WACHAGGA WAHAFIDHINA vs WACHAGGA MALIBERALI.

WACHAGGA WAHAFIDHINA vs WACHAGGA MALIBERALI.

Linapokuja suala la kutunza tamaduni siku zote watu hugawanyika katika pande kuu mbili japo wachache hubaki katikati.

Kuna wale wa mrengo wa kulia ambao ndio huitwa wahafidhina(conservatives) na wale wa mrengo wa kushoto ambao huitwa *maliberali(liberals)*(huru).

Hata miongoni mwetu Wachagga wapo wahafidhina ambao ndio huitwa wa mrengo wa kulia na wapo maliberali ambao huitwa wa mrengo wa kushoto.

Wachagga wahafidhina ni Wachagga ambao wanapigania au kuunga mkono kulindwa, kutunzwa, kuhifadhiwa na kuenziwa kwa tamaduni, hadhi, utukufu na mambo yote yaliyowapa Wachagga umashuhuri na ufahari ambao wamekuwa wanajivunia kwa miaka mingi, wakati Wachagga maliberali wanaona mambo ya kuhifadhi au kuenzi tamaduni hayana haja ya kupewa uzito na hawaoni umuhimu wa kutunza au kujivunia chochote bali maisha yaende popote yanapokwenda ili mradi mtu anaishi kwa uhuru na amani na anaweza kubadilika mwenyewe na kuchagua aina yoyote ya maisha itakayompendeza bila kujihangaisha kuenzi tamaduni za asili.

Mfano wa makundi mengine unaoweza kufanana na huu, ni kwenye biblia katika dini ya Wayahudi kati Mafarisayo na Masadukayo. Wakati mafarisayo wakipigania kuenzi na kubaki na tamaduni za kiyahudi katika dini bila kuchanganyika na watu wa mataifa(gentiles), Masadukayo wao walikuwa wanaunga mkono kuchanganya Uyahudi na baadhi ya tamaduni za Wayunani(Ancient Greece) ambao walikuwa ndio wasomi zaidi wa kale na waliokuwa na ushawishi mkubwa kwa dunia ya kale ikiwa ni pamoja na himaya ya Rumi ya kale(Ancient Rome) iliyokuja kuwa na nguvu sana kwa dunia ya kale na kuendelea kuwa msingi wa tamaduni za kimagharibi mpaka leo hii.

Lakini hata hivyo japo Masadukayo walionekano kama ndio wasomi wanaokwenda na wakati kwa nyakati zile za utukufu na umashuhuri wa Wayunani na baadaye Warumi, lakini ni Mafarisayo ambao ndio kama wahafidhina wa kiyahudi ambao walisaidia zaidi tamaduni za kiyahudi kutunzwa na kuendelea kuwepo mpaka sasa. Hata ma-Rabbi wa dini ya kiyahudi wa leo hii wanakiri kwamba sehemu kubwa ya mafundisho yao imetokana zaidi na mafundisho ya Mafarisayo kuliko mafundisho ya kundi lingine lolote ndani ya dini ya kiyahudi zamani na wanaona kwamba Mafarisayo walifanya kazi muhimu zaidi katika kuhifadhi dini na tamaduni za kiyahudi zilizochangia kuendelea kuwepo kwa dini ya kiyahudi mpaka leo hii ambayo pia ndio msingi wa ukristo.

Kwa upande wetu Wachagga wahafidhina wanataka ushirikiano zaidi baina ya Wachagga, mwingiliano zaidi baina yetu, kutunza na kuelimishana kuhusu historia, tamaduni zote, maadili ya kichagga na kila kizuri kuhifadhiwa, kutunzwa na kuenziwa.

Wachagga wahafidhina wanataka kuona mila na desturi za wachagga zikiendelea kuwepo na kudumu kwa maelfu ya vizazi vitakavyoendelea kufanya mambo makubwa na kurithisha tamaduni hizi na historia kubwa iliyojaa utukufu ndani yake kutoka kizazi kimoja kwenda kizazi kingine na kutotamani kuona mila, desturi, tamaduni na historia yetu vikipotea na kusahaulika kabisa baada ya vizazi vichache kupita.

Kwa upande wa Wachagga maliberali wao hawaoni kama yote haya yana umuhimu wowote, wao kikubwa kuwe na haki, utulivu, amani na maendeleo haya mengine hayana maana, maliberali hawaoni kama kuna haja ya maadili na wanaunga mkono mabadiliko yote ya kijamii kama mienendo ya vijana kutothamini sana maadili na tamaduni zilizopita na kuiga tamaduni zozote zinazoonekana kwenda na wakati, hawajali kuhusu mavazi, vyakula, nyimbo, ngoma, ardhi ya urithi, lugha ya asili ya kichagga, wala urithi wowote ulioachwa kutokea vizazi vilivyopita, badala yake wanaunga mkono kuishi vyovyote unavyofurahia wewe haijalishi sana kama unaendana na maadili ya jamii yako au hauendani nayo.

Karibu kwa maoni, ushauri na Mchango zaidi.

Wewe ni Mchagga Mhafidhina au Mliberali?

KUENZI NA KUTUNZA NYUMBANI KWA ASILI KILIMANJARO
WACHAGGA WAHAFIDHINA vs WACHAGGA MALIBERALI.
WACHAGGA WAHAFIDHINA vs WACHAGGA MALIBERALI.
WACHAGGA WAHAFIDHINA vs WACHAGGA MALIBERALI.

Urithi Wetu Wachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *