biashara hususan suala la masoko. Lakini jambo la pili ni kwamba inaposemekana kwamba wachagga ni kabila la tatu kwa watu wengi Tanzania hakuna taarifa kuhusu kabila /jamii ya watu wengi Tanzania ni ipi. Nimejaribu kufanya utafiti hasa kufuatilia takwimu za mashirika ya kimataifa kuhusu jamii zote kubwa Tanzania na hakuna jamii iliyopo namba mbili kwa watu wengi Tanzania.

Hivyo kwa tawimu za mwaka 2021 kutoka kwenye mashirika ya kimataifa idadi ya wachagga inakadiriwa kuwa ni watu 6,800,000. Kwa idadi hii wachagga ni kabila/jamii ya pili kwa watu wengi Tanzania na moja kati ya jamii 5 zenye idadi kubwa ya watu kwa nchi mbili za Tanzania na Kenya.

Hivyo sasa kwa idadi hii kubwa sana ya watu ambayo ni zaidi ya 10% ya WaTanzania wote wachagga pia wana idadi kubwa sana ya koo. Kwa utafiti uliofanywa na Sir Charles Dundas peke yake katika miaka ya 1920’s aliweza kugundua koo zaidi ya 400 za kichagga kwa Uchaggani kote. Hivyo idadi ya koo za wachagga ni kubwa sana pengine zaidi hata ya 500 na kila moja ina taratibu zake tofauti na historia tofauti.

Kwa maana hiyo kazi ya kutafiti mambo mbalimbali ya kuhusu koo ambayo kiuhalisia ni mengi sana ni muhimu sana yafanyike na watu wa ukoo husika ili kurahisha zoezi hilo sambamba taarifa sahihi na zilizotoka kwa watu wenye kuaminika. Taarifa za kuhusu koo za kichagga kuanzia historia zake mpaka taratibu mbalimbali za koo husika ikiwa ni pamoja na matukio yanayofanywa na koo hizo mpaka sasa yatasaidia kuongeza uelewa mpana sana wa jamii ya wachagga na hata kuongeza mambo mengi kwenye stoo ya fasihi andishi ya mambo ya wachagga.

Watu wengi sana wanatamani kufahamu mambo mengi kuhusu koo zao lakini kutafiti kutoka kwa wazee na watu wengine wa koo husika ni mwanzo mzuri wa kuanzia kwenye utafiti wa jumla kuhusu koo. Koo za wachagga zinapatikana maeneo mbalimbali uchaggani ambapo kuna zile kubwa ambazo zinapatikana kila mahali uchaggani. Kufanya tafiti za koo hizi kutasaidia kufahamu hata tawi la kwanza lilianzia wapi na taratibu za koo husika zikoje.

Kupitia taarifa zitakazopatikana kutoka kwenye koo tutaweza kupata mawazo mengi bora ya namna tunaweza kuimarisha taratibu mbalimbali za jamii yetu ya wachagga. Taarifa za koo zitasaidia pia kuzileta koo pamoja na ndugu kujenga mshikamano zaidi.

Kwa mfano nilikutana na binti aliyetokea kwenye ukoo wa Mbuya wa Mamba, Komakundi ambaye ameolewa kwenye ukoo wa Makyao wa Mamba, Kokirie akanieleza namna ukoo wa Makyao huendesha mambo yao na mikutano ya mwaka ya ukoo ambapo matawi ya ukoo wote wa Makyao waliopo Vunjo, Rombo na maeneo mengine hukutana. Kwa kweli utaratibu wao huo unavutia sana na kuhamasisha sana maendeleo ya ukoo husika na muhimu zaidi unawaweka ndugu karibu na kuwafanya kuwajibika kwa maazimio mbalimbali wanayowekeana.

Hivyo basi napenda kusisitiza kwamba kila mtu afanye utafiti na kuandika kuhusu mambo mbalimbali ya ukoo husika kuanzia taratibu za ukoo huo za zamani mpaka sasa, historia za ukoo huo zinazojulikana kutoka kwa wazee na watu wengine wenye uelewa pamoja na matukio mbalimbali yanayoendelea ya ukoo husika kwa sasa. Kama wahusika watatoa ruhusu taarifa hizi tutazihifadhi kwenye tovuti/website ya www.wachagga.com ambayo itajumuisha mpaka matawi ya ukoo na familia zao family tree kwa ajili ya sisi wachagga kupata maarifa sahihi kuhusu sisi wenyewe na kupata mawazo bora zaidi ya namna ya kuweka taratibu za kuboresha koo zetu.

Kwa mtu yeyote mwenye taarifa za ukoo wake kuanzia historia na taratibu zake nyingine anaweza kuweka hapa kwenye forum ili kuelemisha ndugu zake na hata kupata mawazo zaidi kutoka kwa ndugu zake au matawi mengine ya ukoo yaliyopo maeneo mengine ya Uchaggani.

Karibuni kwa Maoni, Ushauri na Ziada.

You may also like...

Popular Posts

4 Comments

  1. Peter M Mashingia says:

    Hongera sana kwa juhudi hizi.
    Ni njia gani inatumika kutuma na kuhuisha taarifa nyingine ambazo hazipo katika jukwaa hili?

    1. Tuma taarifa inbox ya facebook akaunti ya “Urithi Wetu Wachagga”.

  2. NAOMBA MAKALA YA UKOO WA MSAKI, SAMKI, ASSEY, KESSY, TESHA , SHEWIO,SHAYO,URASSA,TEMU,MATEMU,NYANGE,MAFOLE,

    1. Sawa, Mafole wa wapi?

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *