*Maisha Ya Mchagga Hapa Duniani Na Ahera” By Mangi Petro Itosi Marealle*
Uchambuzi by Mary Assenga.
“MIZIMU”
-Wachagga zamani waliamini na kutambikia mizimu, yaani watu wao walio marehemu. Waliamini mtu akishakufa bado alikwenda kuishi tena kule kuzimuni, lakini si kwa mwili huu tulio nao.
Wachagga walisadiki kuwa hawa mizimu hula na kunywa, na kuweza kuja tena duniani na kudai haki zao walizokuwa wakipata kwa jamaa zao. Wajapo kudai sehemu zao kwa jamaa zao walikuwa wakija wakati wowote wanapotaka; lakini hawaonekani na mtu yeyote kwa sura yao bali huonekana kama katika ndoto au fahamu.
Wachagga walijua kama mtu alikuwa na maovu mengu hapa duniani, hata huko kuzimuni atapata taabu, yaani hataweza kuonana na jamaa zake na kuweza kukaa nao huko. Jamaa zake huku duniani wakifanya tambiko kwa kumuombea kwa ndugu zake wampokee na kushirikiana naye huko ahera ndipo anapopata nafasi nzuri ya kuonana na wale wamjuao na kukaa nao.
Wachagga walijua pia kuwa Wamangi wafapo walikwenda kutawala tena huko ahera kama hapa duniani. Waliamini ya kuwa ikiwa mtu analo tendo baya ambalo hakuwahi kulitengeneza akiwa hapa duniani, aendapo akafa tendo lile ovu litamfuata mpaka aombewe na jamaa zake wa hapa duniani.
Ikiwa hakuombewa kwa tambiko ili apate msamaha huko kuzimu, huyu mtu atapewa mahali pake peke yake asiweze kuonana na jamaa zake; mwishoni atapelekwa katika ahera ya tatu iitwayo “Kiragaifu”, maana yake ni ahera ya watu ambao hutokomea kabisa hata wakawa kama majivu. Jamaa walio hai hawataweza kukutambikia tena kwa kuwa tambiko la watu wa duniani haliwezi tena kuwafikia.
-Kazi ya mizimu ni kudai sehemu na taratibu zao walizokuwa wakitendewa walipokuwa hai hapa duniani. Waliombwa msamaha kwa makosa waliofanyiwa na watu wa hapa duniani, wakatakiwa pia watoe msaada kwa kuondoa maradhi waliyowaletea watu au jamaa zao hapa duniani ambapo huombwa kwa tambiko.
ITAENDELEA ….. !!!
Urithi Wetu Wachagga.
urithiwetuwachagga@gmail.com
Whatsapp +255 754 584 270.
Ni kizazi namba ngapi cha mwisho cha mizimu ambacho hakiwezi kutambikiwa. Au kinachoingia Kiragaifu?