HATA BILA UKOLONI WALA UJIO WA DINI ZA KIGENI WACHAGGA WANGEENDELEA KUWA BORA ZAIDI NA ZAIDI (KUSTAARABIKA).

– Moja kati ya maneno ambayo huwa yananipa ugumu au ukakasi sana kuyatumia ni pamoja na neno hili “ustaarabu” kutokana na asili ya neno lenyewe. Naamini wote tunajua maana ya neno ustaarabu kwamba ni kuishi au kuwa na utamaduni ambao unaonekana kuwa ni wa hadhi ya juu zaidi katika maisha, au kama unavyojulikana kwa kiingereza “civilised”.

– Lakini kwa bahati mbaya asili ya neno ustaarabu ilivyokuja haikumaanisha kupiga hatua zaidi kimaisha katika jamii zetu kutokea pale zilipokuwepo(advancing in life) bali ilimaanisha kuishi kama watu wa jamii nyingine hivyo kupora ile maana halisi. Kwa kifupi neno ustaarabu kwa dunia ya waswahili lilimaanisha kuwa kama waarabu au kuishi kwa tamaduni za waarabu. Yaani kuishi kama waarabu ndio kustaarabika, tafsiri ambayo haikuwa sahihi kwani waswahili nao walikuwa na tamaduni zao ambazo wangeweza kuziboresha kwa namna yao badala ya kukopi kila kitu cha waarabu. Wangeweza kuchukua machache mazuri na mengi mazuri kutoka kwenye tamaduni zao na kutengeneza utamaduni bora kabisa na sio kuchukua mambo yote ya waarabu na kuwa kama waarabu, kwani kwa kufanya hivyo ilikuwa ni sawa na kujitukana wao wenyewe na kutukuza waarabu ambao hata hivyo nao waliwadharau pia.

– Hata hivyo nimekosa msamiati mwingine wa kiswahili uliojitosheleza unaoweza kuwa mbadala wa neno, “ustaarabu” hivyo ili kueleweka kwa usahihi zaidi napaswa kutumia neno hili ambalo kwa sasa pengine tafsiri yake imekuwa na dhana pana zaidi kuliko malengo iliyokuwa imebeba mwanzoni japo neno limebaki vile vile. Hii ni mada ya siku nyingine, kwa leo turudi kwenye mada yetu kwamba “Hata bila ukoloni wala ujio wa dini wachagga wangeendelea kuwa bora zaidi na zaidi”.

– Kuna watu wanashukuru ujio wa ukoloni na wengine wanashukuru ujio wa dini za kigeni kwamba kama sio hizo basi jamii za ulimwengu wa tatu zingekuwa bado hazijapiga hatua kubwa mpaka sasa. Kwa hilo naweza nisizisemee jamii nyingine kwa sababu sifahamu sana mitazamo waliyokuwa nayo juu ya kuwa bora zaidi katika nyanja nyingi katika maisha yao lakini sio wachagga. Wachagga na hasa baadhi ya viongozi wakuu wa wachagga walikuwa na mtazamo mpana na endelevu na walikuwa kwenye mwendelezo wa kukuza na kuboresha maisha kwa namna mbalimbali kwa kutumiza nyenzo walizokuwa nazo sambamba na nyingine walizoona zinawafaa kutoka kwenye jamii nyingine.

– Kwanza kabisa kabla ya kwenda mbali zaidi tuangalie suala la jamii kuigana katika kuboresha zaidi tamaduni zao na maisha yao kwa ujumla. Wengi tunaiangalia Ulaya na kuitamani au kuionea wivu na wengine hata kuichukua kwa namna ilivyopiga hatua kubwa sio tu katika kustaarabika bali hata katika maeneo mengine muhimu kama vile mifumo ya kisiasa, kiuchumi na maendeleo makubwa ya kiteknolojia iliyonayo na hata kuwa chanzo cha kusambaza maendeleo hayo maeneo mengine yote ya dunia hii. Lakini swali ni je, Ulaya walianzia wapi? Je ilitokea tu kwamba wazungu walianza kuwa bora wao wenyewe kutoka ndani ya jamii yao bila kuhusisha nguvu au chanzo kingine nje yao? Hapana hilo sio kweli, kila kitu huwa kina chanzo na sababu.

– Watafiti na wanahistoria wengi wanakubaliana kwamba chanzo cha “ustaarabu” wa Ulaya ni Ugiriki ya kale au Uyunani ya Kale, wanasema hivi, “Ancient Greek is the cradle of European civilisation”, ikimaanisha, “Ugiriki ya kale ndio chanzo cha ustaarabu wa Ulaya”. Hata hivyo ukiangalia ustaarabu wa Ulaya ambao ulisambazwa na himaya ya Rumi ya kale uliigwa kutokea Ugiriki ya kale. Mwanzoni kabisa katika himaya ya Rumi wakati inaanza baada ya kuziangusha himaya nyingi kama Ugiriki, Uajemi ya zamani n.k., hata lugha ya wasomi na ya kufundishia katika shule za huko himaya ya Rumi au Roma ilikuwa ni kigiriki au kiyunani. Yaani kuwa mgiriki au kuongea kigiriki au kiyunani ilikuwa ndio ujanja na usomi. Hivyo Ugiriki ndio ilikuwa chanzo cha kuistaarabisha Ulaya tunayoiona leo hii.

Lakini je Ugiriki wao walipata wapi ujanja na maarifa hayo mpaka kuendelea sana? Kwa mujibu wa mwanafalsafa wa Uingereza Bertrand Rusell kwenye kitabu chake cha “History of Western Philosophy” anaeleza kwamba maendeleo na ustaarabu wa “Ugiriki ya zamani” yaliigwa na kushawishiwa kutoka katika himaya ya “Misri ya zamani”. Misri ya zamani(Sio hii ya sasa ya waarabu) tunaweza kuiona hata kutokea kwenye vitabu vya zamani ilikuwa ni himaya kongwe na iliyopiga hatua kubwa kiasi kwamba hata watafiti na wanasayansi wa leo wanashangazwa na maendeleo ya sayansi na hisabati yaliyokuwa yamefikiwa na Misri kwa maelfu ya miaka iliyopita.

– Sayansi, hisabati na falsafa nyingi zilizoendelezwa huko Ugiriki ya zamani ziliigwa zaidi kutokea Misri ya zamani. Unaweza kuona hilo hata kupitia maandiko ya wanahistoria na wanafalsafa wa Ugiriki ya kale kama vile Herodotus, Thucydides, Pythagorus, Archimedes n.k. jinsi walivyokuwa wanaikubali na kuizungumza Misri ya zamani kwa namna ya kuitukuza sana. Mwanahistoria kama Herodotus wa Uyunani ya kale ameizungumzia sana Misri na mambo yake mengi na ukuu wake mkubwa na jinsi ilivyokuwa chanzo cha kuistarabisha Ugiriki ya zamani.

– Hata hivyo wakati chanzo cha ustaarabu wa Misri kikiwa bado kinatawaliwa na nadharia nyingi mbalimbali mpaka sasa tumeweza kuona kwamba maendeleo na ustaarabu wa jamii mbalimbali mara nyingi chanzo chake kwa sehemu ni maendeleo au ustaarabu unaoigwa kutoka kwenye jamii nyingine. Hivyo tunapozungumzia “ustaarabu” wa wachagga hatuna budi kujua kwamba wachagga walikuwa wana mambo mengi mazuri lakini bado suala la kuiga baadhi ya mambo mazuri kutoka kwenye jamii nyingine zilizopiga hatua kubwa zaidi ni suala la kawaida na bado inabaki kuwa ni jamii hiyo hiyo ya wachagga.

– Kwanza kabisa wachagga walikuwa wameshapiga hatua kubwa kwenye baadhi ya mambo. Kupitia historia tunafahamu kwamba, licha ya kwamba wachagga walikuwa wameshapiga hatua kubwa katika kuboresha mifumo ya kisiasa na kuendelea kujenga mitazamo bora sana juu ya maeneo mengine mbalimbali ya kiimani na kifalsafa lakini pia wachagga tayari walikuwa wameendeleza lugha ya maandishi iliyokuwa inatumika kwenye baadhi ya mafundisho ya rika.

– Kwa juhudi za ndani ya jamii tunaweza kujifunza kwamba watawala wa kichagga waliokuwa na mitazamo mipana na uelewa mkubwa hususan Mangi Rindi Mandara alijitahidi kupunguza sana imani za uongo zilizokuwa zinairuisha nyuma jamii katika mambo mengi ambayo yanahitaji vitendo na uhalisia. Kwa mfano kupiga marufuku ushirikina na uganga kwenye vitu vinavyohitaji uhalisia na uimara kwenye maeneo kama jeshini, kwenye kilimo na shughuli nyingine za kiuchumi. Hii ilikuwa ni hatua kubwa iliyoendelea kupata nguvu katika ardhi yote ya Uchagga.

– Kwa upande wa maendeleo ya teknolojia ya ndani ya Uchagga tumejifunza jinsi wachagga walivyoendeleza teknolojia bora katika eneo la umwagiliaji lililloboresha sana kilimo na kudhibiti njaa tangu karne nyingi zilizopita. Teknolojia hizi za miundombinu ya umwagiliaji zilifanyika kwa kutumia uwezo mkubwa kiasi kwamba ziliwaacha midomo wazi wageni wengi waliotembelea Kilimanjaro hususan wale waliotokea nchi za Ulaya. Alexander Le Roy kwenye kitabu chake cha “Mission To Kilimanjaro” amefanunua vizuri namna fikra za kuleta mapinduzi ya kilimo ya wachagga zilivyopelekea wachagga kuja na ubunifu mkubwa katika miundombinu ya umwagiliaji tangu karne nyingi zilizopita.

– Tumejifunza pia jinsi Mangi Sina Mushi alivyoweka juhudi na msisitizo katika shughuli za kilimo na kupelekea mavuno makubwa ambayo yalihakikisha kwamba wachagga wanakuwa na vyakula vya kutosha wakati wote. Haya yalikuwa muhimu sana kwenye kuhakikisha maeneo mengine ya maisha yanakuwa bora kwani kunapokuwa na njaa hata utulivu wa jamii na ule ustaarabu unapotea. Hili tumeona jinsi lilivyokuwa linawasumbua wamasai mara kwa mara na kupelekea kukimbilia Kilimanjaro kupata msaada kitu ambacho kilipunguza utu na heshima yao mbele za jamii majirani ambao wakati mwingine walikuwa ni maadui zao.

– Katika juhudi za kujifunza mambo mengine kutoka kwenye jamii nyingine ili kuwa bora zaidi tumejifunza kutoka kwenye historia kwamba watawala wa Uchagga walipenda na kuvutiwa na kuwaheshimu watu waliopiga hatua kubwa kuwazidi ambao walikuwa wanatokea nchi za mbali hususan wazungu. Lakini hapo hapo walikuwa wanawadharau watu waongo waongo na wasiokuwa na mambo yanayoeleweka wala kupiga hatua kubwa kwenye maisha yao kama vile watu wanaotokea maeneo mengi duni hususan maeneo ya pwani. Kuvutiwa huku hawakubaki hivi hivi bali walichukua hatua.

– Kutoka kwenye historia tunajifunza kwamba mwaka 1878 Mangi Rindi Mandara katika kuhakikisha kwamba wachagga wanapiga hatua zaidi kimaendeleo kwa kujifunza pia kutoka kwenye jamii nyingine aliwaandikia barua wamisionari wa CMS kutoka London, Uingereza kupitia misheni yao ndogo iliyokuwa Mombasa kuja kufungua shule Kilimanjaro. Mangi Rindi Mandara alitaka wamisionari wale waje kufundisha wachagga baadhi ya mambo ambayo hawakuwa nayo kwanza ikiwa ni lugha ili kurahisisha mawasiliano na mahusiano ya kimataifa sambamba na teknolojia za kutengeneza vitu ambavyo wachagga walikuwa wananunua kutoka nchi nyingine hususan nchi za Ulaya. Lakini kitu kimoja ambacho Mangi Rindi Mandara alikataa ni kusambaza dini au imani tofauti na walizokuwa nazo wachagga kwa kuwa aliona kwa eneo hilo haoni kama kuna kitu kipya au cha tofauti kinachohitaji mabadiliko.

– Wakati mmisionari wa kiingereza Charles New ametembelea Kilimanjaro mwaka 1871 na kwa mara ya pili 1873 Mangi Rindi Mandara alimpa eneo ambalo alitaka afungue shule kwa ajili ya wachagga kujifunza baadhi ya mambo. Hata hivyo Charles New alipoonekana kuvuka mipaka na kujaribu kufanya na kuzungumzia mambo mengine ambayo hayakumpendeza Mangi Rindi Mandara alivamiwa na kufukuzwa Kilimanjaro na kuacha kituo hicho cha shule na misheni aliyojaribu kufungua katika eneo la Kitimbirihu, Mdawi, Old Moshi.

– Mwaka 1884 alipokuja Kilimanjaro Sir Harry Hamilton Johnston kutoka Uingereza akiwa ametumwa na taasisi ya Royal Geographical Society akiwa na barua kutoka kwa Malkia Victoria wa Uingereza kupitia balozi wa Uingereza Zanzibar Sir John Kirk kuja kwa Mangi Rindi Mandara, kwa madai kwamba amekuja kufanya tafiti za kisayansi kuhusu mimea na uoto wa mlima Kilimanjaro Mangi Rindi Mandara alimhoji maswali mengi sana. Baada ya mahojiano marefu Mangi Rindi alimwambia Johnston kwamba anahitaji abaki Kilimanjaro na kufungua shule ili wachagga wajifunze baadhi ya mambo hususan lugha na teknolojia zitakazosaidia wachagga kukuza teknolojia ya kutengeneza vitu wanavyonunua Ulaya kama vile fenicha, bunduki, mizinga, baadhi ya nguo n.k., Hata hivyo baada ya miezi sita Sir Harry Hamilton Johnston aliondoka bila kufanya hivyo.

– Mwaka 1885 wamisionari wa CMS kutoka London, Uingereza waliitikia wito wa barua walizokuwa wanatumiwa mfululizo na Mangi Rindi Mandara tangu mwaka 1878 na kufika Kilimanjaro kwa ajili ya kufungua shule na kituo cha misheni. Mwaka huo huo wa 1885 Askofu James Hannington kutokea London, Uingereza aliyekuja kuhudumu Afrika mashariki alifika Kilimanjaro kuonana na Mangi Rindi Mandara ambaye alimpokea kwa furaha na kufurahia kuja kuanzishwa kwa shule Kilimanjaro lakini baada ya mazungumzo marefu Mangi Rindi Mandara alimweka wazi kabisa kwamba hatahitaji kuenezwa kwa itikadi au imani yoyote zaidi ya dini. Askofu James Hannington ameelezea mazungumzo yake haya na Mangi Rindi Mandara kwenye andiko lake hilo wakati anaondoka Kilimanjaro na msimamo wa Mangi Rindi Mandara ulivyokuwa juu ya uwepo wao Kilimanjaro.

– Hivyo wamisionari wa CMS waliendeleza kituo cha Kitimbirihu kilichoanzishwa na Charles New na kuendelezwa na Harry Johnston. Walijenga shule na hospitali ambapo wanafunzi wa kichagga walianza kuhudhuria na hospitali hiyo kutibu watu. Hata hivyo lengo lao kuu lilikuwa ni kusambaza injili lakini hilo halikuweza kufanikiwa kwa kipindi hicho na mara kwa mara waliingia kwenye mivutano na Mangi Rindi Mandara na hata kutishia kuondolewa. Waliendelea kuboresha mahusiano yao na wachagga kwa kuendelea kutoa huduma hizo mpaka miaka 8 baadaye walipoondolewa na wajerumani ambao walikuwa wamebadilika na kuanzisha ukoloni.

– Mambo yote haya na mengine mengi yalifanyika kabla ya ukoloni ili kuboresha maisha na kutengeneza “ustaarabu” bora zaidi wa wachagga kupitia kukuza uchumi na kuimarisha mahusiano ya kidiplomasia hususan yale ya kimataifa. Tunafahamu kwamba katika miaka ya 1880’s mabalozi wa kichagga walitumwa Ujerumani kuonana na Kaiser Wilhelm II ambaye alikuwa mtawala wa Ujerumani wa wakati huo na rafiki mkubwa wa Mangi Rindi Mandara. Japo mabalozi hawa wanne waliotumwa Ujerumani walirudi Kilimanjaro na taarifa nyingi kutoka huko lakini wangekuwa na elimu kubwa ya kidiplomasia na wanaelewa vizuri lugha nyingine za mawasiliano ni wazi kwamba wangeweza kufanya vizuri zaidi katika misheni hiyo. Hii ndio sababu watawala wa Kilimanjaro walihimiza suala la elimu na kuboresha maisha kwenda kuwa bora zaidi.

– Unaweza sasa kupata picha kwamba mambo yote haya yalifanywa na wachagga wenyewe kabla ya ukoloni na nje ya mipango ya wamisionari. Hii ni ishara ya wazi kwamba bila hata ya wakoloni na nje ya mipango ya wamisionari tayari wachagga walikuwa kwenye mikakati yao wenyewe ya kuendelea kuwa bora sawa na jamii nyingine bora kabisa duniani. Miaka ya baadaye Mangi Petro Itosi Marealle aliandika kwamba wachagga tunahitaji kujifunza sana na kukuza “ustaarabu” wetu kufikia ule wa wazungu na sio mwingine wowote hapa katikati. Mangi Petro Itosi Marealle alikuwa anazungumzia suala la wachagga kuwa na “ustaarabu” endelevu na sio “ustaarabu” uliofungwa na itikadi yoyote ambayo inadumaza au kuzuia kuboreshwa kwa maisha katika nyanja za maisha ya wachagga.

– Hivyo ni wazi kwamba bila ukoloni wala harakati za wamisionari bado wachagga walikuwa wanaelekea kuwa bora zaidi kijamii, kiuchumi na hata kisiasa na huenda wangeweza kutunza zaidi tamaduni zao na kwa namna bora zaidi kwao kuliko ilivyotokea kama jinsi jamii za mashariki ya mbali zimefanikisha hilo.

Karibu kwa maoni au maswali.

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

Whatsapp +255 754 584 270

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *