UKOO WA MMARI.
– Ukoo wa Mmari ukoo mkubwa wenye historia kubwa na uliotoa watu mashuhuri katika historia ya wachagga. Kutoka kwenye historia ukoo wa Mmari huenda chimbuko lake kwa uchaggani ni Siha/Sanya ambapo wanapatikana kwa wingi sana na umewahi kuwa ukoo wenye nguvu na uliotoa watawala imara sana wa himaya ya umangi Siha/Sanya Juu.
– Hata hivyo baadhi ya waandishi wanaamini kwamba ukoo wa Mmari wana asili ya Kibosho na kwamba ndio koo za mwanzo kabisa Kibosho. Waandishi hawa wanakwenda mbali zaidi na kusema kwamba hata mimea ya migomba Kibosho ililetwa na wachagga wa ukoo wa Mmari. Lakini mashaka ya jambi hili yanatokana na kutokuwepo kwa ukoo huu Kibosho au angalau sio ukoo mkubwa unaofahamika huko Kibosho.
– Ukoo wa Mmari wako kwa wingi sana Siha/Sanya Juu na Old Moshi zaidi kuliko sehemu nyingine yoyote ya uchagga. Pengine utafiti zaidi au taarifa zaidi zinahitajika kufahamu undani wa ukoo wa Mmari na namna unavyohusishwa na ukongwe wake Kibosho.
– Huko Siha/Sanya Juu ukoo wa Mmari ulikuwa ndio ukoo unaotoa wanajeshi wapiganaji hodari zaidi katika vita na majemedari wengi mashuhuri walitokea ukoo huu wa Mmari. Hata mtawala wa kwanza mwenye nguvu na shupavu aliyeweza kuendesha vita ndani na nje ya Siha aliitwa Mangi Saiye kutoka kwenye ukoo wa Mmari. Ushupavu na msimamo wa ukoo huu wa Mmari uliendelea kudhihirika kupitia mtawala mwingine mwenye nguvu sana wa Siha aliyeitwa Mangi Ngalami ambaye alisimama imara sana dhidi ya serikali ya wajerumani kiasi kwamba alikuwa ni mmoja ya watawala wa Uchagga walionyongwa pale Old Moshi, Tsudunyi mwaka 1900 yeye pamoja na kaka yake, sambamba na Mangi Meli Mandara na Mangi Molelia wa Kibosho.
– Huko Sanya Juu ukoo wa Mmari uliendelea kuwa na nguvu sana katika eneo kubwa na kutoa watu waliopata ushawishi mkubwa kwenye kiti cha utawala kama vile Naruru, Barba na Kitika. Kwa hakika kama siasa za Siha zisingeingiliwa na siasa zenye nguvu za ushawishi kutoka nje ya Siha hususan Machame ni wazi kwamba ukoo wa Mmari ambao walikuwa na idadi kubwa sana ya watu pia wangekalia kiti cha utawala moja kwa moja na kuwapika Orio, Kileo na hata Mwandri.
– Ukoo wa Mmari unapatikana kwa wingi sana pia Old Moshi na kuna uwezekano kwamba tawi lilitokea Sanya juu na kuhamia Old Moshi au kinyume chake. Huko Old Moshi pia ukoo wa Mmari ni wakongwe na wanaoheshimika. Hata hivyo bado hatujui sana ni lini na kwa namna gani ukoo huu ulipata matawi yake. Au pengine ni kweli chimbuko lake ni Kibosho na kuna namna walisambaa maeneo mengine wakianzia Kibosho.
– Tunaomba mchango wa mawazo kutoka kwa wahusika na wengine wenye uelewa zaidi kuhusu ukoo mashuhuri wa Mmari. Pia kama kijijini kwenu kuna ukoo wa Mmari unaweza kukitaja hapa tuweze kufahamu matawi zaidi ya ukoo wa Mmari yalivyokwenda.
1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Mmari?
2. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Mmari?
3. Kama wewe ni wa ukoo wa Mmari una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu? Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani?
4. Bado mna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo huo kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?
5. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Mmari?
Karibuni sana kwa Mchango zaidi au Maswali.
Kesho tutaendelea na ukoo mwingine.
Urithi Wetu Wachagga
urithiwetuwachagga@gmail.com
Hivi ukoo wa Urio/Orio asili yake ni wapi haswa!!!
Sanya juu.
Urio/Orio, ni miongoni mwa koo za wamasai, ambao walihamia maeneo ya Olmolog mwanzoni kabisa mwa miaka ya 1700 wakitokea Kisongo-Monduli baada ya vita kali na Waarusha (La’arusai) wakiongozwa na mzee maarufu wa kimasai aliyeitwa Laibon Lenana.
Uzao huo wa Orio ni miongoni mwa jamii hiyo walioamua kuendelea mbele zaidi kuingia maeneo ya miinuko ya mlima Kilimanjaro na kujichanganya na wachaga, kwanza maeneo ya Siha ambayo ilikuwa karibu na Olmolog na wengine wakiongozwa na Yansanya Orio waliendelea mbele zaidi kukatiza mto Kikafu na kuingia maeneo ya uwanda wa chini Machame na kuweka makazi yao pembezoni mwa mto Makoa, Kimbushi. Hili eneo lilikuja kuwa maarufu sana baadaye kihistoria na kimila kwa jamii hii ya wahamiaji.
Kutokana na mgogoro walioingia na mtawala wa himaya mpya ya Machame wakati huo, aliyeitwa Ntemi, waliamua kuondoka gapo na kielekea mashariki zaidi na kuweka makazi yao eneo la tambarare liloitwa Lambongo (au Lyamungo kwa leo).
Vizazi vingi viliishi hapo Lambongo na maarufu sana wa jamii hiyo ya Urio ni Urio mwenyewe (mtoto wa Yansanya), Kimboka, Kirenga, na Kashenge ambao walikuja kuwa maarufu kwenye himaya ya upande wa pili wa mtoto Weruweru, iliyokuja kutwa Kibosho wakati wa utawala wa Mangi Sina ambaye naye ni wa uzao wa Kimboka.
Ukoo huo wa Urio umesambaa sana Siha, Kibosho (ambapo hawatumii tena Urio bali Mushi), na maeneo ya Mashariki ya Uchagani, yaani Vunjo.
Baadhi ya uzao wa Urio walioishi Siha walikuja kuhamia Arumeru na kuweka makazi yao kule.