HADITHI ZA DINI YA ASILI YA WACHAGGA KABLA YA KUJA KWA WAMISIONARI WA KIKRISTO – 5

UKUU WA RUWA/IRUWA.

Tumeweza kuona kwamba hadithi ya kwanza katika mfululizo huu wa hadithi za zamani za wachagga inafanana sana na hadithi ya kwenye biblia ya anguko la kwanza la mwanadamu kwenye bustani ya Edeni. Halafu hadithi ya pili inafanana sana na hadithi ya Kaini na Habili.

Kisha tumeona hadithi iliyofuata ya kuangamizwa kwa dunia kwa mara ya pili ni hadithi inayofanana kabisa na hadithi ya gharika ya Nuhu katika biblia. Hivyo dunia kwa mara ya kwanza iliangamizwa kwa lile jitu kubwa lililoitwa Rumu lakini kwa mara ya pili imeangimizwa kwa gharika ya maji moja kwa moja.

Hadithi hizi zinaonekana kuwa na utofauti kidogo na zile za kwenye biblia ambapo zimekaa kuendana zaidi na mazingira ya wachagga. Lakini hata hivyo zina muundo na ujumbe unaoendana kabisa na hadithi zile za kwenye dini za Ibrahim yaana ukristo, uislamu na uyahudi.

Hadithi hizi ziliandikwa na waandishi mbalimbali tangu karne ya 19 wakati dini ya kikristo ndio inaanza kuingia na zilikuwa zinafahamika vizuri na kwa usahihi sana kwa wachagga kabla hata ya wamisionari kuingia Kilimanjaro. Kuna baadhi ya maeneo ya Uchaggani ambapo dini ilichelewa kidogo kukubalika na baadhi ya watu na hadithi hizi ziliendelea kuhadithiwa katika uhalisia wake na wazee wa zamani zaidi.

Baadhi ya watu ambao walikuwa ni watoto wadogo katika miaka ya 1960’s, 1970’s waliweza kuhadithiwa hadithi hizi na bibi zao waliokuwa wazee waliozaliwa katika karne ya 19 hususan katika maeneo ambayo dini ya kikristo ilichelewa kukubalika kama vile Kibosho, Rombo n.k.,. Lakini baadaye dini ya kikristo kwa sehemu kubwa ilifuta hadithi hizi miongoni mwa wachagga kwa sababu ilikuja na hadithi zake zinazokaribiana zilizopata umaarufu zaidi na kusambaa hasa ukizingatia kwamba ndio zilizopo katika kitabu kitakatifu cha kikristo biblia.

Hivyo kitendo cha kwamba kuwa zilikuwa zinafahamika vizuri sana kabla ya kuingia kwa ukristo Uchaggani mwishoni mwa karne ya 19 inadhihirisha kwamba ni kweli zilikuwepo kabla Uchaggani na hazikuigwa kutoka kwenye biblia. Kwanza ni kwa sababu ya usahihi na upekee ambao hadithi hizi zinao na jinsi zinavyoendana na mazingira ya Uchaggani. Lakini pia ingekuwa zimeigwa kutoka kwenye biblia zisingekuwa zimechukuliwa kwenye agano la kale peke, ni dhahiri kwamba zingekuwa zimeiga mambo mengi zaidi kwenye agano jipya pia ambalo ndio limekaa kisasa zaidi.

MTAZAMO WA WACHAGGA KUHUSU RUWA.

Hadithi zilizojenga mtazamo wa wachagga kuhusu Ruwa zinaeleza kwamba wachagga wanaamini kwamba Ruwa ni Mungu mkuu na mpole, ambaye haendani kabisa na hasira wala uovu.

RUWA/IRUWA ANAELEZEWA NA WACHAGGA KUWA NA SIFA ZIFUATAZO.

Ruwa ana nguvu ya kufanya kila kitu. Ruwa habadiliki, kwani Ruwa ni yule yule jana, leo na kesho. Ruwa hadanganyi na mara zote anatekeleza neno lake. Mtu yeyote anapofanya uovu hata kama ni usiku Ruwa anamwona.

Hata Mangi na majeshi yake wanaweza kumzunguka mtu mmoja wakiwa na silaha zote, lakini kama Ruwa hajaruhusu hawawezi kumuua. Hata mtu anapoumwa na kwenda kwa madaktari na waganga wote na kufanya tambiko za aina zote hawezi kupona kama Ruwa hajaruhusu uponyaji wake. Lakini Ruwa huruhusu mizimu hiyo kumtibu mtu huyo na kupona. Mizimu ni wasaidizi wa Ruwa ambao hutumwa na Ruwa kufanya kazi yao kwa niaba ya Ruwa.

Wachagga pia walikuwa wakiwafundisha watoto wao kwamba: Mtoto anapotumwa na wazazi wake halafu akakataa, au mtoto anayegombana na wazazi wake na kubishana nao au kuwagomea au ambaye anafanya maovu kama kuiba na kupelekea mali za wazazi wake kuchukuliwa na watu aliowaibia, mtoto huyo anakuwa amekataliwa na Ruwa na hivyo atakufa kabla hajafikia kuoa.

Pia mtu ambaye ni mwizi anayeiba sana mali za watu, hawezi kujificha kwani Ruwa anamuona na iko siku atamfikisha kwenye baraza la mahakimu ambao watamwadhibu. Mtu pia ambaye ni mhaini(adui wa nchi) ambaye anaita maadui kuivamia nchi yake, ni mtu ambaye amekataliwa na Ruwa na mtu huyo atakufa yeye na ukoo wake wote kwani Ruwa atawaangamiza wote katika ardhi yao.

Ruwa pia anawajali maskini na yatima. Kama mtu anafanya mambo mema bila kubughudhi mtu yeyote, mtu ambaye haibi bali anakula kile kinachotokana na kazi ya mikono yake na ambaye anawaheshimu na kuwajali wazee wake, Ruwa atamfurahia na kumbariki kwa ng’ombe, mbuzi na watoto.Wachagga waliamini kwamba unapoona nyumba au familia imejaa huzuni, basi utakuta kuna uovu na uzembe mwingi ulifanywa na wahusika na zaidi ulifanywa na watangulizi wao au mababu zao na hivyo Ruwa ametuma roho/mizimu kwenye familia hii kuitaabisha. Kwa hivyo wachagga waliwaambia watoto wao, “mwanangu ogopa uovu, fanya mambo mema na bidii kubwa kwenye maisha na Ruwa atakufurahia na kukutumia baraka tele.

Wazee wachagga waliwafundisha haya watoto wao katika nyakati za mchana wa jua kali na watoto waliofundishwa walinyoosha kidole juu mawinguni na kutema mate mara tatu.Hivyo ndivyo wachagga walimtukuza Ruwa. Lakini wachagga waliiogopa na kuitii mizimu kuliko hata Ruwa na walipoulizwa kwa nini wanaonekana kuiogopa na kuitii mizimu/roho kuliko Ruwa, walijibu kwamba, “Kwa mfano Mangi/Mtawala ametuma mjumbe wake aje kuchukua kodi kwako na siku hiyo ukawa huna kabisa kitu cha kumpa, ni nani utakayejaribu kumshawishi au kumridhisha, ni Mangi/Mtawala au mjumbe wake aliyetumwa ambaye ataenda kukuzungumzia vizuri kwa Mangi ambaye atakuonea huruma?”

“Kama utaiongelea vibaya mizimu/roho zilizotumwa na Ruwa kwako, au ukakataa kuzitolea sadaka ambayo imeamuliwa kwa kufuata utaratibu mtakatifu, mzimu/roho huyo atarudi kwa Ruwa na kukushtakia vibaya ambapo Ruwa atapata hasira kali juu yako na kukutumia mzimu/roho wa kigeni asiyetokana na babu zako ambaye atakutaabisha na kukutesa sana na mwisho kukuua kabisa.”Wachagga wakasema. “Kwa sababu hii ndio maana tunaheshimu zaidi mizimu/roho.”

Tumeona kwamba kwa mtazamo wa wachagga Ruwa ni mzuri, Ruwa ndiye mwenye enzi na mamlaka yote, na ndiye anayeongoza na kuamua maisha ya mtu japo ni kwa kutumia watu au wasaidizi wake. Wachagga waliamini kwamba mizimi/roho ni wasaidizi wa Ruwa na kwa sababu mara nyingi walikuwa ni watu wa karibu wa ukoo hao ndio ambao wachagga walijishughulisha nao zaidi na mara nyingi sana huku Ruwa wakijishughulisha naye mara chache sana.

Wachagga wanasema, “Ruwa ndiye mtawala Mkuu, ambaye watu hawajishughulishi naye sana kama jinsi wanavyojishughulisha na wasaidizi wake wa karibu ambao ni mizimu/roho, kwani wao mizimu/roho kama wajumbe wa Ruwa ndio ambao wana madhara makubwa zaidi kwa wachagga kuliko Ruwa ambaye ni mpole na asiyependa uovu wala hasira”.

Ahsanteni.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *