VIJIJI VITATU VINAVYOFUFUA MATUMAINI YA WACHAGGA, KILIMANJARO.
1. KIJIJI CHA Nkweshoo, MACHAME .
2. KIJIJI CHA Mweka, KIBOSHO.
3. KIJIJI CHA Mwika, MWIKA.
Katika ziara tuliyofanya hivi karibuni, hivi ndio vijiji ambavyo vimetushangaza na kutufurahisha kwani tumekutana na vitu muhimu ambavyo hatukutegemea kuvikuta ambavyo ni uwepo wa MAKTABA YA KIJAMII (COMMUNITY LIBRARY) kijijini.
Kipekee tupongeze vijiji hivi kwa hatua hii muhimu inayoleta hamasa na matumaini.
Japo tunajua kwamba maktaba hizi hazitumiwi sana na watu wa vijiji husika kutokana na tabia na mazoea ya jamii zetu zilivyo lakini uwepo wake ni dalili nzuri kwa uhai wa jamii ya Wachagga(inayoelekea kuangamia) katika nyanja zote za kimaisha.
Kimsingi kabisa inapaswa kila kijiji kiwe angalau na maktaba yake moja kama taasisi huru ya kielimu ya kijiji husika. Hii ni sehemu ambayo watu watabadilli sana fikra zao kupitia kujielimisha mambo mbalimbali na jukwaa huru la kujadili mambo muhimu kwa mapana.
Maktaba hii itakuwa na vitabu mbalimbali kama vya kihistoria, kitamaduni, kitaaluma na rekodi mbalimbali za mambo yote yanayohusiana na kijiji husika na jamii ya Wachagga kwa ujumla katika nakala ngumu na hata nakala tete.
Eneo la hii maktaba kunapaswa kuwa ni eneo la mafunzo muhimu kwa ajili ya kuboresha jambo lolote kitaaluma kwa kijiji husika kama vile ujasiriamali n.k.,
Kisha kuwepo kwa njia zozote za kufanya uhamasishaji wa watu kujenga utamaduni wa kuhudhuria kwenye maktaba ya kijamii kila siku jioni kama wanavyohudhuria kanisani, shule, kwenye vilabu vya pombe, shamba hasa wanafunzi, vijana, wasomi na hata wazee ambapo kazi kubwa ni kuhakikisha watu wanapata maarifa mbalimbali muhimu katika taasisi hii ya kijamii mida ya jioni baada ya kazi.
Hii itafanya jamii kuchangamka, kuongeza ushirikiano, kujitambua sana na kutopoteza asili yote kiurahisi. Vitu kama historia ya kijiji na jamii ya Wachagga kwa ujumla itatunzwa hapa, mila, desturi, mbinu mbalimbali na hata uhamasishaji wa mapinduzi yoyote ya kitaaluma yatakuwa hapa. Kuna mengi muhimu ya kujifunza kutoka kwa waliotutangulia yatakayotuongezea maarifa, kujiamini na kulinda utambulisho wetu.
Mamia ya vitabu vya historia vilivyoandikwa tangu karne ya 19 pamoja na uelewa juu ya mifumo na taasisi zilizokuwepo tangu karne ya 17 vitapatikana hapa. Hata wachagga wa miaka 1940’s na 1950’s walifanya mambo makubwa na ya muhimu tunayojivunia leo kwa sababu walikuwa na uelewa mpana zaidi kuhusu wao wenyewe kwa miaka zaidi ya 200 nyuma, uelewa ambao kizazi cha sasa hakina.
Ili kujenga jamii iliyoelimika yenye kujielewa na inayoendelea kuelimika vijijini, sambamba na kuchochea ubunifu, ujasiriamali, biashara na kujiamini katika nyanja nyingine zote za maisha tunahitaji taasisi hizi za kitaaluma kwa wingi sana.
Taasisi hizi ziwe chachu zaidi kwa vijana wanaokuwa, wakue wakijitambua na kujiamini sana na kujenga jamii iliyochangamka inayoleta matumaini na mabadiliko makubwa ya mifumo ya kijamii vijijini itakayoongeza thamani ya maisha ya vijijini na kuwa sahihi sana ya kufanya maisha pia, badala ya kukaa wakiamini na kuogopa ushirikina kama wanavyofanya sasa.
Hii elimu huru ya kwenye jamii isiyo na mwisho wala kikomo na isiyobagua ni muhimu kuliko elimu ya chuo kikuu ambayo mtu anakuwa ameshasahau karibu kila kitu alichosoma miaka michache baada ya kupewa digrii. Hata katika nchi zilizoendelea sana, uwepo wa maktaba za kijamii umechangia sana kuboresha mifumo ya kijamii.
Karibuni kwa maoni.
Urithi Wetu Wachagga
urithiwetuwachagga@gmail.com