HADITHI INAYODHIHIRISHA UKUU WA “RUWA/IRUWA” KWA WACHAGGA.

Zamani katika miaka ya mwishoni mwa karne ya 18 au miaka ya 1790’s kulikuwa na watawala wawili wenye nguvu sana mashariki ya Kilimanjaro. Watawala hawa walikuwa ni Mangi Horombo wa Keni na Mangi Rongoma wa Kilema. Mangi Horombo wa Keni, Rombo akitawala kuanzia kuanzia Mriti/Mamsera mpaka Usseri na Ngasseni upande wa mashariki zaidi huku Mangi Rongoma wa Kilema akitawala kuanzia Kirua Vunjo mpaka Mwika. Hata hivyo baadaye baada ya Mangi Rongoma kufariki Mangi Horombo alikuja kuwa na nguvu zaidi na kutawala kuanzia Kirua Vunjo mpaka Usseri na Ngasseni yaani Vunjo na Rombo yote.

Sasa katika nyakati za utawala na umashuhuri wa Mangi Rongoma kulikuwa na viongozi wawili mashuhuri Kilema, mmoja alikuwa ndiye jenerali mkuu wa majeshi ya Mangi Rongoma na mwingine alikuwa ndiye kama waziri wa fedha wa Mangi Rongoma, ambaye alikuwa anahusika na mambo yote ya ugavi au kununua mahitaji yote muhimu.

Siku moja watu hawa wawili walienda nyumbani kwa kiongozi mwingine mashuhuri huko Kilema ambaye alikuwa ameandaa karamu ndogo iliyokuwa na mbege nyingi. Viongozi hawa wawili waliokuwa mashuhuri Kilema walipewa pombe nyingi wakanywa na kulewa sana. Kisha walianza kuingia kwenye ubishani na mashindano baada ya huyu waziri wa fedha wa Kilema kumtukuza sana Mangi Rongoma.

Kisha jenerali mkuu wa majeshi ya Mangi Rongoma akasema kati ya Ruwa na Mangi Rongoma, Ruwa ndiye mkuu zaidi. Waziri wa fedha wa Kilema akashangazwa sana na maneno ya huyu jenerali mkuu wa majeshi ya Mangi Rongoma na kumwambia, “Wewe umechanganyikiwa au umeingilia na mapepo, kiasi cha kusema kwamba Ruwa ni mkuu kuliko Mangi Rongoma ambaye anatawala dunia yote? Hivi unafikiri leo hii Mangi Rongoma akiamua uuwawe unafikiri Ruwa anaweza kukuokoa kutoka kwenye mikono ya Mangi Rongoma?

Jenerali mkuu wa majeshi ya Mangi Rongoma alijibu na kusema, “Sijachanganyikiwa wala sijaingiliwa na mapepo. Nasema kile ambacho nimekiona. Mara nyingi nikiwa vitani kuna wakati naona kabisa kwamba adui amenizunguka na anakaribia kuniteka mimi na jeshi langu, basi naangalia juu mawinguni na kutema mate mara tatu nikilitaja jina la Ruwa, kisha mara moja adui anakimbia na mimi na majeshi yangu tunakuwa tumeokolewa. Sasa je, Mangi Rongoma angeweza kuniokoa katika muda ule kama alivyofanya Ruwa? Hivi si tungekamatwa siku ile na maadui na tukiwa na Mangi Rongoma mwenyewe na wote tukauawa pamoja?

Waziri wa fedha akasema; “Ndio, Mangi Rongoma angeweza kufanya hivyo kwa sababu watu wote wa dunia hii ni wa kwake.” Viongozi hawa wawili waliendelea kubishana sana mpaka kukaribia kupigana visu, lakini walizuiliwa na watu waliokuwepo katika eneo hilo. Mmoja akisema Ruwa ni mkuu kuliko Mangi Rongoma na mwingine akisema Mangi Rongoma ni mkuu kuliko Ruwa.

Mabishano yao yaliendelea kwa muda mrefu mpaka yakamfikia Mangi Rongoma mwenyewe. Mangi Rongoma aliwasikiliza na kisha akamuuliza yule aliyekuwa anamtukuza Ruwa, je bado anaendelea kudiriki kusema kwamba Ruwa ni mkuu kuliko yeye Mangi Rongoma? Yule jenerali mkuu wa majeshi ya Mangi Rongoma alitazama juu mawinguni na kutema mate mara tatu huku akilitaja jina la Ruwa. Kisha akasema, “Kweli naapa kwa jina lako na kwa jina la baba yangu aliyenizaa, Ruwa ni mkuu kuliko wewe Mangi Rongoma”.

Mangi Rongoma alipomsikia akisema hayo alikasirika sana na kutaka kumuua mara moja hapo hapo, lakini aliogopa kumuua mbele za watu na pia alikuwa ndio nguzo kuu ya majeshi yake. Lakini Mangi Rongoma alijisemea, “Acha kwanza, nitamuua kwa siri, halafu cheo chake cha ukuu wa majeshi nitampa ndugu yake, ambaye ana uwezo mkubwa sana sawa na yeye katika vita kama akipewa nafasi hiyo”.

Hivyo siku nyingi zilipita na watu wakawa wamesahau hayo mabishano na ugomvi uliotokea. Kisha Mangi Rongoma akawaita wote wawili huyo jenerali mkuu wa majeshi pamoja na yule waziri wa fedha wa Kilema kisha akawatuma wote wawili katika safari ya kuelekea Kahe. Kisha alichukua nguo za kawaida kabisa na kumpa yule waziri wa fedha kwa ajili ya safari yao ya kuelekea Kahe. Kisha Mangi Rongoma aliwaita wanajeshi wawili waliokuwa na uwezo mkubwa sana katika vita na waliokuwa na silaha imara na kuwapa zawadi ya nyama kisha kuwapa maelekezo maalum.

Mangi Rongoma aliwaagiza, “Nendeni moja kwa moja katika barabara inayoelekea Kahe kisha mkasubiri kwa chini kule kwenye tambarare pembeni ya bonde la mto Mue; kisha mkifika maeneo hayo mjifiche kuwasubiri viongozi wangu wawili ambao nimewatuma wanaelekea Kahe. Mmoja amevaa kawaida kiraia na yule mwingine amevalia mavazi yangu ya Umangi/mavazi ya kifalme ambayo mimi huwa navaa kila siku. Kisha mtamuua yule ambaye amevalia mavazi yangu ya Umangi/Kifalme. Mkikamilisha jambo hili kila mmoja wenu atapata ng’ombe mmoja.”

Hivyo wanajeshi hawa walichukua silaha zao na kuelekea njia ya Kahe kama jinsi walivyoagizwa na Mangi Rongoma. Kisha kesho yake wale viongozi wawili mkuu wa majeshi ya Mangi Rongoma na waziri wa fedha wa Kilema nao wakaondoka na kuanza safari yao ya kuelekea Kahe kama jinsi walivyokuwa wameagizwa na Mangi Rongoma. Waliendelea na safari yao mpaka walipokaribia katika tambarare za mto Mue ambapo joto lilizidi na hivyo yule aliyekuwa amevalia kifalme alitoka jasho sana kwa sababu walikuwa wamefika kwenye ukanda wa tambarare wenye joto sana.

Hivyo alivyomwambia mwenzake yule waziri wa fedha, “Ndugu yangu hebu kuwa na huruma kidogo tunadilishane mavazi kwa sababu kwa sababu nahisi joto sana ndani ya mavazi haya ambayo sijazoea kuvaa. Waziri yule wa fedha aliposikia maneno haya alifurahia kubadilishana mavazi ili naye avae mavazi ya Umangi/Kifalme kwa sababu alikuwa anamuonea sana wivu mwenzake ndani ya mavazi hayo yaliyokuwa ni alama ya utukufu mkubwa. Hivyo walibadilishana mavazi yao.

Hivyo waliendelea na safari mpaka kufika kwenye bonde katika eneo la tambarare la mto Mue. Walipoanza kuvuka mto Mue walitokea askari hao wawili na kumshambulia yule aliyekuwa amevaa mavazi ya Umangi/Kifalme kama walivyokuwa wameagizwa na kumuulia hapo hapo. Jenerali yule alishangaa sana kiasi kwamba hata alivyoulizwa na askari wale kwa nini ameshangaa hakuweza kujibu. Kisha walimwambia, “Rudi nyumbani sasa kwa Mangi wako, safari yako imeisha, kwa sababu haikuwa safari halisi, Mangi alitaka kumaliza ubishi wenu”.

Askari hao walimvua yale mavazi ya Umangi/Kifalme aliyokuwa amevaa waziri yule wa fedha baada ya kumuua na kuchukua silaha zake pia kisha kuuacha mwili wake eneo lile na kuondoka na wote watatu walirudi kwa Mangi Rongoma kurudisha habari hizo. Siku hiyo Mangi Rongoma alishangazwa na kulia; “Ole wangu, ole wa mtumishi wangu, ole wa kijana wangu, mlinzi wa hazina zangu.” Kisha akawafokea askari wale wawili, kwa kusema; “Mmekosea sana, mtu niliyewaagiza mmuue ni huyu hapa, sio yule waziri wangu wa fedha.”

Askari wale wakamjibu; “Sisi hatujaangalia kushoto wala kulia, tumefanya kama ulivyotuagiza.” Hivyo Mangi Rongoma akamuuliza yule jenerali wake mkuu wa majeshi, “Imekuaje mpaka ukaponea chupu chupu?” Jenerali yule mkuu wa vita akamwelezea safari yote kuhusiana na safari yao na namna kulivyokuwa na joto kali kwenye tambarare.

Kisha yule jenerali mkuu wa Mangi Rongoma akamuuliza Rongoma, “Kwa hiyo ulitaka kuniua? Nimekukosea nini?”. Mangi Rongoma akamjibu; “Nilitaka kukuua kwa sababu ulimtukuza zaidi Ruwa kuliko mimi siku ile mlivyobishana sana na waziri wangu wa fedha.” Lakini leo nimeona kwamba Ruwa ni mkuu kuliko mimi. Siwezi kusahau tukio hili kubwa sana.”

Kisha Mangi Rongoma aliita watu wote, viongozi, watu mashuhuri na matajiri wote, wazee na askari wote wa majeshi. Kisha aliwaeleza watu wote mambo hayo yaliyotokea na kuwaonyesha mkuu wake wa majeshi ya vita kama mfano na shahidi wa Ruwa. Hivyo watu wote walishangaa sana na kutazama juu mawinguni, na kisha kutema mate mara tatu na kusema kwa sauti moja wote; “Ruwa ni mkuu kuliko Mangi.”

Cambridge-Trained African Chief — Chief Thomas Marealle of the Chagga Tribe: The traditional Chagga horn which saluted the new chief during during the ceremony. January 28, 1955. (Photo by Central Office of Information Photograph).

Kisha Mangi Rongoma aliwapa watu ng’ombe nyingi na mbuzi na kondoo wengi na walimtolea Ruwa sadaka nyingi wakati wa mchana.

Hiyo ni moja kati ya hadithi za namna wachagga katika karne za zamani walikuwa wanauelezea ukuu wa Ruwa.

Ahsanteni.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *