HADITHI ZA DINI YA ASILI YA WACHAGGA KABLA YA KUJA KWA WAMISIONARI WA KIKRISTO – 2

Baada ya Ruwa/Iruwa kupotea na kutoonekana tena kiongozi mkuu wa wachagga aliamua kusali kwa kumwomba Ruwa/Iruwa kwa ajili ya asali na maziwa. Ruwa/Iruwa alisikia sala hiyo na kumtuma tena waziri wake msaidizi kwa kiongozi mkuu wa wachagga.

Ruwa/Iruwa alimtuma waziri akamwaambie kiongozi mkuu wa wachagga, “Sasa nimeamua kuwaonea huruma wewe na watu wako. Kuanzia sasa mfahamu kwamba mtaishi mpaka kufikia umri wa uzee, na hata mtakapofikia kufa mtajivua magamba/ngozi kama vile afanyavyo nyoka na kisha kurudi tena katika ujana. Lakini haipaswi mtu yeyote akuone wakati unajivua ngozi hiyo, unatakiwa kuwa mwenyewe wakati unafanya hivyo mtu yeyote asipate kukuona. Ikiwa mtoto wako au mjukuu wako atakuona wakati unajivua ngozi hiyo, utakufa wakati huo huo na hutaweza kuokolewa tena”. Kuanzia hapo wachagga walianza kuishi mpaka kufikia umri wa uzee sana. Kutokana na umri mkubwa sana wa uzee watoto wao waliamua kuwapa wazazi wajukuu wao kwa ajili ya kuwalea na kuwatunza katika umri wa uzee.

Muda ulifika ambapo mzee alipaswa kujivua ngozi kwa ajili ya kurudia tena ujana baada ya Ruwa/Iruwa kumtuma waziri wake amjulishe kwamba wakati wake wa kujivua ngozi umefika. Mzee wa kichagga alifikiria namna ya kumwondoa na kumweka mbali binti mdogo ambaye ni mjukuu wake aliyekuwa anaishi naye ili aweze kufanya zoezi hilo bila kuonekana na mtu.

Mzee alimwagiza mjukuu wake kuleta bilauri kwa ajili ya kwenda kumletea maji. Binti alileta ile bilauri kwa babu yake ambaye alichukua sindano kubwa na kuitoboa toboa vitundu kwa chini kisha kumpa mjukuu wake na kumwagiza akamchukulie nayo maji. Mzee huyu babu yake alijua kwamba huyu binti mjukuu wake hawezi kurudi haraka kwa sababu ameitoboa sana kwa chini bilauri ile ya mbao iliyotengenezwa kutoka kwenye boga kubwa, hivyo maji yatavuja na atapata taabu sana kuijaza.

Binti alikimbia haraka kwenda kuteka maji, lakini baada ya kujaza aliona maji yanavuja na ndani ya dakika chache sana yalivuja yote kwa haraka na kuisha kabisa kwenye bilauri hiyo. Hivyo binti akaanza kazi ya kuziba yale matobo yote haraka haraka na kumaliza. Kisha akajaza upya maji katika bilauri hiyo na kumaliza, akajitwisha kichwani na kuanza safari ya kurudi nyumbani kwa babu yake kumpelekea maji aliyoagizwa.

Binti alipofika nyumbani na kuingia ndani alipigwa na butwaa kwa sababu alimkuta babu yake ameshajivua nusu ya ngozi yake huku akiendelea na zoezi hilo. Babu yake alimwangalia kwa kustaajabu na kisha kupiga kelele kwa nguvu, “Acha iwe hivyo, sasa nakufa, nyie wote mtakufa, nimekufa, na nyie wote lazima mtakufa. Kwa kuwa wewe mjukuu wangu umeingia ndani wakati najivua ngozi. Ole wangu, ole wenu!”

Baada ya hapo Mzee alimalizia kujivua ngozi yake yote na kisha kufariki. Watoto wake na wajukuu wake wote wakaja kukusanyika nyumbani kwake na kumfanyia mazishi. Kisha wakamfukuza yule mjukuu aliyesababisha babu yao kufariki ambapo alikimbilia msituni.

Baadaye binti yule alikuja kuolewa na kuzaa watoto lakini hawakuwa watoto waliofanana na binadamu. Binti yule alikuja kuzaa watoto wenye miguu minne na mkia. Na watoto wake hao ndio wamekuja kuwa kizazi cha nyani, sokwe, mbega na wanyama wengine wa jamii ya nyani. Hivyo nyani, sokwe na wanyama wa jamii ya nyani ni watoto wa yule binti ambaye alimdhalilisha babu yake. Kwa maana hii wachagga walikuwa wanawatambua sokwe na nyani kama watu wa msituni na waliwatambua zaidi kama “watoto waliolaaniwa”.

Sasa baada ya babu yao aliyekuwa Mzee sana kufariki mtoto wake wa kwanza alikuwa na vijana wawili wakubwa wa kiume. Baba yao aliwapa wote wawili urithi wa mbuzi kila mmoja za kwake. Hivyo kila siku watoto hawa walienda msituni kwa ajili ya kukata majani ya kuja kuwalisha mbuzi wao waliopewa na baba yao.Kisha mbuzi wa yule mdogo mtu alikuwa akizaa mapacha kila wakati, huku mbuzi wa kaka mkubwa akizaa kitoto kimoja peke yake. Kaka mkubwa alipata wivu na kukasirika sana na kisha kumwambia baba yao kwamba anahitaji awabadilishie mbuzi hao, yeye achukue mbuzi za mdogo wake na mdogo mtu achukue zile za kaka yake.

Baba yao alikataa na kumwambia, “sio vizuri kumnyang’anya mdogo wako mbuzi zake”, badala yake wewe nawe lisha mbuzi zako vizuri nazo zitazaa mapacha pia. Lakini kaka mkubwa hakuridhika na majibu haya ya baba yao.Asubuhi iliyofuata wote yeye na mdogo wake walichukua mapanga yao na kuelekea porini kwa ajili ya kukata majani kwa ajili ya kulishia mifugo yao kama ilivyokuwa desturi yao. Walipokuwa katikati ya msitu wakati wakikata majani kaka mkubwa aliamua kumshambulia mdogo wake kwa mapanga na kumuua.

Wakati anauawa kaka mdogo alilia kwa uchungu na kwa maumivu makala kiasi kwamba waziri wa Ruwa alisikia sauti ya kilio cha mtu anayekufa. Waziri wa Ruwa alipofika eneo hilo alikuta kaka mdogo tayari ameshafariki. Hivyo waziri wa Ruwa alikimbia mara moja kumfikishia habari hizo Ruwa.

Kisha Ruwa/Iruwa alimwagiza waziri huyo kwenda kwa kaka mkubwa kumjulisha yanayompasa. Halafu mtoze faini ya ng’ombe saba, mbuzi saba na binti mmoja. Mali hizi utampa baba yake azitumie na binti huyo atafanya kazi kwa mama yake mpaka atakapofariki. Waziri wa Ruwa alifanya kama alivyoagizwa, ambapo alimtoza faini muuaji huyu ya ng’ombe saba, mbuzi saba na binti mmoja na kisha kumkabidhi baba yao. Baba yao alimpokea mali zote hizi japo akiwa katika huzuni na masikitiko makubwa.

Na kuanzia siku hiyo adhabu ya kuua kwa wachagga ilikuwa inalipwa kwa gharama hiyo. Kumwaga damu ya mtu kwa wachagga ilikuwa inalipwa kwa gharama ya ng’ombe saba, mbuzi sana na mtoto mdogo mmoja.

Ahsanteni.

Kesho tutaendelea na hadithi ya namna Ruwa alivyoiangamiza dunia.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *