FAHAMU MTAZAMO WA WATU WA NJE YA KUNDI.

Katika maisha, moja kati ya vitu ambavyo vinafanya tuwakubali na kuwaamini watu ni kuamini kwamba wanapeda na kukubaliana na mambo yetu. Mara nyingi tunapomkubali sana mtu na kumfuata mtu huwa tunajiaminisha pia kwamba mtu huyo anapenda mambo yetu na kuamini kwamba anayaunga mkono. Kwa maana hiyo huwa hatusiti hata kutaka kupata maoni yake juu ya mambo hayo yetu na kisha kuamini kwamba maoni hayo ameyatoa kwa nia njema na kwa lengo la kujenga. Hilo linatufanya tuyaamini maoni hayo na kuyafuata.

Ukweli ni kwamba unapaswa kuwa makini sana unapopokea maoni yoyote kwa mtu ambaye yuko nje ya kundi la kijamii ulilopo juu ya kundi hilo. Hiyo haijalishi unampenda au kumuamini kiasi gani, haijalishi ni mtu msomi kiasi gani, mwenye akili kiasi au ni rafiki yako wa karibu kiasi gani. Ni muhimu sana kuwa makini na maoni anayotoa juu ya kundi la kijamii ulilopo ikiwa unategemea maoni yake ili kuchukua hatua yoyote kwenye kundi la kijamii ulilopo.

Sisemi usimwamini mtu huyo kwenye mambo mengine, au kwamba usiamini kabisa maoni yake juu ya mambo yanayohusu kundi la kijamii ulilopo lakini yeye hayupo. Namaanisha uwe makini na maoni yake juu ya mambo yanayohusu kundi la kijamii ambalo yeye sio mhusika. Hii ni kwa sababu binadamu wengi kwa asili, kwa sababu mbalimbali hususan za kibinafsi huwa aidha hawajali au hawana mtazamo chanya juu ya kundi la kijamii ambalo sio wahusika.

Kwa mfano wewe ni mkristo ambaye unajivunia na kupenda sana ukristo na uko tayari kujitoa sana kwa ajili ya ukristo lakini una rafiki yako muislamu anaupenda sana uislamu lakini ambaye unamheshimu sana, mnapenda na kusaidiana sana na unamwamini sana bado unapaswa kuwa makini na maoni yake juu ya mambo yako yanayohusu ukristo. Kwa sababu yeye hayupo kwenye kundi la wakristo ni nadra sana kuwa na maoni sahihi au chanya kuhusu mambo yanayohusu wakristo. Na kinyume chake ni hivyo hivyo pia.

Au kwa mfano wewe ni mchagga ambaye unajivunia sana kuwa mchagga na unapenda sana mambo ya wachagga. Lakini una rafiki yako ambaye ni msambaa, rafiki ambaye unamwamini sana, mnapendana sana na una uhakika kwamba ni rafiki wa kweli kabisa kwako, bado unapaswa kuwa na mashaka na maoni yake juu ya mambo yanayohusu wachagga. Kwa sababu yeye sio mhusika wa ndani ya kundi hilo la kijamii kuna uwezekano mkubwa sana kwamba aidha hajali sana au akatoa maoni hasi juu ya jambo lolote kuhusu wachagga.

Hapa simaanishi kwamba watu wote ni hasi hapana, unaweza kweli kukutana na mtu ambaye sio wa kundi husika na bado akawa anapenda sana mambo ya watu wasio wa kundi husika. Kwa mfano unaweza kukutana na muislamu anayependa sana mambo ya wakristo anayafurahia sana na ana mtazamo chanya kabisa juu yake na anaweza hata kuchangia ujenzi wa kanisa au kujenga kabisa kanisa. Lakini hilo kutokea huwa ni nadra sana kuliko kinyume chake.

Binadamu mara nyingi ni wabinafsi na ndani ya mioyo yao hupenda zaidi vile vya kwao kuliko vingine, japo machoni au mdomoni anaweza kuigiza tofauti lakini ndani ya moyo wake ikawa ni kinyume chake. Lakini pamoja na hayo yote sisemi kwamba watu hao ni wabaya, hapana ni watu wazuri sana tena wakati mwingine kuliko hata watu ambao uko nao kundi moja. Binadamu wameumbwa tofauti ambapo watu wabaya na watu wazuri wako kwenye kila kundi la kijamii. Kwenye kila dini, kwenye kila kabila, kwenye kila nchi, kwenye kila rangi, kwenye kila chama cha siasa, kwenye kila aina ya itikadi kuna watu wabaya na wazuri. Na ni sahihi kabisa kuwa na marafiki kutoka kwenye makundi mbalimbali ya kijamii kama ukiona wanakufaa.

Jambo la muhimu tu ni kuwa makini na maoni ya watu ambao wako nje ya kundi lako juu ya mambo yanayohusu kundi lako la kujamii. Sio mara zote wanakuwa na upendeleo lakini mara nyingi wanakuwa na upendeleo na hata kujisikia wivu.

Kwa nini nimeandika hii makala?

Kwa sababu kuna watu wengi ambao kabla ya kufanya maamuzi hupenda kupata maoni ya baadhi ya watu wanaowaamini ndio kisha baada ya hapo hufanya maamuzi juu ya jambo husika. Sio vibaya kufanya hivyo, lakini ni muhimu kuwa makini na aina ya maoni unayohitaji na aina ya mtu unayemwomba maoni hayo na uhusiano wako na jambo husika. Unaweza kupotea au kushindwa kufanya jambo la maana kwa sababu ya kusikiliza maoni kutoka kwa mtu ambaye sio sahihi na anayekupa maoni ya kubomoa badala ya kujenga.

Jambo hili pia liliwatokea wachagga na kuwagharimu sana na hata mpaka sasa bado wanaendelea kulirudia. Waliwaamini watu ambao hawakuwa na nia njema au sahihi kwao ambao walikuja na maoni au hoja fulani juu ya mambo yanayowahusu zilizolenga kuwabomoa lakini zinazoonyesha nia njema ndani yake na hivyo kupelekea anguko lao. Anguko hilo likarudisha nyuma kila kitu mpaka kubadili mtazamo wa kimaadili uliopelekea kuwadhoofisha kabisa. Wachagga wa leo wanaamini hapo walipo wana maendeleo kwa sababu ya kutokujua walipotoka, ukweli ni kwamba wachagga wamerudi nyuma sana na hapa walipo leo ni nyuma sana ukilinganisha na hatua kubwa sana walizokuwa wamepiga tangu miaka ya zamani sana. Ukiwalinganisha hata na Wakikuyu wa leo hii ambao wachagga walikuwa wamewaacha mbali utajionea kwamba wachagga wamerudi nyuma sana.

Tunaweza kuona hata kwenye historia, waandishi wengi kutoka nje ya wachagga walioandika historia ya wachagga wameandika kwa namna mbalimbali za kuipunguzia hadhi au kubeza kwa namna mbalimbali. Pia hata ukifuatilia watu wengine wanapozungumzia historia za maeneo mbalimbali utakuta wanajaribu kudidimiza au kupunguzia hadhi ile historia ya watu wanaoonekana ni waliopiga hatua kubwa zaidi au maarufu na mashuhuri kuliko wao ili tu, wajisikia vizuri.

Hivyo ni muhimu sana kuwa makini na maoni yoyote yanayohusu kundi letu la kijamii kutoka kwa mtu wa nje. Japo wakati mwingine anaweza kuwa ni mtu wa ndani lakini ambaye ameshabadilishwa mtazamo na maoni ya kutoka kwa watu wa nje. Ni rahisi kusema hapana, yule ni waziri mkubwa anasema hivyo, yule ni Rais ambaye anatupenda na kupenda maendeleo yetu, yule sijui ni Askofu, sijui ni baba wa nchi. Yote hiyo haijalishi ikiwa anatoka nje ya kundi, kwa sababu wote ni binadamu hivyo ni muhimu kuweka umakini kwa maoni yanayotoka kwake na ikiwezekana hakuna haja kabisa ya kuomba maoni yake kwenye jambo hilo. Unaweza kuendelea kuomba ushauri wake kwenye mambo mengine.

Wakati mwingine ni rafiki yako wa kike au kiume ambaye ana maoni tofauti. Sio lazima kubishana naye au kutaka kumashawishi ni kwa kiasi gani wewe uko sahihi, hilo litapelekea mivutano mikubwa sana isiyoisha na isiyo na maana, jambo la muhimu ni kumpuuza na kuendelea na mambo yako bila kuyapa umuhimu maoni yake.

Muhimu zaidi ni kwamba maoni ya watu wa nje, iwe ni watu wakubwa kiasi gani au waliokaa kwenye nafasi za juu kiasi gani hayapaswi kuwa kikwazo kwa sisi kufanya mambo yetu. Kwa sababu watu hao ni watu wa nje na sio wahusika wa mambo haya. Sidhani kama hata Papa Francis anaweza kusikilizwa na waislamu wakaacha kufanya mambo yao kwa sababu yeye ni mtu mkubwa, kwa sababu Papa Francis sio muislamu, hivyo mambo ya waislamu hayamhusu. Hivyo hivyo maoni ya mtu anayetoka nje ya kundi ambalo sio mhusika hayapaswi kufanywa sheria na watu wanaotoka ndani ya kundi hilo au kuwazuia kwa namna yoyote kuendelea mbele kufanya mambo yao.

Kwa mfano ikiwa barabara za Kilimanjaro ni mbovu sio rahisi mtu anayetokea Mbeya au Mwanza akaumizwa kwa ubovu wa barabara za Kilimanjaro zaidi ya watu wa Kilimanjaro wenyewe. Hivyo itakuwa ni makosa na upumbavu ikiwa watu wa Kilimanjaro watamsikiliza mtu wa kutoka Mbeya anayewashauri waridhike na barabara mbovu wakati mtu huyo hatokei Kilimanjaro. Hivyo hivyo inakwenda kwenye mambo mengine yote yanayolihusu kundi husika ambayo yenye mchango usio wa moja kwa moja wa kimaendeleo.

Ahsanteni.

Karibu kwa maoni au maswali.

Urithiwetuwachagga

urithiwetuwachagga@gmail.com

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *