UCHAMBUZI WA KITABU. – SEHEMU YA 2.

*Maisha Ya Mchagga Hapa Duniani Na Ahera” By Mangi Petro Itosi Marealle*

Uchambuzi by Mary Assenga.

Utaratibu Uliofutwa Kabla Ya Kuzaliwa Mtoto;

-Kabla Ya Mtu Kuoa kwa desturi alichagua mke wa umbo na sura nzuri aliye wa ukoo bora au ukoo wa watu makini wasio na matatizo ya asili kama vile magonjwa na mambo mengine yasiyofaa. Kabla ya kufanya chochote ilitakiwa wawe wameoana kwanza kwa kufuata taratibu zote zilizopangwa. Ni tofauti na sasa ambapo mtu unakutana na mtu mjini wala hujui alipotoka, hujui asili yake huelewi matatizo ya kwao unalazimisha tu kuingia naye kwenye maisha hammalizi hata mwaka mnashindwana au mnabaki katika ndoa ya kujilazimisha katika maisha au unaishia kuzaa watoto wenye tabia za ajabu au magonjwa ya ajabu ajabu.

-Ilikuwa inashauriwa wanapokutana mke na mume kwa ajili ya kupata mtoto wasiwe wamekunywa pombe kwani inaweza kumuathiri mtoto atakayezaliwa. Wakiwa wameingiliana usiku kama mwanamke anataka kuzaa mtoto wa sura na umbo zuri ilhali mume hana sura nzuri basi mwanamke hutoka nje asubuhi kutazama maua ya mgomba na maua ya mwitu yaitwayo “machemerii” kwa muda kabla ya kurudi ndani. Wakati wa ujauzito pia mwanamke alikuwa anakula udongo wa kichuguu akiamini kwamba kwa kufanya hivyo mtoto atakayezaliwa atakuwa mwenye afya na nguvu pia wakati huu wa mimba mwanamke hula udongo mwekundu uitwao “kimaande” kutokana na uchu wa mimba.

Wakati Wa Kuzaliwa Mtoto

-Baba na mama mkwe ambaye ni mama wa mume ndio huhangaika sana wakati wa kuzaliwa mtoto. Wanaweza kumwita mkunga kusaidia kuzalisha kama wataona ni vyema, kama mkungwa asipokuwa mama mkwe anaweza tu kuwa mama mwingine ambaye kwa kichagga huitwa “mkeku moende mana”. Mtoto akishazaliwa mkunga huagiza majani yaitwayo kwa kichagga “masunzuku” ambayo huyachovya ndani ya maji ya uvuguvugu na kisha kumfuta nayo mtoto mwili mzima na kumpaka siagi mwili mzima. Mtoto wa umri huu huitwa “mnangu”, maana yake mtoto mchanga.

-Mtoto hupewa dawa fulani ili akitumia maziwa ya mama yasimdhuru kisha hupewa maji ya chemchemi au ndizi iitwayo “mrarao” iliyovumbikwa ndani ya majivu ya moto kabla ya kumenywa ili ipate kuiva vizuri na kuwa laini. Ndizi hii ikishaiva hutafunwa na kutemewa mtoto kinywani ameze. Chakula hiki cha kwanza huitwa “kelya ketocha mana ulaka” maana yake, chakula cha kutoboa koo la mtoto.

-Ilikuwa hairuhusiwi kumwona mtoto kabla yakutimiza miezi mitatu kutokana na imani kadhaa zilizokuwepo. Alama ya kuonyesha nyumba au mahali palipofanywa marufuku ni kusimika mti uitwao kwa kichagga “sale” ulio na majani yaliyopigwa fundo na kusimikwa karibu na mlango wa nyumba ya mzazi. Mtoto apatapo umri wa mwezi mmoja mama huanza kumpikia chakula cha ndizi kinachotiwa maziwa yasiyochacha ndani ya chungu kidogo kiitwacho kwa kichagga “kitosho” na kukipakulia katika kisahani kidogo cha mti ambacho huitwa “iriko” au “kimborikoe”. Kila mlo wa mtoto huitwa kwa kichagga “ndutsa”.

-Mtoto huweza kuwa na tabia mbaya ambazo huaminika kwamba amerithi kwa wazazi hasa baba, au wakati mama ni mjamzito huenda baba au mama alimcheka mtu mwenye sura mbaya, au kucheka mlio wa wanyama au ndege na kadhalika. Tabia hizi ambazo huitwa kwa kichagga “mbaka mbicho” baada ya kugundulika huondolewa kwa mtoto kuoshwa kwa maji yaliyotafutwa ya mvua au chemchemi asubuhi mapema. Taratibu hii ya kuondoa “mbaka mbicho” haifanywi mara moja tu hufanyika tena mtoto aanzapo kubalehe.

-Mtoto akifikisha umri wa miezi mitatu huitwa “mkoku” naye hutafutiwa Yaya ambaye huitwa kwa kichagga “Mori” maana yake mwezi. Yaya huyu hukaa na mtoto wakati wazazi wapo katika shughuli. Na ikiwa wazazi hawawezi kumwajiri yaya, huwa ni kazi yao kumtunza kwa zamu.

Wimbo ambao Yaya humwimbia mtoto wa miezi mitatu ni huu

“Mana kutsie he, eh kutsie, He, nyi kiki kyakapa mana kalia;

“Nyi kiki kyakapa mnangu kalia; He kutsie mana kutsie”.

Maana yake

”Mtoto jinyamazie he, kitu gani kimempiga mtoto akalia, ni kitu gani kilimpiga malaika akalia, jinyamazie mtoto, jinyamazie”.

-Mtoto huendelea kutunzwa mpaka anapofikia kuota meno na hapo hufanyika sherehe kubwa ya kumwimbia na kumshangilia sana na kuchinjiwa mnyama. Kuota meno ni hatua muhimu na ni swala zito sana kwa mchagga na ndio maana ukimpiga na kwa bahati mbaya ukamng’oa jino mchagga kwa desturi utalipa ng’ombe jike na mbuzi mmoja kama fidia.

-Yaya huendelea kumtunza mtoto na kumfundisha vitu vingi kadiri anavyokuwa, humsaidia utamkaji wa maneno mbalimbali, humwelekeza aina nyingi za vitu, miti wadudu, wanyama na vitu ambavyo atahitaji kuchezea kadiri anavyoendelea kukua. Ilikuwa ni marufuku pia mtoto kutumia mkono wa kushoto hivyo ilikuwa ni kazi ya yaya kuhakikisha mtoto anazoe kutumia mkono wa kulia na alipokuwa anakuwa mgumu kutumia mkono wa kulia yaya aliripoti hilo kwa wazazi ambao waliufunga mkono wa kushoto na kitu kizito ili atumie ule wa kulia.

-Mtoto anapoendelea kukua hubadilishiwa mapishi ya chakula chake yakawa tofauti kidogo na yale ya kwanza, mtoto huanza kupikiwa chakula kiitwacho “kimantine” ambacho kwa sehemu kubwa ni chakula cha ndizi.

-Basi mtoto akiendelea vizuri na hatua ya kutembea wazazi waliweza kumpa yaya wake ruhusa aende zake ikiwa wazazi hawa si watu wenye wanyama wengi au upendo; mama na baba watamtunza mtoto wenyewe. Yaya alipewa ujira wake kumlea mtoto. Ujira wa Yaya ni mbuzi mmoja. Jinsi Mchagga ajuavyo kutunza mali yake ya wanyama, wazazi wa yaya wakiwa wema walimsaidia yaya kubadilisha yule mbuzi wapate ng’ombe kwa kumpa mbuzi mwingine wakawa wawili. Ikiwa wazazi wa mtoto na wa yaya ni watu wanaopendana, yaya aliweza kuzidi kumsaidia mtoto kwa muda zaidi ya mwaka mmoja, lakini gharama huwa ile ile, yaani mbuzi mmoja na chakula.

Yaya hodari, mwenye utii na kusaidia vema mtoto alipendwa , na amalizapo kazi yake ya kulea mtoto hakusahaulika kwa wazazi wa mtoto wala kwa mtoto akuapo. Alikaribishwa nyumbani kila mara.

Itaendelea

Urithi Wetu Wachagga.

urithiwetuwachagga@gmail.com

Whatsapp +255 754 584 270.

You may also like...

Popular Posts

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *