UFANANO WA MAJINA YA WATAWALA WA UCHAGGA KILIMANJARO. – 1

SEHEMU YA 1.

Kumekuwepo kwa ufanano wa majina ya watawala wa Himaya za Umangi za Uchagga, Kilimanjaro kwa baadhi ya wamangi au watu wengine mashuhuri katika historia ya Kilimanjaro ambao kwa kiasi umekuwa ukiwachanganya watu ambao hawajaifuatilia historia kwa undani.

Hata hivyo ufanano wa majina ya asili ya Uchagga, Kilimanjaro kwa himaya tofauti za Umangi Kilimanjaro sio jambo la ajabu kwa sababu wachagga wote na watu wamoja na majina ya asili ya kichagga mengi yamekuwa yako maeneo karibu yote. Yaani ni kama leo hii jinsi jamii ya wakristo ilivyo na majina yanayofanana kama vile Josefu, Emanueli n.k. ndivyo jamii ya wachagga ilikuwa na majina yanayojirudia uchaggani kote.

Hivyo ni kwamba sio kwamba tu majina haya yalikuwa kwa watawala bali ni majina yaliyokuwa yakitumika uchaggani kote hivyo inatokea kwa bahati mtawala mwenye jina husika kuingia madarakani akifanana jina na mtawala mwingine wa eneo jingine au wa kipindi kingine katika historia.

Baadhi ya Majina Ya Watawala au Watu Wengine Mashuhuri Yaliyotokea Kufanana na Kupata Umaarufu Mkubwa Katika Historia Ya Wachagga, Kilimanjaro;-

1. MALAMIA.

(i) Malamia wa Kibosho alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Kibosho baada ya Mangi Sianga baba yake aliyemwachia kiti cha umangi mwaka 1911. Mangi Malamia pia alienda kuwa Mangi wa himaya ya umangi Siha/Sanya tangu mwaka 1920 – 1927 alipoondolewa kwa zengwe la kisiasa kutoka Machame.

(ii) Malamia wa Kindi alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Kindi ambayo kwa sasa ni sehemu ya himaya ya umangi Kibosho katika miaka ya 1860’s wakati wa utawala wa Mangi Ngaluma Kibosho wakiwa ni washirika wazuri na Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi.

(iii) Malamia wa Old Moshi alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Old Moshi ambaye ni mtoto wa Mangi Meli Mandara aliyekuja kurithi kiti cha umangi wa Old Moshi baada ya utawala wa baba yake mdogo Mangi Salema. Jina lingine aliitwa Sudi.

(iv) Malamia wa Mamba alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Mamba ambaye katika miaka ya 1750’s ambaye alikuwa ni mtoto wa Mangi Mapfuluke wa Mamba na pia alikuwa ndiye baba yake Mangi Ngawondo.

(v) Malamia tena wa Mamba alikuwa ni Mangi mwingine tena wa himaya ya umangi Mamba katika miaka ya 1880’s ambaye alikuwa ni mtoto wa Mangi Mlawi anayesemekana kwamba aliingia madarakani baada ya kumpindua baba yake Mangi Mlawi. Malamia alikuja kupinduliwa na Karl Peters mwaka 1891 kisha akaingia madarakani ndugu yake aliyeitwa Mangi Kuimbere.

(vi) Malamia wa Usseri alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Usseri, ambaye alikuwa ni mtoto wa Mangi Kafuria na baba yake Mangi Kisuma. Baada ya utawala wa Mangi Malamia wa Usseri ndugu yake aliyeitwa Matolo alifanya mapinduzi na kukalia kiti cha utawala.

2. NDESSERUA.

(i) Ndesserua wa Machame alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Machame kuanzia miaka ya 1850’s mpaka 1870’s. Mangi Ndesserua wa Machame ndiye baba yao Mangi Ngamini, Mangi Shangali na Mangi Ngulelo ambao waliitawala Machame mfululizo baada yake.

(ii) Ndesserua wa Keni, Rombo alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Keni, Rombo katika miaka ya 1880’s akiwa ni mjukuu wa Mangi Horombo kwa mtoto wake Mahunga.

3. KINABO.

(i) Kinabo wa Marangu alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Marangu katika miaka ya 1870’s akiwa ni mshirika mzuri wa Mangi Rindi Mandara ambaye ndiye alikuja kupinduliwa na majeshi ya Mangi Sina wa Kibosho waliomtawalisha Mangi Ndegoruo Marealle badala yake mwanzoni mwa miaka ya 1880’s.

(ii) Kinabo wa Mkuu, Rombo alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Mkuu, Rombo kuanzia kwenye miaka ya 1880’s na kuendelea ambaye alianza kuijengea himaya ya umangi Mkuu, Rombo nguvu kubwa ya ushawishi na kijeshi katika eneo la Rombo kuizidi himaya ya umangi Keni, Rombo iliyokuwa ngome ya Mangi Horombo.

4. SELENGIA.

(i) Selengia wa Mamba alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Mamba mwanzoni mwa miaka ya 1900 akiwa ni moja kati ya watoto wa Mangi Mlawi wa Mamba aliyetawala kwa kipindi kifupi sana.

(ii) Selengia wa Mkuu, Rombo alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Mkuu, Rombo ambaye pia alikuwa ni mtoto wa Mangi Kinabo aliyetawala himaya ya umangi Mkuu baada ya baba yake. Mangi Selengia pia alikuwa pia ndiye Mangi Mwitori wa kwanza wa Rombo.

5. KIRITA.

(i) Kirita wa Old Moshi alikuwa ni mtoto mkubwa wa Mangi Rindi Mandara aliyejiandaa kurithi kiti cha umangi wa Old Moshi baada ya baba yake lakini aliuawa kwa mbinu zilizopangwa na mama yake Meli aliyeitwa Sesembu akishirikiana na ndugu zake wa kutoka kwenye familia ya umangi Kilema. Baada ya kuuawa kwa Kirita kiti cha umangi wa Old Moshi kilikaliwa na Mangi Meli.

(ii) Kirita wa Kilema alikuwa ni Mangi wa Kilema kuanzia mwaka 1905 mpaka mwaka 1925 akirithi kiti cha umangi wa Kilema kutoka kwa baba yake Mangi Fumba. Mangi Kirita alikuja kuuawa kwa sumu inasemekana kutokana na fitna za kisiasa zilizosukwa kutokea Marangu.

6. MLANG’A.

(i) Mlang’a wa Kilema alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Kilema kwa kipindi cha mwaka mmoja tangu mwaka 1900 – 1901 aliporithishwa kiti hicho cha umangi na baba yake Mangi Fumba. Mangi Mlang’a wa Kilema aliuawa kwa kuwekewa sumu mwaka mmoja baadaye kwa fitna ya kisiasa iliyotengenezwa Marangu, kwa sababu inasemakana kwamba Mangi Mlang’a wa Kilema alikuwa na uwezo mkubwa sana kiutawala na pengine uwezo wake mkubwa kiakili na kidiplomasia ungeweza kukuza ushawishi wa Kilema kisiasa dhidi ya Marangu. Baada ya Mangi Mlang’a kuuawa Mangi Fumba baba yake alirudi madarakani na kuitawala tena Kilema mpaka mwaka 1905 alimwachia kiti cha utawala mtoto wake mwingine aliyeitwa Kirita.

(ii) Mlang’a wa Marangu alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Marangu tangu mwaka 1912 mpaka mwaka 1932 alipomwachia kiti cha utawala mdogo wake aliyeitwa Petro Itosi Marealle. Mangi Mlang’a wa Marangu ndiye baba yake wa Mangi Mkuu wa wachagga Mangi Thomas Lenana Marealle na pia ndiye baba yake Mangi Augustine Marealle wa Marangu aliyetawala himaya ya umangi Marangu mpaka mwaka 1962.

7. MLATIE.

(i) Mlatie wa Mbokomu alikuwa ni Mangi wa himaya ya umangi Mbokomu tangu miaka ya 1860’s mpaka 1890’s. Lakini hata hivyo Mangi Mlatie wa Mbokomu alikuwa akiingia katika migogoro na Mangi Rindi Mandara hivyo alikuwa akipinduliwa na kurudi madarakani mara kwa mara. Hata hivyo mwishoni baada ya utawala wa Mangi Mlatie himaya ya umangi Mbokomu ilikuja kutawaliwa na watoto wake watatu tofauti katika vipindi tofauti ambao ni Mangi Msami, Mangi Ngatunyi, Daudi ambaye aliuawa na mwishoni Mangi Philipo.

(ii) Mlatie wa Marangu alikuwa ni mtoto wa Mangi Ndaalio wa Marangu ambaye alikuwa ameandaliwa kurithi kiti cha umangi wa Marangu baada ya kufariki kwa baba yake. Hata hivyo Mlatie alikuwa ni mshirika wa Mangi Rindi Mandara aliyeshirika katika kampeni za kuivamia Usseri lakini kwa bahati mbaya Mlatie aliuawa katika kampeni hizo za Usseri. Baada ya kufariki kwa Mlatie ndipo alitafutwa mrithi mwingine wa kiti cha umangi wa Marangu ambaye ni mtoto wa Mangi Ndaalio na hapo ndipo akapatikana Ndegoruo Marealle aliyekuwa mtoto wa Mangi Ndaalio kwa hawara wake aliyeitwa Nderero aliyekuwa ameolewa huko Mwika kwa Bwana mmoja aliyeitwa Makiponyi Mariki.

ITAENDELEA KESHO.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *