UKOO WA MWANDRI.

– Ukoo wa Mwandri ni ukoo mkongwe sana na maarufu katika eneo la Siha Sanya Juu. Huu ni ukoo ambao uliweka makazi yake ya kudumu katika kijiji cha Wanri, Siha upande wa juu wa hospitali ya Kibong’oto. Kijji hiki cha Wanri miaka ya baadaye kilikuja kuwa maarufu zaidi na muhimu zaidi kwenye masuala ya utawala katika himaya ya umangi Siha/Sanya Juu.

– Ukoo wa Mwandri ndio ukoo pekee uliowahi kutoa watawala wa himaya ya umangi Siha/Sanya Juu ambao haujawahi kuwa na makazi kabisa katika kijiji cha Samaki Maini. Hii ni tofauti na koo zote mashuhuri ambazo zimewahi kutoa watawala wa eneo hili kama vile Kileo, Orio, Mmari n.k. ambao wote waliwahi kuwa na asili katika kijiji cha Samaki Maini.

– Katika nusu ya pili ya karne ya 19 Mangi Ngalami alitawala Siha yote isipokuwa kijiji cha Wanri ambacho kilikuwa chini ya utawala wa Mangi Nkunde kutokea kwenye ukoo wa Mwandri. Baadaye Mangi Nkunde wa ukoo wa Mwandri alikuja kuuawa na watu wa Kibosho akiwa njiani kutokea Machame kuelekea Kibosho akituhumiwa kuhusika kwenye mauaji ya ndugu yao. Hivyo baada ya Mangi Nkunde Mwandri kuuawa kijiji cha Wanri hakikuwa na mtawala na hivyo moja kwa moja kutawaliwa na Mangi Ngalami wa ukoo wa Mmari aliyekuwa mtawala wa Siha yote.

– Mangi Nkunde aliiacha familia yake, mke wake na mtoto wake aliyeitwa Simeon kwa Mangi Shangali wa Machame, hivyo baada ya kuuawa mke wa Mangi Nkunde na mtoto wake walibaki Machame kwa Mangi Shangali. Baadaye Simeon mtoto wa Mangi Nkunde alipokuwa mkubwa alirudi tena Siha/Sanya Juu na kurudisha makazi yake katika kijiji cha Wanri kilichokuwa himaya ya ukoo wa Mwandri.

– Mwaka 1927 Simeon Mwandri mtoto wa Mangi Nkunde kutoka katika ukoo wa Mwandri katika kijiji cha Wanri, Siha alifanikiwa kuwa mtawala wa mwisho wa himaya yote ya umangi Siha/Sanya Juu ambaye ni mzawa wa eneo hilo. Mangi Simeon Mwandri alifanikiwa kukalia kiti cha utawala wa umangi wa Siha baada ya Mangi Malamya kutokea Kibosho kuondolewa madarakani kwa njama za kisiasa zilizotokana na tuhuma mbaya dhidi yake.

– Hata hivyo haikuchukua muda mrefu kabla himaya ya umangi Siha kuanza kutawaliwa moja kwa moja na Machame baada ya Mangi Simeon Mwandri kuondolewa madarakani kwa zengwe lingine la kisiasa lililoasisiwa huko Machame. Hivyo Mangi Simeon Mwandri kutoka katika ukoo wa Mwandri ndiye akaacha historia kuwa mtawala wa mwisho mzawa wa Siha/Sanya Juu kabla ya Siha utawala wa Siha kuchukuliwa na watawala wa Machame.

– Ukoo wa Mwandri ambao ulikuwa ni ukoo wa wapiganaji hodari na waliokuwa na utajiri wa mifugo na wakulima hodari umeendelea kuwa ndio ukoo mashuhuri katika kijiji cha Wanri mpaka leo hii. Ukoo wa Mwandri unapatikana pia katika vijiji vingine vya Siha/Sanya Juu vilivyopo jirani na kijiji cha Wanri kama vile kijiji cha Mae, Fuka n.k.

1. Je, unafahamu nini kuhusiana na ukoo wa Mwandri?

2. Kijijini kwenu kuna ukoo wa Mwandri?

3. Kama wewe ni wa ukoo wa Mwandri una nini cha kutuambia kuhusu ukoo wenu? Huwa mna maadhimisho yoyote au sherehe za ukoo mwezi gani?

4. Bado kuna ushirikiano wowote katika matukio mbalimbali muhimu na ndugu zenu wengine wa matawi ya ukoo huo kutoka maeneo mengine ya Uchaggani?

5. Ni tabia gani unazozifahamu za wachagga wa ukoo wa Mwandri?

6. Wanawake wa ukoo wa Mwandri huitwaje?

7. Una rafiki yako yeyote wa ukoo wa Mwandri?

8. Watu gani mashuhuri unaowafahamu kutoka kwenye ukoo wa Mwandri?

Karibu kwa Maoni na Maswali.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *