JAMII INAYOTUMIA AKILI NDIO JAMII ITAKAYOKUWA MBELE YA JAMII NYINGINE SIKU ZOTE.

– Katika asili kila kiumbe kimeendeleza uwezo mmoja mkubwa zaidi katika moja ya viungo vyake vya mwili kwa ajili ya kuwawezesha kuishi na kudumu katika mazingira yenye kila hatari kwenye dunia tunayoishi leo hii. Kuna viumbe wameendeleza makucha makubwa, wengine miili mikubwa, viumbe wengine wameendeleza nguvu, wengine wameendeleza mbio na kasi, wengine kama vile Simba wameendeleza ujasiri n.k.,

– Lakini binadamu silaha yake kubwa dhidi ya dunia yenye kila aina ya changamoto ameendeleza uwezo mkubwa kiakili. Ukiangalia kila aina ya ugunduzi mkubwa uliofanywa na binadamu duniani na kumpa binadamu faida kubwa zaidi dhidi ya viumbe wengine umefanywa kwa kutumia akili. Tangu ugunduzi wa moto takriban miaka 1,000,0000 iliyopita ambao umekuwa na manufaa makubwa sana kwa binadamu katika kurahisisha mambo mengi na kujihakikishia usalama zaidi umefanywa kwa kutumia akili. Mpaka leo hii ni akili kubwa sana imeendelea kutumika katika ugunduzi wa teknolojia kubwa za vyombo vya moto, mifumo ya teknolojia za habari na mambo mengine.

– Hivyo kadiri akili inavyotumika kubwa ndivyo binadamu wanavyogundua jambo kubwa zaidi na lenye manufaa makubwa zaidi kwa binadamu. Tunaweza kuona kutoka kwenye historia tangu zama za himaya ya kale ya Misri jinsi kutumia akili kulivyoweza kuipa umashuhuri mkubwa na waliweza kugundua na kutengeneza vitu ambavyo mpaka leo hii zaidi ya miaka 5,000 baadaye vinastajaabisha na kushangaza watu.

– Tunaweza kuona pia kutoka Ugiriki ya kale jinsi Athenia ilivyowekeza katika maarifa na kuweza kuwa na umashuhuri mkubwa kuzidi himaya nyingi za Ugiriki ya kale. Licha ya miji kama Sparta kuwekeza sana kijeshi na kuimarika sana lakini bado Athenia iliweza kufanikiwa kwenye mambo mengi zaidi na kuacha jina kubwa zaidi katika historia.

– Lakini hata mpaka leo tunaona wazi kwamba jamii zote na nchi zote zilizowekeza kwenye maarifa na kutumia sana akili ndizo zenye nguvu kubwa ya ushawishi na maendeleo makubwa kiuchumi na hata kuishi katika utaratibu na mpangilio sahihi zaidi. Tunaweza kuona wazi kwamba hata dunia ya leo hii ilistaarabika zaidi baada ya kurudishwa kwa mifumo ya kijamhuri na kidemokrasia iliyoanzia nchini Marekani mwishoni mwa karne ya 18 na kuigwa na karibu nchi zote duniani sasa hivi. Hii ikiwa ni matokeo ya akili kubwa iliyotumiwa na waanzilishi wa taifa la Marekani kujifunza kutoka kwenye mifumo ya uendeshaji wa serikali kutoka kwenye tawala za kale sana za Ugiriki na Roma ambazo nazo zilikuja kuanguka zaidi ya miaka 1,500 kabla ya kuinuka tena kwa mifumo ya kijamhuri kutokana na kupuuza matumizi ya akili.

– Hivyo kama jamii ya wachagga inataka kupiga hatua na kuwa mbele sana haina budi kuwekeza nguvu kubwa katika kupata maarifa na kutumia akili sana. Kwa sababu akili siku zote kupitia maarifa na taarifa hushinda kila kitu, na mtu yeyote anayetumia akili na kujituma sana kwenye maisha atakuwa mbele sana ya wengine kama jinsi unavyoweza kuona nchi zilizoendelea sana ukilinganisha na hizi zetu za Ulimwengu wa tatu zinazoishia kupokea misaada kila siku.

– Kinyume chake ni kwamba tunaposhindwa au kupuuza kutumia akili kupitia kuwekeza sana kwenye maarifa tutajikuta tunatumbukia kwenye imani za kishirikina na kuwa na uvivu mkubwa wa kufikiri na hata kufanya mambo kiakili na hata kimwili. Hata ujasiri ambao ni moja kati ya mambo muhimu sana kwa ajili ya mtu kufanya makubwa kwenye maisha unategemea sana uwezo mkubwa wa kufikiri pia kwani uwezo mkubwa kiakili ndio chanzo cha kuondoa hofu nyingi sana za kufikirika na zisizo na uzito wowote. Hofu hizi zinapewa nguvu na ujinga peke yake lakini zinakuwa kikwazo kikubwa kwetu kupiga hatua.

– Benjamin Franklin(1706 – 1790) ambaye ni moja kati ya watu mashuhuri sana na wenye akili sana walioanzisha taifa la Marekani akiwa pia ni mwanasiasa, mgunduzi na mwanasayansi wa mambo ya umeme aliwahi kusema, “kuwekeza kwenye maarifa siku zote hulipa kwa viwango bora sana”.

– Hata hivyo hakuna kitu kizuri ambacho ni rahisi, hakuna jamii inayofikia mafanikio kwa urahisi au kwa njia ya mkato(shortcut). Kutumia akili ni moja kati ya vitu vigumu ambavyo watu wengi huvikwepa na kukimbilia vitu rahisi na vinavyoleta msisimko katika ubongo kama vile starehe mbalimbali. Hili liko wazi hata kwenye mitandao tu unaweza kuona jinsi watu hawako tayari kusoma makala ndefu hata kama ina manufaa na badala yake kukimbilia makala fupi fupi ambazo hazina maarifa yanayojitosheleza lakini hazichoshi akili. Lakini hata hivyo hali hiyo ina sababu zake za kisaikolojia na manufaa yake ambayo kwa zama hizi yamepitwa na wakati.

– Hivyo sasa sisi wachagga kama jamii tunapaswa kujua kwamba kama kweli tunataka kujitofautisha na kuwa wa kipekee basi tunapaswa kuwa tayari kuumia kwa kuzilazimisha akili zetu kufanya mambo magumu zisizoyapenda lakini yenye manufaa makubwa kwenye maisha. Kuanzia kujifunza kuhusu sisi wenyewe ili kujitambua kisha kujifunza mambo mengine mengi bila kujali sana ugumu wake ili tuweze kujenga tabia hizo kwa vizazi vinavyofuata kama ilivyokuwa inafanyika zamani.

– Tusitegemee kabisa kwamba kuna namna yoyote tunaweza tukafanikiwa kwa kuishi maisha ya mazoea na legelege kama yalivyo katika nchi hizi za Ulimwengu wa tatu na kutegemea kufika popote pa maana. Tusitegemee tunaweza kukaa tukiamini katika urahisi wa mambo, njia za mkato, ushirikina na miujiza ambayo haipo katika uhalisia na kutegemea kwamba tutapiga hatua yoyote ya maana. Inahitajika nidhamu kubwa sana ya kujifunza kwa bidii na kuweka kwenye matendo yale tunayojifunza kwa bidii kubwa sana ili kuonekana wa kipekee na wa tofuati na hivyo pia ndivyo ilivyofanyika zamani.

– Mifano iko wazi kwa nchi mbalimbali duniani zilizowekeza sana kwenye maarifa na kuacha kujidanganya katika ushirikina kama vile Japan, Korea, Ujerumani, Marekani na nyingine zinazokuja kwa kasi kama vile Singapore, Thailand, Malaysia n.k., Watu wengi maarufu kwenye jamii hupenda kuja na hadithi nzuri na rahisi ili kuvutia watu na kujenga ushawishi kiurahisi lakini katika uhalisia mambo sio rahisi kama yanavyoonekana wala sio bahati kama wengi wanavyofikiri bali ni kazi kubwa sana inafanyika, akili nyingi kutumika na ujasiri mkubwa kuhusika pia nyuma ya pazia.

– Tuwe tayari kuumiza akili katika kujifunza na kufanya mengine ili tuweze kurudisha heshima kubwa, kujitofautisha na kuwa wa kipekee.

Karibu kwa maoni au maswali.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *