MAENEO 18 UNAYOPASWA KUYATEMBELEA UCHAGGANI KILIMANJARO

Sasa Wakati Ambao Wachagga Wengi Wanarudi Nyumbani Ndio Huu, Kwa Sababu Ni Kama Jinsi Ilivyo Muhimu Kiimani Kwa Mchagga Ni Vigumu Kukaa Mbali na Ardhi Yake Takatifu Ya Urithi Kwa Kipindi Kirefu.Lakini Kurudi Nyumbani na Kuishia Tu Hapo Kijijini Kwenu Nkwamwasi, Machame au Lesoroma, Usseri, Rombo Unakuwa Kwanza Hujaitendelea Haki Likizo Yako Ya Desemba.

Lakini Pia Hujaitendea Haki Akili Yako Ambayo Unashindwa Kuipa Uzoefu Mpya wa Kutembelea Maeneo Mengine Bora, Muhimu na Ya Kihistoria Uchaggani Kwetu na Badala Yake Unaendelea Kuichosha Kila Siku Kwa Kuishia Eneo Moja Tu, Hapo Kwenye Kitongoji Chenu.Mwezi Aprili Mwaka Huu Tuliweka Hapa Kwenye Ukurusa Huu Maeeno 18 Ya Uchaggani, Kilimanjaro Ambayo Tunafikiri Kila Mchagga Anapaswa Kuwa Ameshayatembelea.

Hata Hivyo Licha Ya Kuweka Maeneo Haya 18 Pekee Kwa Kadiri Ya Tulivyoona Ni Kipaumbele Zaidi, Lakini Mtu Unaweza Kuongezea Ya Kwako Ambayo Unafikiri Kwamba Yalipaswa Kuwa Kwenye Orodha Hii Lakini Yamesahaulika Kimakosa.

Tunasisitiza Kwamba Ni Muhimu Mtu Kutembela Maeneo Mengi Inavyowezekana Kwa Sababu Kuna Mengi Ya Kujifunza, Lakini Hata Ikitokea Umeshindwa Kabisa Basi Usikose Kutembelea Angalau Mojawapo Lililopo Karibu Zaidi na Wewe. Hutajutia Kabisa Ziara Yako, Utafurahia Mengi Mapya Utakayojifunza.

Pia Ni Kwa Faida Ya Uchumi wa Vijijini Uchaggani Fedha Zako Ambazo Kwa Mwaka Mzima Unazitumia Kwenye Miji Mikubwa Ukazitumia Kwa Manufaa Ya Biashara Ndogo Za Vijijini Kwetu. Nitatoa Maelezo Kidogo Ya Namna Ya Kufika Kwenye Kila Eneo Kwa Faida Ya Wale Ambao Wamechagua Kutembela Eneo Husika.

Unaweza Kuweka Comment Hapo Chini Ya Kuwa Ni Eneo Gani Ambalo Limekuvutia na Unapanga Kulitembelea Ili Uweze Kupata Kampani Hapa Hapa Siku Utakayokwenda.

*MAENEO 18 UNAYOHITAJI KUYATEMBELEA UCHAGGANI, KILIMANJARO.*

*1. KANISA KATOLIKI KIBOSHO NA TAASISI ZAKE – KIJIJI CHA SINGA.*-

Hii Ni Parokia Ya Pili Ya Katoliki Kilimanjaro Baada Ya Ile Ya Kilema.

– Ukifika Eneo Hili Ndio Utaelewa Kwa Nini Limekuwa Likizungumzwa Sana na Utafurahia Kulitembelea.

– Ni Eneo Lenye Mazingira Mazuri Sana Kutembelea na Ni Sehemu Pia Unayopata View Nzuri Sana Ya Mlima Kilimanjaro.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – Kibosho Kirima, Nauli 1,000. Shuka Kituo Kinachoitwa Mkoring’a au KNCU Ya Juu. Chukua Boda Boda 1,000 Mwambie Akupeleka Kanisa Katoliki Singa au Kibosho Hospital, Umefika.

KANISA KATOLIKI KIBOSHO, KIJIJI CHA SINGA.
KANISA KATOLIKI KIBOSHO, KIJIJI CHA SINGA.
KANISA KATOLIKI KIBOSHO, KIJIJI CHA SINGA.
KANISA KATOLIKI KIBOSHO, KIJIJI CHA SINGA.

*2. ENEO LA NKWARUNGO MACHAME NA TAASISI ZAKE – NKWARUNGO, MACHAME*

– Hapa Utakutana na Kanisa La Kwanza La Kilutheri Afrika mashariki na Mazingira Yanayovutia Sana.

– Utakutana na Hospitali Ya Kilutheri Machame Nkwarungo na Maeneo Ya Jirani Kama Nkwamwasi, Kyalia, Wari, Nronga n.k., ni Maeneo Yenye Kuvutia Sana.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – Machame, Nauli 1,000. Shuka Kituo Cha Nkwarungo, Umefika.

NKWARUNGO, MACHAME.
NKWARUNGO, MACHAME.
MAKOA, MACHAME

*3. ENEO LA TSUDUNYI, OLD MOSHI NA MAKUMBUSHO YA MANGI MELI MANDARA – TSUDUNYI, OLD MOSHI.*

– Hili ni Eneo La Kihistoria Zaidi Ambapo Ndio Uliokuwa Mji wa Moshi na Centre Ya Kaskazini Ya Tanganyika Kuanzia Karne Ya 19 Ulipoanzia, Mpaka Baadaye Mwaka 1919 Ulipohamia Rasmi Moshi mjini.

– Kwa Sasa Ndipo Zilipo Ofisi za Halmashauri Ya Wilaya Ya Moshi Vijijini na Ndipo Ilipokuwa Shule Kongwe Ya Sekondari Old Moshi Iliyokuwa Mashuhuri Sana Zamani Kama Sekondari Ya Kwanza Ya Serikali Kaskazini Ya Tanganyika.

– Utakutana Pia na Makumbusho Ya Mangi Meli Mandara Pamoja na Kuangalia Movie(Filamu) Ya Vita Yake na Wajerumani Karne Ya 19. Utaweza Kuona Pia Sanamu Ya Mangi Meli Mandara na Mti Walionyongewa Wamangi wa Kichagga Wakiongozwa na Mangi Meli Mandara Mwaka 1900.

– Unaweza Kuendelea na Safari Ya Kupandisha Juu Zaidi Kufika Kijiji cha Kidia, Old Moshi Ambapo Utakutana na Kanisa La Mwanzo Kabisa Kilimanjaro Lilipohamishiwa Baada Ya Kuhama Kitimbirihu na Yalipokuwa Makazi Ya Kudumu Ya Mwanafalasafa na Mwanahistoria wa Mambo Ya Wachagga Mmisionari Dr. Bruno Guttmann(1876 – 1966), Ambaye Alipanga Kuzikwa Hapo Hapo Kidia.

-Ukiwa Kidia Pia Unaweza Kutembelea Maporomoko Makubwa Sana Ya Maji Kilimanjaro Ya Mambori (Mambori Watefalls), Yenye Kuvutia na Kusisimua.

KUFIKA: Fika Kiboriloni, Unaweza Kupanda Daladala au Pikipiki Kwa Haraka 1,500 au 2,000 Mwambie Akupeleke KNCU, Mahakamani, Ofisi za Halmashauri au Makumbusho Ya Mangi Mengi. Au Unaweza Kuwasiliana na Bwana Gabby Mzei Kwa Maelezo Zaidi(0717003078)

MANGI MELI MANDARA
MANGI MELI MANDARA
KIKARARA, OLD MOSHI.
MANGI MELI MANDARA HANGING TREE.
KIJIJI CHA MOWO, OLD MOSHI.
KIJIJI CHA KIDIA, OLD MOSHI.

*4. KILIMANJARO NATIONAL PARK, MARANGU GATE – LYASONGORO, MARANGU.*

– Hili Ndilo Lango Kuu na Kongwe Zaidi La Kupanda Mlima Kilimanjaro na Lililozoeleka, Rahisi na Njia Ya Kupanda Mlima Yenye Makazi kwa Kila Kituo.

– Kwenye Eneo Hili Utaweza Kupata Historia na Rekodi Zote za Watalii Waliowahi Kupanda Mlima Kilimanjaro na Pia Unaweza Nawe Kwenda Day Trip Ya Kupanda Mlima Mpaka “Maundi Crater”, Juu Kidogo Ya “Mandara Hut” kwa Siku Moja na Kurudi Siku Hiyo Hiyo kwa Gharama Nafuu Sana.

– Ni Eneo Zuri na Linalovutia Sana.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – (M) Kilema/Mwika, Shuka Marangu Mtoni Ulizia Gari za Kulekea Getini Kinapa au Panda Bodaboda Kati Ya 3,000 Mpaka 5,000 Mpaka Getini.

KINAPA GATE, MARANGU ROUTE.
KINAPA, MARANGU ROUTE.

*5. CHAGGA ANCIENT CAVES NA NDORO WATERFALLS – LYAMRAKANA, MARANGU.*

– Hapa Utakutana na Historia Fupi Ya Mapango Haya Ya Zamani na Jinsi Yalikuwa Yanatumika Wakati wa Vita.

– Katika Hiki Hiki Kijiji Cha Lyamrakana Utakutana na Maporomoko Ya Maji Yanayovutia Sana Maarufu Kama Ndoro Waterfalls.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – (M) Kilema/Mwika, Nauli 1,500 Shuka Marangu Mtoni. Chukua Boda Boda 1,000 Mpaka Chagga Caves, Unaweza Kupewa Muongozo Hapa wa Kufika Ndoro Waterfalls.

LYAMRAKANA, MARANGU.
NDORO WATERFALLS, LYAMRAKANA, MARANGU.

*6. ZIWA CHALLA – MAMSERA CHINI, ROMBO*

– Ziwa Challa ni Ziwa Maarufu Sana na Lenye Kuvutia Sana, Ukilitembelea Unaweza Kufahamu Zaidi na Maajabu Yake. Ni Eneo Linalotembelewa na Watalii Mara kwa Mara Sana.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – Mkuu, Rombo 3,000. Shuka Mamsera. Pale Unaweza Kuchukua Pikipiki. Ni mbali sana Labda Inaweza Kufika Tshs 10,000. Au Panda Daladala za Moshi – Holili, Fika Holili Kisha Chukua Pikipiki.

ZIWA CHALLA, MAMSERA CHINI, ROMBO.
ZIWA CHALLA, MAMSERA CHINI, ROMBO.

*7. BWAWA LA NDUONI – KIRUA VUNJO*

– Inawezekana Kuna *”Nduwa”* Nyingi Kilimanjaro Kama Zilizopo Huko Vijiji Vya Mmbahe, Marangu na Kwingineko Lakini Tuliweza Kuona Eneo Hili Ni Lenye Kuvutia Zaidi na La Kipekee. Hakuna Uwekezaji Wowote Uliofanyika Mpaka Sasa Lakini Ni Maeneo Unaweza Kutembelea na Kutuliza Sana Akili, na Wenyeji ni Watu Wakarimu Sana.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – Kirua Vunjo, Shuka Mwisho wa Gari, Umefika.

BWAWA LA NDUONI, KIRUA VUNJO.
NDUONI, KIRUA VUNJO.

*8. “CHAGGA LIVE MUSEUM” – KIJIJI CHA KYALA, MARANGU*

– Makumbusho Hii Ya *”Chagga Live Museum”* Iko Pembeni Ya Hotel Ya Kilimanjaro Mountain Resort Karibu na KNCU Kyala.

– Hapa Utakutana na Mzee Maarufu wa Historia za Zamani *”Mzee Mamiro”*, Atakueleza Mambo Kadhaa Ya Kale Kidogo.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – (M) Kilema, Nauli 2,000 Shuka KNCU Kyala. Vuko Barabara, Utaiona Kilimanjaro Resort Hotel na Chagga Live Museum, Pembeni Yake.

CHAGGA LIVE MUSEUM, KYALA MARANGU.
CHAGGA LIVE MUSEUM, KYALA, MARANGU.

*9. MTI MREFU ZAIDI AFRIKA KATIKA MSITU WA KIJIJI CHA TEMA – TEMA, MBOKOMU.*

– Huu Msitu wa Eneo Hili La Mbokomu Ni Msitu Mkubwa, Mnene, Wenye Jiografia Maridadi na Wenye Kuvutia Sana, Kuna Maji Mengi Sana, Kuna Maporomoko Mengi Ya Maji(Waterfalls) na Kuna Unyevu na Manyunyu Ya Mvua Muda Wote. Inawezekana Mbokomu na Marangu Ndio Maeneo Yanayoongoza Kwa Kuwa na Maji Mengi Zaidi.

– Hapa Pia Utakutana na Mti Mrefu Kuliko Yote Afrika Nzima, Wenye Urefu wa Mita 81.5 na Una Umri wa Zaidi Ya Miaka 600. Mti Huu Ambao Kwa Kiswahili Unajulikana Kama *MKUKUSU*, kitaalamu unaitwa *ENTANDROPHRAGMA EXCELSUM*.

KUFIKA: Fika Kiboriloni, Chukua Boda boda Kama 3,000 Hivi Mwambie Akufikishe Kijiji cha Tema, Mbokomu Hapo Utaulizia Utaratibu wa Kuingia Kwenye Huo Msitu Wenye Mti Mrefu Kutoka Kwa Watu wa KINAPA.

MSITU WA MLIMA KILIMANJARO WENYE MTI MREFU AFRIKA, KIJIJI CHA TEMA, MBOKOMU.
MTI MREFU KULIKO YOTE AFRIKA, TEMA, MBOKOMU.

*10. MWEKA KIBOSHO MASHARIKI – MWEKA, KIBOSHO.*

– Eneo hili la Mweka ambayo ndio moja ya njia za kupanda Mlima Kilimanjaro kupitia *”Mweka Route”* lina mazingira yenye kuvutia sana.

– Katika Eneo Hili Ndipo Kwenye Chuo cha Wanyamapori wa Kiafrika cha “Mweka African Wildlife College” na Ni Moja ya Maeneo Unayoweza Kupata Muonekano Bora Sana wa Mlima Kilimanjaro.

– Kwa Sababu Ni Eneo Haliko Mbali na Mjini Watu Wamekuwa Wakitembelea Kupiga Picha na Kufurahia Mandhari Yake.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – Kibosho Mweka, Nauli 1,000 Shuka Mwsiho wa Gari. Umefika.

KIBOSHO, MWEKA.
KIBOSHO, MWEKA.

*11. KANISA KATOLIKI KILEMA NA TAASISI ZAKE – MKYASHI, KILEMA.*

– Hii Ndio Parokia Ya Kwanza Ya Katoliki Kilimanjaro Iliyoanzishwa na Father August Gommenginger na Moja Ya Maeneo Yenye Historia Kubwa.

– Hapa Utakutana na Shule Kongwe Ya Msingi Kilema Ya Ghorofa Tatu, Chuo cha Ufundi PAPA BRIDGE, Hospitali Ya Kilema, Shule za Msingi na Sekondari, Pamoja na Taasisi Nyingine Nyingi Eneo Moja.

– Ni Eneo Kongwe Lenye Historia Kubwa Unalohitaji Kutembelea.

– Ukifika Hapa Kanisa Katoliki Kilema Unaweza Pia Kutembelea Mlima Mtakatifu wa Ngangu Ambapo Ukipanda Mpaka Pale Kileleni Unaweza Kutazama Eneo Kubwa Sana La Mashariki Ya Kati Ya Kilimanjaro.

– Mlima Mtakatifu wa Ngangu ni Mlima Maarufu Kwa Wakristo Kufanya Ibada na Maombi Hususan Yale Maombi Makuu Ya Kufunga.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – (M) Kilema, Naui 2,000 Shuka Kimaroroni Kwenye Kituo Cha Boada Boda. Chukua Boda Boda 1,000 Mpaka Parokia Ya Kilema Kanisani, Mkyashi.

MLIMA MTAKATIFU WA NGANGU, KILEMA.
KANISA KATOLIKI KILEMA.
SHULE KONGWE YA MSINGI KILEMA.
MLIMA MTAKATIFU WA NGANGU, KILEMA

*12. MAPANGO YA SIENYI MACHAME – KIJIJI CHA USWAA NA MASAMA NGIRA, MACHAME.*

– Hili Ni Eneo Linalotisha Zaidi Kuliko Kuvutia Lakini Lenye Mvuto wa Kipekee.

– Eneo Hili Ndipo Inapokutana Mito Miwili Mikubwa Ya Namwi na Marire na Kuwa Mto Mmoja Ambao Mbele Yake Kidogo Unaungana na Mto Mkubwa na Mashuhuri Kikafu Unaoelekea Chini Kwenye Tambarare.

– Eneo Hili Lina Mapango Makubwa Kwa Chini Yanayoenda Umbali Mrefu Yakipita Chini kwa Chini, na Linatambulika Kama Eneo La Mwanzo Zaidi La Makazi Ya Wachagga, Kilimanjaro.

KUFIKA: Fika Kwa Sadala, Panda Gari za Moshi – Masama, Zinazopitia Mula, Shuka Kituo cha Bwani. Unaweza Kuchukua Boda Boda Kuelekea Kwenye Hayo Mapango Ya Sienyi. Lakini Kama Unataka Kushukia Mpaka Huko Chini Mapangoni, Ni Vyema Ukatafuta Waongozaji Hapo Bwani. Peke Yako Hutaweza na Panatisha Sana Pia.

MAPANGO YA SIENYI MACHAME/MASAMA.
MAPANGO YA SIENYI MACHAME/MASAMA.

*13. KILIMANJARO NATIONAL PARK, MACHAME GATE – NKWESEKO, MACHAME.*

– Hili ni Lango La Kupanda Mlima Kilimanjaro Kupitia Njia Ya Machame Katika Kijiji cha Nkweseko, ni Lango La Pili Kwa Umaarufu Baada Ya Lile Marangu.

– Haya Ni Mazingira Yenye Kuvutia Sana na Yenye Hali Ya Hewa Nzuri Sana.

– Njia Hii Ya Machame Pia Unaweza Kwenda Day Trip Ya Kupanda Mlima Kilimanjaro na Kurudi Siku Hiyo Hiyo Kwa Gharama Nafuu Sana.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – Machame, Shuka Mwisho wa Gari, Kyalia. Unaweza Kuchukua Pikipiki Kuendelea Mpaka Getini Kama Tshs 3,000 hivi.

KINAPA GATE, MACHAME ROUTE.
KINAPA GATE, MACHAME ROUTE.
KINAPA GATE, MACHAME ROUTE.

*14. ENEO LA MSITU RONGAI NA GETI LA KUPANDA MLIMA RONGAI ROUTE – RONGAI, ROMBO*

– Huu Msitu wa Rongai ni Moja Ya Maeneo Yenye Kuvutia Sana Kilimanjaro, Ni Moja Kati Ya Njia za Kupanda Mlima Kilimanjaro Kupitia Upande wa Mashariki Kabisa na Ni Maeneo Ya Mpakani Kabisa na Kenya.

– Huu Msitu wa Rongai Ni Mkubwa na Mrefu Ambapo Ukiumaliza Unaingia Mji Mdogo wa Kamwanga Uliopo Mpakani na Wilaya Ya Longido Mkoa wa Arusha.

– Rongai Ni Eneo Lenye Mito na Maji Mengi.

KUFIKA: Panda Gari za Moshi – Tarakea(Rombo), Shuka Mwisho wa Gari Nauli Tshs 4,500. Panda Gari za Tarakea – Kamwanga Shuka Rongai, Umefika. Nauli Kama Tshs 1,000 – 2,000.

MSITU WA RONGAI, ROMBO.
RONGAI ROUTE ROMBO, KINAPA GATE.

*15. KITIMBIRIHU HOLISTIC CENTRE(ENEO TAKATIFU LA KITIMBIRIHU), KITIMBIRIHU – MDAWI, OLD MOSHI*

– Hili ni Eneo Ambalo Liko Katika Kijiji cha Mdawi, Old Moshi Ambalo Limetangazwa Rasmi na Kanisa La KKKT Kuwa Eneo Takatifu La Kanisa na Mradi wa Ujenzi Huo Unaendelea.

– Hili Ndio Eneo Ambapo Dini Ya Kikristo Ilianzia Rasmi Katika Bara Tanganyika Mwaka 1885. Eneo Hili Pia Ndipo Shule Ya Kwanza Ya Kisasa Ilianzia Katika Bara Tanganyika Kwa Misingi Iliyojengwa Tangu Mwaka 1872. Sio Eneo Lilioendelea Sana Kwa Sasa kwa Sababu Lilitelekezwa Kutokana na Migogoro Ya Zamani na Ile Misheni Kuhamishwa Lakini Limeanza Kuchangamka Tena, na Kwa Kuwa Wachagga Wengi Ni Wakristo Basi Ni Eneo Lenye Umuhimu Mkubwa Kiimani Kama Sehemu Ambayo Habari za Yesu Zilianza Kutangazwa.

KUFIKA: Panda Gari za Moshi – Mjohoroni Nauli 500, Shuka Kituo cha Mdawi. Chukua Pikipiki Kati Ya 1,500 Mpaka 2,000, Mwambie Akupeleke Kitimbirihu Kanisani.

KITIMBIRIHU HOLISTIC CENTRE, OLD MOSHI.
KITIMBIRIHU HOLISTIC CENTRE, OLD MOSHI.
KITIMBIRIHU HOLISTIC CENTRE, OLD MOSHI.
KANISA LA KILUTHERI LA KWANZA KIDIA.

*16. ENEO LA KANISA LA KILUTHERI KOTELA – KOTELA, MAMBA*

– Hili Ni Moja Kati Ya Makanisa Makubwa Sana na Lenye Mvuto wa Kipekee. Pia Ndani Ya Kanisa Hili Ndipo Amezikwa Askofu Mkuu wa Kwanza wa KKKT Dayosisi Ya Kaskazini Ambaye Pia Ndiye Mkuu wa Kwanza wa Kanisa La KKKT Tanzania na Mwanzilishi wa Hospitali Ya KCMC Dr. STEFANO REUBEN MOSHI na mke wake NDEAMBILIASIA MOSHI.

– Pembeni Ya Kanisa Hili Kuna Moja Kati Ya Majengo Makubwa na Mazuri Sana Uchaggani “MAMBA ROYAL COMPLEX” Lenye Ofisi Kadhaa Japo Ni Kijijini.

– Unaweza Kuendelea Mbele Kidogo Ukafika Kijiji cha Komakundi, Mamba Kukutana na Wataalamu wa Kufua Vyuma Waliobaki Uchaggani, Wenye Historia Ya Zaidi Ya Miaka 400.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – (M) Mwika, Nauli 2,000 Shuka Kituo Cha Kotela, Mamba. Umefika.

KANISA LA KILUTHERI KOTELA, MAMBA.
MAMBA ROYAL COMPLEX, KOTELA MAMBA.
MAMBA, KOMAKUNDI.
KANISA LA KILUTHERI KOMAKUNDI, MAMBA

*17. KANISA LA KKKT MWIKA NA TAASISI ZAKE – MWIKA.*

– Hili Eneo La Mwika Ni Kati Ya Maeneo Yenye Mazingira Yanayovutia Sana, Ni Eneo Lenye Taasisi Nyingi Hasa za Kanisa La Kilutheri.

– Katika Eneo Hili Kuna Chuo Kikuu cha Kumbukumbu Ya ASKOFU STEFANO MOSHI, Kampasi Ya Mwika, Kuna Mwika Bible School, Chuo cha Uinjilisti Mwika, Kuna Christian Bookshop Mwika, Kanisa Lenyewe, Shule Ya Msingi na Taasisi Nyingine.

– Ni Eneo Lenye Mandhari Bora Sana.

KUFIKA: Panda Daladala za Moshi – (M) Mwika, Shuka Mwisho wa Gari Mwika Sokoni. Angalia Upande wa Kusini, Umefika.

KANISA LA KILUTHERI MWIKA, MWIKA
CHUO KIKUU CHA STEFANO MOSHI (SMMUCO), TAWI LA MWIKA.

*18. ENEO LA MKUU, ROMBO NA TAASISI ZAKE.

– HiIi ni Eneo Muhimu sana Sana Pia Kama Makao Makuu Ya Wilaya Ya Rombo.- Ni Eneo Lenye Majengo Ya kihistoria Kama Vile Majengo Ya Kanisa Katoliki Mkuu, Rombo Ikiwa ni misheni Ya Tatu Ya Katoliki Kuanzishwa Kilimanjaro.

-Lakini Pia Utaweza Kuona Nyumba Ya Kihistoria Ya Mangi Kinabo wa Mkuu, na Kutembelea Taasisi Ya Utamaduniw a Asili Ya Mkuu Cultural Tourism. Utaweza Pia Kuutembelea Mji wa Mkuu, Rombo Kwa Ujumla Wenye Taasisi Nyingi za Wilaya Hiyo.

– Ni Eneo Lenye Mandhari Nzuri Sana Kutembela.

KUFIKA: Panda Gari za Moshi – Mkuu, Nauli Tshs 3,000 Shuka Mwisho wa Gari. Chukua Pikipiki mwambie Akupeleke Eneo Unalotaka Kwa sababu Hapa Taasisi ni Nyingi na Ziko mblimbali.

*Maeneo Haya 18 Tumeona Ni Maeneo Muhimu Zaidi Unayohitaji Kuyatembelea Kwa Ziara Tuliyofanya, Lakini Unaweza Kuongezea Maeneo Mengine Zaidi Unayofikiri Yastahili Kuwepo Kwenye Orodha Hii.*

Nimeweka Maelezo Ya Namna Ya Kufika Kwa Usafiri wa Umma Lakini Hata Kwa Mwenye Usafiri Binafsi Anaweza Kuelekezwa na Wanaotumia Usafiri wa Umma Akafika.

Hizo Nauli Nilizoweka Hapo Ni Wastani wa Bei, Pengine Unaweza Kukuta Bei Ziko Tofauti Kidogo na Hizo Lakini Haiwezi Kuwa Tofauti Kubwa.

Karibuni kwa Maoni na Maelezo Ya Juu Ya Ni Wapi Umevutiwa Kutembelea Ili Tuweze Kupata Kampani Hapa.Unaweza Kushirikisha Ujumbe Huu Kwa Watu Zaidi Kuwakumbusha Kuhusu Utalii wa Ndani Ya Kilimanjaro.

KANISA KATOLIKI MKUU, ROMBO.
ZAHANATI YA KANISA KATOLIKI, MKUU ROMBO.
MKUU, ROMBO

Ahsanteni sana.

Aikenyi Kishari.

You may also like...

Popular Posts

3 Comments

  1. Nimependa sana maelezo kwa yale maeneo yote mazuri ya kutembelea, kwani nimepata kujua wapi nikazuru baada ya kutoka kwenye marekebisho kidogo ya baiskeli yangu nikitoka Moshi mjini. 🙏🏿

    1. Sawa kabisa.

      Karibu sana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *