– Siku ya tarehe 14/Desemba/2024 ambayo ni Jumamosi ya wiki iliyopita ilikuwa ni siku ya kumuapisha rasmi Mangi mpya wa himaya ya umangi Machame Gilbert Shangali kukalia kiti hicho. Mangi Gilbert Shangali ndiye mrithi halali wa kiti cha umangi Machame kwa sasa kwa mujibu wa tamaduni za wachagga ambapo ni mtoto mkubwa wa kiume Mangi Giliard Shangali aliyepita na ambaye alifariki mwaka 2013.
– Mangi Giliard Shangali baba yake Gilbert alikuwa ndiye Mangi wa mwisho Machame mpaka kufikia mwaka 1962 umangi ulipofutwa na serikali mpya ya Tanganyika baada ya kukabidhiwa serikali na waingereza walioondoka na kuachia koloni lao la Tanganyika Territory. Mangi Gilliard Shangali alikuwa ni mtoto wa Mangi Abdieli Shangali, mjukuu wa Mangi Shangali Ndeserua Mushi na kitukuu wa Mangi Ndeserua Mamkinga Rengua Mushi wa Machame.
– Kwanza kabisa nichukue nafasi hii kuwapongeza sana familia ya umangi Machame na timu nzima iliyofanya kazi kubwa ya kufanikisha tukio hili muhimu la kijasiri na la kihistoria. Bila kujali sana msukumo uliopo nyuma yake lakini hii ni hatua muhimu sana ambayo tunaihitaji sana katika maeneo yote ya Uchagga, Kilimanjaro kuifuata kutokana na manufaa makubwa sana iliyonayo kwa jamii ya wachagga na nchi ya Tanzania kwa ujumla. Hongereni sana familia ya umangi Machame na kamati nzima iliyofanikisha tukio hili muhimu la kihistoria.
– Wote tunajua kwamba umangi huu wa sasa tunaopambana kuurudisha ni tofauti kidogo na ule umangi wa zamani kwani wamangi wa sasa hawana mamlaka ya kiserikali wala nguvu za kimaamuzi kwa mambo ya kiserikali kwa sababu tayari tuna serikali ya Jamhuri ya Muungano iliyojitosheleza kiserikali na inayoongozwa kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ngazi zake zote za kimajukumu na utekelezaji. Lakini pamoja na hayo bado itakuwa ni kosa kubwa sana kudhani au kufikiri utawala wa umangi wa sasa hauna umuhimu au hauna maana.
– Utawala wa umangi wa sasa una umuhimu mkubwa sana kijamii pengine kuliko hata taasisi nyingine za kijamii kama taasisi za kidini na kiraia, na ushawishi wake ambao unapaswa kutokana na misingi na umuhimu wa taasisi hiyo kwa zamani una nguvu ya kuirekebisha na kuijenga jamii ya wachagga kuelekea kuwa bora sana. Jambo la muhimu kwa sasa ni umangi huu wa sasa kujitengenezea miongozo na utaratibu ambao utaufuata katika kutimiza majukumu yake ambayo unapaswa kuyatekeleza na umeapa kwayo.
– Umangi huu wa sasa una majukumu mengi na mazito sana kwa sababu unapaswa kwanza kurudisha mambo mengi yaliyopotea au kupuuzwa na kuonyesha ni namna gani yana umuhimu kwa nyakati za sasa, sambamba na kujenga ushawishi wa utekelezwaji wake. Hata hivyo habari njema ni kwamba licha ya kwamba wachagga wamesambaa na kutawanyika sana maeneo mbalimbali duniani, lakini wakati huu teknolojia pia imeendelea sana kiasi kwamba unaweza kuwaunganisha watu kwenye jukwaa moja waliopo Uchaggani na wale waliopo katika kona nyingine zote za dunia na kuwaleta pamoja katika kutekeleza yale muhimu ambayo mnaazimia kuyafanikisha.
– Kati ya mambo ambayo taasisi hizi mpya za umangi zinazoendelea kurudishwa upya uchaggani kote zinapaswa kufanyia kazi ni pamoja na;
1. Kuelimisha, kutunza na kuhifadhi historia kubwa na tukufu sana ya wachagga inayokwenda mpaka zaidi ya miaka 1,000 iliyopita kwa Uchaggani, Kilimanjaro. Historia hii ya kipekee sana imefifia sana kwenye akili za wachagga wa leo na ina ushawishi mdogo sana kwa maisha ya wachagga wa leo kwa sababu ya wao kutoifahamu. Taasisi hizi mpya za umangi zinapaswa kuja na mbinu mbalimbali za kuhakikisha historia hii inafahamika kwani tayari kuna watu nyuma yao ambao wako tayari kusaidia kufanikisha hili kwa namna nyingi sana. Kujitambua na kujifahamu ni hatua ya kwanza katika kupanga kule unakotaka kufika na hivyo kujua kwa uhakika unaweza kufika mbali kiasi gani. Hii ni pamoja na kuhakikisha kwamba vitu kama Sikukuu ya Wachagga(Chagga Day) na matukio mengine yote ya zamani yanarudishwa kwenye utekelezaji wake.
2. Kuelimisha, kutunza na kuhifadhi maadili na sheria mbalimbali za wachagga ambapo nyingine kama vile za mirathi, ndoa n.k., zinakubalika kutumika kwa mujibu wa sheria na kupewa baraka zote na serikali. Tunajua kabisa sheria zote duniani zimetokea kwenye jamii mbalimbali hivyo nasi kama wachagga tuna taratibu zetu katika mambo mbalimbali ambazo zinaweza kuwa bora na manufaa sana kwetu kuliko kutumia sheria nyingi zisizoendana na maadili yetu. Hii inakwenda sambamba na kurudisha nyimbo zote muhimu za zamani kutoka kwa wazee waliopo na mambo mengine yaliyobeba taarifa muhimu za kimaadili, kihistoria na kitamaduni.
3. Kuweka vikao na kuzungumza namna ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii ya eneo husika kama vile changamoto za vijana kukosa miongozo sahihi ya kimaisha, migogoro ya kijamii na hata uelekeo usiokuwa sahihi wa jamii ya eneo husika. Hii inakwenda sambamba na kuhimiza watu kuchangamkia fursa mbalimbali za kimaendeleo kutoka katika maeneo mbalimbali pamoja na kuhimiza wale wenye uwezo kuangalia namna ya kuwekeza nyumbani ili kuamsha ari zaidi ya maendeleo katika maeneo yetu yote ya Uchaggani na kupunguza ile hali ya watu wote kukimbilia mijini ambapo wakati mwingi wanaishi maisha magumu kuliko hata yale waliyoacha kijijini.
4. Mangi anapaswa kuwa kama mkuu wa koo zote za eneo husika ambapo atakuwa anasaidiana na viongozi wa koo mbalimbali kuhakikisha kwamba kila ukoo una uongozi imara sana ambao ndio unahakikisha kuna utekelezaji wa yote yanayoazimiwa kwenye vikao vya kijamii. Uongozi wa koo ukishaimarika na kusimamia koo hizi kwa uhakika hapo tunajua kwamba tutakuwa tumeiokoa jamii yetu ya wachagga kwa sehemu kubwa. Habari njema ni kwamba tayari kuna koo zenye umoja na mshikamano madhubuti sana na hata mifumo bora ya utekelezaji hasa katika wakati huu ambapo teknolojia ya habari na mawasiliano imepiga hatua kubwa.
5. Muhimu zaidi ni kwamba Mangi baraza lake wanaweza kuwa wanajifunza kutoka kwenye maeneo mbalimbali juu ya mambo mengine yanayofanyika vizuri na kuleta kama agenda ambazo ataziwasilisha kwa baraza lake ambalo ni wazee wa ukoo na kujadili namna wanaweza kushawishi utekelezaji wake kwa manufaa ya jamii nzima ya wachagga.
– Jambo la muhimu sana ambalo tunapaswa kujua hapa ni kwamba mafanikio ya kiuongozi ya wamangi hawa wapya yatategemea sana na uwezo wa kiushawishi, kiakili na kiwango kikubwa cha msukumo wa ndani alionao Mangi husika juu ya kufanikisha matamanio yake hayo. Kwa hiyo kama tu ilivyokuwa zamani wale wamangi wenye uwezo mkubwa na wenye maono makubwa na mikakati madhubuti ya namna ya utekelezaji ndio watakaokuwa na mafanikio zaidi hata katika ngazi hii kuliko wale ambao watakuwa wamechukua tu cheo hicho kwa sababu ni warithi.
– Ni muhimu sana vyeo hivi vikatendewa haki na sio ibaki tu kama cheo jina au ule ufahari wa kurithi nafasi ya utawala ambayo haina mchango wowote kwa jamii ambayo imekubali kumtambua mhusika kama kiongozi wao kutoka kwenye mwendelezo wa utawala wa karne nyingi zilizopita.
– Machame ni mwanzo tu, sasa ni muda muafaka kwa himaya zote za zamani za Uchagga, Kilimanjaro kuunda kamati za ndani kuweza kuamua mrithi wa kiti cha umangi atakayekalia kiti hicho na kuandaa tarehe ya tukio la uapisho. Kuna baraka zote kutoka serikalini na unaweza hata kushirikiana na kitengo cha utamaduni mkoa au wilaya au ofisi ya mkuu wa mkoa au wilaya.
– Ukiondoa himaya ya umangi Siha/Sanya juu waliofanya hivyo Desemba/2021 na Machame waliofanya hivyo juzi Desemba/2024 bado hakuna himaya nyingine yoyote imefanya hivyo.
– Himaya za umangi Kilimanjaro zinazopaswa kuandaa tukio la kuapishwa kwa Mangi mpya mrithi halali wa kiti cha umangi ni pamoja na;-
1. Himaya ya Umangi Kibosho.
2. Himaya ya Umangi Uru.
3. Himaya ya Umangi Mbokomu.
4. Himaya ya Umangi Old Moshi.
5. Himaya ya Umangi Kirua Vunjo.
6. Himaya ya Umangi Kilema.
7. Himaya ya Umangi Marangu.
8. Himaya ya Umangi Mamba.
9. Himaya ya Umangi Mwika.
10. Himaya ya Umangi Keni-Mamsera-Mengwe.
11. Himaya ya Umangi Mkuu.
12. Himaya ya Umangi Mashati.
13. Himaya ya Umangi Usseri.
14. N.k.,
– Kwa vyovyote vile hatua hii itaongeza sana wachagga kujitambua na mambo mengine mengi mazuri tusiyoyategemea kuibuka na kutufikisha mbali zaidi.
Karibu kwa Maoni, Ushauri, Maswali.
Urithi Wetu Wachagga.
urithiwetuwachagga@gmail.com
Whatsapp +255 754 584 270.