UCHUMBA MPAKA NDOA KWA WACHAGGA.

1. UCHUMBA.

– Tofauti na jamii nyingi za kiafrika zilivyokuwa zinafanya na mitazamo mingi potofu inayoaminika kwa wachagga ndoa haikuwahi kuwa suala la kumuuza mwanamke wala mwanamke hakuwa mali binafsi ya mume wake. Kutoka kwenye kitabu cha Mangi Petro Itosi Marealle, “Maisha ya Mchagga Hapa Duniani na Ahera” anasema kwa wachagga mwanaume hakuwa na uhalali wa kisheria kwa mujibu wa sheria za wachagga wa kumpiga mke wake isipokuwa tu kwa kosa la kuchepuka au kuonyesha dharau japo hata hivyo sio kwamba mara zote hili lilizingatiwa.

– Katika kuoa kijana wa kichagga hakuweza kupuuzia tabia za binti aliyekuwa anakwenda kumuoa, jambo hili lilipewa kipaumbele kikubwa kwani madhara yake makubwa mbeleni yalijulikana ikiwemo kuvunjika kwa ndoa ambako kulitambulika na sheria za nchi ya wachagga.

– Hata hivyo kwa wachagga wazazi walikuwa na ushawishi mkubwa juu ya ndoa za watoto wao na hivyo kuna ndoa nyingi zilifungwa kwa ushawishi wa wazazi hasa katika kujenga ushirika au muunganiko na familia walizochagua wenyewe. Lakini pamoja na hayo hili halikupelekea wazazi hususan baba wa kichagga kumlazimisha mtoto wake kuolewa kule alikotaka yeye kwani binti naye alipewa uhuru mkubwa wa kuamua kama yuko tayari kuolewa huko au hayuko tayari. Lakini wamama wao mara nyingi waliweza kutumia ushawishi wao kwa siri kujaribu kuunganisha uchumba wa binti yake na kijana fulani bila kujulikana kama amehusika au kutaka uhusika wake kujulikana.

– Lakini licha ya kwamba wakati mwingine binti alihimizwa na kushawishiwa sana na wazazi wake kuingia kwenye ndoa na kijana fulani, kijana huyo alipaswa kujiridhisha kwamba kweli binti ameridhia kwa moyo mmoja kuingia naye kwenye ndoa hiyo. Kijana wa kichagga wakati mwingine aliweza kufanya hilo peke yake lakini mara nyingi alimtuma mama yake au dada yake kwa binti kujihakikishia kwamba amekubali na kuridhia kuingia naye kwenye ndoa. Baada ya kujihakikishia hilo kijana aliomba ruhusa kwa wazazi wa binti kwa ajili ya kutangaza uchumba wake na binti yao.

– Uchumba ulikuwa rasmi na kujulikana na watu wote baada ya binti akisindikizwa na kundi la marafiki zake kutembelea nyumbani kwa kijana wa kichagga ambaye sasa amekuwa mchumba wake rasmi. Kijana aliwapokea katika nyumba yake au nyumba ya wazazi wake ambao waliondoka na kuwapisha katika nyumba hiyo, ambapo kijana akiwa na kundi la marafiki zake wa kiume na binti na marafiki zake wa kike waliimba na kucheza mziki usiku kucha mpaka asubuhi walipokula na kisha kutawanyika.

– Baada ya tukio hilo baba wa kijana alitengeneza madebe mawili ya pombe ya mbege na kisha kumwalika baba wa binti kwa ajili ya kujadili mipango ya ndoa ya watoto wao, tukio ambalo lilikuwa linakaribia kufanana na sherehe ya “engagement” kwa uchumba wa sasa. Tukio hili lilifanyika kwa kijana kumpa binti zawadi ya kwanza ambayo ilijumuisha mkufu ambao kwa wachagga ndio uliochukua nafasi ya “pete ya uchumba” kwani ilimaanisha kwamba baada ya hapo watu wote wanapaswa kujua kwamba binti huyo ameshachumbiwa na hivyo hapaswi kufuatiliwa tena na watu wengine wenye lengo kama hilo.

– Katika tukio hili la kukabidhiwa mkufu wa uchumba pia watu walisherehekea usiku kucha na ilipofika asubuhi mkufu huo wa kichagga ambao ndio ulikuwa kama pete ya uchumba uliwasilishwa na dada wa kijana anayeoa. Pombe iliyotengenezwa kwa ajili ya tukio hili iliitwa, “Wari wo wika ukisa” au (Pombe ya kusherehekea mkufu wa uchumba).

– Endapo binti alikuwa bado hajapelekwa unyago na kwenye mafunzo ya mregho(shule maalum ya kichagga), ilitengenezwa zawadi ya madebe mawili ya mbege kwa ajili ya baba yake ambayo yaliitwa “Nzugari ya mkambo”, na moja likatumwa kwa baba yake. Pombe nyingine iliyobaki ilinywewa nyumbani kwa kijana na baba wa kijana au baba mkwe wa binti. Baada ya hapo hakuna pombe zaidi ya mbege iliyopelekwa mpaka binti alipokuwa ameshaenda kupitia mafunzo ya mregho kwa mabinti wa kichagga. Lakini zawadi za nguo, ndizi, maziwa na kadhalika vilitumwa na dada wa kijana kwa binti.

– Baada ya mafunzo ilifuata sherehe kubwa ambapo ndugu zake walikusanyika pamoja na ndugu wa kijana ambapo watu walisherehekea na kunywa sana nyumbani kwa wazazi wa binti na sherehe hiyo ilifanywa na baba wa binti. Mama wa binti alimpamba binti yake na mikufu yake mwenyewe na urembo mwingine mwingi. Miguuni alifungwa kengele ndogo zilizoitwa Shichyere ambazo pia zilikuwa kama mrembo miguuni na binti alicheza mziki siku yote mpaka jioni. Watu wote waliohudhuria walitoa zawadi mbalimbali ndogo ndogo kwa binti huku mama mkwe wa binti akipeleka vibuyu vya maziwa na sahani za mafuta ya siagi.

– Katika sherehe hii mara nyingi Mangi aliweza kualikwa lakini hata kama hakuwepo basi madebe mawili ya pombe ya mbege yalitumwa kwake. Katika sherehe hii baba wa binti alitamka wazi kwamba hii ni siku rasmi aliyotamani kumpa binti yake mali zake za kwenda nazo kwa mume wake na kuwatangazia wageni waalikuwa wote nao wafanye kama yeye. Hii ilikuwa ni kama sherehe ya send off kwa sherehe za miaka ya sasa. Mali ambazo baba wa kichagga alimpa binti yake siku hii kwa ajili ya kwenda nazo kwenye ndoa zilitegemea na utajiri wake, mwingine aliweza kumpatia binti yake mbuzi mmoja pekee lakini baba tajiri aliweza kumpatia binti yake mpaka ng’ombe kumi.

– Mama wa binti alimpa binti yake mbuzi au jembe la kulima lakini pia ilikuwa ni siku maalum ambapo mama alimpa rasmi binti yake pete pana(leaden ring) iliyoitwa, “Ambolya Kwako” ambayo ilikuwa ni pambo rasmi la binti aliyeolewa. Pia aliendelea kumpamba binti yake siku hiyo na pete nyingine za aina tofauti tofauti. Kaka zake na dada zake pamoja na ndugu wengine wote walifuatia kwa kumpa binti yao zawadi mbalimbali za kila aina, kwa sababu siku hii binti anayeolewa alikuwa anapokea vile ambavyo vilikuwa vinaenda kuwa mali zake ndani ya ndoa pamoja na nguo na mali nyingine ambazo zilikuwa zinatakiwa kuchukuliwa na binti anayeolewa.

– Kama Mangi alikuwepo kwenye sherehe hizi alimwambia binti afike nyumbani kwake ambapo alikabidhiwa mbuzi au mali nyingine. Mchumba wake na binti ndiye mtu pekee ambaye hakutoa zawadi yoyote kwenye sherehe hii lakini hiyo ndio ilikuwa siku maalum ambapo mchumba wake alimvalisha kofia maalum(bride cap) na kutangaza rasmi kwamba huyu ni bibi harusi wake. Baada ya tukio hili wanaharusi hawa vijana walianza kuitana wenyewe kwa wenyewe kwa jina la “Tindi”.

– Baada ya hapo kijana wa kichagga alimwalika Tindi wake nyumbani kwake ambapo walicheza sana muziki kisha binti akarudi nyumbani kwao akiwa na zawadi nyingi mbalimbali alizopewa na mchumba wake pamoja na wazazi wa mchumba wake zilizojumuisha ng’ombe jike ambaye bado ni mbichi kutoka kwa baba mkwe na mbuzi au pete kubwa kutoka kwa mama mkwe wake. Sambamba na hivyo mchumba wake alimpa mbuzi na kisha kuwapa zawadi ndogo ndogo mbalimbali marafiki za mchumba wake waliokuwa wameambatana naye. Zawadi hizi zilihifadhiwa na binti bibi harusi nyumbani kwao mpaka baada ya ndoa ambapo zitatumiwa naye pamoja na mume wake na kama uchumba utavunjika basi zawadi hizi zilirudishwa.

– Baada ya tukio hili binti aliwatembelea ndugu zake wote na kisha baada ya hapo akaenda kuwekwa ndani kama mwali(mpora). Aliishi ndani ya pango lililokuwepo ndani ya nyumba ya mama yake bila kutoka nje wala kuonana na mtu yeyote kwa kipindi cha kama miezi mitatu. Katika kipindi hiki binti hakufanya kazi yoyote zaidi ya kupewa vyakula vya kumnenepesha na alipakwa mafuta laini na siagi kila siku kumfanya alainike zaidi, kupendekeza na kung’aa. Sehemu kubwa ya vyakula alivyokula katika kipindi hiki vilitoka kwa mchumba wake ambaye alituma kwa wingi maziwa, ndizi, “kisusio” na siagi. Mwishoni alituma kondoo mnene ambapo nusu ya kondoo huyo alikuwa tayari ameshapikwa na kutumwa kwa bibi harusi moja kwa moja na nusu nyingine ya kondoo huyo alikuwa hajapikwa ambaye alitumwa kwa wazazi wa binti. Vitu vyote hivi kwa pamoja viliitwa “shindo shelela mana tindi kiporengi” maana yake (vitu vya kumpelekea mwali/bibi harusi aliyewekwa ndani).

Wakati huu ndio wakati ambao pia kijana anayeoa alianza kufikiria suala la kuanza kulipa mahari kwa baba mkwe, yaani kusema mahari kama mahari ukiachana na zawadi zilizotolewa ambazo sio mahari. Lakini hata hivyo ile sehemu muhimu ya mahari iliendelea kusubirishwa zaidi mpaka baadaye kabisa. Kijana anayeoa hakwenda moja kwa moja kwa baba wa binti bali alitumia mwakilishi kama mdhamini aliyeitwa “Mkara” kwa Uchagga ya mashariki au “Mwisi” kwa Uchagga ya magharibi. Mwakilishi huyo alikuwa ndiye mtu wa karibu wa kijana na kuwa karibu tangu wakati wa harusi na kuwa mlezi wa ndoa yao kwa wakati wote wa ndoa hiyo.

– Kwa mfano ilipotokea ugomvi kati ya wanandoa, mtu huyu “Mkara” au “Mwisi” ndiye alikuwa msuluhishi lakini pia ndiye alikuwa kama wakala wa baba mkwe kuhakikisha kwamba kijana huyu aliyeoa binti yake amefuata taratibu zote na kulipa mahari yote kama taratibu za kichagga zilivyotaka. Kwa kawaida katika shughuli hizi za Mkara waliambatana mkara wa kike na kiume pamoja. Mara nyingi ilikuwa kama kanuni kwamba dada wa kijana anayeoa au dada wa mume wa ndoa hii pamoja na mume wake ndio walisimama kama “Wakara” au “Walisi” kwa ndoa ya kijana huyu.

– Baba mkwe mtarajiwa alialikwa kujadili mipango hiyo ya mahari na ndoa. Pombe iliyotishwa kwa ajili ya tukio hili iliitwa, “Wari wo Nzugari ya Miwatu ya Kawi”(sehemu ya pili ya kilichobakia kutolewa). Pombe ya mbege iliendelea kutishwa kwa matukio matatu tofauti nyumbani kwa baba wa binti. Mwishowe madebe matano ya mbege yalitishwa kualika kaka za baba wa mtoto yanayoitwa “Masalenyi lya Kawi” na kupeleka debe moja kwa Mangi ili kuitambua rasmi ndoa hiyo. Pombe hii ilifuatiwa na nusu ya ng’ombe dume kwa ajili ya kuchumbia bibi harusi, japo mara nyingi alichinjwa mbuzi mmoja na nyama yote kupelekwa kwa baba mkwe. Nyama hii iliitwa “Uromu la Mamka”, au “chakula kwa ajili ya mama”.

– Kisha pombe ya mbege ilitishwa na mama wa binti kualikwa nyumbani kwa mchumba wa mtoto wake ambapo alisindikizwa na yule mkara wa kike pamoja na marafiki zake. Pombe hii iliitwa, “Nyi Mamka acha Sangara/tumo kaira kopfo”, ikimaanisha “ni mama mkwe amekuja sokoni akapitia nyumbani kwako”. Ilikuwa kama anajifanya kwamba hakuja kwa ujio maalum bali alikuwa anajipitia tu basi akaamua kupitia hapo nyumbani kwa mkwe wake mtarajiwa.

– Baada ya hapo madebe 11 ya pombe ya mbege yalitengenezwa nyumbani kwa baba mkwe kwa ajili ya watu kusherehekea pamoja na Mangi. Kisha madebe matano ya mbege alipewa baba. Pombe hii iliitwa, “Pombe ya kukamilisha mahari”. Hapo ilifuatiwa na zawadi ya pombe kwa ajili ya wajomba zake binti na kaka zake pamoja na ndugu wengine. Baada ya hapa alialikwa tena mama pamoja na ndugu zake wa kike na madebe matano ya pombe ya mbege yalitishwa na moja lilipelekwa kwa baba yake ndani ya nyumba ya baba yake. Pombe hii iliitwa “Wari wo Mamka” au “Pombe ya mama” ambayo ilifuatiwa na zawadi ya nyama kutoka kwa ng’ombe dume mkubwa na mnene aliyechinjwa kwa ajili hiyo.

TUTAKUJA KUENDELEA NA HATUA YA NDOA NA MAISHA YA NDOA.

Ahsanteni.

Karibu kwa Maoni, Maswali, Ushauri.

Whatsapp/Call +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *