*Maisha Ya Mchagga Hapa Duniani Na Ahera” By Mangi Petro Itosi Marealle*
Uchambuzi by Mary Assenga.
MAFUNDISHO AMBAYO BABU NA BIBI WAFUNDISHAYO WATOTO KAMA HAWA WAKATI HUU WA USIKU NI KAMA HAYA;-
Hiki ni kichagga cha zamani kidogo kwa hiyo kuna baadhi ya misamiati imeshamezwa sana na Kiswahili kwa siku hizi, hivyo usijali sana kama kuna baadhi ya maneno yatakupa utata kuyaelewa.
“Mafundo ga mku ni matetera”. Maana yake: mafundisho na methali ya watu wetu wa kale huongoza maisha vema. Methali zenyewe ni hizi;-
i. “Meku o ngoru karema na ngocha”. Tafsiri yake: “Mzee wa heshima alima akivaa majani”. Ufafanuzi wake ni huu: “Usiwaache wazazi wako katika hali ya shida, hasa wakiwa hawana nguo za kusitiri miili yao; wasaidie upesi.
ii. “Pora yako ngamekurina iyoe ngama undine-wo”. Tafsiri yake: “Ewe kijana wangu uliye jandoni nimekutahiri nawe kesho unitahiri”. Ufafanuzi wake: “Wazazi wamewalea na sasa hawana nguvu tena, kwa hiyo wasaidieni na muwaheshimu”.
iii. “Ipfo nuka kuipfo mdi mlotsu nyama”. Tafsiri yake: “Huko porini kuna mti mzuri wenye nyama”. Ufafanuzi wake: “Enyi watoto mnaopenda kuchungulia mizigo ya watu iliyofungwa kama kwamba mna nyama ndani, jihadharini; mkifuata desturi hii itawaletea madhara. Msidhani kila mzigo mnaouona una nyama ndani.
iv. “Ndewon ngungu, ndanwone chilyilyi”. Tafsiri yake: “Nimemwona mwewe bila kuona kundi la watu lililokusanyika kwa kusudi fulani”. Ufafanuzi wake: “Uendapo kuwinda porini ukaona kwa mbali ndege wakirukaruka karibu yake, ukadhani ni tai wanaruka karibu na mzigo wa nyama usifanye haraka. Chungulia polepole upate kuhakikisha: inaweza kuwa maharamia wamechoka, wakaketi chini ya mti ule na kutupa viatu vyao angani ili kushawishi wapita njia au wawindaji wadhani kuwa viatu vile ni ndege warukao, wafuate mnyama aliyeko chini ya mti, na hivi maharamie wawarukie na kuwafanyia uharamia.
v. “Nyiku ndaina ndutu ya oro ilewuta pfinya ikakima ndafu?”. Tafsiri yake: Ni wapi beberu mdogo alipopata nguvu akaweza kumwonea beberu mkubwa maksai?”. Ufafanuzi wake. “Hata ukiwa na nguvu namna gani au uwezo, usijaribu kumwonea baba, kaka, au mkubwa wako yeyote. Waheshimu na kuwasaidia kwani ndio waliokulea”.
vi. “Kipfilepfile kirundu kechiwa mvuo kilawe”. Tafsiri yake: “Manyunyu ya kiwingu kidogo kilijaribu kwa mvua kisiwe”. Ufafanuzi wake: “Usione mawingu angani ukasema kwamba mvua itanyesha, jaribu kutumia maji ya mfereji ili kunywesha shamba lako”.
vii. “Koicho umbe lo Mangi lomkapo ma ulatire”. Tafsiri yake: “Ukisikia tarumbeta la Mangi likipigwa usikose kwenda”. Ufafanuzi wake: “Lazima uhudhurie kwenye mahitaji yote ya mtawala wako, ukikosa kuhudhuria utaweza kuadhibiwa. Pengine nchi yako iko katika hatari kubwa, na unahitajiwa usaidie”.
viii. “Nyi kiki kyaworo mregoni?”. Tafsiri yake: “Ni kitu gani kimenaswa kwenye mtego?”. Ufafanuzi wake: “Unapotembea ukashtukia mtego ambao umenasa mnyama, na ikiwa hujui mwenye mtego usimwondoe Yule mnyama. Ukimwondoe na mwenyewe akapata kujua, anaweza kukudhuru wewe na nchi yako”. (Methali hii imepata kutokea maeneo ya Kilimanjaro. Kwa mfano mtu wa maeneo ya Kirua Vunjo aliondoa mnyama ambaye alikuwa amenaswa katika mtego uliotegwa na mtu wa maeneo ya Kilema iliyo jirani. Watu wa Kilema walipogundua, waliwadai watu wa Kirua mwishowe wakalipwa kwa sehemu ya Kirua ambayo ilichukuliwa na kuwa sehemu ya Kilema.
ix. “Mtoori o umbe nyi mka”. Tafsiri yake: “Mwenye kutoa habari za siri zako ni mwanamke”. Ufafanuzi wake: “Usizungumze siri na mwanamke hasa siri ya ng’ombe na mali nyingine ya wanyama walioko nyumbani.” (Sababu ya methali hii ni kuwa wanawake huenda kukata majani na humo huenda na humo huenda wakizungumza habari za mali bwana zao walizonazo. Kwa njia hii hutokea Mangi akadai ushuru wa utawala wake kwani amekwisha sikia kwamba fulani anayo mali kadha wa kadha kwa sababu ya uvumi wa mazungumzo ya wanawake).
x. “Ndaiya Mawuki-o-Kisima-Makyaala”. Tafsiri yake: Niite Mawuki bin Kisima wa Mtaa wa Kyaal”. Ufafanuzi wake: (Watu wa Mtaa wa Kyaala eneo la Marangu husemwa kuwa ni watu bahili, kwa hiyo wakikusaidia kitu watakuharibia).
xi. “Ipfue limwi soromu, gengi gakusoroma gakafo”. Tafsiri yake: “Nyani mmoja ametoka lakini huongezeka kidogo kidogo wakazidi”. “Ufafanuzi wake: “Ukiona watu watembeao mmoja mmoja mpakani mwa nchi yenu, kama vile nyani wanavyotembea wakienda kuiba mahindi, nenda pole pole uwachungulie, na wakiwa maadui nenda upesi umpashe Mangi habari”.
xii. “Lya Marashire lilepfaama lyikeera nyama ya Ndafu”. Tafsiri yake: “Manukato yamenukia kupita nyama ya beberu maksai”. Ufafanuzi wake: “Uendapo ukatumwa na Mangi ukamkuta mke wake, ambaye hunukia manukato, usipite karibu yake. Ukipita karibu yake unaweza kuambukizwa harufu ya yale manukato ya mke wake, na ukirudi kwa Mangi, akakusikia ukinukia manukato ya mke wake, ataweza kukudhania umezini na mke wake, hivyo utakuwa katika hatari ya kuuawa”.
xiii. “Aiyo mbero ngifunje kungo, ikalemberia Mkocha”. Tafsiri yake “Huyo ndege anayefanana na kipanga, amevunjika bawa lake, akamsingizia mtu aitwaye Mkocha(maana yake mtu mchokozi).” Ufafanuzi wake: “Usimwone kilema ukamcheka au kucheza naye ukazidi kumuumiza, unaweza kutozwa fidia”.
xiv. “Mooro mecha nyi ga mbogo, ka mooro ga nguwe nyi kiki?” Tafsiri yake. “Urithi mzuri ni wa nyati, je urithi wa nguruwe una faida gani?” Ufafanuzi wake: “Usifanye urafiki na kufanya ukahaba na mwanamke mjane, kwani unaweza kumaliza mali yako kwa kumhonga, na ukijaaliwa kuzaa mtoto, utachukuwa taabu zake zote na za mtoto. Ukizini na mwanamke mwenye bwana utalipa fidia mara moja tu, mke atabaki na mume wake”.
xv. “Molaa tengoni nyi mooru o saro una kigoro kii wanda, mbororo tsikayenda kwi?” Tafsiri yake. “Mwenye kulala katika kibanda kidogo kinachojengwa nyuma ya nyumba kubwa ni sawa sawa na mzinga wa nyuki wenye kitu kisichojulikana ndani yake”. Ufafanuzi wake. “Usimwoe mwanamke mgeni bila ya kuwajua wazazi wake na tabia zao na asili ya ukoo wake. Usiangalie uzuri wa mwili kuliko tabia na asili ya ukoo wake, anaweza kuwa na magonjwa mabaya ambayo yataharibu ukoo wako”.
Watoto hujifunza methali zote hizi na nyinginezo nyingi pamoja na mambo mengi ya kuhusu jamii ya kichagga na maisha kwa ujumla.
ITAENDELEA ….
Urithi Wetu Wachagga.
urithiwetuwachagga@gmail.com
Whatsapp +255 754 584 270.