PETRO M. NJAU (MORENJA).

Mwanafalsafa Mahiri na Mbeba Maono wa Taifa La Wachagga, Kilimanjaro.

– Petro Njau alizaliwa mwaka 1890 katika kitongoji cha Fumvuhu, kijiji cha Kidia, Old Moshi.

Alikuwa ni mwanafunzi mwenye uwezo mkubwa kiakili darasani na alisoma wakati wa utawala wa wajerumani na kuelewa vizuri sana lugha ya kijerumani pia ambapo alihitimisha masomo yake mwaka 1910. Petro Njau alianza kuonyesha dalili za kuwa mwanamapinduzi tangu mapema sana ambapo alitoa changamoto na kujaribu kupambana na zile mila za kichagga alizoziona sio sahihi na alifanikiwa kwa kiasi.

– Petro Njau aliajiriwa kwenye utumishi wa serikali ya wajerumani na baadaye waingereza kama Mwalimu. Baadaye aliendelea kupiga hatua kufikia kuwa Mwalimu mkuu katika shule kadhaa kuanzia Old Moshi, Marangu, Masama na Rombo. Mwaka 1931 aliachana rasmi na kazi ya ualimu kuongeza nguvu kwenye harakati za utaifa na maslahi ya wachagga.

– Yeye na Joseph Merinyo kuanzia katika miaka ya 1920’s walianza kuwa na ushawishi mkubwa kwa wachagga huku nguvu zao kisiasa kwa wachagga zikiongezeka sana. Walianza kuingia kwenye migogoro na mivutano na serikali ya waingereza kwa kupigania maslahi ya wachagga na kujipa uhalali wa kutetea haki za wachagga kama taifa ambalo waingereza walidai hawalitambui, wala hawatambui jamii inayoitwa wachagga kama taasisi inayopigania haki zake.

PETRO NJAU AKIMPAKA MAFUTA MAALUM MANGI MKUU WA WACHAGGA “THOMAS MAREALLE” SIKU YA KUAPISHWA KWA MANGI MKUU.

– Petro Njau pia na mwenzake Joseph Merinyo waliingia kwenye mgogoro na kanisa la kilutheri baada ya uwepo wa wazungu wamisionari waliokuwa wanashindwa kuonyesha heshima inayostahili kwa wachagga na kwa mila za kichagga. Petro Njau na mwenzake Joseph Merinyo walionyesha misimamo dhidi ya baadhi ya mambo ya kanisa yaliyokuwa yanabeza au kupunguzia hadhi baadhi ya mila nzuri za kichagga kwa sababu waliamini kwamba zilikuwepo nyingi ambazo zilikuwa na manufaa makubwa kwa wachagga.

– Mwaka 1931 Petro Njau na mwenzake Joseph Merinyo baada ya kuonekana wana nguvu kubwa sana kisiasa kwa wachagga na wanajitahidi kupambana zaidi kuhakikisha wachagga wanajitambua na kuwa taifa huru walifukuzwa Kilimanjaro na kupelekwa kuishi uhamishoni nje ya Kilimanjaro ili kuwapunguzia nguvu kubwa ya kisiasa waliyokuwa nayo wakati. Walienda mpaka Monduli na baadaye Kondoa, Singida na Kigoma ambapo waliishi uhamishoni nje ya Kilimanjaro kwa kipindi cha miaka 15.

– Wakiwa nje ya Kilimanjaro walizidi kuamarika na kupata uelewa zaidi wa mambo mengi sana kwa walishiriki katika uanzishwaji wa chama cha African Association AA katika miaka ya mwanzoni ya 1930’s na ndio waliopendekeza kuvunjwa kwa chama hicho na badala yake vianzishwe vyama vya maeneo. Walirudi Kilimanjaro katika miaka ya 1940’s wakiwa wameimarika sana kimtazamo na kisiasa huku wakiwa na maandilizi bora zaidi ya kujenga hali ya utaifa na uzalendo kwa wachagga na taifa lao.

– Katikati ya miaka ya 1940’s walianzisha chama cha siasa za wachagga wahafidhina cha Kilimanjaro Chagga Citizens Union (KCCU). Petro Njau mwenyewe ndiye alikuwa mwandishi mkuu wa falsafa na itikadi ya chama cha Kilimanjaro Chagga Citizens Union (KCCU) iliyokuwa imeandikwa kwa ustadi mkubwa kwa namna ambayo inachochea maendeleo makubwa ya kiuchumi na kitaaluma kwa wachagga huku ikiendelea kubakiza mila na tamaduni za wachagga kutoka kwenye vizazi vilivyopita na kuzirithisha kwenye vizazi vijavyo. Kwenye kitabu cha “Miaka 700 Ya Wachagga” hili limefafanuliwa kwa undani sana.

– Chama hiki cha wachagga wahafidhina cha Kilimanjaro Chagga Citizens Union (KCCU) kilipata nguvu kubwa sana miongoni mwa wachagga na kukubalika sana. Chama hiki cha wachagga wahafidhina ndicho kilichopigania kuanzishwa kwa nafasi ya umangi mkuu katika kuwaletea wachagga pamoja kuelekea kufanikisha mambo makubwa zaidi. Chama hiki cha wachagga wahafidhina (KCCU) pia ndicho kilichompendekeza Thomas Marealle kuwa mgombea urais kwenye nafasi ya umangi Mkuu ambaye hakuwepo hata kwenye orodha ya wagombea na wala hakuwa anapewa nafasi kuingia kwenye orodha ya wagombea umangi Mkuu.

– Chama hiki kilipambana mpaka Thomas akaingizwa kwenye ushindani kwa gharama ya kumuondoa baba yake mdogo Petro Itosi Marealle ambaye alikuwa anakubalika sana na wamangi karibu wote wa Kilimanjaro ili kuepusha kuwa na wagombea wawili kutokea eneo moja na Thomas Mandara aliyeonekana bado mdogo kiumri na kiuzoefu. Chama hiki kilimpa nafasi na kumsimamisha Thomas Marealle kama mgombea wao wa nafasi ya umangi mkuu huku msimamizi mkuu akiwa Petro Njau na kwa pamoja waliweza kufanya kampeni kubwa Uchaggani kote na kumpatia ushindi wa kishindo dhidi ya wagombea waliokuwa na nguvu na wenye ushawishi kwa waingereza kama Mangi Abdiel Shangali.

– Petro Njau aliendelea kuwa ndiye msemaji mkuu wa chama cha wachagga wahafidhina KCCU na mtu mwenye nguvu sana ndani ya serikali ya Mangi Mkuu Thomas Marealle. Petro Njau ndiye alikuwa mwandishi mkuu na mashuhuri kwenye gazeti la wachagga la “Komkya” ambalo lilikuwa kama jukwaa la wachagga kujadili agenda zao mbalimbali na lilisomwa sana ndani na nje ya Kilimanjaro na hata nje ya Tanganyika hususan Kenya katika miji ya Nairobi na Mombasa.

– Kupitia gazeti la Komkya Petro Njau aliweza kupigania mambo mbalimbali yanayowahusu wachagga kuanzia tamaduni mpaka kiuchumi. Petro Njau alipendwa sana na kuungwa mkono na wachagga waliokuwa wanaishi nje ya Kilimanjaro kama vile Mombasa n.k., ambao alipigania haki zao za urithi wa ardhi na kuwahimiza kurudi Kilimanjaro kuja kunufaika na kilimo cha kahawa ambacho kilikuwa kinaendelea kukua na kuleta utajiri kwa wachagga kwa kasi kubwa. Kupitia makala za kurasa za Petro Njau kwenye gazeti la Komkya wachagga wengi walirudi Kilimanjaro na kunufaika na mabadiliko ya kiuchumi yaliyokuwa yanaendelea.

– Petro Njau akiwa msemaji mkuu wa serikali ya wachagga iliyokuwa ikiongozwa na Mangi Mkuu Thomas Marealle waliendelea kuhakikisha chama cha wachagga wahafidhina na agenda zake kinaendelea kuwa na ushawishi na kukubalika sana kupitia yale inayoyapigania. Petro Njau kupitia gazeti la Komkya aliandika na kupigania sana pia ardhi ya kubwa ya Kibosho iliyokuwa imechukuliwa na wakulima wageni kwa sehemu kubwa na kuwaacha wachaggga wa Kibosho wa maeneo husika wakishindwa kunufaika vizuri na kilimo cha kahawa kutokana na uhaba wa ardhi na kuishia kufanya vibarua kwenye mashamba hayo.

– Petro Njau katika miaka ya 1950’s aliboresha zaidi falsafa ya chama cha wachagga wahafidhina kuendana na mazingira yaliykuwepo na namna wanaweza kufanya ushirika na vyama vingine vyenye agenda inayoendana na yao kama vile chama cha United Tanganyika Party(UTP). Chama hiki hakiwekeza kwenye kuhubiri ubaguzi na kuchukua wageni bali kuwa na jamii za mataifa mbalimbali ndani ya taifa moja tofauti na ile ya TANU ambayo ilizingatia katika kukosoa sana wageni na kuwageuza maadui hivyo kupuuza mazuri yao na kushindwa kunufaika na yale mazuri yaliyokuwepo ili kupiga hatua kubwa na kwa haraka kama nchi ambazo zilifanya hivyo na sasa ziko mbali.

– Petro Njau alifanya mengi kwa wachagga na hata Tanganyika kwa ujumla lakini mengi ni ya kutafuta sana kwani historia za mashujaa hawa hazijakuja kupewa kipaumbele sana baadaye. Petro Njau ni mtu aliyeheshimiwa sana na kila mtu katika nyakati zake hata na baada ya hapo na ilibidi hata maridhiano ya watu wenye ushawishi Kilimanjaro na chama cha TANU kilichokuja kupewa dhamana na waingereza yalimhusisha sana Petro.

– Petro Njau alifariki mwaka 1986 na kuzikwa nyumbani kwake eneo la Mbaruki, karibu na Kiboriloni akiwa na umri wa miaka 96. Maandishi yake mengi bado yanapatikana kwenye nyaraka mbalimbali za wachagga zamani. Maandiko mengine ya Petro Njau yanapatikana kwenye nakala za magazeti ya zamani ya wachagga ya “Komkya” na “Kusare”.

Ahsanteni.

Karibu kwa Maoni au Maswali.

www.wachagga.com

Urithi Wetu Wachagga (Facebook).

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *