BINADAMU ALIYEISHI MIAKA MINGI ZAIDI DUNIANI KATIKA HISTORIA NI MCHAGGA.

– Katika miaka ya 1930’s aliyekuwa kiongozi mkuu wa serikali ya Waingereza Kilimanjaro Sir Charles Dundas alitembelea Uchaggani katika eneo la Mbokomu, Old Moshi lililopo mashariki ya karibu ya Uchagga, Kilimanjaro, ambapo katika ziara yake Dundas alikutana na Mzee mmoja aliyeitwa Mrukumu ambaye alikuwa na umri wa kati ya miaka 110 mpaka 120.

– Umri wa Mzee Mrukumu uliweza kujulikana kwa sababu kwanza alikuwa ameishi katika tawala za wamangi nane tofauti wa Mbokomu mpaka kufikia miaka ya 1930’s. Lakini pia Mzee Mrukumu alikuwa ni kijana wa zaidi ya miaka 25 wakati mzungu wa kwanza kutembelea Kilimanjaro anafika mwaka 1848 ambapo alifikia Kilema na kisha kwenda Machame. Matukio makubwa yaliyokuwa yanatokea katika eneo lolote la Uchagga, Kilimanjaro yalijulikana Uchagga nzima kwa kipindi hiki wakati huo Machame ikiwa ndio yenye ushawishi mkubwa zaidi.

– Mzee Mrukumu katika kuhojiwa anasema kwamba wakati huo Johannes Rebmann anatembelea Machame yeye alikuwa ndio yuko katika kipindi cha kuoa ambapo kwa rika leo kwa zama zile za katikati ya karne ya 19 kwa Uchagga, Kilimanjaro kijana alikuwa anaoa baada ya miaka 25 lakini hata hivyo baadaye umri wa kuoa uliendelea kupungua zaidi. Mzee Mrukumu aliweza kumsimulia Charles Dundas tukio hilo la Rev. Johannes Rebmann kutembelea Kilimanjaro mwaka 1848 na safari yake mpaka Machame kuonana na Mangi Mamkinga kwa usahihi mkubwa wa taarifa za tukio zima lilivyokuwa. Mzee Mrukumu anaeleza kwamba Johannes Rebmann alifika Uchaggani, Kilimanjaro kipindi ambacho yeye ndio alikuwa kwenye maandilizi ya kuoa hivyo alikuwa na zaidi ya umri wa miaka 25.

– Halafu sasa wakati huu Charles Dundas anamtembelea Mzee Mrukumu katika miaka ya 1930’s akiwa na kati ya miaka 110 mpaka 120 kulikuwa na baba yake mkubwa Mzee Mrukumu huko huko Mbokomu aliyeitwa Mzee Mraishe ambaye alikuwa anakadiriwa kuwa na kati ya umri wa miaka 140 mpaka 150. Mzee Mraishe alikuwa amezaliwa katika rika lililojulikana kama “Makibola”, rika ambalo kwa mujibu wa historia lilianza kabla ya mwaka 1790.

– Mzee Mraishe katika miaka hii ya 1930’s alikuwa na kitukuu ambaye alikuwa katika rika la “Mangusha” ambalo kwenye miaka ya 1930’s lilikuwa ni rika la watu wa wazima na wazee walio wengi kwa maana ya kwamba ni watu waliokuwa na umri wa angalau miaka 50 mpaka 60 na kuendelea. Umri huu wa kitukuu wa Mzee Mraishe ambaye alikuwa kwenye rika la “Mangusha” lililokuwa ni rika la watu wa wazima na wazee walio wengi kwa miaka ya 1930’s linatoa picha nzuri zaidi ya umri wa Mzee Mraishe.

– Kwa mujibu wa Charles Dundas ambaye alimtembelea Mzee Mraishe moja kwa moja na kuonana naye ana kwa ana anasema kwamba Mzee Mraishe alijulikana wakati huo kwamba huenda ndiye alikuwa Mchagga mwenye umri mkubwa zaidi. Dundas anasema Mzee Mraishe kwa sababu ya uzee alikuwa hawezi tena kutembea, haoni wala hasikii vizuri lakini alikuwa anaongea vizuri sana kwa weledi mkubwa na alikuwa na meno yake yote mdomoni.

– Kutokana na maelezo ya Charles Dundas ni wazi kwamba Mzee Mraishe alikuwa na umri usiopungua miaka 140 na pengine ulikuwa unafika hata miaka 150. Sasa kwa rekodi za watu wenye umri mkubwa zaidi duniani katika historia hakuna rekodi inayoonyesha mtu aliyefika umri wa miaka angalau 140. Kwenye takwimu rasmi za Wikipedia zinaonyesha kwamba rekodi ya juu zaidi inaonyesha mtu aliyeishi miaka mingi sana ni mwanamke wa kifaransa aliyeishi miaka 122 akiwa ndiye binadamu pekee aliyefanikiwa kufikisha umri wa miaka 120. Hata hivyo kwa Uchaggani kuna historia za watu mbalimbali tunaowafahamu waliovuka umri wa miaka 130.

– Andiko hili limezingatia taarifa kutoka kwenye nyakati tofauti tofauti na maandiko kutoka kwenye mahojiano na wahusika wenyewe kwa miaka hiyo sambamba na kuchanganya makisio na makadirio pia.

NOTE: Kufahamu Kuhusu Marika Mbalimbali Ya Uchagga Unaweza Kumtembelea Mzee Mmoja Anayeitwa Raphael Sarikoki Mushi Anayeishi Uchaggani, Kibosho Katika Kijiji cha Kitandu. Ni Mzee Ambaye Yuko Katika Miaka 70’s mwishoni au 80’s Mwanzoni Lakini Ana Uelewa Mkubwa Sana wa Historia na Tamaduni za Kichagga na Marika Ya Wachagga, Yeye Mwenyewe Akiwa Anafahamu Rika Lake na Marika Ya Nyuma Yake na Ya Mbele Yake Pia.

Karibu Kwa Maoni au Maswali.

Whatsapp +255 754 584 270

You may also like...

Popular Posts

2 Comments

  1. Mangi mndumii says:

    Fanyeni utaratibu wa lugha itengenezwe dictionary ya lugha kizazi Cha Sasa wengi hatujui kuhusu lugha

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *