Kupitia tafiti mbalimbali za kihistoria na kitamaduni ambazo zilianza tangu karne nyingi zilizopita na kuanza kuwekwa kwenye maandishi na kumbukumbu tangu karne ya 19 tumeweza kuwa na taarifa nyingi sana juu ya asili ya asili ya wachagga. Kama tunavyojua kwamba maarifa hayana mwisho na mtu huwezi kuziba kila pengo lililopo kwenye historia kwa haraka, hivyo bado uwanja wa kuendelea kutafiti zaidi juu ya koo na mwingiliano zaidi upo wazi.
Hata hivyo mpaka sasa tuna taarifa nyingi sana ambazo zina hoja zenye mashiko kwa kiasi kikubwa sana juu ya asili ya wachagga. Kupitia tafiti hizi tunafahamu kwamba jamii ya wachagga imeundwa kwanza na kwa sehemu kubwa na wachagga asilia wenyewe ambao ndio kiini cha tamaduni zote asili za mchagga. Tamaduni hizi za wachagga ziko kipekee kabisa kwa wachagga wa makundi yote na hazipatikani kwa jamii nyingine ambazo zinaaminika kwamba zimeunda sehemu ya jamii ya wachagga ambazo kwa wingi ni Wataita, Wakamba na Wamasai.
Jamii jirani na wachagga ambazo zinafanana sana na wachagga kwa tamaduni na lugha ikiwemo jina la Mungu ni Ugweno na Meru, ambapo Wameru ni kama tawi lililotokea Uchaggani na imekuwa pia ni sehemu ya ukimbizi kwa wachagga kwa miaka katika historia. Ugweno nayo pia ikiwa ni sehemu ya ukimbizi kwa wachagga kwa miaka mingi sana pia. Na kwa nyakati tofauti katika historia maeneo haya yamekuwa kama makoloni ya Uchaggani.
Hivyo tamaduni hizi ambazo ni za kipekee kabisa kwa wachagga ni kama vile, kwanza Mungu wa wachagga anayejulikana kwa jina la “Ruwa/Iruwa”. Hakuna jamii nyingine yoyote Afrika ambayo inamtaja Mungu wao kwa jina la Ruwa isipokuwa tu wachagga/Gweno/Meru na Misri ya kale. Hata Father Alexander Le Roy aliyefanya utafiti mkubwa juu ya dini za jamii nyingi za Afrika mpaka kuandika kitabu kilichoitwa “Religion of the Primitives” alishangazwa kwamba jina la Mungu “Ruwa” lipo kwa wachagga na Misri ya kale ile ya Mafarao pekee. Jamii zinazoaminika kwamba zimechangia kuunda sehemu ya jamii ya wachagga Wakamba, Wamasai na Wakikuyu Mungu wao wanamwita kwa jina la “Ngai” wote kwa pamoja. Wataita ambao ndio wamechangia damu ya kichagga kwa kiasi kikubwa zaidi kuliko hizo jamii nyingine, licha ya kuwa na athari kubwa zaidi katika lugha lakini Mungu wao wanamwita Mulungu.
Tamaduni nyingine ambazo ziko kipekee kwa wachagga na hazipatikani kwenye zile jamii kubwa zinazohushishwa na wachagga ni kama vile jani takatifu la isale, lugha ya wachagga, vyakula, mfumo wa imani pamoja na taratibu nyingine nyingi. Kwa mfano kwa upande wa lugha, mchagga hasikilizana kabisa na mmasai, yaani hawaelewani kabisa. Hasikilizani pia na Mpare wala Mkikuyu, ni lugha tofauti kabisa. Hiyo inazidi kujidhihirisha kwamba mchagga ana upekee ambao unatokana na kundi la wachagga asilia ambao baadaye ndio walichanganyika kwa kiasi na jamii majirani ambazo zilimezwa na nguvu za tamaduni za wachagga asilia.
Hata hivyo Wataita ambao ndio jamii ya jirani na wachagga walioingia kwa wingi zaidi kuchanganyika na wachagga asilia kuliko jamii nyingine yoyote ya jirani athari yao kwa upande wa lugha imeweza kuonekana dhahiri zaidi. Lakini kwa upande wa imani jina la Mungu kwao bado ni tofauti kabisa na wachagga.
Hivyo wachagga asilia ndio waliobeba zile tamaduni karibu zote za asili lakini baadaye wakaingia wageni kutoka jamii za jirani hususan Wataita walioingia kwa wingi zaidi, Wakamba na Wamasai kwa kiasi kikubwa pamoja na Wapare, Wasambaa, Wandorobo na Wakikuyu kwa kiasi kidogo. Hawa jamii za jirani walioingiliana na wachagga kwa kiasi kidogo wamekuwa na athari katika tamaduni za kichagga lakini ni kwa kiasi kidogo ndio maana unaweza kuona kuna utofauti mkubwa wa kitamaduni kati ya wachagga na hizo jamii za jirani.
Lakini pamoja na hayo yote wachagga wengi wamekuwa wakifanya makosa makubwa pale wanapofuatilia asili zao na kufanya hitimisho rahisi kwa kujidanganya na vigezo ambavyo sio sahihi.
Sehemu kubwa sana ya wachagga ukiwauliza, wanaamini kwamba asili yao ni wamasai. Na kigezo kikubwa wanachotumia kuamini wao ni wamasai watakwambia kwamba babu yake au baba wa babu yake au babu wa babu yake alikuwa ametoboa masikio kama wamasai. Na hapa utakuta ni aidha aliona kwenye picha aliyopigwa babu yake zamani au alihadithiwa na baba yake au babu yake kwamba wao walikuwa ni wamasai kwa kigezo kwamba babu zao walikuwa wametoboa masikio.
Kigezo hiki cha kujiita mmasai kwa sababu babu au babu wa babu alikuwa ametoboa masikio ndio upotoshaji namba moja wanaofanya wachagga katika kutafuta asili yao na imekuwa ndio kigezo rahisi kwa wachagga wengi kufanyia hitimisho. Hii pia ndio sababu wachagga wengi wanaamini kwamba asili yao ni wamasai na sio hizo jamii nyingine hususan Wataita na Wakamba. Sio rahisi kukuta mchagga anayekwamba asili yao ni wataita au wakamba, wote wanakimbilia kujiita ni wamasai kwa kigezo hicho cha mababu kutoboa masikio.
Ukweli ni kwamba wengi wamepotoshwa au kujipotosha wenyewe. Licha ya kwamba ni kweli kwamba kuna sehemu ndogo ya jamii ya wachagga iliyoingiliwa na damu ya umasai lakini sio kwa kiasi kikubwa kama wengi wanavyoamini na hasa kwa kutumia kigezo cha kutoboa masikio ambacho ndio sehemu kubwa ya upotofu huu ulipo.
Suala la kutoboa masikio ni utamaduni uliokuwepo ndani ya jamii nyingi sana Afrika na sio wamasai peke yao. Kwanza wachagga wenyewe walikuwa wanatoboa masikio pia. Wakamba, wataita, wakikuyu, wasambaa, wapare, wandorobo na jamii nyingine za mbali kabisa maeneo yote Afrika miaka ya zamani wote walikuwa wanatoboa masikio.
Kimsingi suala la kutoboa masikio pamoja na sehemu nyingine za mwili kama vile pua, ulimi, midomo n.k. pamoja na kujichora tunaweza kuona kwamba upo hata katika jamii ambazo ni primitive mpaka sasa huko katika misitu ya Amazon Amerika ya kusini. Hata Misri ya kale na Ethiopia ambako imethibitishwa kwamba ndipo wachagga asilia walipotokea kulikuwa na utamaduni wa kutoboa masikio na kuyavuta. Huko Ethiopia mpaka sasa bado kuna jamii za vijijini zinatoboa masikio na kuyavuta kama wasamai. Hivyo hatuwezi kushangaa kwa nini wachagga pia walikuwa na utamaduni kama huo.
Lakini kutoboa masikio na kuyavuta zaidi kwa lengo la kuvaa urembo na shanga halikufanyika Afrika na Amerika peke bali hata Asia ya huko China, Japan na Ufilipino utamaduni huu ulikuwepo. Miaka ya zamani sana hata wazungu Ulaya walikuwa na utamaduni huu wa kutoboa masikio.
Inasemekana kwamba katika historia mtu wa zamani zaidi anayefahamika kutoboa masikio ni mtawala wa Misri ya kale aliyeiywa Farao Tutankhamun. Huyu alikuwa ni mtawala wa Misri ya kale kutoka kwenye kizazi cha 18 cha utawala wa Misri wastani wa kama miaka 3,300 iliyopita. Hata hivyo baadhi ya watafiti wa mambo ya kihistoria (anthropologists) wanaamini kwamba utamaduni wa kutoboa masikio asili yake ni Afrika, Kusini la jangwa la Sahara.
Hata tukirudi kwa wachagga wenyewe ambapo tunafahamu kwamba kuna baadhi ya wazee wa zamani kama vile Mangi Ngulelo wa Machame, Mangi Meli wa Old Moshi, Mangi Ndegoruo wa Marangu na hata Mangi Fumba wa Kilema ambao walikuwa wametoboa masikio lakini tunafahamu kabisa kwamba hawakuwa na asili ya umasai.
Kilichotokea ni kwamba jamii nyingi zilikuja kuachana na utamaduni wa kutoboa masikio isipokuwa wamasai peke yao ambao wamekuwa ni watu wagumu kidogo kubadilika na kuacha tamaduni zao za kale ambapo mpaka sasa bado wanatoboa masikio. Hii ndio maana imekuwa rahisi kwetu kumhusianisha mtu yeyote aliyewahi kutoboa sikio kwamba ni mmasai. Zamani ilikuwa ni jambo la kifahari mtu kutoboa masikio, na jambo la aibu kwa mtu ambaye hajatoboa masikio.
Hivyo koo mbalimbali za wachagga tunapotafuta asili zetu tunapaswa kuwa makini sana na upotofu huu wa kuhitimisha kiurahisi kwamba ni wamasai na badala yake kufuatilia kwa kina kufahamu chimbuko la ukoo husika. Hii ni kwa sababu sehemu kubwa zaidi ya jamii ya wachagga wametokea zaidi kwenye wachagga asilia kuliko hizi jamii majirani zilizoingilia Uchagga kwa sehemu na ndio maana hata tamaduni nyingi ni za kichagga kipekee zisizoingiliana na hizo jamii za jirani ikiwemo wamasai.
Hata hivyo jamii za jirani hususan Wataita, Wakamba na Wamasai waliingia kwa kiasi na mchango wao kwenye tamaduni za kichagga upo lakini ni kwa kiasi kidogo sana. Na mfano mzuri mtu unaweza kuangalia kwenye lugha ya kichagga ni kwa kiasi gani inaingiliana na hizo jamii nyingine.
Jambo lingine la muhimu kufahamu ni kwamba jamii jirani na wachagga iliyoongoza kwa kuingia kwa uwingi zaidi ndani ya Uchagga ni wataita(ambapo athari yao imeonekana kwa kiasi kikubwa zaidi ndani ya Uchagga kwa upande wa lugha), jamii jirani ya pili iliyoingia kwa uwingi ndani ya Uchagga ni wakamba na ya tatu ndio wamasai. Hizo jamii nyingine kama Wakikuyu, Wasambaa, Wandorobo na Wapare waliingia kwa kiasi kidogo zaidi. Hivyo inategemewa kwamba basi wachagga wengi zaidi wangekuwa wakijitambulisha zaidi kuwa ni wa asili ya Taita kuliko Masai. Hata asili ya Ukamba ndani ya Wachagga bado iko kwa kiasi kikubwa kuliko Masai lakini sio rahisi kusikia watu wakisema wana asili ya Taita au Ukamba badala yake utasikia tu ni Masai.
Hata hivyo mwisho wa siku tamaduni za wachagga asilia ndio zimetawala na kwa vile ndio sehemu kubwa ya jamii ya kichagga, ndio maana jamii husika wakawa ni wachagga wenye utofauti na upekee katika vitu vingi kutoka kwenye hizo jamii nyingine zote majirani.
Karibu kwa Maoni, Maswali na Nyongeza.
Ni ruksa kusambaza makala hii na ni muhimu pia.
Ahsante sana.