MZEE WA MWISHO ALIYEBAKI.

MZEE WA MWISHO ALIYEBAKI.

– Mzee Pauli Shirima maarufu kama Mzee Lekramu mwenye umri wa miaka 95 anaishi katika kijiji cha Ngaseni, Usseri, Rombo. Mzee huyu Pauli Shirima akiwa na mke wake Masilayo ndiye Mzee wa mwisho uchaggani aliyebaki ambaye anaweza kuongea lugha ya Kingassa kwa ufasaha. Mzee Lekramu anaongea lugha tatu kwa ufasaha kabisa Kingassa, Kichagga na Kiswahili na Kiingereza kwa kiasi pia.

– Kingassa ni lugha yenye historia kubwa sana iliyodumu uchaggani kwa takribani miaka 1,500 mpaka sasa. Lugha hii ilikuwa ikiongelewa na jamii ilichanganyika na kutengeza jamii ya wachagga ambayo iliweza kuhesabu vizazi vingi sana vilivyopita. Ilikuwa ni jamii ya watu hodari sana katika vita na mapambano ambao walikuwa wakiogopwa hata na wamasai waliotokea upande wa mashariki ya Kilimanjaro katika maeneo ya Liotoktok upande wa Kenya ambao walikuwa mashuhuri sana kwa umwamba wao katika vita.

– Baadhi ya watu wamekuwa wakifikiri kwamba lugha hii asili iliyodumu Kilimanjaro kwa takriban miaka 1,500 au zaidi bado ipo, lakini watafiti wengi wanaojaribu kutembelea Kilimanjaro wanagundua kwamba lugha hii haipo tena na hakuna mchagga yeyote kwa sasa anayeweza kuizunguma. Lakini katika utafiti tuliokuwa tunajaribu kufanya tumeweza kugundua kwamba yuko Mzee mmoja pekee aliyebakia ambaye ndiye anayeweza kuizungumza lugha hii kwa ufasaha kabisa.

– Katika kuitembelea Ngasseni na kuhoji wazee mbalimbali hakuna hata mzee mmoja aliyebakia anayefahamu lugha hii na wazee wote walikuwa wakituambia inabidi kuonana na Mzee Lekramu kwani ndiye mkongwe anayefahamu mambo mengi. Tukakutana na Mzee Lekramu ambaye licha ya umri mkubwa alionao wa miaka 95 sasa bado ni Mzee mwenye nguvu sana, mwenye akili sana na mwenye kumbukumbu nyingi sana za zamani.

– Mzee Pauli Shirima au Mzee Lekramu ukiachilia mbali uwezo wake wa kuongea lugha hii kwa ufasaha kabisa lakini pia ana kumbukumbu ya mambo mengi ya zamani sana yaliyotokea akiwemo na hata ambayo alihadithiwa wakati akiwa mtoto. Katika kuzunguka Ngasseni na Usseri kwa ujumla hatujaweza kupata Mzee yeyote mwenye kumbukumbu ya Mangi Nambua mtoto wa Mangi Malamia wa Usseri, Rombo aliyepelekwa kutawala Ngasseni kipindi cha wajerumani kwa ushawishi wa Mangi Ndegoro Marealle wa Marangu.

– Wazee wote wa Ngasseni wanaamini kwamba Ngasseni ni sehemu ya Usseri ambayo haijawahi kuwa na mtawala wake bali imekuwa chini ya himaya ya umangi Usseri kwa miaka yote. Japo ni kweli kwamba Ngasseni imekuwa sehemu ya Usseri kwa miaka yote pengine tangu karne ya 18 au hata kabla lakini katika muongo wa mwisho wa karne ya 19 katika miaka ya 1890’s Ngasseni ilitengwa na Usseri na kuwa na utawala wake yenyewe. Hili lilikuja kwa ushawishi wa Mangi Ndegoruo Marealle wa Marangu ambaye alikuwa anaiogopa sana Usseri iliyokuwa chini ya utawala wa Mangi Matolo kwa wakati huo ambayo ilikuwa na nguvu sana kijeshi na kiuchumi hivyo katika mikakati ya kuidhoofisha akashawishi Ngasseni kuondolewa katika himaya ya umangi Usseri. Hii ni kwa sababu pia askari wapiganaji hodari sana wa himaya ya umangi Usseri walikuwa wanatokea Ngasseni na walichangia kuiwezesha Usseri kuwa himaya imara sana na yenye nguvu kubwa kijeshi.

– Hivyo mwaka 1895 Ngasseni ikawa himaya inayojitegemea nje ya Usseri, japo hata hivyo mtawala aliyepelekwa kuwa Mangi wa Ngasseni alitokea kwenye familia ya umangi Usseri akiwa ni mtoto wa Mangi Malamia ndugu yake na Mangi Matolo. Mangi Matolo alichukua utawala wa Usseri kutoka kuwa mtoto wa Mangi Malamia aliyeitwa Kisuma. Hivyo Mangi Nambua wa Ngasseni naye ni mtoto wa Mangi Malamia na ndugu yake Kisuma.

– Tulishindwa kabisa kupata Mzee mwenye kumbukumbu hii ya Mangi Nambua wa Ngasseni ambayo imebaki kwenye vitabu pekee lakini Mzee Pauli Shirima(Mzee Lekramu) tumekuta ana kumbukumbu hiyo kwa usahihi kabisa na alituelekeza mpaka kwenye Ikulu yake katika kijiji cha Reha, Usseri, Rombo.

– Hivyo lugha ya kingassa yenye historia ya zaidi ya miaka 1,500 Kilimanjaro na kumbukumbu za utawala, uimara na uhodari wa Ngasseni wa maelfu ya miaka umebaki kwa Mzee Lekramu ambaye sasa ana miaka 95 na hivyo zinakwenda kufutika kabisa. Mzee huyu alituambia pia ametembelewa na wazungu mbalimbali mara kadhaa kumhoji maswali mbalimbali.

-Ni Mzee mmoja mwelewa sana, mwenye akili sana, mwenye busara, anayetoa ushirikiano mkubwa na asiye na makuu kabisa, pia ni Mzee ambaye bado ana nguvu sana na ana uwezekano wa kuendelea kuwepo kwa miaka mingi kidogo.

Karibu kwa Maoni au Maswali.

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

+255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *