UCHAMBUZI WA KITABU. – SEHEMU YA 7.

*Maisha Ya Mchagga Hapa Duniani Na Ahera” By Mangi Petro Itosi Marealle*

Uchambuzi by Mary Assenga.

KIFO NA MAZISHI YA WACHAGGA.

-Mchagga yeyote alisemekana hawezi kufa kiurahisi isipokuwa kwa kukosea yeye mwenyewe, yaani ikiwa hakutimizi desturi za ukoo wake au kwa bahati mbaya akiugua na hivi huweza kufa upesi. Kwa hiyo mara auguapo humbidi kufikiri matendo yake kabla hajaugua, yaani alijaribu kufikiri kama alipuuzia kufanya wajibu uliompasa au ikiwa hakutimiza desturi zake za kutambika, au ikiwa amewahi kutokewa na kitu gani katika maisha yake ambacho ni asili ya bahati mbaya kama kurogwa au kuugua.

Mchagga akikaribishwa hawezi kula au kunywa kitu chochote mpaka mwenye nyumba aonje chakula au kinywaji hicho mbele yake, aliogopa sana kurogwa. Hii pia ni moja wapo ya sababu wachagga walikuwa hawali ndani ya sahani mtu peke yake, wote hulia sahani moja.

-Mchagga alijaribu kutambikia kwa mizimu pia kama alifikiri labda kuna namna jamaa zake wa huko kuzimu wanamtaka afanye jambo ambalo amekuwa akilipuuzia. Lakini kama bado itashindikana basi alirudi kwa Mungu(Ruwa) ambaye aliamini yeye ndiye mwamuzi wa mwisho na mwenye mamlaka yote. Ilisemekana kwamba Mungu “Ruwa” hana uchu na mali ya mtu kama mizimu, yeye ni tajiri na karimu wala hana uchu sana na roho za watu.

Hii ndiyo sababu Mchagga hakukimbilia kwake kwanza, aliwahi mizimu kwanza. Ndugu na jamaa za mgonjwa walichinja ng’ombe mjamzito wakati wa mchana jua likiwa utosini kumwomba “Ruwa” amponye mgonjwa wao. Hilo ndilo lilikuwa tumaini la mwisho lililokuwa kwa mgonjwa na jamaa zake.

-Majina ya sifa za “Ruwa” Wachagga wanazomtaja nazo wakati wanamtambikia na kumwomba, na maana yake ni haya; “Ruwa, fumvu lya mku”, maana yake ni kusema Mungu ni kama mlima wa kale na kale kama Kilimanjaro. “Ruwa Matengera” maana yake, Mungu anawatunza wanadamu kuwalisha maisha na kuwalinda katika hatari nyingi. “Ruwa molunga soka na mndo”, maana yake, Yeye ni Muumba na Mwenye kuunganisha watu kama katika taratibu ya ndoa, mtu na mke wake.

“Ruwa”, maana yake ni mkuu achunguliaye watu kwa kuwatunza katika maisha yao kama jua wakati wa mchana. Iwapo Ruwa alimpenda alichukua kiumbe chake, kwani zote ni rehema zake kuishi au kufa. Iwapo mgonjwa amekufa, basi, loo! Kwa wachagga ni kama kinyume cha upendo wa Ruwa: watu hulia na kuhuzunika sana kiasi kwamba wengine hutamani hata kufa naye marehemu.

-Mchagga akifariki taratibu za kumzika ziliandaliwa ambpo alioshwa vizuri na kuvishwa sanda ambayo ilikuwa ni ngozi ya mnyama, kaburi lilichimbwa la urefu kama wa mita sita yakatandazwa majani ya mgomba ndani ya kaburi na miti aina ya “sale” pembezoni mwa kaburi kisha marehemu akawekwa ndani yake akiwa ameketi akiutazama mlima Kilimanjaro kisha wakafukia kwa kufuata utaratibu maalum.

Mchagga akifariki kama alikuwa ameoa/ameolewa alizikwa ndani ya nyumba yake lakini kama alikuwa kijana ambaye bado hajaoa/hajaolewa basi alizikwa shambani nje ya nyumba. Taratibu nyingine kama za kuanua tanga na mambo ya mirathi zilifuata. Baada ya mwaka mmoja kaburi walifukua kaburi kwa kuchimba kutokea nje ya nyumba kuingia ndani wakaondoa mifupi yote na kufukia upya. Mfupa wa fuvu la kichwa na mkono wa kulia waliliweka tofauti na mifupa mingine.

Mifupa ilikusanywa ikawekwa kwenye kigae kama kibakuli hivi wakafunika na juu kisha wakatengeneza sehemu moja shambani katikati ya shamba la migomba sehemu yenye miti ya “masale” wakatengeneza kama mawe au mafiga matatu na kubandika moja juu ya yale matatu, ambapo walikuwa wameshachimba na kufukia ile mifupa iliyokuwa imefunikwa na vigae na kuweka juu yake ndani ya yale mawe/mafiga matatu wakaweka lile fuvu na kichwa na mkono wa kulia. Hapo ndipo ilipokuwa nyumba ya milele ya marehemu.

-Kama marehemu alikuwa na mke aliweza kurithiwa na ndugu wa marehemu kwa kufuata utaratibu maalum. Kama marehemu alikuwa ameoa halafu akafa kabla hajapata mtoto basi mke wake aliweza kurithiwa na ndugu wa marehemu, ambapo ndugu huyu akizaa mtoto na mke wa marehemu watoto hao watakuwa ni watoto wa marehemu na watamwita huyu ndugu wa marehemu baba mdogo licha ya kwamba ndiye baba yao mzazi na endapo atakuwa hawajali au kuwahudumia vizuri wanaweza kumfukuza nyumbani kwao. Watoto wao humtambua marehemu kama baba yao halisi.

ITAENDELEA …..!!

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *