– Ukoo wa Olotu/Ulotu ni tawi la ukoo wa Mallya lenye chimbuko lake katika kijiji cha Sisamaro, Kibosho katika eneo lenye umaarufu zaidi kama Kibosho Maro. Zamani wakijulikana zaidi kama ukoo wa Olotu Mallya hawa ni wachagga wenye ujasiri mkubwa sana katika kukabiliana na changamoto mbalimbali katika maisha ni kati ya koo za wachagga zenye watu jasiri, mashuhuri na matajiri sana pia.
– Kutoka kwenye historia tawi hili la ukoo wa Olotu lenye chimbuko lake Uchaggani katika kijiji cha Maro Kiboshokatika ngome ya ukoo wa Mallya ni kati ya wachagga walioonyesha upinzani mkubwa na kuwa tishio kwa watawala. Wakati wa utawala wa Mangi Sina Kibosho katika miaka ya mwanzoni ya 1870’s tawi la ukoo wa Olotu wa Kibosho Maro mwanzoni hawakuonyesha kukubaliana na kuingia kwa Mangi Sina katika kiti cha utawala na hivyo kuhusika katika kujaribu kufanya uhaini dhidi ya Mangi Sina Kibosho.
– Hivyo baada ya Mangi Sina kugundua njama zilizokuwa zinasukwa dhidi yake na wachagga wa ukoo huu kutokea Kibosho Maro aliwaangukia na kuanza kuwateketeza vibaya. Wachagga wengi wa tawi la ukoo Mallya waliuawa na wengi zaidi walikimbilia maeneo mengine mbalimbali ya Uchaggani. Kuna waliokimbilia upande wa magharibi huko Machame hususan sehemu za Lyamungo wanakutumia ukoo wa Ulotu.
– Hata hivyo wengi walikimbilia upande wa mashariki hususan katika himaya ya umangi Old Moshi wakati wa utawala wa Mangi Rindi Mandara ambapo walipewa hifadhi na kusaidia pia kuongeza katika intelijensia ya ujasusi ya Old Moshi dhidi ya Kibosho hasa katika uhasama na mivutano kati ya Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi na Mangi Sina wa Kibosho. Hata hivyo ndugu wengine wa tawi hili la ukoo wa Olotu walikimbilia upande wa mashariki zaidi na kuweka makazi katika himaya ya umangi Marangu wakati wa utawala wa Mangi Kinabo wa Marangu.
– Ukoo huu wa Olotu wenye chimbuko lake katika kijiji cha Sisamaro, Kibosho waliokimbilia maeneo mengine ya Uchagga hususan upande wa mashariki wameendelea kujitofautisha na kuonyesha makali yao kuwa ni watu wenye asili ya ujasiri na mapambano siku zote ambapo wameendelea kufanya vizuri sana katika nyanja mbalimbali kwenye maisha. Inasemekana kwamba hata mwanamke wa kwanza kuwa rubani Tanzania ametokea kwenye tawi hili la ukoo wa Olotu.
– Ukoo wa Olotu/Ulotu wameendelea kusambaa na kuongezeka sana idadi katika maeneo walioendelea kukimbilia, hivyo ukoo wa Ulotu wanapatikana kwa wingi katika vijiji vya kata ya Lyamungo, Machame mashariki.
– Ukoo wa Olotu wakiwa kama tawi la Mallya bado wanapatikana kwa wingi sana pia katika kijiji cha Sisamaro, Kibosho. Hata hivyo inasemekana kwamba wale Mallya matajiri zaidi ndio hujiita Olotu.
– Ukoo wa Olotu wanapatikana kwa wingi katika kijiji cha Tella, Old Moshi.
– Ukoo wa Olotu wanapatikana kwa kiasi katika kijiji cha Mahoma, Old Moshi.
– Ukoo wa Olotu wanapatikana kwa wingi sana pia katika kijiji cha Kikarara, Old Moshi.
– Ukoo wa Olotu wanapatikana kwa wingi sana katika kijiji cha Mshiri, Marangu.
– Ukoo wa Olotu wanapatikana katika kijiji cha Arisi, Marangu.
Pamoja na kwamba ukoo wa Olotu/Ulotu ni ukoo wa wachagga mashuhuri sana lakini kuna uhaba mkubwa sana wa taarifa juu ya namna walivyogawanyika na kutawanyika, lakini pia vizazi vya sasa vimesahau mengi juu ya historia yao hivyo tunahitaji mchango wa mawazo na taarifa zaidi juu ya ukoo huu.
– Taarifa hizi zitasaidia kuongeza katika utafiti unaoendelea lakini pia utaongeza sana kwenye maudhui ya koo za wachagga hivyo kuhakikisha kwamba vizazi vya sasa na vinavyoendelea kuja havipotezi ile ari, shauku na hamasa ya mapambano makubwa kutoka kwa mababu zao katika kukabiliana na changamoto mbalimbali za maisha kuelekea kufanya makubwa katika ngazi ya ukoo na ngazi ya mtu mmoja mmoja.
Karibu kwa mchango zaidi wa Mawazo kuhusu ukoo wa Olotu.
1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Olotu?
2. Unafikiri ni kijiji gani ambacho kimesahaulika kutajwa lakini kuna ukoo wa Olotu?
3. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Olotu?
4. Kama wewe ni wa ukoo wa Olotu una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu?
5. Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani?
6. Wewe ni Olotu wa kutokea kijiji gani?
7. Bado kuna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo wa Olotu kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?
8. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Olotu?
9. Wanawake wa ukoo wa Olotu huitwaje?
10. Una rafiki yako yeyote wa kutokea kwenye ukoo wa Olotu?
11. Watu gani mashuhuri unaowafahamu kutoka kwenye ukoo wa Olotu?
12. Kuna mnyama yeyote ambaye labda ni mwiko kuliwa na wachagga wa ukoo wa Olotu?
13. Kuna ukoo ambao hawaruhusiwi kuoana na Wako-Olotu kwa sababu zilizowahi kuwepo miaka ya zamani?
Karibu kwa Mchango zaidi au maswali.
Ahsanteni.
Kesho tutaendelea na ukoo mwingine.
Whatsapp +255 754 584 270.