UCHAMBUZI WA KITABU. – SEHEMU YA 6.

*Maisha Ya Mchagga Hapa Duniani Na Ahera” By Mangi Petro Itosi Marealle*

Uchambuzi by Mary Assenga.

NDOA

-Wachagga ni watu wa jamii moja na taifa moja lenye watu wa koo mbalimbali, nao wameishi kwa kuchanganyika sana toka karne nyingi zilizopita. Kwa hiyo desturi na kanuni za maisha yao ni moja katika maeneo yote ya Uchagga kutoka mashariki kwenda magharibi japo unaweza kukuta tofauti kidogo sana zinazotokana na tawala hizi na umbali wa kijiografia.

Lakini desturi zao zote zina kiini kimoja na tofauti ndogo sana zilizopo si kubwa wala za maana sana. Desturi za maeneo yote ya Uchagga ni moja lakini mabadiliko huweko tu katika wingi wa mahari itolewayo.

Sababu za kutoa mahari zilikuwa ni hizi zifuatazo; Wazee wa mvulana na wa msichana hutaka kukamilisha umoja utakaokuwako kati ya koo za mvulana na msichana. Umoja huu hukamilishwa , kwani mali na vyakula vitolewavyo ni vya ujamaa kati yakoo hizi mbili.

-Zamani ilikuwa baba wa mvulana akisaidiana na watu wa ukoo wake ndiye hutoa mahari. Ilikuwa hivi kwa sababu msichana anachukuliwa kama yuko chini ya mume wake atakayemuoa, yeye ndiye anamchukua msichana kwa kumchumbia na baadaye anamtoa kwa wazazi wake na kumpeleka nyumbani kwake kumwoa.

Akishaolewa huwa sehemu ya ukoo wa mvulana. Mahari yanayotolewa hayakuchukuliwa kama bei ya kumnunua mke. Wazazi wa mvulana walitoa mahari ili kukamilisha ujamaa wa koo hizi mbili wakionyesha uwezo wao. Pia ilikuwa ni alama ya kuonyesha upendo baina ya koo hizo mbili, wazee wa mvulana kutoa mali kama shukrani kwa ukoo wa msichana kwa kupewa huyo msichana awe mchumba na baadaye mmoja wa wanawake wa ukoo wao.

Ilikuwa pia njia mojawapo ya kuweza kukutanisha watu wa koo nyingine mbalimbali wakajuana, na taifa la wachagga likaimarika zaidi. Mahari ilitolewa kwa nia safi; Hakuna Mchagga aliyekubali kusamehewa kulipa mahari japo mara nyingi familia za binti zilikuwa zikisamehe mahari ikiwa huyo bwana hana uwezo mkubwa.

Jinsi Mvulana na Msichana Walivyochumbiana.

-Zamani katika Taifa la Wachagga watu walifunga uchumba baada ya kuonana uso kwa uso katika sherehe au ngomani, au, baada ya kuongozwa na wazazi au dada, mvulana alimwendea msichana na kumtaka wafunge uchumba.

Mvulana afikapo kwa msichana humwuliza “Mimi ninakupenda sana na ninataka uwe mchumba wangu; je nawe unanipenda kiasi hicho?” Ikiwa msichana anampenda humjibu, “Ndiyo nakupenda lakini kwanza ukapatane na wazazi wangu, wakikubali basi mimi nitakubali pia kuwa mchumba wako”.

-Mvulana hurudi nyumbani kwao, na kuwaeleza wazazi wake kuwa amekwisha kubaliana na msichana fulani, iliyobakia ni kuwashawishi wazazi wake msichana. Wazazi wake mvulana humjibu, “Sasa usifanye haraka wala sisi hatutataka kuonana na wakwe zako mpaka kwanza tumechunguza tabia za huyo binti na desturi zake, vile vile mpaka tumejua habari za ukoo wao toka hapo zamani kama kuna maradhi mabaya kama ukoma, wizi, uchoyo, ufukara na mengineyo.

Kadhalika msichana naye humweleza mama yake humuuliza “Nimpende huyu kijana?”, Mama naye humwambia, “Ngoja kwanza nitachunguza habari za ukoo wao, kama si watu wakali na wachoyo, wavivu, waongo na wenye laana”. Pande zote mbili, yaani wazazi wa mvulana na wa msichana watapima katika mashauri haya, kila upande peke yake.

Jambo moja kubwa ambalo wazazi wa pande zote wanaloangalia ni kama baina ya koo hizo mbili wamewahi kushtakiana mbele ya Mangi kwa madai kwa jambo lolote, basi watu hawa hawakuozana kamwe.

-Basi baada ya hapo taratibu nyingine za uchumba ziliendelea kwa pande zote mbili kukaribishana nyumbani kwa pombe na kuchinja, walikunywa na kucheza sana mpaka hatua ya uchumba kukamilika. Baada ya hatua ya uchumba kukamilika ziliweza kuanza taratibu za ndoa ambazo nazo zilihusisha michakato mingi sana, hasa sherehe za kualikana pande zote mbili watu wakanywa, wakala, wakacheza sana ngoma na kusherehekea, kujua kucheza vizuri ilikuwa kati ya mambo yaliyoangaliwa sana na wachumba na watu waliotaka kuchumbiana.

Katika maeneo yote ya Taifa la Uchagga ilikuwa ni mwiko kumfanyia harusi ya desturi binti ambaye hakuwa bikra. Heshima ya harusi iliyozingatia desturi za kichagga ilikuwa anafanyiwa tu binti aliyeweza kutunza usichana, hivyo mabinti wa enzi hizo walikuwa wanakuwa mabikra mpaka kufikia kuolewa.

-Baada ya taratibu zote kukamilika mpaka hatua zote za uchumba mahari na harusi kuandaliwa na maharusi wote kupewa mafunzo mbalimbali ya harusi zao, sasa mzee wa kuongoza maharusi huanza kuwaoza hawa wawili na kuthibitisha kama ni kweli waliozwa mbele ya mashahidi wawe mume na mke waliooana kwa sheria ya Kichagga.

Mbele ya mashahidi wale wawili ambao ni wadhamini kwa Kichagga hujulikana kama “Wakara” ambao pia waliwabeba bibi na bwana arusi na watu wengine walioko pale nje, mzee huyu wa kuongoza mambo ya harusi huchukua mkono wa kulia wa bwana kisha akauchukua nao wa kulia wa bibi harusi, na huuweka ule wa mume juu ya mkono wa mwanamke, na kuushikilia hapo akisema, Mbarilie ichu nyi mka opfo”, yaani “Mpokee huyu ni mkeo”.

Bwana harusi ndipo humchukua mke ndani ya nyumba. Wakiingia wale wadhamini huwafuata; wakiisha kuingia ndani ya nyumba ndipo huachiana ile mikono mbele ya wale wadhamini.

ITAENDELEA …..

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *