LEO KATIKA HISTORIA – KILIMANJARO, WACHAGGA NA MLIMA KILIMANJARO.

– Siku Kama Ya Leo Ilikuwa ni Tarehe 11/May Ya Mwaka 1848, Ikiwa ni Miaka 185 Iliyopita Kufikia Siku Ya Leo, Mtu Kwanza Kutokea Nchi za Magharibi Mmisionari wa Kijerumani Johannes Rebmann Aliouona Mlima Kilimanjaro(Aliuita Mlima wa Wachagga(Mountain of the Chagga)) na Kwa Mara Ya Kwanza Mlima Kilimanjaro Ukaanza Kufahamika Kwenye Dunia Ya Magharibi na Moja Kwa Moja na Umaarufu wa Wachagga Pia Ukaanza Kuongezeka.

– Johannes Rebmann Akitokea Mombasa Kuelekea Kilimanjaro Kupitia Taita na Taveta Aliandika Kwenye Kijitabu Chake cha Kumbukumbu Diary, “Asubuhi Ya Leo Tumeukaribia “Mlima wa Wachagga” na Kuuona Kwa Karibu Sana.” Rebmann Akaendelea Kusema, “Ikiwa ni Muda wa Saa Nne Kamili Asubuhi Nimevutiwa na Kufurahi Sana Kuona Kama Wingu Jeupe Likimeremeta Angani, Muongozaji wangu Amekiita Kile Kitu Cheupe Kinachomereta “beredi(baridi)” lakini hata hivyo imekuwa bayana kabisa kwangu kwamba kitu kile cheupe nilichokiona sio kitu kingine zaidi ya “barafu”.

– Johannes Rebmann alipopeleka taarifa Ujerumani kwamba “mlima wa Wachagga” uliopo Afrika mashariki umefunikwa na barafu kwenye kilele chake alichekwa sana na jamii ya wanataaluma. Wanataaluma hao katikati ya karne ya 19 walidai kwamba haiwezekani barafu kuganda kwenye eneo lililopo karibu kabisa na mstari Ikweta achilia mbali kukaa kwa muda mrefu. Jamii ya wanataaluma waliamini kwamba Johannes Rebmann atakuwa amechanganyikiwa kwa sababu pengine aliugua malaria iliyompanda kichwani.

– Hata hivyo Johannes Rebmann licha ya kuchekwa na kusanifiwa na jamii ya wanataaluma lakini bado aliendelea kushikilia msimamo wake kwamba alichokiona kwenye kilele cha mlima Kilimanjaro sio kitu kingine zaidi ya barafu iliyoganda na kufunika kilele cha mlima huo aliouita, “Mountain of the Jagga”. Baadaye ilikuja kuwa bayana kwamba mmsionari mjerumani Johannes Rebmann alikuwa sahihi. Historia inamkumbuka kama mtu wa kwanza kupelekea taarifa kwenye dunia ya magharibi juu ya uwepo wa mlima Kilimanjaro katika eneo la Afrika mashariki.

– Kuna taarifa potofu zinazosambazwa na watu wasio na uelewa sahihi pengine kwa sababu ya ujinga au wengine kwa makusudi kwamba wachagga sio jamii moja na wala jina wachagga halikuwepo bali limekuja juzi juzi baada ya watu wa eneo kuamua kujiita wachagga wakati hawana mahusiano yoyote. Kwa leo sitaingia tena ndani kurudia kufafanua hili lakini nataka taarifa hii ya Johannes Rebmann iwafikie watu hao kwamba miaka 185 iliyopita Johannes Rebmann alikuta jamii ya watu wanaoishi Kilimanjaro ikiitwa wachagga na yeye mwenyewe akauita mlima Kilimanjaro kwa jina la “mlima wa wachagga(Mountain of the Jagga)” kwa lafudhi ya Kijerumani.

JOHANNES REBMANN ALICHOKIKUTA UCHAGGANI 1848.

Johannes alifikia katika himaya ya umangi Kilema mwaka huo wa 1848 wakati huo ikiwa chini ya utawala wa Mangi Masaki. Johannes Rebmann alivutiwa sana na utawala wa Mangi, lakini alivutiwa sana pia na urembo na umaridadi wa mavazi ya wachagga hasa urembo wa bangili na shanga kwa wanawake. Rebmann alivutiwa pia na urembo wa shanga katika mavazi na mwonekano wa tofauti wa Mangi aliyeonekana kuwa na mwonekano wa tofauti na raia wake. Yaani ile hadhi yake ya kuwa ni mtawala kwa mwonekano ilikuwa bayana. Johannes mwaka uliofuata alitembelea pia Machame kuonana na Mangi Mamkinga.

– Hiyo ndio iliyokuwa picha ya mtazamo wa wageni kwa namna Uchagga ilivyokuwa kwa wastani wa miaka 200 iliyopita. Na leo imetimia miaka 185 tangu Johannes Rebmann kuuona mlima na kuwa mtu wa kwanza kuifungulia dunia ya magharibi kwa wachagga, Kilimanjaro.

Karibu kwa Maoni au Maswali.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *