UKOO WA MCHAU.

– Mchau ni ukoo maarufu wa wachagga ulioenea katika vijiji vingi mbalimbali vya Kilimanjaro japo sio kwa wingi sana. Ukoo huu unapatikana kwa wingi kuanzia upande wa katikati magharibi ya wachagga mpaka katikati mashariki ya Uchagga. Wachagga wa ukoo wa Mchau ni watu makini na kuna wasomi wengi wa fani mbalimbali wanaofanya vizuri katika taaluma mbalimbali ndani na nje ya Kilimanjaro na hata nje ya nchi.

– Kutoka kwenye historia jina Mchau linaonekana kupatikana maeneo mengi ya Uchagga na limetumika kwa wamangi kadhaa wa miaka iliyopita. Tukianzia upande wa magharibi zaidi katika iliyokuwa himaya ya umangi Kindi ambayo baadaye ilikuja kuingizwa kuwa sehemu ya himaya ya umangi Kibosho iliyoko upande wa magharibi wa Kibosho kulikuwa na Mangi aliyejulikana kwa jina la Mchau.

– Mangi Mchau wa iliyokuwa himaya ya umangi Kindi alikuwa ni mtoto wa Mangi Musuo baba yake ambaye alifariki dunia wakati Mchau akiwa bado ni mtoto mdogo. Mke wa Mangi Musuo aliyeitwa Nang’umbe ambaye ni mama yake Mchau alikusanya ushawishi kwa wachagga wa himaya ya umangi Kindi na kukalia kiti cha utawala kwa niaba ya mtoto wake aliyekuwa bado mdogo. Lakini ndugu yake Mangi Musuo aliyeitwa Majenga alipindua utawala wa Nang’mbe na kukalia kiti cha umangi hivyo ikamlazimu Nang’umbe mke wa Mangi Musuo kukimbilia uhamishoni Machame kwa Mangi Rengua yeye na mtoto wake mdogo Mchau, hii ikiwa ni mwishoni mwa karne ya 18 au mwanzoni mwa karne ya 19.

– Mangi Rengua wa Machame aliivamia kwa lengo la kumsaidia Nang’umbe lakini alipofika alifanya maelewano na Mangi Majenga wa Kindi na kumtawalisha tena upya katika kiti cha utawala na hivyo ikamlazimu Nang’umbe na mtoto wake Mchau kukimbilia tena uhamishoni Uru. Baadaye Mchau kuwa mtu mzima yeye na mama yake Nang’umbe walirudi Kindi kwa msaada wa majeshi ya Uru alifanikiwa kukalia kiti cha umangi wa Kindi, na kwa kuwa alikuwa ndiye mrithi halali wa Mangi Musuo alipata kuungwa mkono kiurahisi na wachagga wa Kindi na hivyo kuwa Mangi rasmi wa himaya ya umangi Kindi.

– Mangi Mchau alikuwa ni Mangi imara sana na hodari sana katika vita na mapambano na hivyo baada ya kuingia madarakani aliweza kujiimarisha sana katika kiti cha utawala. Alikuwa ni Mangi mwenye ujasiri wa kipekee na aliongoza jeshi imara sana chini yake, wacha wa Kindi walijengeka kuwa ni watu imara, jeuri na hodari sana katika vita na mapambano. Kutokana na uimara na uhodari wake katika vita Mangi Mchau alijenga ngome imara sana Kindi na hivyo kuamua kuasi na kujitoa kwenye utawala wa mabavu wa Machame bila kuogopa wala kujali wakati huo Machame ikiwa chini ya utawala wa Mangi Mamkinga. Uimara huu wa Kindi ulipekea hata Mangi Mamkinga wa Machame kusita kuivamia Kindi baada ya Mangi Mchau kuamua kuasi. Mangi Mchau wa Kindi alifanya vita na mapambano mengi ndani na nje ya Kilimanjaro.

– Mangi Kirenga wa Kibosho aliweza kuimarisha mahusiano yake na Mangi Mchau wa Kindi ambaye alikuja kuwa ni msaada mkubwa alioutegemea dhidi ya maadui zake ndani ya Kibosho. Hivyo baadaye ulipotokea mgogoro mkubwa Kibosho wa wenyewe wa wenyewe kati ya Mangi Kirenga na ndugu yake Tatuo Mangi Kirenga alienda kutafuta msaada kwa mshirika wake Mangi Mchau wa Kindi. Mangi Mchau aliingia moja kwa moja kwenye mapambano huko Kibosho kumsaidia mshirika wake Mangi Kirenga dhidi ya ndugu zake wakiongozwa na Tatuo pamoja na baba yao Kashenge. Mangi Mchau alifariki katika mapambano haya ambayo yaliishia kumwondoa Mangi Kirenga madarakani na utawala kwenda kwa ndugu yake Tatuo.

– Baada ya Mangi Mchau kufariki Kibosho iliyoongozwa na Tatuo iliivamia Kindi ili kuiadhibu kwa kumuunga mkono Kirenga. Hata hivyo wachagga wa Kindi waliweza kukimbilia uhamishoni Kahe kukwepa majeshi ya Kibosho lakini baada ya kuishi uhamishoni kwa muda mrefu kiasi kwamba uhasama wao na Kibosho ukawa umefifia, Nang’umbe mama yake Mangi Mchau aliwaongoza tena wachagga wa Kindi kurudi Kindi na kisha kiti cha utawala wa umangi wa Kindi kukaliwa na mtoto wa Mangi Mchau aliyeitwa Malamia. Hadithi kamili ya himaya ya umangi Kindi ilikotoka na mwendelezo wote ipo kwenye kitabu cha Miaka 700 Ya Wachagga.

– Mtawala mwingine wa Uchagga kwa jina la Mchau alikuwa ni Mangi wa Mwika mtoto wa Mangi Kyasimba. Mangi Mchau wa himaya ya umangi Mwika alikuwa ni mtoto wa Mangi Kyasimba na mjukuu wa Mangi Sunsa II, akiwa pia ni kitukuu wa Mangi Sunsa I wa Mwika. Mangi Mchau wa Mwika pia ndiye baba yake Mangi Mbararia wa himaya ya umangi Mwika aliyekuwa mtawala wa hodari wa Mwika tangu mwaka 1880 mpaka mwaka 1902 alipokimbilia uhamishoni Nairobi baada ya kuasi dhidi ya serikali ya wajerumani. Mangi Mchau wa Mmwika pia ni ndugu yake Mangi Tengio wa Mwika ambaye ndiye baba yake Mangi Ndemasi Solomon wa Mwika.

– Ukoo wa Mchau ambao umeendelea kusambaa zaidi kwa Marangu maeneo ya Makomu katika kijiji cha Kyala pengine na Nduweni unahusishwa kuwa na ukaribu pia na ukoo wa Mrema wa maeneo hayo. Hata hivyo ukoo wa Mchau umesambaa sana na unapatikana maeneo mengine mengi zaidi ya Uchagga kutoka magharibi kuelekea mashariki.

– Ukoo wa Mchau unapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Kimanganuni, Uru.

– Ukoo wa Mchau unapatikana kwa wingi katika kijiji cha Okaseni, Uru.

– Ukoo wa Mchau unapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Ongoma, Uru.

– Ukoo wa Mchau unapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Korini Kati, Mbokomu.

– Ukoo wa Mchau unapatikana kwa wingi sana katika kijiji cha Tella, Old Moshi.

– Ukoo wa Mchau unapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Mahoma, Old Moshi.

– Ukoo wa Mchau unapatikana kwa wingi katika kijiji cha Kidia, Old Moshi.

– Ukoo wa Mchau unapatikana kwa uchache katika kijiji cha Kikarara, Old Moshi.

– Ukoo wa Mchau unapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Mowo, Old Moshi.

– Ukoo wa Mchau unapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Kyala, Marangu.

Tunahitaji kupata taarifa zaidi kuhusu ukoo wa Mchau ili kutunza historia tukufu sana ya wachagga Kilimanjaro. Ni ukoo unaonekana kupata kwenye baadhi ya vijiji lakini kuunganisha mahusiano yake ya kihistoria na sasa bado ni changamoto. Hivyo tunahitaji kufahamu zaidi ili kuboresha maudhui ya kihistoria kuhusu ukoo huu pamoja na koo za wachagga Kilimanjaro kwa ujumla.

Karibu kwa mchango zaidi wa Mawazo kuhusu ukoo wa Mchau.

1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Mchau?

2. Unafikiri ni kijiji gani ambacho kimesahaulika kutajwa lakini kuna ukoo wa Mchau?

3. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Mchau?

4. Kama wewe ni wa ukoo wa Mchau una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu?

5. Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani?

6. Wewe ni Mchau wa kutokea kijiji gani?

7. Bado kuna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo wa Mchau kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?

8. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Mchau?

9. Wanawake wa ukoo wa Mchau huitwaje, na kwa nini?

10. Una rafiki yako yeyote wa kutokea kwenye ukoo wa Mchau?

11. Ni watu gani mashuhuri unaowafahamu kutoka kwenye ukoo wa Mchau?

12. Kuna mnyama yeyote ambaye labda ni mwiko kuliwa na wachagga wa ukoo wa Mchau?

13. Kuna ukoo ambao hawaruhusiwi kuoana na Wako-Mchau kwa sababu zilizowahi kuwepo miaka ya zamani au nyingine zozote?

Karibu kwa Mchango zaidi au maswali.

Ahsanteni.

Kesho tutaendelea na ukoo mwingine.

www.wachagga.com

Urithi Wetu Wachagga (Facebook).

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *