UTARATIBU WA KUMILIKI ARDHI KATIKA NCHI YA WACHAGGA.

Katika desturi na kitamaduni nyumbani kwa mchagga ni katika nyumba yake ambayo ipo katikati ya shamba lake la urithi(kihamba). Mchagga bila nyumbani katika kihamba chake ni sawa na samaki nje ya maji. Hili lilikuwa dhahiri zaidi hasa katika miaka ya zamani. Mchagga pia alikuwa na ardhi kwa ajili ya kilimo cha maharage, viazi katika mashamba ya mgombani na pia shamba la mahindi kule chini porini kwenye tambarare.

Hasa zaidi katika miaka ya zamani wakati kila ukoo ulipokuwa ukiishi katika eneo lao fulani kwa ajili ya ukoo husika ardhi ilikuwa ni mali ya ukoo na maeneo ya ukoo husika yaligawanywa na kiongozi mkuu wa ukoo. Lakini hata mpaka baadaye na kwa kiasi mpaka sasa ardhi ya eneo ni mali ya ukoo na hata Mangi hakuweza kugawa ardhi hiyo moja kwa moja kwa mgeni asiye wa eneo hilo. Ikiwa mgeni anaomba eneo la kuishi na hivyo kuhitaji ardhi Mangi alimwagiza kutuma maombi kwenye ukoo wa eneo husika analotaka kuishi kisha aliingizwa kwenye ukoo huo na kupatiwa ardhi ambayo ni ya ukoo husika.

Baadaye ardhi yote ya eneo ilikuja kuwa chini ya mamlaka ya Mangi ambaye alikuwa na mamlaka ya kugawa ardhi sio tu ile isiyotumika lakini hata ile ambayo haitumiki, iliyotelekezwa na hata nyumbani kwa mtu kwenye migomba kabisa lakini kumetelekezwa, na hata kuwahimiza wamiliki ambao hawana matumizi na ardhi yao kuikabidhi kwa Mangi. Hii iliweza kusaidia Mangi kugawa ardhi kwa watu wasiokuwa na ardhi kwenye maeneo ambayo yametelekezwa au kuachwa bila kutumika.

Hata hivyo mara nyingi Mangi hakuweza kugawa ardhi ya mtu hivi hivi moja kwa moja bila ridhaa ya mhusika na wakati mwingine hilo likitokea mhusika huweza kudai kurudishiwa ardhi yake na hilo likatekelezwa kwa kufuata utaratibu uliopangwa baada ya yule aliyepewa kupatiwa eneo jingine na kuhama. Gharama alizolipa yule aliyehitaji ardhi zilienda kwa Mangi ikiwa ardhi hiyo haikuwa chini ya umiliki wa mtu yeyote au kununuliwa moja kwa moja kutoka kwa mmiliki ambaye ni wa ukoo husika ambaye mhusika ameomba kuingia.

Kama ardhi hiyo ilikuwa na nyumba ya makazi ya mhusika basi gharama hiyo itaongezeka kwa kuongeza ng’ombe mmoja juu ya gharama ya kawaida ya ardhi hiyo. Ardhi yoyote haikuruhusiwa kuuzwa wala kumilikiwa na mtu mwingine bila Mangi mwenyewe kuambiwa. Japo mtu binafsi angeweza kuamua kuuza ardhi yake kwa mgeni kwa kufuata utaratibu uliopo lakini hili halikuwa rahisi kutokea kwa sababu ukoo mzima ulijitokeza na kumzuia kwa kutaka kumlipa kiasi chochote alichoahidiwa kama gharama ya ardhi hiyo ili kuhakikisha ardhi husika inabaki kuwa ni mali ya ukoo. Hivyo moja kwa moja ukoo unabaki kuwa ndio wenye haki ya mwisho ya umiliki wa ardhi ya eneo lolote katika nchi ya wachagga.

Mashamba makubwa ya ulezi kwa ajili ya watu wote yalipimwa na kugawanywa na Mangi mwenyewe. Hivyo hivyo hata mashamba makubwa ya mahindi kule kwenye ukanda wa chini katika maeneo ya tambarare yalikuwa ni majukumu ya Mangi kuyagawanya. Hata hivyo mahindi ni mazao ambayo yalikuja kuanza kulimwa baadaye, miaka ya zamani sana mahindi hayakuwa ni moja ya mazao yanayolimwa na wachagga.

Lakini ulezi umekuwa ukilimwa tangu miaka ya zamani sana, pengine kuanzia tangu wachagga walipogundua na kuendeleza teknolojia ya mifereji(mifongo) na umwagiliaji. Mifereji(mifongo) katika nchi ya wachagga ilimilikiwa na wale walioitengeneza ambapo kwa miaka ya nyuma mara nyingi walikuwa ni watu wa ukoo fulani. Hivyo watumiaji wengine walilipa bili ya matumizi ya maji hayo ya miefereji kwa wamiliki kadiri ya matumizi waliyohitaji.

Hata hivyo mgawanyo wa maji ya mifereji hususan baadaye ilikuja kuwa ni jukumu la Mangi ambaye aliweza kuyahamisha kutoka kwa watu wa eneo fulani kupeleka sehemu myingine. Na ilikuwa ni utamaduni kwamba siku za soko ilikuwa ni siku ya maji yote ya mifereji kuelekezwa kwa Mangi.

Ahsanteni.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *