HADITHI YA ZAMANI YA WACHAGGA “CHAGGA LEGEND” KUHUSU NAMNA MLIMA KILIMANJARO ULIVYOTOKEA.

Siku zote huwa ni kawaida kwa watu wa jamii kuwa na hadithi zao za kale (legends) ambazo huwa ziko kama utani lakini zilizobeba mafundisho fulani ya kwenye jamii. Tunafahamu kwamba kuna hadithi maarufu ya wachagga kuhusu “Kibo na Mawenzi” ambavyo ni vile viwili vya juu vya mlima Kilimanjaro inayoelezea sababu ya vilele vile kuwa na mwonekano unaonekana namna ile. Ni hadithi fulani inayoelezea kama ugomvi uliopelekea vilele kuwa na muonekano uliopo.

Lakini sasa kuna hadithi ya zamani ya kichagga (Chagga Legend) ambayo sio maarufu sana kama ile ya “Kibo na Mawenzi” yenyewe ikielezea kilichosababisha mlima wenyewe kutokea. Hii huendani muhimu zaidi kuliko ile lakini iliyobeba pia mafundisho muhimu. Hadithi yenyewe ya wachagga ya zamani inaeleza hivi;

– “Hapo zamani za kale nchi ya Uchagga ilikuwa ni tambarare yote kama kule kwenye ukanda wa tambarare kabla ya kuanza kupandisha milimani, lakini katika nchi ya Uchagga kulikuwa na kijana mmoja wa kichagga aliyeitwa Tone ambaye alikuwa ni kijana mbishi/mtata na mwenye kejeli mbaya. Tone alikuwa na ujasiri wa kutamka waziwazi kwamba anatamani Mungu, “Ruwa” alete njaa kubwa katika nchi ya Uchagga ili aweze kuona itakavyokuwa. Watu walichukizwa na kauli zake hizo na kumwonya kwamba awe makini na maneno yake kwa sababu kile anachokiomba huenda kikatokea. Lakini Tone hakujali chochote wala kusikiliza maonyo hayo badala yake aliendelea kupiga makelele kusisitiza “Ruwa” alete njaa kubwa katika nchi ya Uchagga.

– Mara ikawa kweli, “Ruwa” akaleta njaa kubwa katika nchi ya Uchagga iliyotaabisha watu na wanyama wa porini na hivyo watu sambamba na viumbe wengine wengi walikufa kwa njaa hiyo. Na hivyo watu waliazimia kumuua Tone ambaye ndiye walimlaumu kwa kuwaletea mateso hayo. Tone aliisikia hatari hiyo ya kuuawa na kuanza kukimbia hovyo huku na kule kutafuta msaada wa mtu atakayemhifadhi na kumlinda dhidi ya kuuawa na watu, lakini hakuna mtu aliyekuwa tayari kumlinda Tone kwani hata baba yake mzazi hakuwa tayari kumlinda bali yeye mwenyewe alitishia kumuua Tone kwa mikono yake mwenyewe.

– Kisha Tone alikimbilia msituni kujaribu kuomba msaada kwa wanyama wakubwa kama tembo na nyati, lakini wote walikataa kumpa msaada na kumfukuza. Mwishowe Tone alifanikiwa kupata msaada kwa mtu aliyekuwa anaishi msituni peke yake ambaye alimuonea huruma na kumchukua,na kumhifadhi ndani ya nyumba yake ili watu wanaomtafuta ili wamuue wasipate kumwona.

– Mtu huyu aliyempa hifadhi Tone msituni alikuwa anaishi na ndama wawili ambao hapo awali walikuwa ni mawe lakini walibadilika kwa njia za ajabu na kugeuka kuwa ng’ombe. Mtu huyu aliyemuokoa Tone alimuonya asijaribu kuwafungulia ndama hao kwenye banda lao wala kufungua stoo ya maziwa kwa sababu siku atakayofanya hivyo atakufa. Tone baada ya kuonywa hivyo na mtu huyu alijichekea moyoni mwake, na siku moja wakati mmiliki wake ameondoka kwenda kwenye safari zake za mbali alifungulia ndama hao wakatoka nje.

– Ghafla moja ndama hao walioitwa Meru na Tenu walitoka mbio na kukimbia. Tone aliogopa kwamba wanaweza kupotea alianza kumkimbilia Tenu lakini Tenu aliendelea kukimbilia mbali. Kisha Tone alimuita Tenu, “Tenu nisubiri”. Tenu akamjibu, “Njoo hapa nakusubiri”. Lakini Tone alipomsogelea Tenu alirusha mlima mkubwa ambao Tone alipaswa kuupanda ili kumfikia ambao ni mlima Soko au kilima Soko.

– Tone alifanikiwa kupanda mlima Soko mpaka kileleni lakini alipofika kileleni alimkuta Tenu ameshakimbia tena mbali zaidi. Tone akisisitiza huku akilia, “Tenu Tenu nisubiri mwenzako”, Tenu akasimama akamwambia aje anamsubiri, lakini Tone alipokaribia kumfikia Tenu akamrushia mlima Soweko na kisha kukimbilia mbali zaidi. Tone aliendelea kumkimbilia kwenye kilima hicho kirefu, lakini alimwacha mbali kisha Tenu akasimama kumsubiria Tone alimwomba tena na kumsisitiza amsubirie.

– Waliendelea kukimbizana na kila mara Tenu aliendelea kufanya kama mchezo ambapo Tone alimwomba na kumsisitiza amsubiri alijifanya kumsubiri Tenu lakini kila mara alipomsogelea alimrushia mlima mwingine wa kupanda ili kumfikia. Tenu aliendelea kumrushia milima ya kupanda akianza na kilima Lasoe, kisha Pofu, ikafuatia ile milima ya Kirua Vunjo na Kilema, kama Legho, Lyakishonyi, Ngangu, Kitembonyi, Marangu na kuendelea. Tenu aliendelea kumrushia Tone ile milima ya vile vilima vya Kishingonyi Mwika, pamoja vilima vyote vya Mamsera na Mengwe, Rombo.

– Tone alilia kwa nguvu sana na kwa uchungu akisema; “Tenu tafadhali, nimechoka sana mwenzako naomba uwe na huruma na unisubirie.” Tenu alimjibu, “Njoo haraka, nimekuonea huruma, nakusubiri.” Hapo Tone alikimbia haraka sana na kukaribia kabisa kumkamata Tenu na ndipo Tenu kwa nguvu sana kuliko awali alimrushia mlima Mawenzi. Maskini Tone alitakiwa kupanda mlima mkubwa sana wa Mawenzi lakini alijitajidi sana na alipofika kwenye kilele cha Mawenzi alilia kwa sauti kuu kama ya Simba. “Tenu, Tenu, rafiki yangu, nionee huruma, nakufa mimi.”

– Tenu alimjibu kwa sauti kubwa kama ya radi nzito sana: “Njoo haraka sasa kweli nakuonea huruma, nakusubiri hapa.” Akiwa anahema kama mtu aliyechoka sana na anayekaribia kukata roho Tone alimfuata Tenu huku akiyumbayumba na hapo ndipo Tenu kwa nguvu sana alimrushia mlima Kibo. Mara moja Tenu alikimbia mbio mithili ya farasi mpaka kwenye kilele cha Kibo lakini Tone alipambana naye mbio kumfuata huko huko. Kisha walipotelea huko na kamwe hawajawahi kuonekana tena mpaka leo.”

Hiyo ndio hadithi ya zamani, “legend” inayozungumzia namna mlima Kilimanjaro ulivyotokea kutoka kwa wachagga wenyewe.

– Hadithi ya zamani ya wachagga, (Chagga legends) mbali na kuwa na mengi ya kufundisha lakini pia inaonyesha dalili kwamba huenda wachagga walikuwa wanafahamu kwamba kwenye kilele cha Kibo cha mlima Kilimanjaro kuna shimo kubwa la crater ndio maana Tone na Tenu wanasemekana kwamba walipotelea huko na hawakuwahi kuonekana tena mpaka leo. Pengine hiyo ilikuwa ndio sababu ya wao kupotelea huko. Kama hiyo ndio sababu basi huenda kuna wachagga wasiojulikana waliwahi kufika kileleni kabla ya Hans Meyer na Ludwig Purtscheller wakiambatana na Yohane Lauwo.

Una maoni gani?

Courtesy: Charles Dundas, Kilimanjaro and It’s people.

urithiwetuwachagga@gmail.com

Whatsapp +255 754 584 270

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *