ELIMU YA ASILI YA WACHAGGA.

– Kwanza kabla ya kuingia kwenye mada yetu ya elimu ya asili tujiulize elimu ni nini na chimbuko lake.

– Elimu ni ule mchakato wa kupokea mkusanyiko wa taarifa na maarifa yaliyotokana na uzoefu wa watu katika maeneo mbalimbali yakakusanywa kwa kipindi kirefu na kuendelea kurithishwa kutoka kizazi kimoja kwenda kingine. Maarifa haya pia yanaweza kutokana na tafiti zilizofanyika katika eneo husika na kujulikana namna linavyofanya kazi na hivyo kufundishwa kwa watu kwa manufaa yao na jamii kwa ujumla.

– Katika hali ya kawaida watu wengi huwa na mtazamo kwamba pengine sasa hivi ndio kipindi ambacho watu wana elimu zaidi au maarifa mengi kuliko miaka iliyopita kwa sababu vitu vingi zaidi vimezidi kugunduliwa. Ukweli ni kwamba kwa sasa maarifa yaliyopo au yanayoweza kupatikana ni mengi kuliko wakati mwingine wowote katika historia, lakini sio kweli kwamba watu wa sasa hivi ni wasomi zaidi au wajuzi wa mambo ukilinganisha na nyakati za nyuma. Hii ni licha ya kwamba kwa sasa watu wako kwenye nafasi ya kuwa na maarifa mengi na mkubwa ukilinganisha na nyakati zilizopita lakini kwa sababu mbalimbali watu hawajihangaishi na maarifa hayo.

– Kwenye kitabu cha “Sapiens, the Brief History of Humankind” kilichoandikwa na Yuval Noah Harrari anaeleza kwamba katika kipindi ambacho binadamu walikuwa kwenye hatua ya “forager” au “hunter gatherers” kabla ya mapinduzi ya kilimo miaka 12,000 iliyopita watu kwa wastani walikuwa na elimu kubwa ya kujielewa hususan kimazingira kuliko ilivyo kwa wastani katika karne ya 21. Hii haimaanishi kwamba maarifa yalikuwa mengi kuliko sasa, inamaanisha kwamba watu wengi walikuwa na maarifa mengi kuliko sasa ambapo japo kuna watu wachache wenye maarifa makubwa sana lakini wengi ni wajinga.

– Hivyo watu wa zamani hawakuwa wajinga kama wengi wanavyofikiri, waliweza kuyaelewa mazingira yao vizuri na kuendana nayo kwa usahihi kuliko hata watu wa sasa wanayaelewa mazingira yao na kuendana nayo. Hii inakwenda mpaka karne za sasa ambapo kuna watu wanaweza kudhani labda wachagga wa karne ya 19 walikuwa wajinga ukilinganisha na wa sasa lakini ukifuatilia unagundua mambo mengi walikuwa wanayaelewa vizuri kuliko wa sasa.

– Kwanza walikuwa wanatumia lugha yao ya asili hivyo mambo mengi walikuwa wanaweza kuyaelezea kwa usahihi zaidi, walikuwa na maandishi yao japo hayakutumika sana, walikuwa wanaelewa kuhusu vyakula vyao na madhara yake mwilini kuliko ilivyo sasa, walikuwa wanaelewa kuhusu mifugo yao afya zao na kila kiungo kilichopo ndani na nje ya mifugo hiyo na kazi zake kwa mfugo husika na manufaa yake kwa watu. Walikuwa wanafahamu kuhusu madawa mengi sana ya asili kwa undani sana ambayo hata dawa za kisasa zinatengenezwa kutokea huko. Walijua kwa undani kuhusu historia zao kwa mamia ya miaka iliyopita, afya ya mtu, saikolojia ya mtu n.k., Tofauti ni kwamba mazingira yao yalikuwa ni tofauti na sasa na ukijaribu kuwafikiria katika mazingira ya sasa unaweza kuona ni wajinga lakini ukilinganisha namna walivyokuwa wanayafahamu mazingira yao na wa sasa wanavyoyafahamu mazingira yao basi wao walikuwa wanajitambua zaidi.

– Mfano tu ni eneo la historia ambapo wachagga wa leo wanashindwa kufahamu historia yao hata ya miaka 60 tu iliyopita wakati wakati wa karne ya 19 ndio waliohadithia historia tunazozisoma leo za miaka 200 mpaka 300 kabla ya karne ya 19. Hiyo peke yake ni ishara kwamba walikuwa kuna mambo mengi wanawazidi kizazi cha sasa.

– Tumeweza kuona pia kwenye historia kwamba wageni wengi kutoka Ulaya waliomtembelea Mangi Rindi Mandara Kilimanjaro walishangazwa na uwezo wake mkubwa wa kufahamu mambo mengi sana kuhusu wachagga wenyewe ukilinganisha na watawala wengi wa Ulaya wa kipindi chake walivyokuwa wanafahamu mambo mengi kuhusu nchi zao, tamaduni zao na siasa zao. Kitu ambacho leo hata ukiwauliza watu wengi kuhusu nchi yao ya Tanzania utakuta hawajui.

– Hata hivyo licha ya kwamba kuna elimu kubwa sana y asili katika maeneo mengi ambayo nyingi ni muhimu na inafaa kutumika hata katika maisha ya sasa na kuwa na manufaa lakini ni lazima tukubali kwamba kuna maeneo mbalimbali ambapo jamii zilikuwa zinazidiana duniani katika kwa ukubwa wa maarifa. Uwezo mkubwa wa kufikiria na kuweza kuja na maarifa makubwa ulitokana zaidi na bidii ya jamii husika hususan kile ambacho utamaduni wao ulikuwa unahimiza na sio utofauti wa kijenetiki kwani binadamu wote kwa asili tunalingana kwa uwezo wa asili kiakili.

– Hivyo zile jamii ambazo kwa bahati ziliweza kuweka mkazo katika ubunifu wa uendelezaji uwezo mkubwa kimaarifa zilifanya vizuri zaidi na jamii nyingine zilizojichanganya nazo zilishawishiwa nazo kuiga na mengi mazuri na kupiga hatua japo sio rahisi jamii moja iwe na mambo yote mazuri.

– Mwanafalsafa wa kiingereza wa karne ya 20 Betrand Russel katika kitabu chake cha “History of Western Philosophy” anaeleza kwamba wagiriki wa zamani mwanzoni hawakuwa na maarifa makubwa waliyokuja kuwa nayo baadaye ambayo ndio msingi wa kitaaluma, na maendeleo ya Ulaya ya leo. Bali wagiriki wa kale waliiga mambo mengi kutoka Misri ya kale ambayo ilikuwa imepiga hatua kubwa sana kitaaluma kwa kipindi cha wastani wa miaka 3,000 kabla mpaka kufikia kujenga mapiramidi yanayohusisha hisabati ngumu ambayo yanashangaza watu hata leo. Wagiriki wa kale wa taaluma mbalimbali kama vile Pythagorus, Archimedes, Socrates, Plato, Aristotle, Alexander the Great n.k. waliiga na kuendeleza maarifa hayo katika taaluma mbalimbali na kupata mafanikio makubwa na umaarufu ndio hata mpaka leo bado kuna kanuni nyingi za kwenye masomo mbalimbali tunajifunza kwamba wao ndio walioanzisha.

– Baadaye Wagiriki waliivamia Misri na kuiangusha wakati wa utawala wa Alexander the Great kisha na wao baadaye wakaja kuangusha na himaya ya Roma wakati wa zama za Pompey na Julius Caesar. Betrand Russel anaeleza kwamba hapo ndipo himaya ya Roma iliiga mambo mengi kutoka huko Uyunani au Ugiriki ya zamani na kuyatumia kuitawala Ulaya yote ambayo nayo iliiga mambo mengi kutoka Roma na kuiendeleza Ulaya.

– Lakini hii haimaanishi kwamba maarifa ya asili ya jamii fulani ndio yako dhaifu kulinganisha na jamii nyingine bali kweli kuna maeneo ambayo wengine waliendelea zaidi kwa sababu nilizozielezea hapo juu huku wengine wakifanya vizuri katika maeneo mengine kuzidi hata wao. Ndio maana hata Dr. Bruno Guttman alieleza wazi kwamba mifumo ya kijamii ya wachagga inaonekana kuwa imara zaidi na yenye manufaa ukilinganisha na mifumo ya kijamii ya kwao. Lakini kutokana na kwamba yule anayekutawala ndiye anaamua lipi lionekane ni la maana na lipi lionekane ni la kijinga basi kwa sababu mbalimbali hususan za kisiasa wanaamua kuonyesha kwamba elimu yenu yote ni upuuzi mtupu na hakuna cha kuhifadhi wala kutumia utatumia vya kwake au vile anavyotaka yeye.

– Kwa sababu hii elimu ya asili ilipuuzwa na kutupilia mbali kwa sababu hakuna mtu aliyetaka kujihangaisha kuangalia elimu kubwa muhimu iliyokuwa inaenda kupotea ambayo ilikuwa imetunzwa, kuendelezwa na kurithishwa kwenye jamii husika kwa maelfu ya miaka. Sasa elimu ya kigeni ambayo ilitoka magharibi japo hatuwezi kupuuza mchango wake mkubwa iliyotuletea katika kuiendeleza jamii yetu lakini tunapaswa kujua kwamba imekuja na gharama zake. Kwanza kwa sehemu kubwa inakuja na lugha yake na kuua zile za asili au hata kama itatumia za asili kuna misamiati mingi itatoholewa kutoka kwenye lugha yake. Pia imekuja na maandishi yake hivyo kuua kabisa yale maandishi ya asili ambayo kwa wachagga pia yalikuwepo.

– Pamoja na hayo bado elimu hii ya kigeni pamoja na manufaa yake makubwa ambayo hatuwezi kuyabeza kwani ndio iliyotufikisha hapa tulipofika bado ina mapungufu mengi pia ndani yake. Licha ya kupuuza eneo muhimu la kiroho kama tulivyozungumza jana lakini pia hata kitaaluma sio kwamba linagusa maeneo yote kama ilivyokuwa kwa elimu ya asili, badala yake linagusa baadhi yaliyochaguliwa na kuonekana ni ya muhimu.

– Hivyo kuna maarifa mengi ya kwenye elimu ya asili yaliyopuuzwa ambayo yana umuhimu mkubwa na yenye msaada mkubwa kwa watu yakizingatiwa. Prof. R. Sambuli Mosha amejaribu kuyaelezea mambo haya mengi kwa kina katika kitabu chake “The Heartbeat of Indigenous Africa, the Study of Chagga Education System” kama tutakavyoendelea kuona.

Ahsanteni.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *