UKOO WA KINABO.

– Kinabo ni ukoo mashuhuri wa wachagga unaotokana na watawala waliowahi kupita zamani na kupata umaarufu au umashuhuri katika himaya husika. Ukoo huu unapatikana kwa kiasi maeneo ya Lyamrakana, Marangu na kwa wingi kiasi maeneo ya Mkuu, Rombo. Huu kwa sehemu kubwa ni ukoo wa watu makini na wasomi zaidi ambao wanafahamiana kwa karibu na wenye kujivunia sana historia yao umashuhuri sana iliyopita miaka ya zamani.

– Kutoka kwenye historia ukoo wa Kinabo umetokana na watawala waliojulikana kwa jina la Kinabo waliotawala kwa nyakati tofauti katika himaya ya umangi Marangu na himaya ya umangi Mkuu, Rombo. Katika himaya ya umangi Marangu Mangi Kinabo akiwa ni mtoto wa Mangi Itosi wa Marangu alitawala katika miaka ya 1850’s akisaidiwa na Mangi Rindi Mandara wa Old Moshi baada ya kufariki kwa kaka yake Mangi Ndaalio. Mangi Kinabo ambaye mwanzoni alishirikiana na mke wa Mangi Itosi aliyeitwa Msanya walikimbilia Old Moshi na kusaidiwa na majeshi ya Mangi Rindi Mandara kuitawala Marangu. Baadaye Mangi Kinabo alikuja kuangushwa na majeshi ya Kibosho yaliyoongozwa na Mangi Sina Mushi na kumweka madarakani Ndegoruo Marealle. Hadithi nzima ya mivutano, uhasama na vita kati ya majeshi ya Old Moshi na majeshi ya Kibosho katika eneo hilo imeelezwa kwa kina zaidi ndani ya kitabu cha “Miaka 700 Ya Wachagga”.

– Katika himaya ya umangi Mkuu, Rombo Mangi Kinabo alitawala kuanzia kwenye miaka ya 1870’s akiwa ni mtoto wa Mature na mjukuu wa Kimbarika. Mangi Kinabo wa Mkuu, Rombo anatambulika na historia kama mtawala aliyekuwa maarufu mwenye nguvu kubwa kijeshi na aliyekuwa na ushawishi mkubwa katika ukanda huo wa mashariki ya mbali ya Uchagga, Kilimanjaro. Mangi Kinabo wa Mkuu, Rombo anafahamika pia kama mtawala aliyekuwa jasiri, mkorofi sana, aliyeogopwa na kuheshimiwa lakini aliyekuwa mfanyabiashara mashuhuri katika nyakati zake. Aliiunganisha na kuitawala himaya ya umangi Mkuu, Rombo mpaka mwanzoni mwa karne ya 20 na ameacha historia kubwa ya kukumbukwa. Hadithi yote kuhusu utawala wa Mangi Kinabo na historia yote iliyofuatia ya vizazi vyake imeelezwa kwa kina katika kitabu cha “Miaka 700 Ya Wachagga”.

– Hivyo unaweza kuona kwamba ukoo wa Kinabo kwa maeneo yote umetokana na watawala ambapo ni kizazi cha umangi ndio maana utakuta sehemu kubwa ya watu wanaotokana na ukoo huu wanatumia pia “Moshi” kama jina la ukoo hususan wachagga wa kizazi cha Mangi Kinabo wa Marangu. Hivyo jina Kinabo linatumika na watu wachache huku watu wengi wa kizazi hicho wakitumia “Moshi” kwa sababu Kinabo ni sehemu tu ya watawala kati ya watawala wengi ambao vizazi vyao wanatumia “Moshi” kama jina la ukoo.

– Kwa maana hiyo ukoo wa Kinabo umesambaa zaidi kwa kiasi katika maeneo hayo husika yaliyoelezwa kwa kina zaidi na kwa mtiririko katika kitabu cha “Miaka 700 Ya Wachagga”.

– Hivyo ukoo wa Kinabo unapatikana kwa uchache sana katika kijiji cha Lyamrakana, Marangu.

– Ukoo wa Kinabo unapatikana kwa wingi katika kijiji cha Makiidi, Mkuu, Rombo.

– Ukoo wa Kinabo unapatikana kwa kiasi Mkuu Mjini katika kata ya Kelamfua, Mkuu, Rombo.

Tunahitaji kufahamu zaidi kuhusu ukoo wa Kinabo.

Karibu kwa Mchango zaidi wa mawazo na taarifa kuhusu ukoo wa Kinabo.

1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Kinabo?

2. Unafikiri ni kijiji gani ambacho kimesahaulika kutajwa lakini kuna ukoo wa Kinabo?

3. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Kinabo?

4. Kama wewe ni wa ukoo wa Kinabo una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu?

5. Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani?

6. Wewe ni Kinabo wa kutokea kijiji gani?

7. Bado kuna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo wa Kinabo kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?

8. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Kinabo?

9. Wanawake wa ukoo wa Kinabo huitwaje, na kwa nini?

10. Una rafiki yako yeyote wa kutokea kwenye ukoo wa Kinabo?

11. Ni watu gani mashuhuri unaowafahamu kutoka kwenye ukoo wa Kinabo?

12. Kuna mnyama yeyote ambaye labda ni mwiko kuliwa na wachagga wa ukoo wa Kinabo?

13. Kuna ukoo ambao hawaruhusiwi kuoana na Wako-Kinabo kwa sababu zilizowahi kuwepo miaka ya zamani au nyingine zozote?

Karibu kwa Mchango zaidi au maswali.

Ahsanteni.

Wiki ijayo tutaendelea na ukoo mwingine.

www.wachagga.com

Urithi Wetu Wachagga (Facebook).

urithiwetuwachagga@gmail.com

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *