WACHAGGA NI KAMA WAYUNANI WA KALE.

*WACHAGGA NI KAMA WAYUNANI WA KALE.*

Muundo na Mifumo Ya Kisiasa Ya Jamii Ya Wachagga Inafanana Kwa Karibu Sana na Muundo na Mifumo Ya Muundo na Mifumo Ya Kisiasa Ya Wayunani wa Kale.

Nitajaribu Kueleza Ufananano Katika Kujaribu Kuongeza Pia Uelewa wa Mahusiano Ya Wachagga Baina Yao Wenyewe na Baina Yao na Watu Wengine.

*WAYUNANI WA KALE NI NANI?

*Wayunani wa Kale ni Jamii Iliyoishi Eneo La Kusini Mashariki Ya Bara La Ulaya na Magharini Ya Bara La Asia Katika Eneo Ambalo Leo Kwa Sehemu Kubwa ni Sehemu Za Nchi Ya Ugiriki, Uturuki, Kusini Ya Italia na Maeneo Mengi Ya Visiwani Katika Bahari Ya Mediterranean Tangu Mwaka 1,200 Kabla Ya Kristo Mpaka Mwaka 600 Baada Ya Kristo. Uyunani Ndio Chimbuko La Ustaarabu wa Ulaya Ya Leo Ambao Pia Ndio Tamaduni na Falsafa Zake Vilienea na Kujenga Ushawishi Maeneo Mengi Sana Duniani Ambayo Wazungu Aidha Walifika Moja kwa Moja Kutawala au Wamefikisha Tamaduni Hizo Kwa Namna Nyingine Ya Ushawishi Kuanzia Sayansi, Dini, Falsafa, Siasa, Mbinu za Kivita, Hisabati n.k.,.

Japo Inafahamika Kwamba Wayunani wa Kale Walijifunza Vitu Vingi Kutoka Misri Ya Kale Ambavyo Ndio Chanzo cha Sehemu Kubwa Ya Maarifa na Ustaarabu Waliouendeleza Lakini Wayunani Ndio Chanzo cha Maarifa na Ustaarabu wa Ulaya Uliokuja Kuenezwa Kwa Sehemu Kubwa na Rumi Ya Kale Ambayo Ndio Ilikuja Kuwa na Nguvu Zaidi Baada Ya Kuiangusha na Kuitawala Uyunani.

Wanafalsafa wa Uyunani Ya Kale Ndio Chanzo Cha Maarifa Mengi na Makubwa Sana Ya Kale Yaliyotengeneza Misingi Ya Falsafa za Dini za Magharibi, Mashariki Ya Kati na Hata Kwa Kiasi Mashariki Ya Mbali, Sayansi, Tamaduni na Msingi wa Lugha za Magharibi Pamoja na Miundo Yake na Mifumo Yake. Kwa Mfano Mwanafalsafa Mashuhuri Zaidi Aliyefanya Kazi Kubwa Zaidi Katika Kutengeneza Falsafa za Kanisa Katoliki Mtakatifu Agustino wa Hippo Katika Karne Ya 4 na Karne Ya 5 Alijifunza Mambo Mengi Kutoka Kwa Mwanafalsafa wa Uyunani ya Kale Kutokea Athenia Aliyekuwa Pia Mwanafunzi wa Socrates Anayejulikana Kama Plato. Maandiko Mengi Ya Falsafa za Plato Yalimjenga Sana Mtakatifu Agustino wa Hippo(St. Augustine of Hippo) Aliyefanya Kazi Kubwa Ya Kutengeneza Falsafa Ya Kanisa Ambaye Anaheshimiwa Sana Dini Katoliki Pamoja na Protestanti Pia Akiwemo Martin Luther Mmoja Kati ya Waanzilishi wa Mwanzo wa Harakati za Kiprotestanti. Mwanafalsafa Mwingine Mashuhuri wa Kanisa Katoliki wa Karne Ya 13, Mtakatifu Tomaso wa Akino(St. Thomas Aquinas) Aliimarishwa Sana na Maandiko Ya Falsafa za Mwanafalsafa wa Uyunani Ya Kale Aliyewahi Kuwa Mwanafunzi wa Plato Maarufu Kama Aristotle. Wanafalsafa wa Dini Ya Kiislamu Pia Kama Wakina Al-Kindi, Muhammad ibn Zakariya al-Razi wa Karne Ya 9 na 10, Averroes Ibn Rashd wa Karne Ya 12, n.k.,. Wamejifunza Mambo Mengi Sana Kutoka Kwa Mwanafalsafa wa Uyunani Ya Kale Aristotle Ambaye Wanafalsafa Hawa Wanamtambua Kwa Jina Maarufu “Mwalimu wa Kwanza”(First Teacher). Sehemu Kubwa Ya Falsafa Zilizojenga Misingi Ya Dini Ya Kiislamu Pia Zilitokana na Aristotle.

Aristotle Pia Ndiye Alikuwa Mwalimu wa Alexander the Great, Mbabe wa Kivita na Mtawala Aliyetawala Eneo Kubwa Zaidi Duniani Katika Historia Akitokea Macedonia Ya Uyunani Ya Kale. Japo Historia Takatifu Ya Dini za Kikristo na Kiislamu ni Ilichukuliwa Ile Ya Wayahudi Lakini Falsafa Zilizojenga Misingi Ya Kiimani Ya Dini Hizi ni Kutoka Uyunani Ya Kale. Tamaduni za Uyunani Ya Kale Zimeingia Kwa Kiasi Kidogo Mpaka Kwenye Dini Ya Wabudha Ambapo Iliingia Baada ya Alexander Mashuhuri(Alexander the Great) Kuipiga na Kuitawala Asia Ya Kati Kutokea Asia Magharibi Iliyokuwa Uajemi Kuelekea India Akitokea Macedoni Ya Uyunani Ya Kali. Pia Wanahisabati na WanaFizikia wa Uyunani Ya Kale Pythagoras Aliyegundua Dhana Ya Hisabati Ya Pythagoras theory na Archimedes Aliyendua Nadharia Ya Fizikia Ya “Archimedes Principle”, Wote Hawa Pamoja na Wengine Wengi Sana ni Wanafalsafa na Wanataaluma Wengine wa Uyunani Ya Kale Ambao Wamechangia Kwa Sehemu Kubwa Maarifa Yaliyoibadilisha Dunia Ya Leo Kitaaluma, Kisayansi, Kiteknolojia, Kidini, Kitamaduni, Kifalsafa, Kimitizamo, Kisiasa, Unajimu na Mambo Mengine Mengi.

*UFANANO WA WACHAGGA NA WAYUNANI WA KALE.

*Wachagga Kama Walivyokuwa Wayunani ni Jamii Moja Lakini Iliyoundwa na Vijamii Vingine Vidogo Vidogo Tofauti na Jamii Nyingine Za Zamani Zilizokuwa Chini Ya Utawala Mmoja Mkubwa wa Kifalme au Kikabila. Katika Uyunani Kama Ilivyokuwa Katika Uchagga Kulikuwa na Wayunani wa Athenia, Wayunani wa Spata, Wayunani wa Korinto, Wayunani wa Argo, Wayunani wa Sirakusa, Wayunani wa Korintho, Wayunani wa Theba, Wayunani wa Macedonia, Wayunani wa Rodo, Wayunani wa Egina, Wayunani wa Eretria n.k., Hivyo Hivyo Katika Uchagga Kuna Wachagga wa Siha, Wachagga wa Machame, Wachagga wa Kibosho, Wachagga wa Uru, Wachagga wa Old Moshi, Wachagga wa Kirua, Wachagga wa Kilema, Wachagga wa Marangu, Wachagga wa Mkuu, Wachagga wa Usseri n.k., Muundo Huu Ni Tofauti Sana na Muundo wa Jamii Nyingi Lakini Imetokea Kwamba Wachagga na Wayunani Wamefanana Katika Hili.

Jiografia Ya Uyunani Kama Ilivyo Jiografia Ya Uchaggani Imeundwa Kwa Milima na Mabonde Makubwa Ilichangia Kuleta Mgawanyiko Ambao Zamani za Kale Uliwatenganisha Wayunani Kuwa Katika Makundi Hayo. Jiografia Ya Uchaggani Pia Imeundwa Kwa Milima na Mabonde Makubwa Ambayo Yamechangia Kuwatenganisha Wachagga Kuwa Katika Makundi Ya Jamii Ndogo Ndogo Za Wachagga na Kuwafanya Waonekana Kama Sio wa Jamii Moja.

Kama Walivyo Wachagga Hata Wayunani wa Kale Hawana Wasiwasi Kabisa Juu Ya Kwamba Wao ni Jamii Moja Yenye Asili Moja, Dini na Imani Yao Ni Moja, Tamaduni za Msingi ni Moja, Msingi wa Lugha Ni Mmoja Lakini Wanaishi Katika Himaya Ndogo Ndogo za Tofauti. Wachagga Nao Dini na Imani Yao Ya Kale Ni Moja, Msingi wa Tamaduni za Kichagga Ni Mmoja, Msingi wa Lugha Ya Kichagga Ni Mmoja Lakini Pamoja na Kuishi Katika Himaya Ndogo Ndogo za Kichagga Hawajawahi Kusahau Kwamba Wao ni Wamoja.

Wayunani Kama Ilivyo Kwa Wachagga Hawajawahi Kuwa na Lengo Moja La Kisiasa Kwa Pamoja Bali Kila Himaya Ilifanya Siasa Zake za Ndani Ya Himaya Yake Kivyake na Mara Nyingi Waliunganisha Majeshi Kwa Ajili Ya Kupambana na Maadui Kutokea Nje Ya Uyunani na Baada Ya Vita Kila Mtu Alirudi Kwenye Himaya Yake na Pale Ilipotokea Himaya Moja Ya Uyunani Imeingilia Himaya Nyingine Ya Uyunani Ilikuwa Ni Kwa Ajili Ya Kubadilisha Kiongozi Kwa Malsahi Yao Na Sio Kwa Lengo La Kuichukua na Kuitawala. Hata Baada ya Uyunani Kuungana na Kuwashinda na Kuwaondoa Waajemi Ambao Tofauti na Wayunani Wao Walikuwa Chini Ya Mtawala Mmoja, Lakini Baada Ya Vita Wao Wayunani Walirudi Katika Himaya Zao Ndogo Ndogo. Hali Kadhalika Kwa Wachagga Kila Himaya Ilikuwa na Mangi Wake na Hakuna Mangi Mmoja Aliyetaka Kuwa Mangi wa Eneo Jingine Moja Kwa Moja Zaidi Ya Kumweka Mangi Mwingine Kutoka Eneo Hilo Hilo Tena Kutoka Katika Ukoo Huo Huo wa Mangi. Kwa Mfano Vunjo na Rombo Yote Walipoungana Kupambana na Wamasai Mara Kadhaa Chini Ya Mangi Horombo, Baada ya Vita Kila Mtu Alirudi Katika Himaya Yake Kuendelea na Shughuli Zake. Kesi Pekee Iliyowahi Kutokea Uchaggani wa Mangi wa Eneo Moja Kutaka Kuwa Mangi wa Eneo Jingine Moja Kwa Moja Ni Kesi Ya Mangi Abdiel Shangali Mushi wa Machame Aliyekuwa Mangi wa Machame na Siha Moja Kwa Moja, Ambapo Hata Hivyo Hili Lilifanyika Karne 20 Kwa Njia Ambazo Ni Za Kidiplomasia na Propaganda za Kisiasa na Sio Kwa Nguvu Ya Kijeshi Kama Ilivyokuwa Zamani Lakini Hata Hivyo Baadaye Hilo Liliondolewa na Siha Kuwa na Mangi Wake Tena. Suala la Kuunganisha Himaya Zote Kuwa na Kiongozi Mmoja Halikuwahi Kufikiriwa Wala Kutokea Kwa Wayunani Wala Wachagga, Kwa Sababu Hata Kipindi Cha Mangi Mkuu Wachagga Walikuwa na Mangi Mkuu Mmoja wa Kilimanjaro Yote Ambaye Alikuwa Juu Ya Wamangi Wote Kimamlaka Lakini Kila Eneo Lilibaki na Mangi Wake Pia.

Wayunani Walianzisha Makoloni Katika Maeneo Mengi Hasa Ambayo Yalikuwepo Katika Mwambao wa Bahari Ya Mediterranean Kuanzia Karne Ya 7 KK Mpaka Katika Zama za Alexander the Great Ambaye Alikuja Kuitawala Mpaka Misri Ya Kale na Baadaye Utawala Wake Ukaendelezwa na Kizazi Cha Kifalme Cha Ptolemi Mpaka Utawala Huo Ulipokuja Kuangushwa na Majeshi Ya Rumi Yakiongozwa na Emperor Augustus Katika Zama za Utawala wa Cleopatra Karibu Miaka 300 Baada Ya Ptolemi wa Kwanza Mwaka 30 KK Misri Ilipoanza Kuwa Koloni Rasmi La Rumi Ya Kale. Wachagga Nao Walikuwa na Makoloni Nje Ya Kilimanjaro Kama Vile Kahe na Arusha Chini Yaliwahi Kuwa Makoloni Ya Himaya Tofauti za Uchagga Kwa Nyakati Tofauti Kama Vile Machame, Kilema, Old Moshi, Kibosho na Mamba. Ugweno Pia Iliwahi Kuwa Koloni La Kilema, Meru na Ukamba Yaliwahi Kuwa Makoloni Ya Machame Japo Meru Ilikuwa Zaidi Washirika Kuliko Koloni, Taveta na Ugweno Yaliwahi Kuwa Makoloni Ya Old Moshi Pia Usambara na Maeneo Mengine Ya Tanga Yaliwahi Kuwa Mawakala wa Old Moshi n.k.,.

Kama Ilivyo Uchagga Katika Uyunani Ya Kale Japo Mara Nyingi Himaya Zenye Nguvu Ziliweza Kuzikalia Kimabavu Himaya Nyingine Lakini Hazikuwahi Kulazimisha Utawala wa Moja Kwa Moja. Kwa Mfano Athenia na Spata Mara Nyingi Zilikuwa na Nguvu Kuliko Himaya Nyingine na Wakati Mwingine Kuziamrisha na Kuzilamisha Kufuata Matakwa Yao Lakini Hawajawahi Kuzilazimisha Kutawaliwa na Spata Moja Kwa Moja Kwa Kuondoa na Kuodoa Uongozi Wao, Hili Ni Jambo Lililokuwa Gumu Sana Kulikuta Katika Himaya Nyingine. Lakini Hata Kwa Wachagga Ilikuwa Hivyo Hivyo, Machame Iliwahi Kuitawala Kibosho Kwa Miaka Mingi na Kuiamrisha Kwa Mambo Mbalimbali Lakini Haijawahi Kusema Inaitawala Moja Kwa Moja na Kumuondoa Mangi wa Kibosho Zaidi Tu Walikuwa Wakimwamrisha Kufuata Matakwa Yao, Hata Kibosho Walipokuja Kuikalia Machame Ilikuwa Hivyo Hivyo. Mangi Horombo Aliwahi Kuitawala Vunjo na Rombo Yote Lakini Alizipa Uhuru Himaya Zote Zilizokuwa Chini Yake Kimamlaka Kuendelea Kuwa na Wamangi Wao na Kuendesha Siasa Zao za Ndani Bila Bugdha Japo Waliamrishwa Kufuata Matakwa Yake. Old Moshi Iliwahi Kuzikalia Kimabavu Uru, Mbokomu, Vunjo Yote na Rombo Lakini Japo Wakati Mwingine Waliweza Kumbadilisha Mangi Aliyekuwepo Madarakani na Kumweka Wanayemtaka Wao Lakini Hawakuwahi Kuzuia Himaya Yoyote Kuwa na Mangi Wao. Hali Kadhilika Kilema Ilipoikalia Vunjo Yote Kimabavu na Hata Kipindi Kibosho Walipoiangusha Old Moshi na Kuikalia Kimabavu Kwa Muda Waliishia Kumweka Mangi Mwingine Kutoka Ukoo Huo Huo wa Mangi Lakini Hawakuamua Kwamba Wataitawala Wao Moja Kwa Moja. Hali Hii Ilikuwepo Kwa Wachagga na Wayunani Ilikuwa Pia Hivi Hivi.

Wayunani Kama Ilivyo Kwa Wachagga Walikuwa Pia na Vita Vya Wenyewe Kwa Wenyewe Vilivyopiganwa na Kwa Makundi, Yaani Kunakuwepo na Makundi Mawili Ya Himaya Yanaungana na Kupigana Dhidi Ya Kundi Jingine au Himaya Nyingine Kwa Sababu Mbalimbali Hasa Za Kisiasa. Kwa Mfano Kundi Moja La Uyunani Likiongozwa na Athenia Lilijumuisha Himaya za Athenia, Argo, Korintho, Sirakusa n.k., na Kuunda Muungano wa Deliana Lilipambana Dhidi Ya Kundi Jingine La Uyunani Likiongozwa na Spata Lililoundwa na Spata, Theba na Eretria na kuunda Muungano wa Peloponesia. Wakati Mwingine Spata Peke Yake Iliweza Kupigana na Muungana wa Deliana. Lakini Pamoja na Kuungana Huku Bado Hakuna Himaya Moja Iliyotawala Nyingine Moja Kwa Moja, Kwa Mfano Philip II, Baba Yake Alexander the Great Kutokea Macedonia Iliyopo Kaskazini Ya Uyunani Ya Kale Aliiangusha Uyunani Yote na Kuikalia na Kutengeneza Umoja Ulioitwa Muungani wa Korintho Kwa Ajili Ya Kupambana Kuiangusha Uajemi Iliyokuwa na Nguvu Sana Lakini Bado Hakuingilia Siasa za Ndani Ya Himaya Nyingine za Uyunani Moja Kwa Moja. Hata Alexander the Great Mwenyewe Alipochukua Madaraka Na Kuwa Mtawala wa Uyunani Yote na Kuziangusha Himaya Zenye Nguvu Kama Uajemi na Nyingine za Asia Bado Alizipa Uhuru Mkubwa Sana Himaya Nyingine za Ndani Ya Uyunani Huku Nyingine Kama Athenia Zikiwa na Demokrasia Ya Viwango Vya Juu Sana. Hali Kadhalika Kwa Wachagga Kutokea Kwenye Mitaa Kuelekea Kwenye Himaya Kulikuwa na Vita Nyingi Sana za Wenyewe Kwa Wenyewe na Nyingi Zilipiganwa Kwa Ushirika na Kuungana. Baadaye Mapigano Yalikuja Kuwa Makubwa Zaidi Baina Ya Himaya na Muungano wa Himaya, Kwa Mfano Vunjo Iliwahi Kuungana na Keni Rombo Kwenda Kuvamia Maeneo Yaliyoko Upande wa Mashariki Zaidi Ya Rombo Ya Mashati na Usseri. Old Moshi Waliungana na Uru, Mbokomu, Kirua, Kilema, Marangu, Mamba na Keni, Rombo Kwenda Kuivamia Usseri. Usseri, Rombo Iliwahi Kuungana na Kibosho Kwenda Kuivamia Mashati Rombo. Usseri, Rombo Iliwahi Kuungana na Old Moshi Kwenda Kuvamia Maeneo Ya Mrao, Kirwa na Mashati, Rombo. Kibosho Waliungana na Kirua, Kilema na Mamba Kwenda Kuivamia na Kuiangusha Old Moshi. Old Moshi waliungana na Marangu, Uru, Kilema, Kirua na Mamba Kwenda Kuivamia Kibosho, Old Moshi Pia Waliungana na Uru, Kilema na Kirua Kwenda Kuivamia Marangu na Kuikalia Kimabavu. Old Moshi Pia Waliungana na Marangu, Kilema, Kirua na Uru Kwenda Kuisaidia Machame Dhidi Ya Kibosho. Vita Hivi Baina Ya Wachagga Wenyewe Kwa Wenyewe Vilifanyika Lakini Hakuna Himaya Ambayo Ilifuta Utawala Kwenye Himaya Nyingine na Kuitawala Moja Kwa Moja Bali Iliendelea Kuikalia Kimabavu Huku Ikitoa Uhuru wa Himaya Husika Kufanya Siasa Zake za Ndani Kwa Uhuru Kama Ilivyokuwa Kwa Uyunani Ya Kale.

Uyunani Ya Kale Pia Ilipoteza Lugha Yao Ya Maandishi Iliyodumu Kwa Miaka Takriban 500 Kabla Ya Mwaka 800 KK Na Kuja Kutengeneza Lugha Nyingine Ya Maandishi Baadaye, Wachagga Nao Walikuja Kuendeleza Lugha Nyingine Ya Maandishi Mpaka Kufikia Karne Ya 19 Ambayo Haikuwa Imepiga Hatua Kubwa Kama Lugha Nyingine za Maandishi Zilizopita Karne Nyingi Nyuma.

Karibu Kwa Maoni, Maswali au Mchango Zaidi.

WACHAGGA KAMA WAYUNANI WA KALE
WACHAGGA KAMA WAYUNANI WA KALE
WACHAGGA KAMA WAYUNANI WA KALE
WACHAGGA KAMA WAYUNANI WA KALE
WACHAGGA KAMA WAYUNANI WA KALE

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *