WENGINE WATAJISIKIAJE/WATATUCHUKULIAJE/WATATUONAJE?

– Sisi binadamu kwa asili ni viumbe wa kijamii, yaani ni viumbe ambao tuko kwenye jamii ambazo kwa namna moja au nyingine zina ushawishi fulani kwenye maamuzi yetu binafsi tunayofanya.

– Asili hii ya kuwa ndani ya ushawishi wa kijamii imepelekea kwamba huwa tunatamani kila tunalofanya liwe linakubalika kwanza na kila mtu au watu fulani wawe wanalikubali ndio tupate ujasiri wa kulifanya, bila kujali hata kama jambo lenyewe lina maslahi kwa watu au manufaa kwako binafsi. Kwa sehemu kubwa huu ndio umekuwa msukumo mkubwa sana wa mambo tunayofanya na tusiofanya katika maisha. Tunafikiria kwanza watu watasemaje au kutuonaje.

– Hata hivyo licha ya kwamba asili hii iko katika saikolojia ya kijamii ya binadamu (social psychology), lakini ni udhaifu mkubwa kuifuata katika zama ambazo umuhimu wake umepitwa na wakati.

– Kwa sababu endapo watu watashindwa kufanya mambo muhimu kwao, na zaidi mambo ambayo ndio wanayoyapenda wao kutoka moyoni, kwa kuhofia kwamba wengine watawaonaje au kuwachukuliaje basi jamii nzima au nchi nzima itabaki kuwa duni na iliyodumaa kutokana na watu kuoneana aibu. Ni jambo la kijasiri sana pale mtu anapoachana na hofu ya kuhusu wengine watanionaje na kuchukua hatua ya kufanya jambo lenye manufaa kwake binafsi au kwa jamii yake.

– Tukija kwenye ngazi ya mtu mmoja mmoja tunajua kwamba watu wengi wameacha/wanaacha kufanya mambo muhimu kwao na kwa maisha yao kwa kukaa na hofu hii kwamba wengine watanichukuliaje. Tabia hii ambayo inasababishwa na kukosa ujasiri imekuwa ni moja ya sababu inayowakwamisha watu kufanya mambo muhimu kwao na kwa maisha yao.

– Kama ilivyo kwamba hupaswi kuacha kufanya mambo muhimu na ya kimaendeleo kwako binafsi kwa kuhofu watu watakuchukuliaje, kadhalika hupaswi kuogopa kufanya mambo yanayoiongezea hadhi jamii yako ambayo nayo inakuongeza hadhi na heshima wewe mwenyewe kwa kuogopa watu wengine watakuchukuliaje.

– Kwa sababu jambo la muhimu tunalopaswa kufahamu ni kwamba hakuna mtu wa kukusemea wewe au jamii yako atakayezungumza kwa kukutendea haki zaidi ya wewe mwenyewe. Ukisubiri watu wakusemee kuna uwezekano mkubwa wakakusemea kwa ubaya au wasiseme kwa namna ambayo ungependa wewe isemwe. Ukweli ni kwamba huwa hatufurahii tukisemwa vibaya, lakini ajabu ni kwamba bado tunataka watu ambao hawana mtazamo chanya na sisi watusemee badala ya kujisemea wenyewe. Mwisho wa siku kwa sehemu kubwa aidha wanatupuuza au kutusema vibaya au kwa namna isiyotamanika.

– Tunapaswa kuchukua hatua bila kujionea aibu kwa namna yoyote kujizungumzia wenyewe kwa namna ambayo tungependa izungumzwe na kusukuma agenda ambazo zinatuongezea hadhi na thamani mbele ya watu wa jamii zote za dunia. Tunafanya yote haya kwa faida yetu wenyewe kwani kwa kusukuma mbele agenda zinazotuzungumzia kwa mtazamo chanya inasaidia kutuweka kwenye nafasi nzuri ya kuheshimiwa na kuaminiwa zaidi. Mwisho wa siku hili ni faida kwetu sote kama jamii kwa ujumla.

– Sifa sahihi tunazoruhusu ziende nje ndizo zinazosababisha tuchukuliwe vile tunavyochukuliwa au tutakavyochukuliwa. Hata chuki unayoweza kuiona kutoka kwa watu wa jamii nyingine ni kwa sababu ya namna baadhi ya watu waliamua kusambaza sifa zetu kwa wengine na matokeo yake huwa tunayaona wenyewe. Hivyo jambo hili ni jambo la muhimu kwetu kulizingatia kwa sababu namna wengine wanatuhubiri inachangia hata kutuongezea au kutupunguzia kujiamini katika kukabiliana na changamoto mbalimbali kwenye maisha.

– Hivyo kuogopa kufanya mambo yenu ambayo yanaiongezea hadhi jamii yenu ni udhaifu mkubwa na tafsiri yake ni kwamba umeamua/mmeamua kujiweka chini ya watu hao, kujiweka chini ya maoni yao na kuogopa kufanya mambo ambayo yana maslahi kwako na kizazi chako kwa kuogopa maneno ya watu wasiohusiana na jambo lako hilo.

– Hiyo haijalishi kwamba watu hao unaowaogopa ni nani, anaweza kuwa ni mchumba wako, mwenzi wako, mchungaji wako, mwalimu wako, mentor wako. Kujiweka chini yake kwa kuepuka kufanya mambo yenye manufaa kwako kwa kuogopa kwamba yatafanya asijisikie vizuri wakati ni kwa gharama ya kujidumaza wewe mwenyewe, ni kushindwa kujithamini na kujiheshimu, na ni udhaifu mkubwa kihisia.

– Mtu imara na asiye na udhaifu wa kihisia ndani yake huishi kwa ujasiri kwa namna inayompendeza ndani yake mwenyewe, bila kujali wengine watamuonaje, hasa inapokuwa ni kwa gharama ya kujidumaza yeye binafsi.

– Ni kweli kwamba huenda baadhi ya watu hawatafurahia baadhi ya maamuzi yako, lakini hilo wewe halikuhusu wala halipaswi kukusumbua kwa sababu huishi ili kuwafurahisha wengine bali unaishi kwa ajili yako mwenyewe ilimradi tu hujaingilia uhuru wa wengine. Hata hivyo watu wengi unaohofia kwamba watakuchukuliaje au kukuchukia wala hawatajali sana na wengine watakufurahia na kukuchukulia kwa mtazamo chanya. Lakini licha ya kwamba watakuwepo watakaochukulia kwa mtazamo hasi bado hilo halipaswi kukusumbua kwa namna yoyote ile wala kukuzuia wewe kuishi au kufanya yale unayotaka wewe kwa uhuru kabisa.

– Hivyo tunavyoamua kufanya mambo yetu kwa msimamo, mwisho wa siku watu watatuzoea na hata baadaye wengi watatupenda pia kama tutakuwa na msimamo. Watajua ndivyo tulivyo na hakuna namna ya kutubadilisha zaidi ya kutupenda kama tulivyo kwa sababu hata hivyo hakuna mtu tuliyemkosea chochote.

– Kama unahofia kwamba kwa kuchukua hatua fulani inayokuongezea hadhi au kuiongezea hadhi jamii yako watu wengine watakuchukia, unapaswa kujua kwamba wale wa kukuchukia tayari wanakuchukia kwa sababu tu ya kwamba unatokea kwenye jamii hiyo, lakini hakuna chochote kilichoharibika mpaka sasa kwa wao kukuchukia, hivyo hakuna haja ya kukaa na hofu isiyo na mashiko. Lakini pia mtu asiyependa maendeleo yako sidhani kama unapaswa kujali kuhusu kutaka kumfurahisha kwani huyo ni kama adui yako, na sidhani kama kuna mtu mwenye akili timamu ambaye hujihangaisha kuishi kwa namna ya kumfurahisha adui yake.

– Hivyo tufanye mambo yetu kwa uhuru bila kukaa kuhofia wengine wanatuchukuliaje. Kama watu wanachukia wachagga watakuchukia tu kwa sababu wewe tayari ni mchagga na hakuna namna unaweza kubadilisha hilo ili kumfurahisha. Moja kati ya mambo yanayorudisha nyuma watu na jamii kwa ujumla ni hofu ya kuogopa maoni ya watu wengine juu ya maamuzi yake.

– Kuna daktari mmoja huko Marekani aliyekuwa anahudumia watu wenye matatizo ya akili alisema amekutana na watu wengi aliowahudumia ambao wana tatizo la kisaikolojia la kutojali maoni ya watu wengine juu yao, ambao wamejenga ushawishi mkubwa kwa watu na wamepata mafanikio makubwa kwenye maisha yao kwa kuwa na tatizo hilo. Huyo daktari akawa anashauri watu wa kawaida wadhibiti hofu hiyo ya kujali kuhusu wengine wanawachukuliaje na wataweza kujenga ushawishi mkubwa na kufanya mambo makubwa sana kwenye maisha yao.

NOTE: Tabia ya kufikiria wengine watakuchukuliaje kijamii ni tabia ya binadamu iliyotokea kwenye “evolutionary psychology” ambayo ilikuwa ina umuhimu mkubwa sana zamani sana(prehistoric times) katika maisha ya binadamu, katika nyakati ambazo mazingira yalilazimu hilo lakini kwa sasa haina maana tena, ni jambo lililopitwa na wakati lakini ambalo bado liko ndani ya saikolojia ya binadamu.

Ahsanteni.

Karibu kwa maoni au maswali.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *