UFANANO WA MAJINA YA WATAWALA WA UCHAGGA KILIMANJARO. – 3

SEHEMU YA 3.

15. SIRIA.

(i) Siria wa Siha/Sanya Juu alikuwa ni mtawala wa ukoo wa Kileo katika kijiji cha Samake(Samaki Maini) Siha/Sanya Juu akiwa ni mtoto wa Iranja aliyeishi katika miaka ya 1760’s.

(ii) Siria wa Uru alikuwa ni Mangi wa himaya ndogo ya umangi Shimbwe katika himaya ya Uru. Siria akiwa ni mtoto wa Mangi Molonyi wa himaya ya umangi Uru aliyerithi kiti cha utawala wa himaya hiyo kutoka kwa baba yake Molonyi lakini baada ya kugawana na kaka yake Mangi Msengo ambaye alitawala upande wa magharibi ya Uru huku Mangi Siria akitawala eneo la katikati la Shimbwe, Uru.

(iii) Siria wa Old Moshi alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Old Moshi katika miaka ya 1700’s. Siria alikuwa ni mtoto wa Mangi Saliko na mjukuu wa Mangi Sunsa wa himaya ya umangi Old Moshi. Mangi Siria wa Old Moshi alijiimarisha sana kwenye kiti cha utawala wa himaya ya Old Moshi na baada ya kufariki alimwachia kiti cha utawala mtoto wake aliyekuja kuwa maarufu zaidi kama Mangi Ndetia ambaye ndiye baba yake Mangi Rindi Mandara Mashuhuri.

16. MREMI.

(i) Mremi wa Uru alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Uru katika miaka ya 1700’s. Mangi Mremi wa Uru akiwa ni mtoto wa Mangi Warsingi alifanikiwa kukalia kiti cha umangi wa Uru baada ya kumfanyia fitina kwa Mangi Rengua wa Machame, kaka yake aliyeitwa Molonyi ambaye ndiye alikuwa mrithi halali wa kiti cha umangi wa Uru baada ya baba yao Mangi Warsingi. Hata hivyo kwa msaada kutoka kwa Mangi Siria wa Old Moshi Molonyi kaka yake alifanikiwa kurudi kwenye kiti cha umangi wa Uru lakini hali ya utawala ilizidi kuwa ngumu kutokana na mivutano hiyo ya kisiasa na hivyo Mremi kulazimika kukimbilia uhamishoni Mbokomu. Kutokana na fitna za kisiasa za wafuasi wa Mangi Mremi, Mangi Molonyi aliuawa na askari wa Mangi Mamkinga wa Machame kwa amri ya Mangi Mamkinga mwenyewe na hivyo Mangi Mremi kurudi kutawala sehemu mojawapo ya Uru kwa kipindi kirefu sana mpaka kifo chake, huku maeneo mengine yakitawaliwa na ndugu zake wengine Mawishe na Msengo.

(ii) Mremi wa Kilema alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Kilema katika miaka 1700’s. Akiwa ni mtoto wa Mangi Ngowi wa Marangu, Mremi alirithi kiti hicho kutoka kwa baba yake. Wakati Marangu ilipovamiwa kisha Ngowi na mtoto wake Mremi kukimbilia Kilema waliweza kupata utajiri wa kutosha kutokea Marangu walipokuwa wanatawala na kukimbilia Kilema ambapo Ngowi alifanikiwa kukalia kiti cha umangi wa Kilema. Hivyo baada ya utawala wake alimtawalisha mtoto wake mkubwa Mremi. Mangi Mremi aliitawala himaya ya umangi Kilema na kisha kumtawalisha mtoto wake aliyeitwa Nyange baba yake na Mangi Kombo ambaye pia ni babu yake na Mangi Mangi Rongoma Mashuhuri.

17. MAWALA.

(i) Mawala wa Kibosho alikuwa ni kiongozi wa ukoo wa Massawe wa Kibosho Umbwe katika miaka ya 1880’s. Mawala wa Kibosho wa ukoo wa Massawe alikuwa ni baba yake Rafaeli Massawe ambaye ni maarufu sana katika eneo la Kibosho Umbwe kwenye kituo maarufu cha daladala kinachojulikana mpaka leo kwa jina la “Kwa Rafaeli.”

(ii) Mawala wa Marangu alikuwa ni kiongozi msaidizi wa Mangi Ndegoruo Marealle wa Marangu katika miaka ya 1880’s/1890’s. Mawala wa Marangu alikuwa mjumbe mzuri wa Mangi Ndegoruo Marealle katika misheni mbalimbali za utawala uchaggani na alisaidia sana kumrahisishia shughuli za kiutawala Mangi Ndegoruo Marealle hasa katika eneo la Rombo. Mawala wa Marangu inasemekana kwamba alitokea katika himaya ya umangi Mwika kwenye ukoo wa Towo na kupewa eneo zuri la kuishi Marangu katika kijiji cha Samanga na Mangi Ndegoruo Marealle na kufanya kazi kama mjumbe wake aliyemwamini sana.

18. KIWARIA.

(i) Kiwaria wa Machame(Masama Roo), alikuwa ni kiongozi wa ukoo wa Swai Machame katika kijiji cha Roo katika miaka ya 1840’s. Kiwaria wa ukoo wa Swai alikuwa ni mtoto wa Nzengwa na baba yake Nsaiya.

(ii) Kiwaria wa Machame Foo alikuwa Mangi wa Machame katika miaka ya mwishoni mwa 1700’s. Mangi Kiwaria aliyemwandaa vizuri sana mtoto wake alikuwa ni baba yake Mangi Rengua wa Machame ambaye alikuja kujiimarisha sana na kuwa na nguvu kubwa sana kijeshi na kiutawala kufikia kutawala nusu ya Kilimanjaro na kuifanya Machame kuwa himaya yenye nguvu sana tangu mwanzoni mwa miaka ya 1800’s.

19. SALIA.

(i) Salia wa Old Moshi alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Old Moshi kwenye miaka ya 1850’s. Mangi Salia aliitawala Old Moshi inasemekana baada ya kusuka njama za kumuua kaka yake Mangi Ndetia ambaye ni baba yake Mangi Rindi Mandara. Hata hivyo Mangi Salia alikuja kupata ajali ya moto na kufariki na hivyo kiti cha utawala wa Old Moshi baadaye kuja kukaliwa na Rindi kwa msaada wa mama yake Mamchaki na mjomba wake Tukia ambao walikishikilia kwa muda kabla ya kumkabidhi Rindi aliyekuja kwa maarufu zaidi kama Mangi Rindi Mandara Mashuhuri.

(ii) Salia wa Mengwe, Rombo alikuwa ni mtoto wa Mangi Salema wa himaya ya umangi Mengwe, Rombo. Salia akiwa ni mtoto wa Mangi Salema alijaribu kugombea kukalia kiti cha umangi wa himaya ya umangi Keni-Mriti-Mengwe dhidi ya Mangi Wingia Ngache wa Mriti/Mamsera katika miaka ya 1950’s. Hata hivyo Salia licha ya kuwa ushawishi na kuweka ushindani mkubwa lakini hakufanikiwa kumshinda Wingia Ngache kwenye nafasi hiyo ya umangi wa Keni-Mriti-Mengwe iliyokuwa imeachwa wazi na Mangi Herman Tengia aliyekuwa ameondolewa.

20. KIRENGA.

(i) Kirenga wa Marangu alikuwa ni mtawala wa ukoo wa Mboro, Marangu katika kijiji cha Sembeti/Lyamrakana katika miaka ya 1720’s. Kirenga ndiye mtawala wa ukoo wa Mboro aliyekuwa amechukua hatamu ya uongozi baada ya kushindwa vita na ukoo wa Lyimo na kuondolewa Lyamrakana kwa nguvu.

(ii) Kirenga wa Kibosho alikuwa ni Mangi wa Kibosho mwanzoni mwa miaka ya 1800’s. Kirenga alikuwa ni mtoto wa Mangi Kashenge ambaye alirithi kiti cha umangi wa Kibosho kwa nguvu wakati baba yake akiwa bado yuko hai. Mangi Kashenge alishirikiana na mtoto wake mwingine aliyeitwa Tatuo ili kumwondoa Mangi Kirenga madarakani na kumtawalisha Tatuo. Maamuzi haya ya Mangi Kashenge baba yao yalipelekea vita kubwa na mbaya sana Kibosho ya wenyewe kwa wenyewe, lakini hata hivyo mwishoni vita ilikuja kuisha na Tatuo kukalia kiti cha umangi wa Kibosho na kutawala.

21. MRAISHE

(i) Mraishe wa Marangu alikuwa ni kiongozi wa ukoo wa Mongi wa Samanga, Marangu katika miaka ya 1890’s. Mraishe alikuwa ni mtoto wa Mnanu na pia alikuwa ni baba yake Ngapanyi na babu yake Samanya wa ukoo wa Mongi wa Samanga, Marangu.

(ii) Mraishe wa Mbokomu alikuwa ni mzee wa huko Mbokomu anayefahamika kama mtu aliyeishi miaka mingi sana kufikia umri wa miaka 150. Mraishe wa Mbokomu alihojiwa mwaka 1926 na Charles Dundas ambaye anasema waliweza kufanya mahesabu ya umri wake kupitia rika na kugundua kwamba alikuwa amezaliwa katika miaka ya 1780’s na alikuwa bado yuko hai mpaka miaka ya 1930’s.

22. SUNSA.

(i) Sunsa wa Old Moshi alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Old Moshi katika kipindi cha mwanzoni mwa miaka ya 1700’s. Sunsa ambaye alikuwa ni mtoto wa Mangi Tarimo na pia alikuwa ni baba yake Mangi Saleko na babu yake Mangi Siria wa Old Moshi.

(ii) Sunsa wa Mwika walikuwa ni watawala wawili wa himaya ya umangi Mwika ambapo kulikuwa na Sunsa wa kwanza na Sunsa wa pili waliotawala katika kipindi cha mwishoni mwa miaka ya 1700’s. Sunsa wa kwanza ni mtoto wa Mangi Urio wakati Sunsa wa pili ni mtoto wa Mangi Sunsa wa kwanza. Kisha Mangi Sunsa wa pili ni baba yake na Mangi Kyasimba. Mangi Kyasimba aliyekuwa mtawala wa Mwika katika nyakati za Mangi Horombo wa Keni ndiye baba yao Mangi Mchau na Mangi Tengio na pia ndiye babu yao Mangi Mbararia wa Mwika na Mangi Ndemasi Solomon wa Mwika.

23. ITOSI.

(i) Itosi wa Marangu alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Marangu katika miaka ya mwanzoni mwa 1800 katika enzi za utawala wa Mangi Horombo. Mangi Itosi wa Marangu ambaye ni mume wa Msanya ndiye baba yao Mangi Kinabo wa Ndaalio wa Marangu, Mangi Kinabo wa Marangu na Mangi Marenga wa Marangu. Mangi Itosi wa Marangu pia ndiye babu yake Mangi Ndegoruo Marealle wa Marangu.

(ii) Petro Itosi wa Marangu alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Marangu tangu mwaka 1932 mpaka mwaka 1946. Mangi Petro Itosi pia alikuwa ni Mangi Mwitori wa jimbo la Vunjo, Uchagga akiwa ni mtoto wa mwisho wa Mangi Ndegoruo Marealle na moja kati ya wamangi waliokuwa na ushawishi mkubwa Kilimanjaro katika karne ya 20.

24. MASANJUA/MASANJUO.

(i) Masanjuo wa Marangu alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Marangu katika miaka ya 1760’s. Mangi Masanjuo akiwa ni mtoto wa Mangi Ngarawiti wa Marangu alisemekana kwamba hakuwa mrithi halali wa kiti cha umangi wa Marangu na hivyo aliondolewa na kuwekwa ndugu yake aliye Iwite kisha Mangi Masanjuo mwenyewe kukimbilia Mamba.

(ii) Masanjua wa Usseri, Rombo alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Usseri, Rombo katika miaka ya 1750’s. Mangi Masanjua wa Usseri, Rombo alikuwa ndiye baba yake Mangi Kafuria wa Usseri, Rombo aliyepambana na majeshi ya Mangi Horombo na kushindwa lakini hata hivyo baadaye ndiye aliyepelekea anguko la Horombo. Hivyo Mangi Masanjua wa Usseri, Rombo ndiye baba yake Mangi Kafuria na babu yake Mangi Malamia na Mangi Matolo wa Usseri, Rombo.

25. IRINGO.

(i) Iringo wa Old Moshi aliyejulikana kama Kaale Iringo ambaye yeye alizaliwa na ndugu yake aliyetwa Tuu pamoja na kaka yao ambaye ni Mangi Saliko, wote ni watoto wa Mangi Sunsa wa Old Moshi walioishi katika miaka ya mwanzoni ya 1800’s.

(ii) Iringo wa Kibosho alikuwa ni mtoto wa Mangi Orio na mjukuu wa Mangi Yansanya aliyeishi Kibosho katika miaka ya 1700’s. Iringo ni mjukuu wa Mangi Yansanya ambaye hakufanikiwa kurithi kiti cha utawala wa umangi wa Kibosho baada ya baba yake kujiuzulu.

MWISHO.

Ahsanteni.

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *