ELIMU YA KIROHO NA ELIMU YA KIAKILI (SPIRITUALITY AND INTELLECTUALISM).

– Tunapozungumzia elimu ya kiroho au mambo ya kiroho watu fikra zao huenda moja kwa moja na kufikiria kuhusu dini zao, madhehebu yao, kanisani kwao n.k.,. Hata hivyo ni kweli kwamba dini na madhehebu mbalimbali yanazungumzia zaidi mambo ya kiroho na yanahimiza sana watu waimarike katika eneo la kiroho kwa lengo la kuishi katika ukamilifu zaidi kwenye maisha ya hapa duniani na mengine ambayo yanaaminiwa na wengi kwamba yapo baada ya maisha haya.

– Hii ni kwa sababu mtu akiweza kuishi kwa ukamilifu katika eneo la kiroho ni wazi kwamba anaweza kuwa na maisha yenye utulivu na yenye kumridhisha sana binafsi mtu kitu ndicho haswa binadamu anatafuta kwenye maisha yake. Yaani binadamu kwenye maisha yake anatafuta ukamilifu wa mwili na nafsi kwa maana ya kuridhika na kufurahi. Na hii ndio sababu eneo hili la kiroho linakuwa na umuhimu mkubwa kwani hata licha ya bidii kubwa ya mambo ya mwili kufanyika lakini matokeo yanategemewa kupatikana katika eneo la kiroho.

– Hivyo ni muhimu kabla mtu hajahusisha moja kwa moja elimu ya kiroho na dini akafahamu kwa usahihi eneo hili la kiroho ni lipi na limekaaje ili aweze kujua hata hiyo dini yenyewe inapaswa kumsaidiaje au kumsaidia katika nini. Dini na madhehebu mbalimbali ni taasisi ambazo kazi yake ya msingi ni kumwongoza na kumsaidia mtu kuimarika katika afya ya kiroho ili awe na maisha yenye ukamilifu kama jinsi ilivyo kwamba hospitali ipo kwa ajili ya kumsaidia mtu kuimarika katika afya ya mwili ili awe mzima kiafya. Hivyo dini ni taasisi ambazo kazi yake ya msingi ni kutoa huduma za kiroho kama jinsi ilivyo kwa hospitali ni taasisi ambayo kazi yake ya msingi ni kutoa huduma za kimwili.

JE ENEO LA KIROHO NI LIPI? KAMA MWILI UNAVYOJULIKANA.

– Watu wengi hufikiri kwamba eneo la kiroho la mtu liko mbali kabisa na eneo la mwili. Wakati eneo la akili linaegemea zaidi katika mantiki(logics) za kiakili, eneo la kiroho la mtu ni eneo la hisia za mtu kwa ujumla na hisia za mtu zinaathiriwa na vitu vilivyopo ndani ya mwili wa mtu. Hivyo eneo la kiroho la mtu ambalo ni eneo la hisia zake linaathiriwa na matendo ya kemikali(hormonal reactions) ambazo ziko ndani ya mwili wa mtu japo sio eneo linaloweza kushikika au kuonekana.

HISIA ZA MTU NI ZIPI?

– Binadamu anahisia nyingi sana kiasi kwamba nyingi wanasaikolojia wameshindwa hata kuzielezea kiurahisi au nyingine ni mchanganyiko wa hisia ndani ya hisia kuu. Lakini zinazofahamika zilizozoelekea ni pamoja na hisia za furaha, upendo, imani, chuki, hasira, wivu, tamaa, wasiwasi, utulivu, huruma, maumivu, hofu, woga, huzuni, hamu ya kula, tamaa ya kufanya mapenzi, kuridhika, kushangazwa n.k.

– Eneo hili la hisia ndio eneo ambalo mambo ya kiroho yanaratibiwa na ndio eneo linalompelekea mtu kutafuta msaada wa kiroho. Hata dini na madhehebu mengi ahadi zao zinatokea katika eneo hili la kumwahidi mtu udhibiti wa hisia hizi hususan hisia hasi. Kwa mfano eneo kama hisia za hofu mbalimbali ambazo zinawatesa sana watu wengi kama vile hofu za nguvu za giza, hofu za magonjwa, umaskini, vifo, maisha baada ya kifo, njaa, kukataliwa n.k., ni moja kati ya maeneo ambayo yanawafanya watu wengi kutafuta msaada kwenye taasisi za kidini ambazo zinawapa nafuu ya kuwa na matumaini chanya juu ya mambo yajayo. Kwa maana hiyo hisia hiyo ya hofu na nyingine zingeondolewa kwa binadamu pengine wasingehitaji msaada huo wa kiroho.

– Kwa hiyo taasisi za dini zipo kwa ajili ya kuhudumia eneo hili la kiroho kama jinsi taasisi za afya kama vile hospitali ziko kwa ajili ya kuhudumia eneo hili la kimwili na taasisi za kitaaluma kama vile mashule na vyuo viko kwa ajili ya kuhudumia eneo hili la akili.

– Kwanza tujue kwanza mtu aliyeimarika kiroho yukoje. Mtu aliyeimarika kiroho ni mtu aliyeweza kudhibiti hisia zake zisimpeleke kufanya mambo yanayomletea uharibifu wa rohoni. Kama vile kudhibiti hisia ya tamaa anajieousha na wizi, uzinzi, uongo n.k,. kudhibiti hisia za wivu anajiepusha na chuki pamoja na uharibifu mwingine mwingi, kujiepusha na hofu anajenga ujasiri wa kukabiliana na mambo muhimu n.k.,

– Swali kwa wengi ni kwamba kwa nini sasa eneo hili la kiroho bado lina changamoto sana licha ya kuwepo kwa taasisi nyingi za kidini kwa ajili ya kulihudumia. Tunaweza kuwalaumu watu kwa kutoweka mkazi kwenye mambo ambayo wamekuwa wakisisitizwa sana kuweka mkazo, au tunaweza kulaumu taasisi hizi za kidini kwa kujisahau na kuweka mkazi katika kujinufaisha binafsi zaidi na kupuuza eneo la ukuaji wa kiroho wa watu wake ambalo ndilo kazi yake kuu. Lakini lawama zote hizo bado hazisaidii sana kubadili chochote kama watu hawajajitambua na kuelewa dhana nzima ya eneo la kiroho na elimu yake kwa ujumla.

– Prof. R. Sambuli Mosha katika kitabu chake cha “The Heartbeat of Indigenous Culture, the Study of educational system”, amejaribu kuelezea kwa kutumia mfumo wa elimu wa wachagga zamani namna ulivyokuwa unafanya kazi na kusaidia katika elimu zote mbili ya kiroho (spirituality) na ya kiakili(intellectualism). Prof. Mosha anaeleza kwamba elimu ya akili (intellectualism) ambayo kwa sehemu kubwa imekuja na mifumo ya magharibi na namna ya kufikiri ya kimagharibi imeliacha nyuma eneo la kiroho. Hii ni tofauti na elimu ya wachagga zamani ambayo ilijumuisha vyote viwili elimu ya akili ya elimu ya kiroho kwa pamoja na hovyo changamoto zote kwa pamoja zikawa zimetatuliwa. Kwa sababu eneo hili la kiroho ni eneo linalotokea kwenye jamii husika na ni somo lililokuwa linarithishwa kwa vizazi na vizazi.

– Prof. R. Sambuli Mosha anaeleza kwamba leo hii ni rahisi kukuta mtu msomi mkubwa ambaye amepata elimu ya magharibi lakini kuna mambo mengi ya msingi yanayomshinda kufanya. Labda ni mlevi kupindukia au ametelekeza familia au hawezi kuelewana na mtu yeyote au hata anasumbuliwa na hofu za kishirikina au hata ni mwizi. Inakuwa ni aibu sana kwa watu wasomi wakubwa namna hiyo kufanya mambo ambayo ni ya hovyo kijamii. Na hapo ndipo udhaifu wa mfumo wa kimagharibi uliozingatia elimu ya kiakili “intellectualism” peke yake na kupuuza elimu ya kiroho “spirituality” ambayo iliimarisha jamii ya wachagga kwa miaka mingi bila kuwa na matatizo makubwa ya kijamii.

– Hiyo sio kusema kwamba elimu ya akili “intellectualism” sio muhimu hapana, ni muhimu sana lakini inaposhindwa kuambatana na elimu ya kiroho “spirituality” inakuwa haijhakamilika na hivyo watu wanaoonekana kuwa ni wasomi wanaweza kuishia kuwa watu wa hovyo sana kwa kuegemea kwenye elimu ya upande mmoja peke yake.

– Wagiriki wa kale waliokuwa wasomi sana walikuwa na falsafa yao moja iliyokuwa inaitwa “Stoicism” ambayo baadaye ilikuja kuendelezwa na Warumi wa kale au Waroma akiwemo mtawala wa Roma aliyekuwa mashuhuri sana aliyeitwa “Marcus Aurelius”. Japo ilikuwa ni falsafa na sio dini lakini ilikuwa ni elimu ya mwongozo wa maisha ya kiroho. Falsafa hii ya Stoicism ilipata umaarufu mkubwa hivyo kuendlezwa wakati wa Roman Empire lakini hata sasa bado kuna watu wanaiendeleza na kuiishi akiwemo mwandishi Ryan Holiday. Hii ni kusema kwamba mtu anaweza kukuza eneo lake la maisha ya kiroho kwa mchanganyiko wa falsafa na dini au kimojawapo.

– Prof. R. Sambuli Mosha amejaribu kufafanua na kuonyesha kwamba mfumo wa elimu wa wachagga ulikuwa umejitosheleza katika eneo la akili na roho na kufananisha uimara wa elimu ya kiroho ya wachagga na falsafa ya “Stoicism” ya Wagiriki wa kale na Waroma. Na kwamba mfumo wa elimu hii ya wachagga ulikuwa umejitosheleza kiasi kwamba uliweza kuleta uwiano wa mambo na kujenga jamii bora na iliyojiheshimu kuliko mfumo wa elimu ya akili wa kimagharibi ambao umeegemea eneo moja peke yake la akili “intellectualism” na kuacha watu kupotea kwa kukosa nguzo nyingine muhimu.

– Hivyo anajaribu kuonyesha ni namna gani watu wanapaswa kurudi na kujifunza kutoka kwenye elimu hii ya asili katika eneo la kiroho ili kuongezea katika mengine mengi ambayo tayari yanafahamika katika kuiimarisha jamii.

Tutaendelea na mfululizo wa makala haya katika eneo hili.

Ahsanteni.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *