NAMNA PEKEE YA KUEPUKA UKUU WA KITAMADUNI WA KIGENI (FOREIGN CULTURAL SUPERIORITY) NI KURUDI KWENYE JAMII/MAKABILA YETU.

– Kumeendelea kuwa na mwamko wa baadhi ya watu na jamii mbalimbali duniani ambao wameendelea kuamka na kujitambua kwa kufahamu kule tulikotoka na kugundua kwamba mifumo yetu karibu yote tuliyonayo ya kijamii, kiuchumi na hata kisiasa ni ya kigeni. Jambo hili limekuwa likiwakereketa baadhi ya watu wenye kujali kuhusu vile tunavyotazamwa na wale ambao tumeazima tamaduni zao na mambo yao yote na sasa tunayatumia.

– Wakereketwa hawa kama vile dada yangu Nkasafari Mashio na wengineo ambao wanaendelea kuongezeka kila siku Afrika na duniani kwa ujumla wanaona ni jambo la aibu na kujidharaulisha sana kwa sisi kuendelea kutumia mifumo hiyo kana kwamba sisi wenyewe hatuna akili za kutosha kufikiria kufanya mambo hayo kwa namna zetu na fikra zetu wenyewe. Hili linawaongezea hasira zaidi kwa kugundua kwamba wale ambao tumeazima tamaduni zao wanaonekana ni wakuu kwetu(superiors) na siku zote tutabaki kuwa chini yao(inferiors) kwani tunatumia vya kwao na tumepuuza vya kwetu, kwa sababu haiwezekani kujivunia na vitu vya watu wakati wenyewe wapo na wanatuangalia.

– Lakini changamoto kubwa iliyopo katika eneo hili la watu kuchukia vya wageni au kama ilivyozoeleka zaidi kuitwa ukoloni ni kuingia kwa unafki na utapeli wa wanasiasa, hususan wanasiasa mademagogi(demagogue politicians). Wanasiasa mademagogi ni wale wanasiasa ambao hutafuta umaarufu wa kisiasa kupitia kuteka hisia za watu, kwa mfano mwanasiasa kujifanya anapenda sana dini ili watu wa imani wamwone ni mcha Mungu na kumpenda kwa sababu hiyo wakati yale mambo muhimu ya kiserikali yanayomhusu anaboronga. Au mwanasiasa kujifanya ameletwa na Mungu au kujifanya anawapenda sana wananchi na kuwaonea huruma wakati huo huo pengine anavunja katiba ya nchi au kuumiza sana watu wengine wasiokuwa na hatia.

– Wanasiasa mademagogi wameingilia sana eneo hili la kujifanya wanachukia mambo ya kigeni kama wanavyoita wenyewe ukoloni au ubeberu lakini tatizo ni kwamba hawana nia yoyote ya dhati ya kufanya jambo lolote dhidi ya agenda hiyo wanayoizungumza zaidi ya ubabaishaji na hadaa bali nia yao ni kuteka hisia za watu peke yake ili waonekane ni wazalendo na kupendwa na watu kisha kutumia umaarufu huo wa kisiasa kufanikisha mambo yao mengine.

– Kwa sababu ukweli ni kwamba hao wanasiasa wanaojifanya kuchukia ukoloni/ubeberu ndio wanufaika wa kwanza wa mifumo ya ukoloni au ubeberu kwani hata nchi yenyewe tu wanayoiongoza imetengenezwa na hao wakoloni/mabeberu na mifumo yote inayotumika imewekwa na hao mabeberu na haijawahi kubadilishwa. Kwa mfano baada ya Waingereza kukabidhi madaraka ya serikali ya Tanganyika kwa chama cha TANU mwaka 1961 na kuondoka bado inakuwa ni unafki mkubwa kwa mwanasiasa kama Julius Nyerere kukwambia anachukia ukoloni kwani ukoloni haujaondoka bali wale waliouleta ndio wameondoka. Hii ni kwa sababu yeye mwenyewe Julius Nyerere ameendeleza mifumo hiyo hiyo ya kikoloni kwa maslahi yake binafsi tena bila hata kujihangaisha kuiboresha kwa maslahi ya wananchi, lakini anatumia kauli nyepesi kama hizo kukuhadaa wewe umwone ni mzalendo anayepambana na ukoloni. Hii ni kwa sababu anajua kwamba ni watu wachache sana wenye uwezo wa kufikiri kwa kina vya kutosha kuona unafki huo wa kisiasa ambao umelenga zaidi kuhadaa watu. Huwezi kusema unachukia ukoloni wa waingereza wakati bado unaipa kipaumbele lugha ya kiingereza ambayo ni sehemu ya ukoloni wenyewe. Mtu anayechukia uislam sio rahisi umkute amevaa kanzu, au angalau hawezi kuipitisha kanzu kama vazi rasmi eneo lolote lile. Vinginevyo mtu huyo ni mnafki.

Cambridge-Trained African Chief — Chief Thomas Marealle of the Chagga Tribe: The traditional Chagga horn which saluted the new chief during during the ceremony. January 28, 1955. (Photo by Central Office of Information Photograph).

– Mifumo yote tunayotumia kuanzia ya kielimu, dini, serikali, siasa, majina yetu, sheria zetu, namna za kufikiri, lugha tunazotumia, maandishi tunayotumia, uvaaji wetu na karibu kila kitu ni vya kigeni. Yaani hata namna za kufikiri kwetu ni za kigeni ndio maana tunadharau vya kwetu, hivyo ukuu wa kitamaduni wa kigeni (foreign cultural superiority) hauepukiki kiurahisi. Kwa hiyo mwanasiasa anayetumia kauli nyepesi za kujifanya anachukia mambo ya magharibi au ukoloni na ubeberu anakuhadaa tu kuteka hisia zako za kuchukia mambo ya kigeni ili umhesabu kama ni mzalendo na anapigania mambo ya kwetu dhidi ya hayo ya kigeni.- Swali linalokuja ni je, tunafanyaje kuachana na mifumo ya kikoloni ambayo inakuwa kama inatudhalilisha mbele za wale walioileta, ambapo wao wanaendelea kuwa “superior” kwetu kwa sababu ni kama tumekodi akili zao na fikra zao na ndio tunazotumia badala ya kutumia akili zetu?

– Kwanza jambo la muhimu ni kufahamu kwamba sio rahisi na sio lazima kuachana na kila kitu kwa sababu kuna mawazo mengine yako dunia nzima na chanzo chake ni eneo moja tu, ambao zaidi ni Ulaya na Marekani. Lakini hata hivyo bado tuna nafasi ya kupunguza sana mambo ya kuletwa na kubaki zaidi na mambo yetu, jambo ambalo litatuongezea heshima kubwa na kujiamini zaidi mbele za watu wengi duniani. Tunaweza kupunguza sana mambo ya kigeni na kubaki na machache sana ambayo hayaepukiki au hakuna urahisi wa kuyaondoa moja kwa moja.

– Kuondokana au kupunguza mambo mengi ya kuletwa ambayo ni kama kutukuza utamaduni wa kigeni dhidi ya ule wa kwetu sio tu ni jambo linalowezekana bali maeneo mengi sana duniani yamefanya hivyo. Kwa mfano nchi nyingi Afrika zinatumia kiingereza kama lugha rasmi au lugha ya mawasiliano lakini ukienda Ulaya ni Uingereza peke yake labda na nchi nyingine chache sana ndizo zinazotumia kiingereza nchi nyingine zote za Ulaya zinatumia lugha zao za asili na sio kiingereza au kifaransa kama jinsi ilivyo kwa nchi nyingi Afrika.

– Hata hivyo ukweli ni kwamba Afrika hakuna nchi ambayo imetokea kwenye asili bali nchi zilizopo zilikuwa ni makoloni yaliyotengenezwa na wazungu mwishoni mwa karne ya 19 na kisha baadaye katikati ya karne ya 20 yakapewa uhuru na kugeuka kuwa nchi. Lakini nchi hizi ambazo ndani yake kuna jamii mbalimbali zinazostahili kuitwa nchi hazina msingi wowote wa pamoja kiutamaduni badala yake ni kama jamii zilizolazimishwa kukaa pamoja bila kuelewa ni kitu gani kinawaunganisha. Kisha wale watu waliokabidhiwa madaraka kipindi kile hichi hizi zinapewa kile kilichoitwa ni uhuru, kwa sababu zao binafsi wakaamua kuendeleza staili ya ukoloni kwa sababu ndio namna pekee inayowezekana na hivyo kuyaita makoloni hayo ni nchi japo hazina kitu chochote cha asili kinachoziunganisha.

– Hapo sasa ndipo ugumu unapokuja wa nchi hizo kushindwa kusimama katika misingi yake ya asili kama nchi moja kwa sababu haipo na haiwezi kuja kwa sababu tayari kuna mifumo ya kigeni. Hivyo hata ukisema unajivunia nchi yako, bado unakuwa unamtukuza Mzungu kwani hiyo nchi yako aliyeitengeneza ni Mzungu ikiwa kama koloni na kuijengea misingi na kuiwekea mifumo kisha baadaye akaamua kuiachia ikawa kama nchi huru. Hivyo kabla hujajivunia nchi yako inakuwa ni sahihi zaidi umshukuru kwanza Mjerumani kwa kuitengeneza nchi yako hiyo kisha ndio useme unajivunia. Hili ni jambo linaloleta ukakasi kwa wale wanaojali sana juu ya ukuu wa wazungu kwetu, ambao unaambatana na kubezwa na kudharauliwa.

– Swali lingine linalokuja ni kwamba ni nini sasa kinaweza kufanyika ikiwa nchi zenyewe zilizotoka kwenye makoloni ndani yake kuna jamii nyingi ambazo hazina msingi wa pamoja na ambapo hatuwezi kuondokana na (cultural superiority) ndani ya nchi ambazo zilikuwa ni makoloni ya wazungu? Je kila jamii ijitoe na kuunda nchi yake ili isimame katika misingi yake ili kuhakikisha tamaduni za wenyeji zinapewa kipaumbele?

– Kwanza kabisa hilo sio jambo rahisi kwa sababu kwanza utazalisha kosa la uhaini ambalo ni kati ya makosa makubwa sana katika nchi na pili hutaweza kwa sababu huwezi kushindana na serikali ambayo sio rahisi kukubaliana na jambo hilo. Eneo kama Biafra huko Nigeria la kabila la Igbo liliwahi kujaribu kupigana vita na serikali ya Nigeria mwishoni mwa miaka ya 1960’s ili kuwa nchi huru kutoka kwenye nchi ya Nigeria lakini hawakufanikiwa. Na maeneo mengine kadhaa pia wamejaribu hilo bila mafanikio. Hata wachagga wahafidhina walikuwa na mpango huo lakini ulikuja kuvurugika. Halafu sio lazima iwe hivyo kwa sababu kuna njia nyingi za kufanya kuhakikisha kila jamii inasimama kwenye misingi yake, na jambo hili limefanyika maeneo mengi duniani. Muhimu tu ni kutambua kwamba ukuu wa tamaduni za kiafrika dhidi ya zile za wageni utapatikana ndani ya makabila ya Afrika kwa sababu hakuna kitu chochote cha pamoja kinachoitwa Afrika nje ya makabila ya Afrika.

– Kila kitu cha kujivunia kuhusu Afrika au tamaduni za wenyeji dhidi ya zile za wageni kipo ndani ya makabila au jamii za kiafrika na sio sehemu nyingine yoyote ile. Kwa maana hiyo kauli kama “kilichobaki kwenye makabila ni kutambika tu” ni kauli ya kipuuzi na ya kinafki ambayo haijafikiriwa kwa usahihi iliyotolewa na mtu mwenye maslahi yake binafsi kwa lengo la kuhadaa watu na kuwapotosha huku ikishangiliwa na watu wasiotaka kuifikiria kwa kina.

– Sasa kwa sababu hatuna Afrika ya pamoja tukiendelea kujidanganya kwa kudhani kwamba tutaweza kukabiliana na (cultural superiority) ya wageni kwa kuitaja Afrika kwa pamoja au mojawapo ya nchi ambayo ilikuwa ni koloni la wazungu Afrika lililogeuzwa kuwa nchi katikati ya karne ya 20 kama vile Tanzania au Kenya tutaendelea kupoteza muda na kupoteza kabisa hata kile tunachoweza kuokoa sasa. Hivyo sasa ni lazima tufikirie katika mazingira haya tunafanya nini kukwepa fedheha ya kutegemea fikra za wageni kuendelea kutuongoza na badala yake kurudi kwenye vile vya kwetu kama walivyofanya wengine wanaojitambua duniani kama vile China, Korea, Vietnam, Cambodia, Uarabuni, Singapore, nchi karibu zote za Ulaya n.k.,

– Hili linawezekana kwa nchi hizi za Afrika zilizoanzishwa na wazungu kama makoloni kuwa ni federations na kisha jamii mbalimbali kuwa kama majimbo ndani ya federal governments ambayo yana uhuru wa kutosha kuendeleza tamaduni zao huku mambo mengine machache muhimu ndio yakiwa yanasimamiwa na serikali kuu (federal government). Hata chama cha KCCU kilikuwa na wazo kama hili katika miaka ya 1950’s. Tofauti na hapo ni vigumu sana kupata namna nyingine ya kuziheshimisha tamaduni zetu ili kuweza kutetea utu na heshima yetu mbele za wale ambao ni kama wanatuchora vile ambavyo bado hatujaweza kuwa na akili za kutosha kufikiri na kuachana na tamaduni zao na kuanza kujitegemea kama walivyofanya wenzetu wengi duniani hususan katika nchi za mashariki ya mbali.

– Jambo hili sio geni kwani limefanyika katika nchi nyingi sana duniani na hakuna changamoto kubwa iliyotokea kama jinsi tunavyoaminishwa na wanasiasa wenye malengo na nia zao tofauti tofauti. Kwa mfano nchi ya Afrika Kusini ina lugha rasmi 13 na hata wimbo wa taifa unaweza kuimbwa kwa lugha zote 13. Nchi ya Ubelgiji ina lugha rasmi tatu ambazo ni Kifaransa, Kiholanzi na Kijerumani na zote zinatumika kama lugha rasmi ambapo kila kabila likitumia lugha yao na nchi ina utulivu na maendeleo. Nchi ya Bosnia & Herzegovina pia ina lugha rasmi tatu na hata ina maraisi watatu pia na inafanya vizuri kabisa bila kuharibu mipaka yake. Pamoja na tamaduni nyingine zote mbalimbali zinaendelea kufanywa kipekee na kila jamii kivyake. Hata Yuval Noah Harrari ameandika kwenye kitabu chake cha “Sapiens, A Brief History to Mankind” kwamba hakuwezi kuwa na shida yoyote kwa kila jamii kuishi tamaduni zake ikiwa kila mtu ataheshimu za mwenzake, kimsingi hiyo itaongeza zaidi chachu ya maendeleo kuliko kuipunguza.

– Hivyo ni muhimu sana kuepuka hadaa na uongo wa wanasiasa wanaosema Afrika ni moja kwa kauli za juu juu za kisiasa bila kuingia ndani zaidi na kuelewa nini hasa kinachopaswa kufanyika. Afrika sio moja kama jinsi Ulaya sio moja wala Asia sio moja, na hata Uarabuni pia sio moja. Ndio maana ni zaidi ya nusu karne imepita huku kauli hizo za kisiasa zikisemwa lakini hakuna mafanikio yoyote ya kuunganisha nchi hizi, zaidi tumeona nchi nyingine zikiendelea kuvunjika na kuunda nchi mpya. Afrika itakuwa imara kwa kuimarisha tamaduni za jamii moja moja au kabila moja moja ndani ya Afrika badala ya kuwa na (bogus thinking) ya kusema Afrika ni moja bila kufikiri kwani ambayo haiwezi kuingizwa kwenye utekelezaji hata kwa hatua moja.

– Kupambana na ukuu wa kitamaduni wa kigeni (cultural superiority) kama walivyofanya wenzetu wa nchi nyingi za nje ya Afrika kutawezekana kupitia kuhuisha tamaduni za jamii za kiafrika ambazo ni makabila ya Afrika. Tofauti na hivyo hatuna namna nyingine zaidi ya kufanya bali kuendelea kukaa chini ya ushawishi wa mawazo na mitazamo ya wageni hususan wazungu na mifumo yao katika kila nyanja ya maisha yetu.

Ahsanteni.

Karibu kwa Maoni.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *