TUTAWEZA KUJIAMINI KAMA TUTATUMIA VYA KWETU NA KUVITHAMINI.

– Ni jambo liko wazi kwamba hakuna mtu anaweza kujisikia fahari na kutembea kifua mbele ikiwa anatumia vitu ambavyo sio vya kwake. Mtu anayetumia vitu vya wengine kwa vyovyote atajiona yeye ni dhaifu(inferior) kwa hao anaotumia vitu vyao.

– Kwa mfano wewe huwezi kujiamini na kujivunia ikiwa unaishi kwenye nyumba ya mtu mwingine ambaye yupo na kila mtu anajua hiyo sio nyumba yako bali ni ya mtu mwingine. Huwezi kujiamini kumzidi mtu ambaye umeazima nguo yake unaivaa, kwa namna yoyote ile mtu yule atakuwa anaonekana mkuu zaidi(superior) kuliko wewe. Hivyo hata linapotokea jambo lolote la muhimu mtu yule mwenye mali na wewe unatumia mali yake atapewa kipaumbele zaidi kuliko wewe ambaye ni kama tegemezi kwake.

– Sasa mambo haya kisaikolojia yanakwenda kwenye mambo mengine mengi. Pale ambapo tumetupa mambo yetu mengi kwa kupotoshwa kwa namna mbalimbali kwamba hayafai na kutumia mambo ya wengine ndio umekuwa mwanzo wa sisi kutumia vya kuazima visivyo vya kwetu na mwanzo wa kuona kwamba wale wengine ambao tunatumia mambo yao ndio watu wakuu na wa maana zaidi.

– Kwa mfano tumetupilia mbali elimu yote ya asili licha ya mambo mengi muhimu na mazuri yaliyoko huko na badala yake tumebaki hatuyajui kabisa licha ya kwamba kuna mengine hatuna kabisa mbadala hata kutoka kwenye elimu ya kigeni. Tumetupilia mbali historia na hatujali kabisa na badala yake tunajifunza historia za wengine, hili linapelekea tuone hao wengine ni bora kuliko sisi na mashujaa kuliko sisi kwa sababu ndani ya vichwa vyetu kuna historia zao na sio zetu. Hapa kwa vyovyote vile ni lazima tutaona kwamba wao ni imara na wakuu kuliko sisi kwa sababu sio tu kwamba vya kwetu hatuvijui bali tunavidharau kabisa.

– Kwa vyovyote vile mtu usiyeheshimu vitu vyako na vya kwenu huwezi kujiheshimu hata wewe kwani wewe mwenyewe ni sehemu ya vitu hivyo vya kwenu. Sasa unapokuwa hujipendi wala kujiheshimu unakosa ile hali binafsi ya kujiamini(self esteem) ambayo ndio inayokufanya ujiamini mbele za wengine na kuchukua hatua bila kujali hao wengine ni nani na wanasema nini dhidi yako.

– Mtu anayekwambia kwamba kukumbatia mambo ya kwenu na kuyapenda ni ubinafsi ni mtu ambaye anataka kukudhibiti kwa kuanza kukutenganisha na mambo yanayokujengea kujiamini. Hii ni kwa sababu lazima kuna mambo utakayoyakumbatia, kwani huwezi kubaki hivi hivi, sasa usipothamini na kukumbatia ya kwenu ni wazi kwamba utakumbatia ya wengine na hivyo utaacha kujiamini wewe mbele za hao wengine ambao umekumbatia ya kwao.

– Kwa mfano ni sawa na mtu anayekwambia usiishi kwenye nyumba yako bali ukaishi kwenye nyumba ya mtu mwingine. Hata kama unaishi kwenye nyumba ya mtu huyo mwingine bure mwisho wa siku yeye ndiye atakuwa mkuu kuliko wewe na wewe utaonekana dhaifu(inferior) kwake na hilo litapelekea wewe kuhesabika kama mtu wa chini na yeye kuwa mtu wa juu yako. Hii ni tofauti kama ungekuwa unaishi ndani ya nyumba yako ungekuwa unajiamini na moja kwa moja unakuwa kwenye nafasi ya kuwa na hadhi sawa na mtu huyo na ikiwa utaweka bidii una nafasi ya kuwa hata (superior) kwake.

– Ni kweli kwamba sio kila utamaduni wako unaweza kuuendeleza au kuutumia kwani mwingiliano wa kitamaduni ni muhimu na una msaada mkubwa na sio tamaduni zako zote zinafaa. Lakini angalau unapaswa kujitahidi kutumia zaidi vya kwako kwa kiasi kikubwa kadiri inavyowezekana na kutumia vingine pale inapolazimu. Watu wote makini na wenye kujiamini duniani wamefanya hivyo. Hii sio kwa sababu unataka kung’ang’ania sana vya kwako bali unatafuta kujiheshimu na kuheshimiwa na wengine kwa kuishi ndani ya nyumba yako hivyo kulinda utu na heshima yako.

– Hii sio dhana rahisi kueleweka kwa baadhi ya watu kwa haraka lakini ukitafakari kwa kina utaielewa vizuri na madhara yake makubwa. Inafikia mahali mtu anajisikia aibu na kila kitu chake kama vile majina ya kwao, lugha ya kwao, hata kijijini kwao na kupenda na kuthamini vya wengine ambavyo vinamfanya yeye kuonekana (inferior) kwa hao wengine. Haya yote yanaweza kutatuliwa kwa kufahamu ukweli kuhusu mambo ya kwenu na ubora na uimara wake na hivyo kuona umuhimu na ukuu wake ukilinganisha na hata na hayo ya wengine.

– Upotoshaji mkubwa na kupuuzwa kwa mambo mazuri ya kwetu sambamba na kujengewa dhana kwamba ni ubinafsi/ukabila kukumbatia na kupenda mambo ya kwetu ndio chanzo cha kuyakimbia na kubaki tunaelea hewani kisha kuyadharau na hata kuyachukia. Lakini ukipata muda kuyafahamu na kulinganisha na ya wengine bado utaona mengi yana thamani kubwa sawa au hata kuzidi hayo ya wengine.

Ahsanteni.

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *