UKRISTO ULIVYOINGIA KATIKA NCHI YA WACHAGGA NA MWANZO WA SHUGHULI ZA MISHENI KILIMANJARO.

UKRISTO ULIVYOINGIA KATIKA NCHI YA WACHAGGA NA MWANZO WA SHUGHULI ZA MISHENI KILIMANJARO.

Mpaka kufikia karne ya 19 wachagga hawakuwa wanafahamu chochote kuhusiana na ukristo wala biblia japo walikuwa na mfumo wa dini zao za asili ambazo baadhi ya mambo kama vile hadithi na taratibu za utoaji sadaka zilikuwa zinaendana na zile za agano la kale katika biblia. Hivyo ukristo ulikuja kuenezwa na wamisionari kutokea nchi za Ulaya ambako ukristo ilikuwa umeshadumu kwa zaidi ya miaka 1,000 na maeneo mpaka miaka 2,000.

Mwaka 1848 Johannes Rebmann aliyekuwa mmisionari wa kijerumani chini ya misheni ya Church Missionary Society (CMS) ya London, Uingereza akitokea Mombasa alikuwa ni mmisionari wa kwanza na mzungu wa kwanza kuitembelea nchi ya wachagga Kilimanjaro. Johannes Rebmann alifanya safari tatu Kilimanjaro akitokea Mombasa mwaka 1848 na 1849. Katika safari yake ya kwanza Kilimanjaro Rev. Johannes Rebmann alitembelea Kilema peke yake na kuonana na Mangi Masaki wa Kilema na kuzungumza naye mambo mengi hususan injili ya Yesu Kristo na habari za kwenye biblia. Katika safari yake ya pili na ya tatu Kilimanjaro Rev. Johannes Rebmann alitembelea Kilema na Machame na aliona na Mangi Mankinga wa Machame pia. Mwaka 1849 Johannes Rebmann alijaribu kumhubiria Mangi Mamkinga wa Machame injili ya Yesu Kristo na habari za mbinguni kama zinavyoelezwa kwenye biblia. Mangi Mamkinga hakumwelewa Johannes Rebmann wala hakuvutiwa na habari zake za injili ya kikristo. Baadaye mmisionari huyu wa kijerumani wa misheni ya (CMS) Rev. Johannes Rebmann aliporwa mali zake zote Machame, hivyo akaondoka Kilimanjaro kurudi Mombasa na hakuwahi kurudi tena Kilimanjaro.

Mwaka 1871 mmisionari wa muingereza kutokea London, Uingereza Rev. Charles New wa misheni ya (United Methodist Church Mission) alifika Kilimanjaro. Rev. Charles New alionana na Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi ambaye alimpa eneo la Kitimbirihu kwa ajili ya kuanzisha shule kwa ajili ya wachagga. Rev. Charles New alijaribu kupanda mlima Kilimanjaro na baada ya hapo alanzisha kituo kidogo cha shule katika eneo la Kitimbirihu, Old Moshi mwaka 1872 kisha kuondoka na kuelekea Mombasa. Mwaka 1873 mmisionari wa Kiingereza Charles New alirudi tena Kilimanjaro kwa ajili ya kupanda tena mlima Kilimanjaro sambamba na kuendeleza shule aliyoanzisha Kitimbirihu. Hata hivyo Rev. Charles New aliingia kwenye mgogoro na Mangi Rindi Mandara inasemekana kwa kutokulipa kodi aliyotakiwa na hivyo kujikuta akiporwa karibu mali zake zote na askari wa Mangi Rindi Mandara. Rev. Charles New aliondoka Kilimanjaro na kufariki njiani akiwa anaelekea Mombasa kwa hofu na uchovu kabla ya kufika Pwani.Mwaka 1878 Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi aliandika barua kwa misheni ya CMS ya London, Uingereza kupitia mawakala wake wa Taveta na kupitia kituo chao cha misheni kilichokuwepo Mombasa akihitaji walimu wa kuja kuendeleza shule ya Kitimbirihu kwa ajili ya kuwapatia elimu wachagga.

Mwezi Machi, Mwaka 1885 Bishop James Hannington aliyekuwa Askofu wa kwanza wa kanisa la Anglikana Afrika mashariki alifika Kilimanjaro kumtembelea Mangi Rindi Mandara. Bishop James Hannington alipita Kilimanjaro kwa ajili ya kufuatilia maendeleo ya kuanzishwa kwa kituo cha misheni Kilimanjaro na wamisionari wa (CMS) kisha alielekea Uganda ambapo miezi saba baadaye aliuawa na askari wa Kabaka Mutesa wa himaya ya Buganda. Hata hivyo Mangi Rindi Mandara alimweka wazi Bishop James Hannington kwamba yeye hahitaji wachagga kuhubiriwa injili ya kikristo wala kubatizwa bali anachohitaji ni kuanzishwa kwa shule itakayofundisha ufundi wa teknolojia za aina mbalimbali hususan utengenezaji wa bidhaa zenye ubora wa viwango vya zile zinazokuja kutokea Ulaya sambamba na masomo ya lugha yatakayorahisisha mahusiano ya kidiplomasia na nchi za ng’ambo.

Miezi michache baadaye mwezi Julai mwaka 1885 wamisionari wawili wa CMS Edmond Alexander Fitch na Joseph Alfred Wray walifika Kilimanjaro na kuanzisha kituo cha misheni katika eneo la Kitimbirihu, Old Moshi. Miaka miwili baadaye wamisionari wengine wawili William Ernest Taylor na William Morris waliungana nao katika misheni ya Kitimbirihu, Old Moshi. Hata hivyo Mangi Rindi Mandara aliendelea kuwazuia kueneza injili au itikadi nyingine ya tofauti na hata kubatiza wachagga na badala yake aliwataka walete walimu zaidi kwa ajili ya kufundisha.

Wamisionari hawa wa CMS katika kituo cha Kitimbirihu walianzisha shule na hospitali ambapo walianza kufundisha na hata kutoa huduma za afya kwa wachagga lakini hawakuweza kubatiza mchagga yeyote. Mwaka 1889 mmisionari mwingine wa CMS Albert Remington Steggall alifika Kilimanjaro akiwa daktari Dr. Baxter kwa ajili ya kuendeleza hospitali iliyoanzishwa na misheni ya Kitimbirihu ambao waliungana na wamisionari waliotangulia katika kituo cha CMS Kitimbirihu, Old Moshi wakiwa na vifaa zaidi kwa ajili ya kufundishia, kutibu na mikakati zaidi kwa ajili ya kuendeleza na kukuza kituo hicho cha misheni ya Kitimbirihu. Mwaka 1892 mmisionari mwingine wa CMS Arthur Wallace McGregor naye alifika Kilimanjaro na kuungana na wenzake katika kituo cha misheni ya Kitimbirihu.

Mmisionari Albert Remington Steggall alijifunza lugha ya kichagga na kuanza kutafsiri maandiko mbalimbali kwa kichagga kama vile kitabu cha nyimbo za injili na kitabu cha injili ya Matayo mtakatifu. Mangi Rindi Mandara alifariki mwezi Septemba mwaka 1891 nyumbani kwake Tsudunyi, Old Moshi na kiti chake cha utawala kurithiwa na mtoto wake Mangi Meli Mandara.

Askofu Alfred Tucker, aliyekuwa Askofu wa Anglikana Afrika mashariki siku ya tarehe 21 Februari 1892 aliwabatiza wachagga wawili ambao ni Tomasi Kitimbo Ringo na Samuel Nene Tenga katika misheni ya Kitimbirihu, Old Moshi. Wachagga hawa wawili waliobatizwa na Askofu Alfred Tucker mwaka 1892 walikuwa ndio wakristo wa kwanza Tanganyika nzima ukiondoa eneo la Pwani ya Bagamoyo.

Mwezi Agosti Mwaka 1890 wamisionari watatu wa Kifaransa wa kanisa katoliki wa shirika la Roho Mtakatifu (Holy Ghost Fathers) maarufu pia kama Spiritans walifika Kilimanjaro wakitokea Zanzibar kupitia Mombasa. Wamisionari hawa waliongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Afrika mashariki Father Raoul de Courmont akiwa sambamba na wasaidizi wake Father Alexander Le Roy na Father August Gommenginger. Wakiwa Mombasa walikutana na kijana Nderingo kutokea Kilema, Kilimanjaro aliyeungana nao katika safari yao ya kuelekea Kilimanjaro.

Kwa ushawishi wa Nderingo wamisionari hawa wa kifaransa walifikia katika himaya ya Kilema ambapo walionana na Mangi Fumba wa Kilema na kufanya naye mazungumzo na kuingia mkataba wa kuweka makazi Kilema. Wamisionari hawa walimwahidi Mangi Fumba wa Kilema kwamba wataanzisha kituo cha misheni Kilema. Kisha walielekea Old Moshi kuonana na Mangi Rindi Mandara na kutaka kuanzisha kituo cha misheni lakini walikuta tayari kuna wamisionari wa CMS ambao walishawataarifu kwamba watafute eneo jingine Kilimanjaro la kuanzia kwa sababu Old Moshi imeshachukuliwa na waprotestanti wa CMS. Wamisionari hawa wa kanisa katoliki waliondoka wakaelekea Machame ambapo waliweza kukutana na Mangi Ngamini wa Machame na kufanya naye mazungumzo. Mangi Ngamini aliwakaribisha Machame na kuwahimiza waanzishe kituo cha misheni ya kanisa katoliki Machame lakini kutokana na kukosekana kwa utulivu Machame katika kipindi hiki kwa sababu ya uhasama mkubwa na vita kati ya Kibosho na Machame wamisionari wa kanisa katoliki waliona hawawezi kuanzisha kituo cha misheni kwa wakati huo.Kisha wamisionari hawa wa kifaransa wa kanisa katoliki wa shirika la Holy Ghost Fathers walielekea Kibosho kuonana na Mangi Sina ambaye walifanya naye vikao kwa ajili ya kupata ruhusa ya kuanzisha kituo cha misheni ya kanisa katoliki Kibosho. Mangi Sina hakuonyesha dalili ya kutaka urafiki na wamisionari hao na alionekana kuwa mkali sana kwao, pia aliwaonyesha dalili ya vitisho ambavyo viliwafanya kujiona hawako salama Kibosho hivyo waliondoka na kuona kwamba mazingira ya kuanzisha misheni Kibosho bado ni magumu.

Wamisionari hawa wa kanisa katoliki walirudi Kilema na kwa mazingira hayo waliona Kilema ndio sehemu pekee watakayoweza kuanzisha misheni ya kwanza ya kanisa katoliki kwa kuanzia. Mangi Fumba wa Kilema aliwapa ardhi, ushirikiano na uhuru wa kituo cha misheni na taasisi nyingine. Wamisionari wawili Askofu Raoul de Courmont na Father Alexander Le Roy waliondoka Kilimanjaro na kumwacha Father August Gommenginger kwa ajili ya kuanzisha kituo cha kwanza cha misheni ya kanisa katoliki Kilema.Lakini kwa sababu kulikuwa bado hakuna msaidizi yeyote ilibidi Father August Gommenginger arudi Old Moshi akisubiri kutumiwa wasaidizi kutokea Zanzibar na Bagamoyo na kwa jili ya kuanzisha kituo cha misheni ya Kilema. Mwaka uliofuatia Father August Gommenginger alitumiwa wasaizi wengi akiwa Brother Blanchard sambamba na masista mbalimbali waliokuja Kilimanjaro na kusaidia katika ujenzi wa kituo cha misheni ya katoliki Kilema. Mwaka 1892 baada ya ujenzi kukalimilika kituo cha misheni ya Kilema kilifunguliwa rasmi.

Mwaka 1892 Father August Gommenginger alipanga kuelekea Kibosho kwa ajili ya kuanzisha kituo cha misheni ya kanisa katoliki Kibosho baada ya kujihakikishia kwamba Kibosho ni salama baada ya vita kati ya wajerumani na Kibosho vilivyopelekea Mangi Sina kusalimu amri kwa wajerumani. Lakini mwaka huo huo wa 1892 Mangi Meli Mandara wa Old Moshi naye alipigana vita na wajerumani na kuwashinda na kisha kuwafukuza Kilimanjaro. Hivyo Mangi Meli Mandara aliwafukuza wazungu wote waliokuwepo Kilimanjaro ikiwemo wamisionari wa kanisa katoliki walikuwepo Kilema ambao walilazimika kukimbilia Mombasa wakitelekeza kituo chao cha misheni ya Kilema. Baadaye mwaka 1893 wajerumani walirudi tena kupigana vita nyingine na Mangi Meli Mandara wakamshinda akasaliti amri kwa wajerumani na hivyo wamisionari wa kanisa katoliki wakarudi tena Kilimanjaro na moja kwa moja Father August Gommenginger akaenda kuanzisha kituo cha misheni ya kanisa katoliki Kibosho. Walipata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Mangi Sina na hivyo wakaanzisha kituo cha misheni ya pili ya kanisa Katoliki Kilimanjaro katika kijiji cha Singa. Baadaye mwaka 1894 baada ya kusimamisha kituo cha Kibosho kwa kushirikiana na wasaidiz wengi aliokuwa wametumiwa kutokea Pwani Father August Gommenginger aliondoka katika kituo cha misheni ya Kibosho na kumwachia Father Martin Rohmer aliyekuwa ametokea Bagamoyo kukuza na kukiendeleza kituo hicho na yeye kurudi katika kituo cha misheni ya Kilema.

Baadaye mwaka 1898 wamisionari wa kanisa katoliki wakiongozwa na Father Allegyer walianzisha kituo cha tatu cha misheni ya kanisa katoliki katika eneo la Mkuu, Rombo baada ya kupewa eneo la kuanzisha kituo hicho cha misheni na Mangi Kinabo wa Mkuu. Mangi Kinabo wa Mkuu, Rombo hakuvutana nao sana kwa sababu ya uzoefu ambao tayari walikuwa nao kutoka kwenye maeneo mengine. Baadaye misheni nyingine za kanisa katoliki ziliendelea kuanzishwa katika maeneo mengine ya Kilimanjaro.

Baada ya vita ya pili kati ya majeshi ya Mangi Meli Mandara na wajerumani, serikali ya wajerumani iliwafukuza wamisionari wa kutokea Uingereza CMS waliokuwa wameweka kituo cha misheni yao katika eneo la Kitimbirihu, Old Moshi kwa madai kwamba wanawahujumu wajerumani. Serikali ya wajerumani haikuwapenda wamisionari hawa kwa sababu walikuwa ni waingereza hivyo waliwatuhumu kwamba wanashirikiana na Mangi Meli kuwahujumu hivyo waliwafukuza na kuwaalika wamisionari wa kutoka Ujerumani kama wao. Wajerumani waliwaalika wamisionari wa kilutheri kutoka Leipzig, Ujerumani na mwaka 1893 Askofu Alfred Tucker wa CMS alikabidhi kituo cha misheni ya Kitimbirihu, Old Moshi kwa wamisionari wa kilutheri wa Leipzig Mission Society (LMS).

Mwishoni wa mwaka 1893 wamisionari wa kwanza wa misheni ya kiultheri ambao ni Traugott Passler, Albin Bohme, Emi Muller, Gerhard Althaus na Robert Fassman walifika katika kituo cha Kitimbirihu, Old Moshi walichorithi kutoka kwa CMS kwa ajili ya kuanzisha shughuli za misheni za kanisa la kilutheri. Lakini kutokana na kwamba mivutano na uhasama kati ya wajerumanina wachagga wa Old Moshi ilikuwa bado iko juu sana walishauri ni bora wakasubiri kwamba hasira ya wachagga Old Moshi ipoe kwani walikuwa wameshindwa vita ya pili na wajerumani mwaka huo huo na kuingia hasara kubwa hivyo bado wako kwenye simanzi ya hali ya juu.

Hivyo wamisionari wa kilutheri waliondoka katika kituo cha Kitimbirihu, Old Moshi na kuelekea upande wa magharibi na kuanzisha kituo kipya cha misheni cha Nkwarungo, Machame. Wakati huu Traugott Passler aliyekuwa amehudumu katika misheni huko India kwa muda mrefu tangu mwaka 1875 ndiye alikuwa kiongozi wao. Traugott Passler alimruhusu Albin Bohme kurudi Ujerumani mwaka ulifuatia wa 1894 kutokana na afya yake kudhoofika sana. Emil Muller alibaki kwenye kituo cha misheni ya kilutheri ya Nkwarungo, Machame mpaka mwaka 1920. Mwaka 1920 aliondoka kurudi Ujerumani kisha alirudi tena mwaka 1931 na kukaa kwenye misheni ya Nkwarungo kwa miaka miwili tena.Mmisionari Gerhard Althaus wa kanisa la kilutheri aliyekuwa mkubwa zaidi katika wasaidizi wa mwanzo wa Leipzig Mission Society(LMS) alianzisha kituo cha misheni ya kanisa la kilutheri Mamba katika eneo la Ashira mwaka 1894 na alidumu hapo kwa kipindi cha miaka kumi na sita mpaka mwaka 1910. Mwaka 1896 Robert Fassman alirudi Old Moshi na kuanzisha kituo cha misheni ya kanisa la kilutheri Old Moshi katika eneo la Kidia mwaka 1896 ambapo alidumu kwa miaka 14 mpaka mwaka 1910.

Wamisionari wengine wa mwanzo wa kanisa la kilutheri walioendelea kuja katika miaka iliyofuata ni pamoja na Johannes Raum aliyekuja Kilimanjaro mwaka 1895 akahudumu katika misheni za Machame, kisha akaanzisha misheni ya Siha mwaka 1898 akishirikiana na Emil Muller, baadaye akaenda kuhudumu Ashira, Mamba na Kidia, Old Moshi pia, Johannes Raum alihuduma misheni mapak alipofariki mwaka 1936. Johannes Schanz alikuja Kilimanjaro mwaka 1901 na kuhuduma katika misheni mbalimbali zikiwemo misheni ya Mbokomu na Kidia, Old Moshi mpaka mwaka 1912. Julius Augustiny alifika mwaka 1907 na kuhudumu mpaka 1912 na Sista Elizabeth Warhl alifika mwaka 1914 na kuhudumu mpaka mwaka 1938.

Dr. Bruno Guttman ni mmsionari mwingine aliyeacha alama kubwa kuliko wamisionari wote katika nchi ya wachagga Kilimanjaro. Bruno Guttman alifika Kilimanjaro akitokea Ujerumani kama mmisionari wa misheni ya kilutheri mwaka 1902 na kuhudumu katika misheni ya kilutheri Ashira, Mamba kwa kipindi cha miaka miwili. Kisha alihamia katika kituo cha misheni ya kilutheri ya Nkwarungo, Machame kwa kipindi cha miaka miwili mpaka mwaka 1906 alipoenda kuanzisha kituo cha misheni ya kilutheri Masama. Dr. Bruno Guttman alianzisha na kutumika katika kituo cha misheni ya kilutheri Masama kwa kipindi cha miaka mitatu tangu mwaka 1906 mpaka mwaka 1909 kisha alirudi nyumbani Ujerumani.

Dr. Bruno Guttmann alirudi Kilimanjaro katika misheni ya Masama mwaka 1906 kisha kuondoka Masama na kwenda na kuanza kuhudumu kama mkuu wa kituo katika kituo cha misheni ya Kidia, Old Moshi tangu mwaka 1910. Akiwa anahudumu katika kituo cha misheni ya Kidia, Old Moshi Dr. Bruno Gutmann alifanya kazi kubwa sana ya kuandika kazi nyingi sana kuhusu wachagga katika tasnia mbalimbali. Dr. Bruno Gutmann aliandika jumla ya vitabu 25 na makala 476 ya mambo mbalimbali kuhusu wachagga ambapo vitabu kama vinne juu ya hayo vilikuwa na zaidi ya kurasa 1,000 ikiwemo kutafsiri biblia ya agano jipya lote kwa kichagga.

Hivyo kuanzia hapo ukristo ulianza kushika kasi katika nchi ya wachagga na kubadilisha mambo mengi na mitazamo mingi ya asili iliyokuwepo. Hata hivyo bado kutokana uzito wa masula ya kiimani na kiroho bado hakiuwa rahisi kuondoa kabisa imani za asili zilizokuwepo kwa haraka kwani ziliendelea kuwa na nguvu huku zikiendelea kufanyika sambamba na imani za kikristo. Hata sasa bado zipo japo kwa kiasi kidogo sana lakini vizazi vimeendelea kurithisha japo ni kwa kufanya sambamba na dini zilizopo.

Ahsanteni.

Karibu kwa Maoni, Ushauri au Maswali.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *