– KNCU ni Taasisi Iliyokuwa Nyuma Ya Maendeleo Makubwa Ya Wazawa Kilimanjaro Mpaka Kufikia Miaka Ya 1960’s. Ni Taasisi Iliyoanzishwa Kutokea Kwenye KNPA kama chama cha wakulima wazawa mwaka 1924 kabla ya kugeuka na kuwa chama cha ushirika cha wazawa KNCU mwaka 1930. Taasisi hii iliweza kuwaweka wachagga mbele sana kiuchumi na hata kisiasa na kujenga misingi bora na kuendelea kuimarisha taasisi ambazo kama zisingebomolewa baadaye basi Kilimanjaro ingekuwa iko mbali sana kwa sasa, pengine hata kwenye uchumi wa dunia ya kwanza.
– Hata hivyo KNCU haijafa, bado ipo isipokuwa tu kuanzia iliporudi tena imedorora sana/imedumaa, kwa sababu mbalimbali, yaani imelala.
– KNCU kama chama kiliweza kukua na kuimarika mpaka kufikia miaka ya 1960’s kwa sababu ya ari kubwa ya mafanikio na utajiri wa fedha waliyokuwa nayo wachagga tangu miaka ya 1910’s. Tumesoma kwenye kitabu cha Eva Stuart Watt cha “Africa’s Dome of Mystery” ambaye alishuhudia kwa macho yake katika miaka ya 1920’s jinsi wachagga walivyokuwa na ari kubwa ya kutajirika kupitia kilimo cha kahawa kiasi cha kupelekea ardhi kupiganiwa kwa nguvu zote na mashamba yote kupandwa kahawa kwa kasi kubwa sana.
– Eva Stuart Watt anasema hayo mapambano ya kugombania mashamba ili kutajirika kupitia kahawa yalikuwa ni ya kipekee kabisa, hakuwahi kushuhudia sehemu nyingine yoyote ikiwemo huko Kenya ambapo alikuwa ameishi kabla. Anasema ilikuwa inashangaza vile watu walikuwa na ari na makini katika kuhakikisha kila sehemu ya shamba imepandwa miche ya kahawa katika kupambania utajiri.
– Umoja, uongozi bora sambamba na ari ya utaifa na uzalendo vilisaidia sana kujenga taasisi imara sana Kilimanjaro zilizopelekea kujenga uhakika wa kuwa na bidhaa zenye ubora. Hili lilichangiwa sana na kuwa na mipango madhubuti sambamba na kuwekeza sana katika utaalamu.
– Baadaye serikali kuu ya wachagga iliyotokana na kuboreshwa sana kwa mifumo ya utawala iliyoendelea kuboreshwa zaidi tangu miaka ya 1920’s ilikuja na sera bora zaidi za kiuchumi na hivyo kuendelea kufanya vizuri zaidi. Matumaini makubwa ya kufika mbali sana kiuchumi katika sekta zote yaliongezeka sana baada ya serikali ya wachagga kuimarika zaidi katika miaka ya 1950’s katika sekta zote za kiuchumi na sio kilimo peke yake.
– Hata hivyo baada ya serikali ya wachagga kudhoofishwa na baadaye kuangushwa mwanzoni mwa miaka ya 1960’s mambo yalianza kuyumba kiasi. Lakini hata hivyo bado KNCU haikuyumba sana kutokana na misingi imara sana iliyokuwa imejengwa kuanzia kwenye vyama vya msingi vya ushirika Uchaggani kote. Na hata mpaka leo hii bado kila mchagga anaijua KNCU ilipo katika kijiji chake au kata yake.
– Lakini hata katika miaka ya 1960’s licha ya sera ya serikali ya awamu ya kwanza kutokuwa na mpango wowote na vyama hivi vya ushirika wala kuviwezesha kama ilivyokuwa inafanyika hapo kabla bado vilionekana kuendelea kukomaa na kukua kwani vilikuwa ni tumaini kubwa kwa wazawa. Ndipo katika miaka ya 1970’s serikali ya awamu ya kwanza iliamua kuvifuta kabisa na kuleta taasisi mbadala za masoko ya bidhaa za kilimo ambazo hazikuweza kuwa na mchango wowote zaidi ya kuishia kufa kwa sababu wahusika waliopewa vyeo huko hawakuwa na uelewa wala uzoefu na biashara husika.
– Watu wengi wanakubaliana kwamba kusudio la Julius Nyerere lilikuwa ni kuvifuta vyama hivyo kwa sababu aidha za kisiasa au za kibinafsi. Lakini katika hali ya kawaida kufuta vyama vya ushirika vilivyokuwa vinajitahidi kufanya vizuri huku vikiwa na uzoefu mkubwa na vilivyodumu miaka mingi ili ulete taasisi nyingine zisizojua chochote juu ya biashara ya ushirika ni sawa na kumwamsha mgonjwa aliyelala ili umpe dawa feki ya usingizi. Reginald Mengi kwenye kitabu chake cha “I can, I must, I will”, anasema kwamba vyama vya ushirika vilikuwa na faida kubwa sana na mchango mkubwa sana kwenye uchumi wa maeneo husika lakini hajui ni kwa nini Julius Nyerere aliamua kuvifuta.
– Ali Hassan Mwinyi kwenye kitabu chake cha “Safari Ya Maisha Yangu” anakiri kwamba kufuta vyama vya ushirika lilikuwa ni kosa na hivyo aliamua kuvirudisha. Hivyo baadaye vyama hivi vya ushirika viliruhusiwa kuendelea kufanya kazi. Lakini hata hivyo wakati huu vinarudishwa vilikuwa vimefutwa na kuvurugwa kabisa na serikali ya awamu ya kwanza hivyo havikuwa na nguvu tena wala ari na mwamko kama ilivyokuwa nayo kabla ya kufutwa na Julius Nyerere. Lakini kibaya zaidi licha ya kurudishwa vimekuwa vinaingiliwa sana na serikali mara kwa mara, kitu ambacho ni kikwazo kikubwa kwa maendeleo yake.
– Hivyo sasa changamoto kubwa ya KNCU kwa sasa ukiachana na changamoto nyingine nyingi za ndani ni kuingiliwa na serikali. Siku zote taasisi, shirika, chama au jambo lingine lolote kuingiliwa na serikali mara nyingi huishia kubomoa zaidi kuliko kujenga. Hii ni kwa sababu serikali ni watu, na watu hao ni wanasiasa ambao siku zote huwa ni watu wa mipango mifupi mifupi kwani muda wao wa kukaa katika nafasi zao ni uchaguzi mpaka uchaguzi na hakuna uhakika kama ataweza kurudi kwenye nafasi yake. Hivyo hawawezi kuweka mipango ya muda mrefu katika jambo na mara nyingi wakiingilia jambo huingiza maslahi yao kwenye jambo hilo aidha ya kisiasa au ya kibinafsi yaani lengo lao huwa ni aidha kupata umaarufu wa kisiasa kwa ajili ya uchaguzi ujao au kunufaika binafsi kwa fedha au mali.
– Rais wa 40 wa Marekani aliyeitwa Ronald Reagan aliwahi kusema, “serikali sio suluhisho la matatizo yetu, bali serikali yenyewe ni tatizo”. Ndio maana wataalamu wengi wa masuala ya utawala wanaamini kwamba ili mambo yaende vizuri serikali inapaswa kupunguza kuingilia mambo yasiyoihusu na kuachia mamlaka au taasisi husika. Kwa mfano kama jambo linapaswa kutatuliwa mahakamani serikali inapaswa kuiachia mahakama badala ya kuingilia.
– Kitu kikubwa ambacho serikali inapaswa kufanya katika kuisaidia nchi ni kupunguza matumizi yake kisha kupunguza kodi kwa wananchi ili iepuke kuwa mzigo au kikwazo kwa ukuaji wa uchumi wa nchi na kuziacha biashara zistawi. Hivyo gharama za uendeshaji wa serikali zinapokuwa chini na hivyo kodi kupungua, biashara zinastawi na uchumi kukua hivyo kupunguza umaskini.
– Sasa chama cha ushirika KNCU ambacho huingiliwa sana na serikali mara kwa mara na kupewa maagizo mbalimbali huwezi kutegemea kwamba kinaweza kukua. Kwa sababu hujui ni lini serikali itakuja na kuamua kutoa maagizo yoyote ambayo yataweza kukiporomosha tena ikiwa kimekuwa. Mara nyingi serikali inaingilia vyama hivi kwa sababu za kisiasa kutokana na kwamba vinajumuisha watu wengi ndani yake na hivyo mwisho wa siku inabomoa kuliko kujenga. Hata usajili wa chama cha ushirika una mchakato mrefu na kuhusisha hatua nyingi kuliko kampuni ya kawaida.
TUNAPASWA KUWA NA KAMPUNI/MAKAMPUNI BINAFSI KAMA MBADALA WA KNCU.
– Tofauti na KNCU ya sasa KNCU ya zamani iliweza kufanikisha mambo mengi na makubwa kwa sababu kulikuwa na mamlaka za wazawa zilizokuwa na nia ya dhati ya kufanikisha hayo mambo makubwa. Kulikuwa pia na uzalendo wa hali ya juu kwa sababu wanufaika walikuwa ni wazawa wenyewe na wenye mamlaka pia ni wazawa wenyewe. Lakini kwa sasa wenye mamlaka ni watu tofauti ambao hawana manufaa ya moja kwa moja na kuimarika kwa KNCU kiuchumi wala kiufahari.
– Hivyo kwa mazingira ya sasa ni sahihi zaidi kuwa na kampuni binafsi kama mbadala wa KNCU itakayoendeshwa kama kampuni binafsi ambayo itakuwa na sheria zake na masharti kwa namna ambayo yataleta uwajibikaji kwa watu na kuweza kufanikisha makubwa. Inaweza kuwa ni kampuni zaidi ya moja na kujihusisha na bidhaa zaidi ya moja. Kampuni binafsi ni nzuri zaidi kwa sababu haziingiliwi na serikali kiurahisi na kama kuna changamoto za ndani ya kampuni zinatatuliwa mahakamani.
– Kampuni hizo zitakuwa na kazi ya kusimamia ubora wa bidhaa kwa kuhakikisha masharti yote yaliyowekwa kuhusu ubora yanazingatiwa kama ilivyokuwa inafanya KNCU ile ya zamani. Kampuni hiyo au hizo zinahakikisha bidhaa bora kabisa ndizo zinaingia sokoni na zinapatikana kwa uhakika ili kuhakikisha zinateka soko hilo kwa uhakika. Kazi kubwa ya kampuni hizo inakuwa ni kusimamia mnyororo wa ongezeka la thamani(value chain) mpaka mwisho huku zikinufaika kwa makato inayolipwa kutoka kwa wakulima.
– Mtaji wa kampuni hiyo au hizo unaweza kuanzishwa na mwekezaji yeyote na kisha kuendelezwa kwa mfumo wa kununua hisa kwa watu ambao ni wachagga wenyewe. Hivyo kadiri wachagga wenyewe watakavyohamasika kununua hisa zaidi ndivyo kampuni itakavyoweza kutanuka zaidi na biashara kukua na wao kuzidi kunufaika. Muhimu ni kuzingatia uendeshaji bora sana wa kampuni ambao utajenga imani kwa wawekezaji wake na kuwa suluhisho la kuondoa umaskini Uchaggani.
– Hii ndio moja ya njia za uhakika zaidi za kurudisha ule utukufu wa zamani chini ya KNCU na hata kufanya vizuri zaidi ya ilivyokuwa inafanyika zamani. Kuamsha na kuboresha maisha ya jamii ya wachagga na kuifanya Kilimanjaro kuwa hai tena kwa wale walioamua kuishi Kilimanjaro. Nchi ya Tanzania inaruhusu biashara huria kwa hiyo hakuna kitu kinachoshindikana isipokuwa kuweka bidii kubwa na maarifa kwa sababu kama iliwezekana zamani, sasa hivi inawezekana vizuri zaidi ya ilivyowezekana zamani.
Karibu kwa Maoni au Maswali.
Wazo la KNCU kuwa Kampuni binafsi yenye wanahisa kutoka Kilimanjaro ni zuri lifanyiwe kazi
Ahsante sana