UCHAMBUZI WA KITABU. – SEHEMU YA 9.

*Maisha Ya Mchagga Hapa Duniani Na Ahera” By Mangi Petro Itosi Marealle*

Uchambuzi by Mary Assenga.

IMANI YA WACHAGGA.

“RUWA”

-Wachagga huamini “Ruwa”(Mungu) kwamba ni Mkuu kupita mizimu yote wanayotambikia. Huyu Ruwa hasumbui wanadamu kwa sababu ndogondogo kama vile mizimu iwasumbuavyo ikiwa haikutambikiwa. Tambiko alilotolewa Ruwa ni tofauti na tambiko la mizimu kwa hali na sababu.

Wachagga humjua Ruwa toka kwa wakale wao. Hawa walisema kuwa wanadamu na viumbe vyote ni lipuko la Ruwa. “Walipasuka” kutoka kwake(Ruwa Mopara Wandu). Walimpa Ruwa heshima wakimtaja kwa majina haya manne yaelezayo heshima na kazi zake.

(a) “Ruwa” maana yake, aeneaye popote kama jua limulikalo ulimwenguni mwote pasiwepo kiumbe ama kitu kiwezacho kujificha

(b) “Matengera” maana yake, aleaye viumbe vyote kwa taratibu zake kwa amani.

(c) “Fumvu lya Mku” maana yake, mlima wa kale

(d) “Molunga Soka na Mndo”, maana yake ni kwamba kwa uwezo wake kila kiumbe chake chenye uhai huwa na taratibu ya kuwa mke na mume, watu wakazaliana, kama vile kuunga shoka na mundu, jambo ambalo ni gumu sana.

-Wakaamini kwamba yeye kwake ni juu “nginenyi” (kwenye jiwe kubwa la rangi ya samawati lionekanalo mbinguni). Kwa majina hayo manne Ruwa, Matengera, Fumvulya Mku, na Molunga Soka Na Mndo, ni sifa zake pekee na ndizo nguzo za imani ya Mchagga.

Wachagga wamtambikiapo Ruwa huua beberu mweusi kabisa kila mahali ama mwekundu au mweupe kabisa, asiye na doa lolote, ambaye hakukatwa mkia, kwani kwa desturi Wachagga hukata mbuzi beberu mikia kabla hawajaweza kupanda.

Huyu mbuzi huuliwa mahali palipoinuka kwenye kilele cha nyumba ya kichagga, majina yale manne ya heshima zake hutajwa na mzee mkuu wa ukoo wa huyo mgonjwa anayetambikiwa, na jamaa zake hutazama juu “nginenyi” na kuomba Ruwa amponyeshe mtu wao.

-Mzee huyu husema maneno ya namna hii: “Iyoe Ruwa Mangi Matengera, Iyoe Fumvu lya Mku, Molunga Soka na Mndo, lokuinenga ndaina yi ya ufano lopfo ili ukire mndu chu odu hoi na hoi Mangi”. Akiisha sema hivyo mbuzi huuawa. Mbuzi mwenyewe hatemewi mate kama wale wa kutambikia mizimu.

Saa za kutambikia Ruwa zilikuwa wakati jua limesimama katikati angani, yaani ni kama saa sita mchana. Ikiwa kuna mawingu basi walibahatisha tu. Wakishamchinja walikula nyama wakaenda zao. Hali kadhalika ikiwa mnyama aliyechinjwa ni ng’ombe, alitafutwa ndama mwenye rangi moja tu au ng’ombe wa miguu minane yaani ng’ombe mwenye mimba. Ruwa alitambikiwa/kutolewa sadaka ikiwa nchi ina njaa kuu au maradhi makali.

-Wachagga waliamini kwamba watu wa jamii zote walilipuka kutoka kwa Ruwa na polepole wakajaa ulimwenguni. Husema kuwa Ruwa anawapenda kwa sababu hawasumbuliwi naye kama vile wachawi na mizimu wanavyosumbua kwa kutaka gharama na tambiko za namna nyingi kila siku.

Tambiko/sadaka kwa Ruwa ni moja na hutolewa kwa sababu moja tu.

Katika imani ya wachagga hakukuwa na shetani, mapepo wala malaika.

-Lakini pamoja na yote hayo kwa sababu ya kutishwa sana na uchawi na mizimu karibu wingi wa matambiko ulitolewa kwa mizimu. Wazee waamkapo kila asubuhi walifungua nyumba wakatoka nje na kutazama upande wa kaskazini kunako mlima Kilimanjaro na kuinua kichwa wakatema mate mara nne, “Tuu, tu, tu, tu”, wakamwita Ruwa kwa majina na sifa zile nne na kumshukuru kwa uzima walioamshwa nao kwa asubuhi alfajiri tu, na ni wazee wanaume tu wenye mamlaka ya kufanya hivyo; wanawake wajane wazee pia huweza kufanya hivyo.

Hivyo ndivyo Wachagga walivyomjua Ruwa kuwa ni mkuu kupita viumbe vyote; nay a kuwa Ruwa ndiye mwenye nguvu kupita mizimu yote juu ya roho za binadamu, kwani kwake ndiko walimwengu walikolipuka wakaja kuzaliana duniani.

ITAENDELEA ……!!

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *