UKOO WA MMARI.

UKOO WA MMARI.

– Ukoo wa Mmari ukoo mkubwa wenye historia kubwa na uliotoa watu mashuhuri katika historia ya wachagga. Kutoka kwenye historia ukoo wa Mmari huenda chimbuko lake kwa uchaggani ni Siha/Sanya ambapo wanapatikana kwa wingi sana na umewahi kuwa ukoo wenye nguvu na uliotoa watawala imara sana wa himaya ya umangi Siha/Sanya Juu.

– Hata hivyo baadhi ya waandishi wanaamini kwamba ukoo wa Mmari wana asili ya Kibosho na kwamba ndio koo za mwanzo kabisa Kibosho. Waandishi hawa wanakwenda mbali zaidi na kusema kwamba hata mimea ya migomba Kibosho ililetwa na wachagga wa ukoo wa Mmari. Lakini mashaka ya jambi hili yanatokana na kutokuwepo kwa ukoo huu Kibosho au angalau sio ukoo mkubwa unaofahamika huko Kibosho.

– Ukoo wa Mmari wako kwa wingi sana Siha/Sanya Juu na Old Moshi zaidi kuliko sehemu nyingine yoyote ya uchagga. Pengine utafiti zaidi au taarifa zaidi zinahitajika kufahamu undani wa ukoo wa Mmari na namna unavyohusishwa na ukongwe wake Kibosho.

– Huko Siha/Sanya Juu ukoo wa Mmari ulikuwa ndio ukoo unaotoa wanajeshi wapiganaji hodari zaidi katika vita na majemedari wengi mashuhuri walitokea ukoo huu wa Mmari. Hata mtawala wa kwanza mwenye nguvu na shupavu aliyeweza kuendesha vita ndani na nje ya Siha aliitwa Mangi Saiye kutoka kwenye ukoo wa Mmari. Ushupavu na msimamo wa ukoo huu wa Mmari uliendelea kudhihirika kupitia mtawala mwingine mwenye nguvu sana wa Siha aliyeitwa Mangi Ngalami ambaye alisimama imara sana dhidi ya serikali ya wajerumani kiasi kwamba alikuwa ni mmoja ya watawala wa Uchagga walionyongwa pale Old Moshi, Tsudunyi mwaka 1900 yeye pamoja na kaka yake, sambamba na Mangi Meli Mandara na Mangi Molelia wa Kibosho.

– Huko Sanya Juu ukoo wa Mmari uliendelea kuwa na nguvu sana katika eneo kubwa na kutoa watu waliopata ushawishi mkubwa kwenye kiti cha utawala kama vile Naruru, Barba na Kitika. Kwa hakika kama siasa za Siha zisingeingiliwa na siasa zenye nguvu za ushawishi kutoka nje ya Siha hususan Machame ni wazi kwamba ukoo wa Mmari ambao walikuwa na idadi kubwa sana ya watu pia wangekalia kiti cha utawala moja kwa moja na kuwapika Orio, Kileo na hata Mwandri.

– Ukoo wa Mmari unapatikana kwa wingi sana pia Old Moshi na kuna uwezekano kwamba tawi lilitokea Sanya juu na kuhamia Old Moshi au kinyume chake. Huko Old Moshi pia ukoo wa Mmari ni wakongwe na wanaoheshimika. Hata hivyo bado hatujui sana ni lini na kwa namna gani ukoo huu ulipata matawi yake. Au pengine ni kweli chimbuko lake ni Kibosho na kuna namna walisambaa maeneo mengine wakianzia Kibosho.

– Tunaomba mchango wa mawazo kutoka kwa wahusika na wengine wenye uelewa zaidi kuhusu ukoo mashuhuri wa Mmari. Pia kama kijijini kwenu kuna ukoo wa Mmari unaweza kukitaja hapa tuweze kufahamu matawi zaidi ya ukoo wa Mmari yalivyokwenda.

1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Mmari?

2. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Mmari?

3. Kama wewe ni wa ukoo wa Mmari una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu? Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani?

4. Bado mna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo huo kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?

5. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Mmari?

Karibuni sana kwa Mchango zaidi au Maswali.

Kesho tutaendelea na ukoo mwingine.

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *